WAOMBAJI NDIO KUNDI LA WATU MUHIMU ZAIDI KANISANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Katika kanisa waombaji ni watu muhimu sana.
Katika kanisa waombaji ndilo kundi la watu muhimu zaidi.

1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma;''


Katika andiko hili ni kanisa zima linaelezwa kuomba kila mara lakini katika kanisa la leo kanisani kuna watu wachache tu ndio waombaji, kuna vikundi vya maombi na wengine wala hawana habari na maombi, wao ni kutoa hitaji tu ili waombewe na waombaji, lakini kazi ya kuomba kwa juhudi ni ya kanisa zima na sio kikundi kinachoitwa cha maombi. Kama kuna kikundi cha maombi kanisani basi kanisa zima linatakiwa kuwa katika kikundi hicho maana waombaji ndilo kundi muhimu zaidi kanisani.
Kanisa Lazima Liwe Na Waombaji Wengi, Binafsi Nawaona Waombaji Kama Watu Wa Muhimu Zaidi Kanisani. 
Waombaji Hubeba Siri Za MUNGU. 
Waombaji Hupokea Ufunuo Kutoka Kwa MUNGU Na Pia Waombaji Hupokea Maono.
 Ndugu Hakikisha Unakuwa Mwombaji Wa Kuliombea Kanisa, Kujiombea Wewe Mwenyewe, Kuombea Taifa Na Kuwaombea Ndugu Wote Wa Kiroho Na Kimwili 

Wakolosai 4:2 ''Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; '' 

Kanisa zima linaagizwa kudumu sana katika maombi lakini katika kanisa la leo kuna kikundi tu cha maombi na wengine wako busy na maisha yao.
Maombi sio karama hata wengine wasiwe waombaji.
Maombi sio kipaji bali ni agizo la wateule wa MUNGU wote.
Maombi sio kipawa hata wengine wawe nacho na wengine wasiwenacho, bali maombi ni ya kanisa zima la MUNGU.
Ni muhimu sana kanisa zima kuwa waombaji maana pia bila kuwa waombaji hata kuzishinda dhambi itakuwa ni ngumu.
Maombi Ni Maisha, Maombi Hayana Msimu Ni Ya Siku Zote. Kwenye Maombi Msikilize ROHO MTAKATIFU, Ukiomba Bila Kumsikiliza ROHO Hutaomba Kitu Sahihi Kinachohitajika Muda Huo. 
Kama hatuombi hata udhihirisho wa nguvu za ROHO MTAKATIFU utakuwa mdogo sana kanisani.
Kanisa kama haliombi ni rahisi sana kutekwa na mambo ya dunia.
Ni lazima kanisa tuombe na tena tuombe katika ROHO MTAKATIFU.

1 Yohana 5:14 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.''

 Tukisimama na YESU KRISTO siku zote hakuna mchawi atayesimama mbele yetu
 Ndugu Usiache Kuwaombea Watu Wengine Wanaohitaji Msaada Wako, Maombi Ya Mwenye Haki Yafaa Sana akiomba Kwa Bidii

Yakobo  5:15-16 '' Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na BWANA atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. ''

 Lakini Pia Watu Wote Wanatakiwa Wajue Kujiombea Wenyewe, Usipende Kulala Huku Umewatwisha Mzigo Wengine Kukuombea. Ndugu Tambua Kwamba Ukiniambia Kukuombea Nitakuombea Sana Lakini Sitakuombea Kwa Ufasaha Na Uchungu Kama Ambavyo Wewe Mwenyewe Ungeomba, Naweza Nikakuombea Leo Lakini Kesho Nikasahau Na Bado Hujajibiwa Lakini Ungeomba Kwa Juhudi Na Mimi Ningekusaidia Hapo Matokeo Yangekua Dhahiri Sio Wewe Kulala Huku Umeajiri Watu Wengine Wakuombee, Hiyo Ni Mbaya. 
Kanisa zima la MUNGU tunatakiwa tuwe waombaji.
Kama Mtu Anaumwa Hapo Ni Sawa Hakuna Mjadala Ila Kumwombea Maana Ni Agizo La BWANA YESU Tuweke Mikono Juu Ya Wagonjwa Na Watapona.
Marko 16:17-18 '' Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.'' 

Sasa kama wewe huwa huombi basi hakika utakuwa unawategemea tu watu wengine kukuombea, na kama utawategemea sana watu  Biblia inasema umelaaniwa wewe unayetegemea wanadamu maana moyoni mwako utamwacha MUNGU kwa kuwaingiza wanadamu ili wawe msaada wako na si MUNGU(Yeremia 17:5)

Katika maandiko hapo juu tunaona Biblia inasema watu wa kanisa wataweka mikono juu ya wagonjwa na wagonjwa hao watapona. Je kama hata kujiombea wewe huwezi utawezaje kuwaombea wagonjwa hata wapone?
Kama kanisa lote la KRISTO litazingatia maombi basi kazi ya kutoa mapepo au kuombea wagonjwa wasingeachiwa wachungaji tu bali hata wateule wote wangeifanya kazi hiyo.
Leo katika makanisa wachungaji wana mizigo mizito maana kuna washirika akisikia tu paka analia usiku basi anampigia simu mchungaji ili amuombee maana amevamiwa na wachawi.
Wakati mwingine unatakiwa wewe mwenyewe ujivike ujasiri na kuomba kwa imani.
YESU unaye kama alivyonaye mchungaji.
Kufunga unaweza kama wanavyofunga wengine kwa maombi, Hivyo ni muhimu sana kuwa muombaji.
Tatizo la wengi ni watenda dhambi ndio maana hata kuomba hawawezi.
Tatizo la wengi wako busy na dunia ndio maana hata kuomba hawawezi.
Tatizo la wengi hata kusoma Neno huwa wanafungua Biblia jumapili tu wakati wa Neno busy, ndio maana hata nguvu ya kuomba hawana.
Kanisa zima linatakiwa kuzingatia maombi na utakatifu.

Waebrania 4:16 ''Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.''

Kanisa lote linatakiwa sana kuzingatia utakatifu na maombi.
Mkono Wa MUNGU Wa Uponyaji Upo Katikati Ya Waombaji, Unaweza Kumwekea Mkono Mtu Yuko Mwanza Huku Wewe Uko Lindi Na Mtu Huyo Akapona Maana Mponyaji Ni MUNGU. 
 Ndugu Usiache Kujiombea Na Kuombea Wengine.
Ndugu Usitegee Maombi, Omba Kwa Imani Na Dumisha Utakatifu Wote.
Bwana YESU anasema;
 ''Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.Luka 11:9-10'' 

Kundi la waombaji ni kundi la muhimu sana katika kanisa.
Maombi yanaweza kuileta baraka na maombi yanaweza kulifanya kanisa liwe hai.
Ndugu nakuomba sana uwe muombaji na hamasisha kanisa zima kuwa waombaji.
Kama wewe ni mtu wa maombi na kufunga na kukesha hakika MUNGU akubariki sana maana wewe unalitimiza kusudi jema la MUNGU la maombi.
Niseme tu kwako muombaji kwamba; 

 MUNGU Baba Wa Mbinguni Akubariki, Akupiganie, Akuwezeshe, Akushindie na kukutetea.
Akulinde, Akupe Furaha, Akupe Amani na Akujalie Afya Njema.
Akufanikishe, Akuinue, Akupe Ujasiri na Akusaidia katika yote.
Akupe Njia ya ushindi, Akuepushe Na Mabaya Yote, Akuokoe Na Maadui Wote.  
Akushike Mkono, Akuongoze Katika Mema na Akupe Ufahamu mzuri wa kumtukuza yeye.
Akutegulie Mitego Ya Shetani na Akufunike Kwa Damu Ya YESU KRISTO maana wewe ni mtu muhimu sana katika kanisa la MUNGU.
Bwana YESU anasema ;

''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.-Yohana 14:13-14 ''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments