TANGU MWANZO HAIKUWA HIVI

Na PASTOR AMOS KOMBA, UFUFUO NA UZIMA MTWARA

UTANGULIZI
Mathayo 19:3 – 8
3 Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu? 4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? 6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe. 7 Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha? 8 Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.
Yesu anawafundisha mafarisayo kuwa kuwapa wake zao talaka haikuwa hivyo tangu mwanzo. Kwa maneno mengine Yesu anawaambia kuwa kuna aina ya maisha mnayoishi sasa hayakuwa hivyo tangu mwanzo. Kuna utaratibu wa namna ya kuishi kwenye ndoa ambao Mungu aliuweka. Sasa kwa sababu ya ugumu wa moyo wa wanandoa wakamwomba Musa awape ruhusa ya kutoa hati ya talaka. Kuna mambo yamewatokea watu wengi leo ya kuyabadili maisha yao na kuishi maisha ambayo sio yao, maisha mabaya ila haikuwa hivyo tangu mwanzo. Mwanzo ulikuwa unaishi maisha mazuri lakini sasa unaishi maisha ambayo hayaridhishi kabisa.
Watu wengi leo tupo na maswali mengi sana juu ya aina ya maisha tunayoishi sasa. Na hakika wengi maswali yetu yamekosa majibu ila mimi nakuombea Yesu awe kwako majibu ya maswali yako yote. Pia watu wengi ukiwasikiliza hali zao za sasa namna wanavyojisema utamsikia mtu yupo kwenye wakati uliopita tu. Utamsikia mtu anasema mimi zamani nilikuwa nafunga sana, mimi zamani nilikuwa mwombaji sana, mimi zamani nilikuwa na biashara nzuri sana, na pesa, mimi zamani tulikuwa tunapendana na mke au mume wangu, mimi zamani nilipokuwa shuleni nilikuwa wa nakuwa wa kwanza au wa pili.
Watu wengi wapo mimi zamani, zamani zamani hata hawajui kwa nini leo wapo hapo walipo. Ila mimi leo nina habari njema kwako; ni kweli upo hivyo ulivyo leo ijue kuwa haikuwa hivyo kwako tangu zamani. Kuna mambo au matukio yametokea kwako yakapelekea wewe uyaishi hayo maisha unayoishi leo na shetani amekubakisha kwenye kuyakumbuka yaliyopita tu na uyaishi hayo maisha. Lakini leo Mungu atakutokea hapo ulipo kwa Jina la Yesu. Unachotakiwa wewe ni kusikiliza kwa makini sana na Mungu atakusaidia kwa Jina la Yesu.
Ni vizuri kujua maisha yako wewe hayaanzi kwenye ulimwengu wa mwili bali maisha yako huanzia ulimwengu wa roho. Ulimwengu wa roho ndio unaotoa majibu wewe uwe nani katika ulimwengu wa mwili na ni vizuri kujua ukishinda rohoni umeshinda na mwilini. Watu wengi sana hatujui siri hii kuwa mafanikio ya mtu huanzia rohoni. Na kama mafanikio ya mtu yanaanzia rohoni vile vile mabaya yanayokupata leo nayo yanaanzia rohoni. Na Biblia inaweka wazi kuwa Mungu alitubariki sisi kwa baraka zote katika ulimwengu wa roho.
Waefeso 1:3
3 Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
3 Yohana 1: 1 – 2
1 Mzee, kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli. 2 Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.
ULIMWENGU WA ROHO NI BAYANA
Mungu aliumba ulimwengu wa aina mbili. Aliumba ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili na kila ulimwengu una viumbe vyake. Sasa watu kwa sababu wanaishi katika ulimwengu wa mwili hawauoni ulimwengu wa roho. Na wanajipa majibu kuwa hakuna ulimwengu mwingine kama huu lakini hapana kuna ulimwengu mwingine unaoitwa ulimwengu wa roho. Huko ndiko anaishi Mungu na malaika wote watakatifu na wachafu. Na ulimwengu wa roho ni bayana.
Waefaso 1:3
3 Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo;
Waefeso 1:20
20 aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho
Waefeso 2:6
6 Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu;
Waefeso 3:10
10 ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;
Waefeso 6:12
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
UKWELI WA KUWEPO ULIMWENGU WA ROHO
Kwenye Biblia kuna vitu vinavyothibitisha kuwa ulimwengu wa roho upo. Nitaeleza vitu vichache kati ya vingi. Hata wakati Mungu alimuumba mtu yaani wewe na mimi, kabla ya kumfanya katika mavumbi ya ardhi Mungu alimuumba mwanadamu kwanza katika ulimwengu wa roho. Na ndiyo maana katika Biblia Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu aliwaumba mwanamume na mwanamke. Kitabu cha Mwanzo 1:26 - 28 imeandikwa 26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. 28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Na Mwanzo 2:7 imeandikwa 7 BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Hii sura ya pili ni yule aliyeumbwa tayari kwenye ulimwengu wa roho ndio analetwa sasa katika ulimwengu wa mwili. Kwa hiyo Adamu na mkewe waliumbwa kwanza kwenye ulimwengu wa roho au kwa maneno mengine walianzia rohoni kabla ya mwilini.
1. CHAKULA NA KINYWAJI CHA ROHONI
Unaona kuna chakula cha kiroho na kinywaji cha kiroho. Hii inafanya ukweli wa kuwepo ulimwengu wa roho.
1Wakorintho 10:3 – 4
3 wote wakala chakula kile kile cha roho; 4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.
2. MWILI WA ROHONI
Biblia inatuweka wazi kuwa ikiwa ipo miili ya asili na miili ya rohoni. Maana yake ukiwa au ukiingia katika ulimwengu wa roho hutumii huu mwili unaotokana na mavumbi bali unatumia mwili wa rohoni. Ndio maana wachawi wanapita popote kwenye nyumba ili kuja kuwaloga watu hata kama ufunge mageti yote, milango yote, wachawi wataingia tu kwa sababu wanavaa mwili wa rohoni na ile miili yao huiacha nyumbani kwao; na wanawanga na miili ya rohoni. Leo nakuombea wewe unayenisikiliza Mungu akulinde na wachawi kwa Jina la Yesu. Dawa ya wachawi wasiingie kwako ni Damu ya Mwanakondoo na sio kuwajiri wamasai wakulinde na wachawi maana wamasai hawana uwezo wa kuwazuia wachawi kuingia ndani ya nyumba yako. Na sio kufunga milango na madirisha bali Damu ya Mwanakondoo kwenye nyumba yako, familia yako, watoto wako, masomo yako, ofisi yako, biashara yako.
1 Wakorintho 15:44
44 hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.
3. NYUMBA NA DHABIHU ZA ROHO
Ndugu zangu ulimwengu wa roho ni bayana. Ulimwengu wa roho kweli upo. Unaona mpaka kuna nyumba za rohoni na dhabihu za rohoni.
2Petro 2:5
5 wala hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu;
4. NYIMBO ZA KIROHO
Ulimwengu wa roho una nyimbo zake. Yaani Neno la Kristo linapokaa kwa wingi ndani yako na linajazwa na Roho Mtakatifu unanena kwa lugha mpaka unaanza kuimba lugha ya roho. Hizo ni nyimbo za rohoni natamani sote tuliopo hapa na wale wa askari wenzetu wanaokuja kujiunga na jeshi la Bwana la Ufufuo na Uzima Mtwara na sote tunene kwa lugha mpaka tunaimba tenzi za rohoni kwa Jina la Yesu. Tukifika huko tutaupindua pindua ufalme wa giza hapa Mtwara na Mtwara yote itaokolewa na Bwana wetu Yesu Kristo atatawala mji.
Waefeso 5:19
19 mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;
Wakolosai 3:16
16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.
5. UFAHAMU WA ROHONI
Unaona mpaka kuna na ufahamu wa rohoni. Kama huna ufahamu wa rohoni utaonewa mpaka basi. Mimi unayenisikiliza hapa leo nisingekuwa na ufahamu wa rohoni leo nisingekuwa hapa kabisa maana kuna wengi ambao hawakupenda niwe hapa nilipo na hao sio wengine ni wachawi na waganga wa kienyeji. Wameshanishitaki sana kwa uongo na bado wanaendelea ila ufahamu wangu wa kiroho unanifanya mimi nisonge mbele wacha wao waseme ila mimi nafanya kazi ya Mungu niliyotumwa kwayo. Kazi zangu zitanishuhudia mimi sipo kama wanavyosema wao bali mimi nipo kama Neno la Mungu linavyosema. Ukiona mtu anakushitaki sana, anakufuatilia sana jua umemzidi kwa kila kitu na anahofu alichonacho utakichukua ndio maana yupo bize na wewe tu.
Watu wengi hatupendi kujifunza Neno la Mungu hivyo hatuna maarifa ya Neno la Mungu. Lakini unapochukua hatua ya kujifunza masomo ya awali na kuja kanisani na kuhudhuria ibada zote na kwenye vipindi vya maombi ya mkesha hakika yake utafanya mapenzi ya Mungu na utakuwa na hekima na ufahamu wa rohoni.
Wakolosai 1:9
9 Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;
Sasa umeweza kujua ulimwengu wa roho ni bayana na maisha ya mtu huanzia rohoni; ndio maana tumeona hata Mungu alitubariki kwa baraka zote katika ulimwengu wa roho. Ila sasa hizi baraka ambazo Mungu ametubariki nazo katika ulimwengu wa roho kuzimiliki haziji hivi hivi ni lazima upigane vita vya kiroho ushindane na wote wanakuzuia usizimiliki baraka zako. Kuna watu walibarikiwa kimaisha basi wakaridhika na zile baraka wakasahau kuna kushindana kwenye vita vya kiroho na adui akaja akaharibu maisha yao na baraka zao na leo umeachwa kwenye wakati uliopita tu kwamba mimi hivi na vile. Achana na hayo leo fanya vita na walioharibu maisha yako kwa Jina la Yesu.
Waefeso 6:12
12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
2Wakorintho 10:3 – 5
3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) 5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;
Unaona kushinda na kufanya vita na tena maandiko matakatifu yanasisitiza tuzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani.
Waefeso 6:10 – 11
10 Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
Biblia inasisistiza kuwa hodari katika Bwana ili tuweze kuzishinda hila za shetani. Shetani anajua maisha ya mtu yanaanzia rohoni na ndio maana wewe ulipoyapata mafanikio kidogo tu ukaridhika na kanisani huji tena. Na ndio maana siku ile ya uovu ilipofika kwako shetani alikukuta huna silaha za Mungu na akayaharibu maisha yako na leo umefungwa kabisa na shetani na kubaki kuwa hadithi ambazo hazina maana. Ila mimi nataka nikuambie hapana haikuwa hivyo tangu mwanzo simama tena shindana, fanya vita na Mungu atakutetea.
Mungu mwenyewe tunayemwabudu ni Mungu wa vita, Yeye anapenda vita. Maandiko yanaongea hivi tena na tena.
Kutoka 15:3
3 BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake.
Kutoka 17:16
16 akasema, BWANA ameapa; BWANA atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.
Kama Mungu wetu ni Mungu wa vita basi inatupasa hata sisi kufanya vita. Kiwango chako cha kushindana vita vya rohoni ndio mafanikio yako wewe kwa maana kila unayemwona leo amefanikiwa ni ana vita nyingi sana za kiroho alizopitia na kuzishinda. Hebu jaribu kuwaza kuhusu wana wa Israeli Mungu alipowatoa katika nchi ya Misri na kuwaongoza na kuwapeleka katika nchi ya Kaanani. Halafu Mungu huyu anafika mahali anawaacha ili wapigane vita na kila walipokuwa wanashinda hivyo vita waliimiliki hiyo nchi. Kwa maana nyingine wasingeweza kumiliki hiyo nchi kama wasingepigana. Baadae wana wa Israeli wakaingia katika nchi ya Kaanani na Mungu akayaacha mataifa matano ili kuwafundisha vita wana wa Israeli wasiovijua vita. Hii ni kwa sababu Mungu anajua kama huwezi kushindana huwezi kupokea zile baraka za rohoni.
Waamuzi 3:1 – 4
1 Basi haya ndiyo mataifa ambao BWANA aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani; 2 ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule; 3 aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi. 4 Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za BWANA, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa
Leo upo hivi ulivyo ni kwa sababu huombi maombi ya vita. Leo tutafanya vita vya kiroho na wote wanaotuzuia kwa Jina la Yesu. Leo una madeni, magonjwa, huchumbiwi, huna akili shule, biashara, magomvi katika familia, huna kazi, umelongwa hii ni kwa sababu wewe umekamatwa kwenye ulimwengu wa roho na wachawi na mashetani, lakini leo tushindane tufanye vita vya rohoni na nakuhakikishia tutashinda kwa Damu ya Mwanakondoo. Nataka tupige vita sasa.
Ufunuo 12:11
11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
UKIRI
Baba Mungu ninakuja kwako leo ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya kwa kujua na kutokujua. Naomba unisamehe dhambi zote nilizozitenda kwa mawazo, maneno na matendo kwa Jina la Yesu. Ninakaribia kiti chako cha rehema siku ya leo. Siku ya leo nikiwa na akili zangu timamu namkiri kuwa Yesu ni Bwana na Mwokozi wa maisha yangu. Bwana Yesu ninaomba unifanya kwa upya leo. Ninaukataa kila uovu nilioutenda ukanifanya niwe hivi nilivyo leo kwa Jina la Yesu. Ninakuomba Bwana Yesu ulifute jina langu kwenye kitabu cha mauti na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Amina.
Siku ya leo nimegundua haikuwa hivi tangu mwanzo, kuna adui ambaye amebadilisha maisha yangu yakawa hivi nilivyo. Imeandikwa Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndiye jina lake, leo nazivaa silaha za Bwana ninawafuata wote walioniletea magonjwa, walioiba nyota yangu ya kuolewa, biashara, kuajiriwa, na walioniletea utasa kwa Jina la Yesu. Ninatumia moto wa Mungu ninawateketeza adui majini, mashetani, mapepo, majoka, mazimu, wachawi, na waganga wa kienyeji kwa Jina la Yesu.
Imeandikwa kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama bali ni juu ya falme na mamlaka na wakuu wa giza katika ulimwengu wa roho. Kwa Jina la Yesu ninavaa mwili wa rohoni ninawafuata majini, mashetani, mapepo, majoka, mazimu, wachawi, na waganga wa kienyeji ninawapiga kwa Jina la Yesu. Imeandikwa nao wakamshinda kwa Damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao ambao hawakupenda maisha yao hata kufa, leo ninawashinda kwa Damu ya Mwanakondoo.
Leo ninarejesha kwa namna ya rohoni vipawa vyangu, nyota yangu, kazi yangu, uzao wangu, mume/mke wangu, ndoa yangu, afya yangu, utajiri wangu kwa Jina la Yesu. Ninaomba kila kilichoharibiwa na adui kurudi kwangu leo kwa Jina la Yesu. Kama vile Bwana alivyoniumba na vipawa, leo ninapokea vipawa vyangu kwa Jina la Yesu. Ninaviwekea ulinzi vipawa vyangu kwa Damu ya Mwanakondoo. Ninatamka maisha ya ushindi, baraka, afya njema, kwa Jina la Yesu. Amina.
*** INFORMATION MINISTRY MTWARA ***
KARIBUNI KANISANI TUPO MTAA WA MANGAMBA CHINI KARIBU NA GETI LA SHULE YA SEKONDARI YA MTWARA GIRLS BARABARA YA KUELEKEA UWANJA WA NDEGE WA MTWARA .
UNAWEZA PIA KULIKE NA SHARE NA COMMENT KWENYE PAGE YANGU HII YA PASTOR AMOS KOMBA UKIFANYA HIVYO UTAKUWA UMEWASAIDIA MAMIA KWA MAELFU KULIPATA NENO NA MUNGU NA WATU WAKAFUNGULIWA NA KUWA HURU FANYA HIVYO MUNGU ATAKUBARIKI SANA.
UNAWEZA KUONA SHUHUDA NA UPONYAJI KWA NJIA YA VIDEO TEMBELEA YOUTUBE SEARCH PASTOR AMOS KOMBA AU UNAWEZA KUNIFOLLOW INSTAGRAM NA TWITTER KWA KUANDIKA PASTOR AMOS KOMBA.
*** INFORMATION MINISTRY MTWARA ***
Baruapepe: amos.komba2000@gmail.com
Simu: +255713 442 785 au +255754 447 232

Comments