NAFASI NA UZITO WA AGANO LA KALE NA AGANO JIPYA KATIKA BIBLIA-2

Na Askofu Mkuu Silyvester Gamanywa.

Msomaji wangu mpendwa, karibu kwenye sehemu ya tatu ya mada yetu. Katika utangulizi wa makala ya kwanza nilitoa muhtasari wa mtiririko wa uchambuzi wa maagano yaliyomo katika Biblia. Lakini baada ya kuona baaadhi ya maoni ya wasomaji nimegundua uwepo wa upungufu wa katika uelewa kuhusu maagano yenyewe. Makala ya leo nimeona nitoe kipaumbele cha uchambuzi wa kufafanua moja kwa moja kuhusu nafasi na uzito wa agano la kale na agano jipya. Nina imani kwa wale wenye kutafuta kuijua kweli mada hii itarahisisha uelewa na michango yao itakuwa na tija kwa wasomaji wa ukurasa huu. Karibu sana.
USAWA NA TOFAUTI
Maagano yote ni sawa kwa maana yote ni maagano yaliyotoka kwa Mungu, yamebeba jumbe kutoka kwa Mungu, yametunza amri, sheria na maagizo kutoka kwa Mungu, na yanafaa kwa kujifunza elimu ya Mungu! (2 Tim.3:16)
Tofauti kubwa iliyopo ni kwenye matumizi yake kulingana na nyakati, walengwa na mazingira yake. Katika Agano la Kale yako maandiko ambayo matumizi yake yaliwalenga watu maalum ambao ni taifa la Israeli, kwa mazingira ya wakati wao, lakini sasa hayatumiki katika mazingira yetu mataifa mengine ambayo si wana wa Israeli hayakutambulika wala kuwa sehemu ya Agano hilo (
Katika Agano Jipya maandiko yake yameandikwa kwa ajili ya matumizi ya kanisa la Kristo ambalo ni mjumuiko wa watu wote (wayahudi na mataifa mengine wasio wayahudi), na ndimo ilimo miongozo ya kutusaidia kufanya mapenzi ya Mungu kwa wakati wote katika mazingira yetu (Yh.3:16-18; Mt.28:19-20; Mk.16:15-18)
UKOMO WA MATUMIZI
Agano la kale lilitabiri ujio wa agano jipya likijitabiria kuwa na ukomo wake katika matumizi (Yer.31:31-32). Agano Jipya limetabiria Agano la Kale kuwa ni kuukuu, linazidi kuchakaa na liko karibu na kutoweka (Ebr.8:13)
Agano jipya limebeba maneno ya Yesu Kristo ambayo alisema mbingu na nchi zitapita lake maneno yake ni ya milele (Mt.24:15; Mk.13:31; :Luk.21:33) Humo ndimo yalimo maneno yenye UZIMA na Nguvu za kumfanya mtu kuwa na mabadiliko ya kiroho na ahadi zake ni zile za kiroho na za milele(Yh.6:63)
HISTORIA
Mwanzoni mwa maandiko ya Agano la Kale utakuta linasimulia jinsi Adamu wa kwanza alivyotengana na Mungu na kupoteza bustani ya Edeni kwa sababu ya dhambi (Mw.3), lakini ukilisoma Agano Jipya utakuta lenyewe linatangaza jinsi binadamu ambavyo amerejeshwa katika uhusiano na Mungu kwa njia ya Adamu wa mwisho (Rum. 3—6).
WALENGWA
Katika Agano la Kale utamkuta Mungu anashughulika na taifa lake teule ya wana wa Israeli; bali katika Agano Jipya utamkuta Mungu anashughulika na Kanisa la Kristo (Mat.16:18). Na ujumbe wake mkuu wa kinabii utakuta Agano la Kale likitabiri ujio wa Masihi (Isa.53) na Agano jipya linamfunua Masihi ni nani (Yn 4:25–26).
UTAKASO
Agano la Kale lilikuwa na matendo ya kimwili ya sheria, la dhabihu za wanyama nk (Walawi 1 - 7) wakati ambao Agano Jipya linayo dhabihu ya Yesu, na tunda la Roho kwa ajili ya matendo mema (Ebr. 9:10, 10:12, 13:15; Galt. 5:22 - 24; Efe. 2:10; Rum. 12:1 - 2; Mat.19:17;)
Agano la Kale halikuwa na utakaso wa kusafisha dhamiri ya mtu na kumkamilisha mbele za Mungu (Ebr. 9:9; 10:11) lakini katika Agano Jipya ndimo mwamini anasafishwa dhambi zake na kuziondoa kabisa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Ebr 10:14 - 17; 2Kor 3:9; Kol.1:27; Mat. 5:48; Flp 2:5, 3:9 - 17; Efe 4).
Agano la Kale lilifanyika kwa tohara ya kimwili (Mw. 17:9; Kut. 12:48; Yh 7:22) Lakini Agano Jipya linafanyika kwa tohara ya moyo kwa njia ya toba (Mdo. 2:38, 3:19; Rum. 2:25 - 29; Flp. 3:3; Col. 2:11 – 13)
Agano la Kale watu wake hawakuwa na fursa ya ujazo wa Roho Mtakatifu(Rum. 7:6; Ebr. 8:7 - 9; Matt. 5:21 – 45)Agano Jipya waaminio halisi wanayo fursa ya kumpokea Roho Mtakatifu (Mat. 5:21 - 48, Rum. 7:6, Galatians 2:20; Ebr. 8:10 – 12)
IBADA
Agano la Kale ibada zake zilifanyikia kwenye hema/hekalu la kibinadamu( Ebr. 9:13; Galt 3:12; Walawi 18:5; 2 Kor. 3:16). Katika Agano Jipya kila mwamini ana fursa ya kumwabudu Mungu katika roho kupitia Yesu Kristo (Yh. 4:23 - 24, 16:23 - 27; Ebr.6:20, 10:23; Rum. 8:9 - 39; Efe. 2:18 - 22; 2 Kor. 3:6)
Agano la Kale halikutoa njia ya kuwasiliana na Mungu Baba (Ebr. 9:6 - 8; 10:19) Agano Jipya limetoa njia kwa mwamini kuingia patakatifu pa mbinguni kwa Mungu Baba (Mt. 27:51; Ebr. 4:14 - 16; Efe 7:25 - 27; Yh.16; Galt 4:6 - 7; Rum 8:15; Efe 2:18)
BARAKA
Agano la Kale lilibeba ahadi za baraka za kimwili (Kut. 19:5 - 6; Kumb.28; Walawi 26; Kumb.29:9) Liliahidi ya Kwamba mtu binafsi au taifa atabarikiwa kimwili (kiafya na kiuchumi nk) au kulaaniwa kwa (umasikini utumwa, maradhi nk) kwa kutegemea kutii au kutokutii sheria na amri zote za Mungu.
Agano Jipya limejengwa juu ya ahadi za kiroho. ((Efe. 1:3; Yh 3:16; Ebr. 8:6, 9:15; Rum 8; Luk18:29 – 30)


“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (MT. 28:19-20)
Kutokana na maandiko tuliyosoma hapa juu, napenda tupitie uchambuzi wa misamiati ifuatayo: “Mataifa yote”, “ubatizo kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, na “wanafunzi”,
MATAIFA YOTE
Yesu Kristo alipowatuma wanafunzi wake kwa mara ya kwanza kufanya mazoezi ya huduma ambayo alikusudia kuwaachia, aliwazuia wasiende kwenye miji ya watu wa mataifa (wasio wayahudi) na wasiingie kwa wasamaria:
“Hao Thenashara Yesu aliwatuma akawaagiza, akisema, katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendelea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” (Mt.10:5-6)
Sababu ya msingi ya kuwakataza ni kwa kuwa bado alikuwa hajafanya ukombozi kwa ajili ya ulimwengu wa binadamu wote. Lakini baada ya kusulubishwa, kufa na kufufuka kwake, ndipo sasa alipofungua mlango wa kwenda kwa mataifa yote. “mkawafanye mataifa yote” au “mkawafanye makabila yote” kuwa wanafunzi.
UBATIZO
Yesu Kristo aliagiza mchakato wa kuwafanya “mataifa” kuwa wanafunzi kwa “ubatizo”. Pamoja na malumbano ya muda mrefu kuhusu “ubatizo”; hapa napenda kueleza maana sahihi ya ubatizo kama ilivyotambulika enzi za karne ya kwanza.
Tuanze kwanza na tafsiri ya msamiati. Ubatizo ni tendo la kuzamisha au kuzika majini. Mtu wa kwanza kuendesha shughuli ya kubatiza alikuwa ni Yohana na akajulikana kama “Yohana Mbatizaji”. Yeye alibatiza kwa maji kwa maana alikuwa akiwazamisha majini wayahudi waliokuja kwake kutubu. "Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa." (YN. 3:23 )
Ubatizo ulitumika kama alama ya “kuwa chini ya mamlaka”. Wote waliobatizwa na Yohana walifanyika wanafunzi wa Yohana. Kila aliyetubu na kubatizwa na Yohana alitambuliwa kuwa ni mwanafunzi wa Yohana. Ushahidi wa ubatizo kuwa ni ishara ya kuwa chini ya mamlaka ya mwenye kubatiza ni kama ilivyoandikwa:“Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari.” (1 Kor.10:1-2)
Yesu Kristo aliwaagiza wanafunzi wake waende kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi kwa kuwabatiza wawe chini ya mamlaka ya Yesu Kristo, wawe wanafunzi wa Yesu Kristo. Uchambuzi mwingine muhimu katika ubatizo kwenye eneo hili ni maana ya kubatizwa kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.
Kwanini kwa jina la Baba? Kwa sababu Mungu Baba ndiye aliyetuchagua kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu na kutufanya wanawe kwa njia ya Yesu Kristo.(Efe.1:3-5). Kwanini kwa jina la Mwana? Kwa sababu Mwana wa Mungu ndiye alyefanyika dhabihu msalabani kwa ajili ukombozi wetu, kwa damu yake (EFE. 1:7-12). Kwanini kwa jina la Roho Mtakatifu? Kwa sababu Roho Mtakatifu ndiye mwenye kutuzaa mara ya pili na kututia muhuri baada ya kuamini Injili: (EFE. 1:8, 13-14)
WANAFUNZI
Msamiati wa pili ni neno “wanafunzi” ambalo limetajwa mara 244 katika Biblia. Kwenye Agano Jipya limetajwa mara 243 na Agano la Kale mara 1 tu. Kwa hiyo tunaweza kusema neno ‘wanafunzi” limetawala kwenye Agano Jipya kwa 99.6% na katika Agano la Kale 0.4%
Msamiati wa kiyunani uliotumika ni “matheteuo” ukimaanisha "kumfanya mtu kuwa mwanafunzi"
Aina ya mwanafunzi anayelengwa hapa ni "mtu anayefundishwa kwa vitendo kupata ujuzi au maarifa kutoka kwa mkufunzi wake"

Kanuni ya uanafunzi ni kupata ujuzi fulani kwa viwango vya ubora vya kuwafanya wengine kuwa wanafunzi. Lengo kuu la kuwa mwanafunzi ni kujifunza kutoka kwa mwalimu na kupata ujuzi kwa kiwango kile kile alichonacho mkufunzi wake. Ndiyo maana Yesu alisema ya kwamba "mwanafunzi hampiti mwalimu wake..." lakini "...yamtosha kuwa kama mwalimu wake" (Mt.10:24-25)
Hii ilimaanisha kwamba "Mwanafunzi" hawezi kumzidi ujuzi "mkufunzi" wake wakati anapokuwa anajifunza kila jambo kutoka kwa mkufunzi wake. Lakini ilikuwa ni wajibu wa kila mkufunzi kuhakikisha anamrithisha mwanafunzi wake ujuzi wake ili naye afikie uwezo wa kuwafanya wengine kuwa wanafunzi kwa viwango vya ubora vya mkufunzi wake
Huyu mwanafunzi ni mtu aliyekubali kujitoa kwa hiari kuwa chini ya mwalimu maalum ambaye ni bingwa wa falisafa au ujuzi maalum. Kuwa mwanafunzi ni jukumu la kudumu maisha yote. Ni tofauti na kwenda chuoni kuchukua mafunzo na kurudi kuendelea na maisha mengine. Mwanafunzi aliyekubali kuwa chini ya mwalimu awe ni Rabi au Kocha anakuwa amechagua kutumikia ujuzi au maarifa atakayopata kutoka kwa mkufunzi wake.
Enzi za karne ya kwanza, walikuwepo wanafunzi wa makundi mbali mbali au watu mbali mbali. Mathalan dini ya kiyahudi ilikuwa na wanafunzi wake ambao waalimu wao waliitwa marabi. Mafarisayo nao walijiita kuwa wanafunzi wa Musa kwa sababu walisomea sheria za torati ya Musa. Lakini pia alikuwepo Yohana Mbatizaji ambaye naye alikuwa na wanafunzi wake.
Kwa misingi hii ndiyo maana Yesu aliwaita na kuwatenga baadhi ya wafuasi wake na kuwafanya wanafunzi wake kwa maisha yao yote. Aliwapa masharti akisema “Mtu yeyote akitaka kunifuata sharti ajikane mwenyewe na abebe msalaba wake kisha anifuate kila siku.” (Luk.9:23) Hii ilikuwa ni fulltime job.
Lakini pia Yesu aliwatengeneza wanafunzi wake “kujifunza kutoka kwake kuwa na tabia ya upole na unyenyekevu wa moyo.” (Mt.11:29) na pia kuwaandaa kuzifanya kazi zile zile alizokuwa akizifanya na kuwapa fursa ya kufanya kwa ukubwa kuliko yeye. “Amin amin nawaambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.” (Yh..14:12)
Kwa hiyo Yesu, aliwafundisha wanafunzi wake kwa maneno na kwa vitendo, na akawapa fursa ya kufanya mazoezi ya kazi zile zile ambazo alikuwa akizifanya. Nia na madhumuni yake ni kuwakabidhi madaraka ya kuja nao kufanya kazi ile ile ya kufundisha wengine kwa maneno, tabia na vitendo.
Walipokuwa wamehitimu na yeye mwenyewe amemaliza muda wa kuwepo kwake duniani, ndipo akawapa amri na mamlaka ya kwenda kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi na kuhakikisha wanawafundisha YOTE ALIYOWAAMURU
Sasa unaona jinsi ambavyo, msamiati wa wanafunzi ulivyo na matumizi maalum ambayo ni tofauti na “kuwa na wafuasi”. Yesu alikuwa na wafuasi ambao ni kama mashabiki tu waliomfuata sio kujifunza kutoka kwake bali kupata miujiza ya mikate. Siku moja aliwakemea wakamkimbia wote. Lakini wale waliokubali kuwa wanafunzi wake fulltime wao walisema twende wapi kwani kwako ndiko kuna maneno ya uzima.
Njia ya kutenegeneza wanafunzi wa Yesu, ni kujifunza maneno ya Yesu aliyowafundisha wanafunzi wake na kisha kuyafanya kuwa ndio mtindo wa maisha ya kila siku. Na maneno ya Yesu yanapatikana katika Agano Jipya. Tukilazimisha mafunuo yaliyojengwa katika katika Agano la kale matokeo yake ni kutenegeza wanafunzi wa Musa na Eliya na Elisha na kamwe wanafunzi hao hawawezi kuleta mabadiliko ya kiroho kwa kizazi cha agano jipya.

Comments