MWINJILISTI NI NANI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Mwinjilisti ni mtu yule anayeeneza habari njema za Wokovu wa YESU KRISTO kwa wanadamu.
Wokovu ni kazi ya MUNGU iliyofanyika Msalabani ili wanadamu watiifu kwake waupate uzima wa milele.
Maisha ya Wokovu ni hatua ya kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi.
Mwinjilisti ni mtu yule mwenye injili ya kweli KRISTO YESU inayookoa na kuwaleta watu kwake YESU KRISTO.
Uinjilisti ni kitendo cha kuwaleta watu kwa YESU ili waokolewena YESU KRISTO.
Maana nyingine ya uinjilisti ni uvuvi wa watu.
Unawavua watu ili watoke kwa shetani na waje kwa MUNGU aliyewaumba, ambaye ameandaa Wokovu kupitia Mwanaye Pekee YESU KRISTO.
Neno uinjilisti linatokana na Neno injili na maana ya injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU.
Waefeso 4:11-12 '' Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe;''


Ni kweli kabisa kuna watu maalumu ambao ROHO MTAKATIFU amewatenga ili watumike kwenye kanisa kama wainjilisti lakini kazi ya kufanya uinjilisti ni ya wakristo wote.
Tumeokolewa na YESU ili tuwalete na wengine wote kwa YESU.

Mwinjilisti halisi ni yule mwenye injili ya KRISTO na hakai nayo tu ile injili bali anaipeleka kwa watu ili waje kwa YESU KRISTO.

MWINJILISTI HALISI NI YULE MWENYE VITU HIVI VITATU;

1.   Atangazaye injili ya YESU KRISTO inayookoa.

Zaburi 105:1 ''Haleluya. Mshukuruni BWANA, liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake.''

-Njia mojawapo ya kutanganza Neno la MUNGU au injili ni pamoja na kuwajulisha watu matendo ya MUNGU na mpango wa MUNGU.
-Mwinjilisti anatakiwa kutangaza Neno la MUNGU kila sehemu ambayo MUNGU atampa kufika. Usiogope kutangaza injili maana injili ni uweza wa MUNGU uletao wokovu Kwa kila aaminie?


Warumi 1:16-20 '' Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa MUNGU uuletao wokovu, kwa kila aaminiye ............. ''
-Injili lazima itangazwe ndipo itawafikia watu na anayetakiwa kuitangaza injili ni mimi na wewe tuliookolewa na Bwana YESU.
Isaya 58:1 ''Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.''

 
Piga kelele, usiache kuwaonya watu makosa yao kupitia Neno la MUNGU alilokupa.
Piga Kelele, usiache kuwahubiria watu ili waache dhambi zao na waokoke.
Kama watu wako, wanaendelea na dhambi na wewe huwahubirii ili wageuke kutoka kwenye dhambi basi wewe sio mwinjilisti maana hufanyi kazi ya uinjilisti uliyopewa.


2.    Anayehubiri injili ya YESU KRISTO kwa watu wote.

Marko 16:15-16 '' Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''
Kazi ya kuhubiri injili sio ya mchungaji tu au mwinjilisti tu au mwalimu tu bali ni ya wateule wa MUNGU wote.
Kama katika kanisa kila mtu atajitambua kwamba ana wajibu wa kuhubiri injili basi hakika ni maelfu ya watu wangekuwa wanaokoka kila siku.
Watu wengi leo wanagombania madhabahu kanisani kuhubiri wakati dunia nzima inawasubiri wao ili waipelekee injili.
Kuna watu akinyimwa madhabahu kuhubiri anahama kanisa, huko ni kutokujitambua.
Kuna watu akinyimwa madhahabu kuhubiri anaanza kumsema vibaya mchungaji na kumzushia mambo mabaya kumbe chanzo ni kwa sababu hajapewa nafasi ya kuhubiri.
Ndugu zangu, migogoro mingi makanisani wakati mwingine hutokea kwa sababu watu wameshindwa kujua kwamba wao ni wainjilisti na wanatakiwa kuipeleka injili ya MUNGU mbele.
Ninachojua mimi Peter ni kwamba; Kanisani tunahubiriwa na Mchungaji ili na sisi tuipeleke injili hiyo kwa watu wengine. Madhabahu ya kanisani ni ya Mchungaji na kutokana na madhabahu hiyo sisi tunajifunza maarifa ya kiMUNGU ili tukawasaidie na wengine.
Ukikosa kazi ya kufanya ndio wewe inakuwa ni rahisi kuwasema vibaya watumishi wa MUNGU.
Kazi ya kuipeleka injili ni ya watu wote waliokombolewa kwa damu ya YESU.
Ndugu ipeleke injili ya KRISTO mbele maana ndio mpango wa MUNGU wa kuitwa kwako ili uujilie Wokovu wake.


3.   Anayeeneza injili ya YESU KRISTO.

Wafilipi 1:5-6 '' kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi. Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya KRISTO YESU ;''
Katika maandiko haya mtume Paulo anafurahi kwa sababu katika Mji wa Filipi kuna watu walikuwa wanaieneza Injili ya MUNGU. Hata leo kunatakiwa kuwepo watu katika kila mahali wa kuieneza injili ya YESU KRISTO.
Wainjilisti ni waeneza injili ya KRISTO.
Kama kuna karama anatakiwa kuwa nayo kila Mteule basi ni karama ya uinjilisti yaani kuwapelekea watu habari njema za ufalme wa MUNGU.
Kama kuna huduma anatakiwa kuwa nayo kila Mteule wa MUNGU basi ni uinjilisti yaani kuwapelekea watu Neno bla MUNGU.
Nawapenda Waimbaji wa nyimbo za injili na kwaya zote maana wanaieneza Injili kupitia nyimbo zao, kama tu waimbaji hao wameimba nyimbo katika mpango wa MUNGU wa injili na sio mambo ya kidunia.
Ziko njia nyingi sana za kuieneza injili ya KRISTO kwa watu wote.
Kusambaza vipeperushi vya Neno la MUNGU ni kuieneza injili.
Kugawa vijarida vya Neno la kweli la MUNGU ni kuieneza injili ya KRISTO.
Kuwashuhudia watu waje kwa YESU ni kuieneza injili ya KRISTO iokoayo.
Ziko njia nyingi sana ya kuieneza injili.
Kila Mwanakanisa anatakiwa kuwa mwinjilisti wa kuipeleka injili kwa watu wote.

Hayo ndio mambo matatu yanayomthibitisha mtu kuwa ni Mwinjilisti nionanyo mimi Peter Mabula.
Kazi ndizo zinatakiwa kututambulisha sisi na sio majina ya kujiita tu Mchungaji au Mwinjilisti au Mtume au Nabii.
Mitume pia katika Biblia walikuwa wainjilisti maana kazi yao ilikuwa ni kuipeleka injili ya KRISTO mbele.
MUNGU anaweza akakupa hata karama zaidi ya mbili kama tu unazifanyia kazi karama hizo kwa kuwaleta watu kwenye Wokovu wa KRISTO.
Watu wengi katika zama za Biblia walikuwa ni wainjilisti na walihakikisha wanaipeleka injili mbele.
Hebu ona mfano huu.
Matendo 21:7-8 ''Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja.
Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.''

Mtume Paulo katika safari yake ya injili, nadhani hii ilikuwa safari kama sio ya pili basi ni ya tatu, alifika katika mji Kaisaria na kumkuta Mwinjilisti Fillipo.
Kwanini namwita Filipo kwamba ni Mwinjilist?
Ni kwa sababu alikuwa mhubiri wa injili, kila mmoja wetu anatakiwa kuwa mhubiri wa injili.
Mitume kama mifano mizuri ya kuhubiri injili walihubiri mchana na usiku na nyumba kwa nyumba wakati mwinggine.
Ona mfano huu;
Matendo 20:19-21 '' nikimtumikia BWANA kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie MUNGU , na kumwamini Bwana wetu YESU KRISTO.''


Ndugu zangu, tunatakiwa sana tuihubiri injili siku zote.
Namna ya wewe kuihubiri injili inaweza kuwa tofauti na ya kwangu lakini kama wote tunamhubiri YESU KRISTO anayeokoa hakika sisi ni wainjilisti na tunafanya uinjisti.
Kuna watu wanaitwa majina ya Mwinjilisti lakini hawaipeleki injili , hao wana majina ya kiinjilisti lakini sio wainjilisti, Mpeleka injili ndio Mwinjilisti.
2 Timotheo 4:4 '' Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.''

 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments