UWEZO WA ADUI KUZUIA NENO LA MUNGU

Na Mtumishi Dk Frank P. Seth
“Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka” (Luka 8:12).
“13Akawaambia, Hamjui mfano huu? Basi mifano yote mtaitambuaje? 14Mpanzi huyo hulipanda neno. 15Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. 16Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; 17ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. 18Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, 19na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. 20Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia” (Marko 4:13-20).
BWANA Yesu alisema maneno haya wakati akieleza maana na mfano wa Mpanzi. Bwana alionesha namna tatu za adui kupingana na neno la Mungu kwa wale WASIKIAO; achilia mbali kundi ambalo wamezuiwa kabisa hata kusikia:
i. Watu wenye Mioyo kama NJIA
Hawa wanaweza kusikia lakini HUSAHAU ghafla! Kama vile hawajawahi kuhuburiwa. Kila wanachoambiwa wanasahau tu; ni kama kinaingia sikio hili na kutokea jingine. Wakifanya dhambi au kosa fulani, ndipo hustuka wakisikia neno fulani likihubiriwa, na kuchomwa mioyo yao kwa maana waliambiwa lakini HAWAKUSIKIA (hawakutenda kwa sababu walisahau au lile neno lilikaa kimya ndani yao).
Tabia ya watu hawa sio wasomaji kabisa wa neno la Mungu. Wameshikiliwa chini na adui wasiweze kabisa kusoma. Hata wakisoma au kusikia neno, wao huona linamfaa mwingine zaidi kuliko wao! Neno limewekwa mbali nao wasije wakasikia wakaamini wakaoka katika CHANGAMOTO zao au MAMBO yanayowazonga.
ii. Watu wenye Mioyo kama MWAMBA
Hawa huwa wepesi kupokea na kuchangamka sana mara wapatapo kujua siri fulani za Ufalme wa Mungu. Ila hawajui kwamba Neno huja kwa kusudi maalumu la kuwavusha katika CHANGAMOTO au HATUA fulani za kimaisha. Zile changamoto zikija, wanashindwa kujua kwamba huo ndio muda muafaka wa kulitumia lile neno kuvuka “ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa”.
Kabla ya kukutana na bahari ya Shamu, tayari Musa alikuwa na fimbo mkononi. Alipomlilia Mungu, aliulizwa, “Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. 16Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu (Kutoka 14:15, 16). Watu wengi wanaoangamia walikuwa na neno la kuwavusha ila walikosa “kina” mioyoni mwao kwa sababu mioyo yao ni kama mwamba! Adui akawaweza upesi.
iii. Mioyo Iliyozongwa na Miiba
“Hawa ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai”. Tabia ya watu hawa ni kuwa na mambo mengi. Wako busy kila mahali na kila wakati hata kama u-busy wao hauzai.
Umewahi kukutana na mtu ana mambo mengi asubuhi hadi jioni? Anatoka na kuingia kama kuna kitu kinamwambia “zunguka”. Akiwa ofisini mara anaingia ofisi hii mara ile, mara kashika gazeti mara anazungumza na watu mambo hayapo hata kwenye ratiba yoyote. Mara kashika Facebook mara WhatsApp, Ghafla! Imefika jioni anarudi nyumbani. Muulize kafanya nini leo? Atakukodolea macho tu kwa maana asilimia themanini au zaidi (80%) ya muda wake alipoteza wala hajui alichofanya.
Mtume Paulo akieleza uwezo huu wa adui wa kuzui neno, aliita KUPOFUSHWA FIKRA. “3Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” (2 Wakorintho 4:3, 4).
Nabii Isaya alisema zaidi ya upofu; watu hawa ni viziwi wenye mioyo mizito (wazito wa kuelewa)! BWANA alimnukuu nabii Isaya alipokuwa akifafanua mfao wa Mpanzi, “13Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. 14Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona. 15Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya” (Mathayo 13:13-15).
Tufanyeje Basi?
Omba macho yako yatiwe nuru yaweze kuona, masikio yako ya ndani yasikie na moyo wako ufanywe kuwa udongo tifutifu uwezao kupokea neno na kuzaa. “6Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo” (2 Wakorintho 4:6). Omba pia kwa ajili ya wale unaowashuhudia habari za Bwana ili nao nuru ya Injili iwazukie.
Frank P. Seth

Comments