NITAVUMILIA MPAKA MWISHO

Na Askofu Mkuu Sylivester Gamanywa

"Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokoka." (MT 10:22)
Mpendwa rafiki wa ukurasa huu! Naomba nikusimulie habari ya safari yangu niliyoianza zaidi ya miaka 34 iliyopita!
Safari yangu ilianza kwa kishindo na hamasa kubwa na ahadi nzito za mafanikio kiasi ambacho nilidhani mambo yangu yatanyooka kwa muda mfupi baada ya kupokea maono ya safari yangu!
Kama ilivyo kawaida ya safari ya imani, Changamoto hazijitokezi mwanzoni! Lakini kwa kadiri safari inavyokwenda ndivyo na Changamoto zinavyozidi kujitokeza na nyingi zikiwa za kushtukiza! Hazipigi "hodi" wala hazingoji "karibu"
Namshukuru Mungu kwamba bado hajaniacha wala kunipungukia! Katikati ya Changamoto zote yuko pamoja nami.Kwa msaada wake bado ninaona mbele niendako. Najua ni mbali na safari ni ndefu. Lakini nilikotoka ni mbali zaidi kuliko niendako!
Ni kweli changamoto ni nyingi mno zinazotishia kutokufanikiwa! Ni kweli nimeshapata hasara ya mengi kwenye hii safari! Nikihesabu gharama za safari iliyoko mbele yangu najikuta sina akiba ya kumaliza safari! Siwezi hata kukopa maana sikopesheki tena ! Vyote hivi ni vikwazo vya kutosha kuahirisha safari iliyobakia.
Changamoto kubwa zaidi ni kwamba hata kama ningeamua kuahirisha safari na nirudi nyuma nilikotoka; gharama za kurudi nyuma ni kubwa zaidi kuliko mbele niendako hivi sasa!
Hata hivyo, pamoja na yote haya, sina mpango wa kuahirisha safari ya kwenda mbele! Sirudi nyuma! Sikubali kushindwa! Sivunjiki moyo! Sikati tamaa! Sina njia mbadala!
Naomba Usinicheke! Sijachanganyikiwa kabisa! Akili zangu ni timamu bado! Nikioanacho mbeleni kiko wazi zaidi, na halisi zaidi, kuliko nilipoanza safari hii huko nyuma! Nikionacho mbeleni kina thamani kubwa ya kufidia hasara zote nilizopata katika safari nzima na ziada yake haitakuwa na mwisho!
Hiki ndicho kinachonihamasisha na kunitia moyo zaidi ya kwamba baada ya kufika huko mbele niendako; sitasafiri kwa taabu tena; na mateso, dhiki, adha yangu ya sasa yatabaki ni historia!

Comments