SABABU SABA(7) ZA KWANINI TUMEOKOKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU la uzima wetu sasa na uzima wa milele.
Kuokoka ni kuhakikisha Bwana YESU KRISTO yuko ndani yako na unamtii yeye na Neno lake.
''....  
Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia(Mitume), Mwamini Bwana YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.-Matendo 16:30-31''

Kuokoka ni jambo la lazima sana kwa kila anayehitaji uzima wa milele.
Kuokoka kuanza na kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi kisha unaishi ukilitii Neno la MUNGU.

Kwanini ni muhimu sana kuokoka?
Biblia inasema baada ya kifo hukumu. 
Waebrania 9:27 ''Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;''

Anayetenda dhambi akifa na dhambi zake anaenda kuzimu.
Mteule wa KRISTO mtakatifu akifa anaenda mbinguni.

Wanadamu wengi wakionywa kwamba waache dhambi husema wanahukumiwa na hutoa sababu kwamba anayeweza kuwahukumu ni MUNGU tu.
Hukumu ni Siku ya mwisho tu ila sasa ni maonyo tu na maonyo hayo yanaletwa na Neno la MUNGU kupitia watumishi, hivyo watumishi wakati mwingine huonekana kama wanahukumu kumbe wanawasaidia watu. Hakuna mwanadamu anayetakiwa kumhukumu mwanadamu mwenzeke.
Nikisema acha uzinzi na usaliti wa ndoa maana ni dhambi sio nakuhukumu Bali nakuambia kweli ya MUNGU.
Nikisema acha dhambi na okoka sasa ni kwa lengo la kukusaidia wewe.

Ni mhimu sana kumpokea YESU na kuanza kuishi katika kusudi la MUNGU la wokovu.
Baada ya kuokoka naomba utambue kwamba wewe umekuwa mtumishi wa MUNGU wa kuwasaidia na wengine ili waje kwenye wokovu.
Biblia inasema kuhusu aliyeokoka kwamba;
''Kwa maana MMEOKOLEWA kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;-Waefeso 2:8''

Biblia inasema tuliompokea YESU kama Mwokozi tumeokolewa.
Kuna watu hudai hakuna kuokoka duniani lakini Neno la MUNGU ndio kweli na kweli hiyo inasema kawmba tuliompokea YESU tumeokolewa na sio tutaokolewa bali tumeokolewa tayari.
Kama hujaokolewa basi nakusihi okolewa leo kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha mataaktifu ya wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

Baada ya kuokolewa naomba ujue mambo 7 muhimu haya yafuatayo.
Hiki ndicho kiini cha somo langu la Leo kwamba ''Tumeokoka ili?''


TUMEOKOKA ILI:

1. Tumeokoka ili tuurithi uzima wa milele.

Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.'' 

Tumeokoka ili tuupate uzima wa milele, hiyo ndio ahadi kuu ya MUNGU kwetu.
Kazi yetu baada ya kuokoka ni kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU na Kulitii.
Uzima wa milele ni kitu muhimu cha kwanza ambacho kila mwanadamu anahitaji, lakini Uzima huo uko katika YESU KRISTO pekee, hivyo anayeuhitaji uzima wa milele atubu dhambi na kuokoka kisha aendelee kuukulia wokovu kwa mafundisho na utakatifu.

2. Tumeokoka ili tumtumikie YESU KRISTO.

Yohana 12:26 '' Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, BABA atamheshimu.'' 

Kazi ya waliookolewa na Bwana YESU ni kumtumikia yeye.
Kumtumikia YESU ni kumfuata yeye kwa kujitenga na dhambi zote na mambo yote mabaya ya dunia.
Ukimtumikia YESU hakika MUNGU atakuheshimu.
Na wewe ukiheshimiwa na MUNGU Muumbaji wako hakika una heri kuu.
Kama umeokoka na humtumikii KRISTO nakuomba anza leo kumtumikia; kwa kuishi maisha matakatifu, kushuhudia wengine injili, mtumikie kupitia uimbaji au kufundisha, Mtumikie kwa mali yako na mtumikie kwa kujitoa kabisa ili umpende yeye tu.
 

3. Tumeokoka ili tuishi maisha matakatifu.

1 Petro 1:15-16 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

Kazi nyingine ya wateule wa MUNGU ni kuishi maisha matakatifu.
 Ni muhimu sana kujua kwamba umeokolewa na BWANA YESU ili uanze kuishi maisha matakatifu.
Ni jukumu la kila mkristo aliyeokolewa na KRISTO kuishi maisha matakatifu.
Utakatifu hautakiwi kuwa wa msimu tu bali wa kudumu.
Aliyetuokoa ni mtakatifu hivyo na sisi ili tumpendeze yeye inatupasa sana kuishi maisha matakatifu.

4. Tumeokoka ili tuwe kielelezo cha matendo mema kwa watu wote.

1 Tiomotheo 1:16 ''Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.'' 

Mtu aliye kielelezo cha mema ni mtu wa mfano wa kujifunzia watu walio nje.
Ni muhimu sana wateule wa MUNGU wakawa kielelezo cha mema ili dunia ijifunze kwao jinsi ya kuishi maisha matakatifu.
Kama dhambi itatawala kanisani hakika itakuwa ngumu watu wa nje kuja kanisani maana hawaioni tofauti kati yao na kanisa. Kama kanisani kuna wazinzi, wachawi, watoa rushwa , wezi na Nk. Ni ngumu kuwapata watendao dhambi hizo ili waje kanisani.
Mfano ndugu wa kanisani amezini na mtu wa nje, je itawezekana vipi huyo wa nje kuja kanisani? maana anajua kabisa huwa anatembea na mtu wa kanisani.
Ni muhimu sana kanisa zima likawa kielelezo cha matendo mema ili watu wote wajifunze.
Sio Mchungaji tu ndio awe kielelezo lakini mama mchungaji na wazee wa kanisa ni wadhambi, haifai kuwa hivyo.
Sio wazee tu ndio kielelezo lakini vijana ni wadhambi, haifai kuwa hivyo.
Kanisa lote linatakiwa liwe kielelezo cha matendo mema.
Tumeokolewa ili tuwe kielelezo cha mema kwa watu wote.


5. Tumeokoka ili tuwalete wengine kwa YESU.

Mathayo 10:7-8 ''Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.   ''

Tumeokoka ili tuwalete wengine kwa YESU.
Ndugu naomba ujue kwamba umeokolewa na Bwana YESU ili uwalete familia yako yote kwa YESU.
Umeokolewa na YESU ili uwalete wafanyakazi wenzako wote kwa YESU.
Umeokolewa ili uwasaidie wanafunzi wenzako kiroho.
Umeokolewa ili uwasaidie wafanyabiashara wenzako kiroho.
Mama umeokolewa ili uwasaidie wamama wenzako jinsi ya kumcha MUNGU aliye hai.
Baba umeokolewa ili uwafundishe wababa wenzako jinsi ya kumcha MUNGU wa mbinguni.
Tumeokolewa ili tuwalete watu wote kwa YESU.
MUNGU ametupa pia mamlaka katika kuhubiri kwetu ili yeye MUNGU aponye na kuwafungua watu kupitia sisi.
Ni muhimu sana kujua wajibu wako ndugu uliyeokolewa na BWANA YESU.
 
6. Tumeokoka ili tuwe na ushirika na ROHO MTAKATIFU.

2 Kor 13:14 '' Neema ya Bwana YESU KRISTO, na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU ukae nanyi nyote.'' 

Tumeokolewa ili tuwe na ushirika na ROHO wa MUNGU.
Kuwa na ROHO wa MUNGU ndani yako na kumtii itakusaidia kutimiza kusudi la MUNGU kwako na itakusaidia kudumu katika Mwokozi wako YESU KRISTO.
ROHO MTAKATIFU ndiye msimamizi wa kanisa la KRISTO duniani hivyo ili tumpendeze MUNGU tunatakiwa sana tuwe na ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ndio mwalimu wa kweli ambaye tukilihudhuria darasa lake hakika hakuna  cha kidunia au cha kipepo kitakachoturudisha nyuma.
Ili tushinde dhambi na mambo yote ya dunia inatupasa sana tuwe na ROHO MTAKATIFU.
Ni heri sana kuwa na ushirika wa ROHO wa MUNGU.
  7. Tumeokoka ili tuufundishe ulimwengu jinsi ya kumwabudu MUNGU aliye hai.

Zaburi 29:2 ''Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.'' 

MUNGU wa kweli ni mmoja tu na huyo amejifunua pekee katika Neno lake Biblia.
MUNGU aliye hai huabudiwa katika kanisa la KRISTO YESU duniani.
Wateule wa MUNGU humwabudu MUNGU aliye hai na inawapasa sana kumwabudu katika Roho na kweli.
 Kama dunia inamtaka MUNGU Muumbaji basi inawapasa sana kwenda kumwabudu katika kanisa la KRISTO duniani.
Waliookoka ni kanisa hai la KRISTO Duniani.
Tumeokolewa na BWANA YESU ili tuwafundishe wanadamu wote jinsi ya kumwabudu YAHWEH MUNGU wetu aliyetuumba.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments