CHIMBUKO LA UTATA WA MIGONGANO YA TAFSIRI YA BIBLIA (SEHEMU YA KWANZA)

Na Askofu mkuu Siliyvester Gamanywa.

UTANGULIZI
Baada ya kupokea maoni na maswali mengi kuhusu mada ninazowasilisha kwenye ukurasa wangu, nimegundua ya kwamba kuna haja ya kutoa mada itakayochambua kuhusu chimbuko la utata wa migongano ya tafsiri ya Biblia na kuwachanganya wengi wasiojua uwepo wa changamoto hizi.
Kimsingi, kila mwenye kutoa maoni au mafundisho au maelekezo yanayohusu maandiko kutoka katika Biblia lazima ni mwathirika wa shule za nadharia za kitheolojia ambazo zimekamata fikira za wasomaji wa Biblia.
Ndiyo maana naona bora niwasilishe japo kwa kifupi kuhusu makundi makuu ya shule za nadharia ambazo zimechangia kwa sehemu kubwa kutufikisha kwenye utata mkubwa tunaokumbana nao kila siku katika kujifunza Biblia.
Kimsingi kuna makundi makuu matano ya Shule za Nadharia (an organized group of ideas, also called a system) ambayo ni miongoni mwa yale yanayodai kutafsiri biblia kwa usahihi kwa hivi sasa. Makundi hayo yanatambulika kwa majina yafuatayo:
1. Theolojia ya Utaratibu (Systematic Theology)
2. Theolojia ya Kibiblia (Biblical Theology)
3. Theolojia ya Agano (Covenant Theology)
4. Theolojia ya Mpango (Dispensational Theology)
5. Thelojia ya Ahadi (Promise Theology)
CHIMBUKO LA MAKUNDI YA SHULE ZA NADHARIA ZA THEOLOJIA
Kati ya makundi haya matano yapo makongwe mawili yaliyotanguliwa kabla ya mengine ambayo ni "nadharia ya theolojia ya Agano (CT) na pili "nadharia ya theolojia ya Mpango" (DT)
Kimsingi viongozi wa kikanisa wa kila kanisa utakalokwenda utakuwa wamejengwa katika mojawapo ya mikondo ya nadharia mojawapo kati ya hizo. Mahubiri yao au machapisho yao lazima yataangukia kati ya ama kwenye theolojia ya Agano au Theolojia ya Mpango.
Nadharia za Theolojia hizi mbili zinatokana na mbinu ya tafsiri ya utaratibu katika mafunzo ya Neno la Mungu
Mfumo huu wa Thelojia ya Agano ulianza wakati wa Matengenezo ya Kanisa (miaka ya 1200 mpaka 1700 B.K) ikiwa ni harakati za kupinga mafundisho ya Kanisa katoliki lakini ikiwa imechanganyikana na kujiepusha na mambo ya kiyahudi kama vile sheria lakini kwa wakati huo huo kujaribu kusimama kwenye mafundisho ya Neno la Mungu
MITINDO NA MIFUMO YA TAFSIRI ZA KINADHARIA
Aidha, kuna aina kuu mbili za mbinu za tafsiri ambazo hutumiwa na hayo makundi matano ya shule za nadharia ambazo ni i) Maana zilizofichika au mifano (Allegorical), ii) Halisi (Literal)
Makundi mawili ya Shule za Nadharia ndiyo yenye mifumo ya kimsingi, na makundi matatu yaliyosalia yameendelezwa kwa kutumia moja wapo ya msingi mmojawapo wa mifumo ya kimsingi. Theolojia ya Utaratibu (ST) inatumiwa na watheolojia wa nadharia za “Agano” (CT) na “Mpango” (DT); wakati ambapo “thelojia ya kibibilia” hutumiwa zaidi na watheolojia wa “Ahadi”
Sababu ya kuwepo kwa mifumo tofauti ni kutokana na watu kutumia njia tofauti za kutafsiri Biblia. Wengine huona maana iliyofichika nyuma ya kila neno. Hawa ndio wa kundi la mafumbo na mifano (allegory). Lakini wengine hufikiri kwamba Mungu humaanisha kile alichosema na hivyo kitafsiri Biblia kihalisia. Hii inajulikana kuwa ni mbinu ya kuitafsiri Biblia kwa uhalisia.
Mwalimu mwenye kutumia mfumo wa Theolojia ya Utaratibu (ST) huanza na mtiririko wa vichwa vya masomo na kuichambua Biblia kwa utaratibu akijaribu kuyagawanya maandiko kwa ajili ya mafundisho yanayolingana na vichwa vya masomo.
Kuna aina mbili za theolojia zinazotokana na mtindo huu wa kujifunza Biblia, lakini kila moja ina mwelekeo tofauti katika tafsiri. Moja ni Thelojia ya Agano (CT) ambayo mbinu ya kutafsiri kwa kutazama maana zilizojificha na mifano maarufu kama (allegorical interpretation method). Ya pili ni Theolojia ya Mpango (DT) ambayo hutumia mbinu ya kutafsiri kwa uhalisia (Literal interpretation method)
‘Nadharia ya Agano’ imejengwa katika mawazo ya ‘maagano ya matendo’ na ‘agano la neema’. Haya ni mawazo ambayo hayatokani moja kwa moja na fundisho la Neno la Mungu. Watheolojia wa Agano hufikiri kwamba maagano ya matendo ndio uhusiano kati ya mtu na Mungu kwa njia ya kufanya kitu fulani.
.
Nadharia ya Mpango” (DT) yenyewe huona Biblia imegawanywa kwenye mtiririko wa nyakati na muda au mipango tofauti ambayo haihusiani ambayo Mungu alikuwa akifanya mabadiliko ya njia za kuhusiana na binadamu.
Katika “Nadharia ya Mpango” (DT) kuna mgawanyiko wa vipindi saba. Waalimu wengi wenye kutumia mfumo huu hufikiri kwamba kila mpango unatofautiana na mingine ha kamwe haiingiliani, kiasi kwamba njia ambayo Mungu alishughulika na watu katika muda fulani sio njia ile ile aliyoshughulika na binadamu katika muda mwingine tofauti.
Kipindi cha unyofu (Innocence), Kipindi cha dhamiri (Conscience) Kipindi cha Utawala wa binadamu (Human Gorvenment), Kipindi cha Ahadi (Promise) Kipindi cha Sheria (Law), kipindi cha Neema (Grace), Kipindi cha Milenia (Millennial Kingdom of Christ)

MIGONGANO YA TAFASIRI ZA SHULE ZA NADHARIA
Lengo langu katika mada hii kwa mujibu wa kichwa cha somo ni kubainisha chimbuko la utata wa migongano ya tafsiri ya Biblia. Nia sio kuzidi kuwachanganya wasomaji wangu, bali ni kutoa elimu ni kwanini tunatofautiana katika kuisoma na kuielewa Biblia moja ile ile. Natamani msomaji wangu utambue kwamba kujua chimbuko la tatizo ni sehemu ya ufumbuzi wake. Nimeamua kuchagua shule 2 tu za nadharia za kitheolojia ambazo ni kongwe ili tujifunze jinsi zinavyotofautina na kupingana. Na hizi si nyingine bali ni ‘Nadharia ya Mpango’ (DT) na ‘Nadharia ya Agano’ (CT).
Kama ambavyo nilizitambulisha kwenye mada iliyopita ya kwamba ‘Nadharia ya Mpango’ (DT) huyatafsiri maandiko kwa mlengo wa tafsiri halisi; na nikasema ‘Nadharia ya Agano’ (CT) yenyewe huyatafsiri maandiko kwa mlengo wa "mifano" (figurative) na baadhi ya maeneo hutumia tafsiri halisi (Literal).
Kwa mujibu wa mada yenyewe nimejaribu kuchagua baadhi ya mambo machache sana ambayo nadharia hizi zinatofautiana ili kutoa picha ya migongano ya kitheolojia. Baadhi ya mambo ambayo yana migongano ya tafsiri na tutaanza na mitazamo tofauti kuhusu Israeli, kuhusu torati, kanisa na Agano Jipya:
MITAZAMO KUHUSU ISRAELI
Nadharia ya Mpango (DT) inatambua Israeli katika Biblia ni halisi na uzao wa kimwili wa Yakobo. Lakini Nadharia ya Agano (CT) inatafsiri kuna maeneo yanayohusu Israeli halisi ya uzao wa Yakobo na mahali pengine Israeli ni mfano unaolenga Israeli ya kiroho
Nadharia ya Mpango (DT) hutafsiri 'Israeli ya Mungu' katika Gal 6:16 humaanisha Israeli halisi peke yake; Nadharia ya Agano (CT) huitafsiri Gal 6:16 ina maana ya Israeli ya kiroho sanjari na Gal.3:39; Rum 9:6 na Flp. 3:3
Nadharia ya Mpango (DT) nabii zote katika AK kuhusu Israeli zinaihusu Israeli halisi na sio kanisa.
Lakini Nadharia ya Agano (CT) inasema nabii katika AK baadhi ni kuhusu Israeli halisi na baadhi ni kuhusu Israeli ya kiroho
Nadharia ya Mpango (DT) inafundisha ya kwamba kusudi kubwa la Mungu katika historia linahusu Israeli halisi; lakini Nadharia ya Agano (CT) inasema kusudi kubwa katika la Mungu katika historia ni Kristo na pili kanisa
Nadharia ya Mpango (DT) warithi wakuu kupitia Agano la Ibrahimu walikuwa ni Isaka na Israeli halisi. Nadharia ya Agano (CT) inasema warithi wakuu wa Agano la Ibrahimu walikuwa ni Kristo na Israeli ya kiroho
Nadharia ya Mpango (DT) inatafsiri Yesu alitoa ufalme halisi kwa Israeli; lakini kwa kuwa Israeli waliukataa, mpango huo umeahirishwa na kusogezwa mbeleni umesogezwa mbeleni. Lakini Nadharia ya Agano (CT) alileta ufalme wa kiroho ambao ulikataliwa na Israeli halisi na baadaye ukapokelewa na Israeli ya kiroho
MITAZAMO KUHUSU TORATI
Nadharia ya Mpango(DT) inasema torati sheria za torati zimekoma. Lakini Nadharia ya Agano (CT) yenyewe inasema sheria za torati zina matumizi ya aina 3: kuzuia dhambi katika jamii, kuongoza kwa Kristo, na kuwaelekeza wakristo kuishi katika utauwa. Sheria za kiibada (ceremonial laws) zimekoma; sheria za kiraia (civil laws) zimekoma lakini sheria za kimaadili (moral laws) bado zinaendelea kutumika
Nadharia ya Mpango (DT) inasema sheria za torati katika Agano la Kale hazifanyi kazi kwa sasa isipokuwa zile zilizorejewa katika Agano Jipya. Lakini Nadharia ya Agano (CT) inasema sheria za AK bado zinafanya kazi isipokuwa zile ambazo zimebadilishwa na Agano jipya
MITAZAMO KUHUSU KANISA
Nadharia ya Mpango (DT) inatambua uwepo wa watu wawili waliotofautiana hatma zao: Israeli ni duniani na kanisa ni mbinguni. Lakini Nadharia ya Agano(CT) inatambua mtu mmoja tu ambaye ni Kanisa ambalo limekuwepo tangu AK na kudhihirika katika AJ
Nadharia ya Mpango (DT) inatafsiri kanisa lilizaliwa siku ya Pentekoste; lakini Nadharia ya Agano (CT hutafsiri kanisa lilianzia katika Agano la Kale (Mdo 7:38) na kufikia ukamilifu wake katika Agano Jipya
Nadharia ya Mpango(DT) inafundisha kwamba kanisa halikutabiriwa katika AK bali likikuwa ni siri iliyofichika mpaka wakati wa AJ! Lakini Nadharia ya Agano(CT) inafundisha ya kwamba ziko nabii nyingi katika AK zilizotabiri kuhusu kanisa la AJ
MITAZAMO KUHUSU AGANO JIPYA
Nadharia ya Mpango (DT) inatafsiri 'Agano jipya' lililotajwa katika Yer.31:31-34 ni kwa ajili ya Israeli halisi na sio sawa na Agano Jipya la kwenye injili ya luka 22:20; Lakini Nadharia ya Agano (CT) inasema agano jipya la Yer. 31 ndilo hilo la Luk 22; na yote yanalenga Israeli ya kiroho kuwa mujibu wa Ebr.8
ITAENDELEA

Comments