TAMBUA MAJIRA NA NYAKATI ILI UWEZE KUSTAWI


Na Mch. Rick Mongi – Efatha Ministry Morogoro


Kwanini tuwe na majira na nyakati?
 
Majira ni vipindi mbali mbali kulingana na wakati ulioamuliwa.
Kuna wakati wa mchana na wakati wa usiku, Mungu anafuata majira na nyakati ndo maana akamwekea mwanadamu ili yamuongoze katika maisha yake.
Muda ndio unaotofautisha waliofanikiwa na wasiofanikiwa. Ukishindwa kutumia muda vizuri huwezi kufanikiwa
Usipo jua muda ni ngumu kustawi. Muda ndio unatofautisha waliofanikiwa na ambao hawafanikiwa.
Kwakuwa kila jambo lina wakati na majira yake jua kuwa sio kila siku utakuwa mtu wakuomboleza, kulia, kutupwa, kularua nk.
Ili uweze kustawi unatakiwa kwenda na majira na nyakati, matumizi ya muda ndio yanayomfanya mtu afanikiwe, kila mwanadamu ameumbwa kwa kusudi alilofungwa katika muda.
Hivyo ukishindwa kuutumia muda wako vizuri lazima ushindwe, ndio maana kuna muda wa kuzaliwa na muda wa kufa.
Kuwa na saa haimaanishi una muda na sio kila menye saa ana muda, wengi wana saa lakini hawana muda na kuna watu wana muda lakini hawana saa.
Yesu aliitwa Alfa na Omega ili kumsaidia mwanadamu aliefungwa katika muda maana yake mwanzo na mwisho.
Ukijua kwenda na muda ni lazima ufanikiwe.
Efeso 5:15-17 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. “

Hekima ndio inayotuongoza kuukomboa wakati kwa sababu zama tulizopo ni zama za uovu.
Kukusudia uovu ni kujirudisha na kujikandamiza. Ukishindwa kuukomboa wakati huwezi kufanikiwa kwa sababu hiyo msiwe wajinga, fahamuni yaliyo mapenzi ya Mungu kwakuwa hii ni zama ya uovu, tambueni yaliyo mapenzi ya Mungu
Warumi 12:2 “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. “
Kila iitwapo leo, tafuta kutimiza mapenzi ya Mungu. Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. ” Sio kila mtu asemae bwana bwana ataingia ufalme wa Mbingu bali kila atakaetimiza mapenzi ya Mungu.

Kila jambo linalofanyika duniani ni kwa majira na nyakati zake, ukifanya jambo pasipo wakati wake ujue litaonekana kituko na matokeo yake ni kutokufanikiwa. Usipojua muda ni vigumu kustawi, muda ndio unaosababisha watu waptie wanayopitia.
Mhubiri 3:1-9 “Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.
Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa;
Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza;
Wakati wa kutupa mawe, na wakati wa kukusanya mawe; Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia;
Wakati wa kutafuta, na wakati wa kupoteza; Wakati wa kuweka, na wakati wa kutupa;
Wakati wa kurarua, na wakati wa kushona; Wakati wa kunyamaza, na wakati wa kunena;
Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani.
Je! Mtendaji anayo faida gani katika yale anayojishughulisha nayo? “

Kwakua kila jambo lina majira na wakati wake ndio maana sio kila wakati ni wa kulia, kuomboleza, kushindwa, kuchukia, kuteseka nk. Sio wakati wote wa kunyamaza, kuna wakati wa kunena sio wewe bali ni wakati wake.

Ni hatari sana kufanya jambo nje ya wakati, kwa hiyo usipojua majira na nyakati ni vigumu sana kufanikiwa.
Yohana 2:1-4 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. “
Yesu alimjibu mamaye, wakati wangu bado akimaanisha majira na nyakati bado, wakati ulipofika, majira na nyakati ukajidhihirisha.
Mungu anaenda na muda, ukienda kinyume na muda huwezi kufanikiwa.

Comments