SIKUKUU YA CHRISTMAS.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalom mtu wa MUNGU.
Karibu tujifunze.
Kwanza Nakutakua sikukuu njema ya Christmas.

Ndugu mmoja aliniuliza swali kuhusu sikukuu ya Christmas, nilichelewa kumjibu lakini ngoja nimjibu muda huu huku na wengine wakijifunza kitu.
Jambo la kwanza kujua ni kwamba YESU hakuzaliwa tarehe 25 December, YESU wala hakuzaliwa miaka 2000 iliyopita, ila alikuja miaka 2000 iliyopita ili kutuokoa wanadamu. Sasa ili hilo lifanyike aliamua kufanyika mwanadamu ndio maana tunaona akipitia tumbo la Mariamu, lakini sio kwamba ule ndio ulikuwa mwanzo wake.
Waisraeli walimshangaa sana YESU aliposema kwamba kwamba kabla Ibrahimu hajazaliwa yeye YESU yupo.
Yohana 8:58 "YESU akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko."

Kwa sababu YESU alikuwepo kabla ya Ibahimu na huyo Ibrahimu aliishi miaka 2000 kabla ya YESU kuja duniani basi hakika YESU hakuanza miaka 2000 iliyopita.
Sasa naomba utambue kwamba tarehe 25 December tunafanya kumbukumbu ya YESU KRISTO kuja ulimwengu kutuletea ukombozi.
Ifanye kila December 25 yako ya kila mwaka kama siku ya kukumbuka kuja kwa Wokovu duniani. Usikubali kuifanya December 25 kuwa ni Birthday ya YESU, YESU hana birthday kwa sababu hakuanza na wala hana mwisho (Mika 5:2)
Siku ya Christmas tunakuwa na furaha, hana Mimi hufurahi kwa sababu tu ninakumbuka kuja kwa Bwana YESU kuniokoa.
Hivyo uwe na tabia ya kuitumia December 25 kwa ajili ya MUNGU na sio vinginevyo.
Na sio December 25 tu au jumapili tu Bali siku zote katika maisha yako zitumie katika MUNGU.
Neno langu la Sikukuu hii mwaka huu linatoka Mathayo 1:21 Ambapo Malaika akasema juu ya Mariam kwamba
"Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake YESU, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao."

Kazi iliyomleta Bwana YESU duniani ni kutuokoa hivyo naomba tudumu kwenye wokovu wake na tuwasidie na wengine kuja kwa YESU.
YESU wakati anazaliwa Malaika ambao ni jeshi la mbinguni walishangilia na kumsifu sana MUNGU{Luka 2:8-14}
na siku hiyo hiyo YESU mwanaume wa ajabu anazaliwa watu wenye heshima na watawala walimsujudia {Mathayo 2:11} hao walijua kuwa aliyezaliwa ni MFALME wa wafalme na BWANA wa mabwana.
Pia YESU alizaliwa kwenye hori la ng'ombe ashilio la kwamba wanyama wapumzike maana hakuna tena sadaka ya kuteketezwa kama ilivyokuwa zamani maana YESU ni dhabihu idumuyo milele ili watu wasamehe dhambi zao na kuurithi uzima wa milele bure kupitia yeye 
Waebrania 9:12-15 ''wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele.  Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili;  basi si zaidi damu yake KRISTO, ambaye kwamba kwa ROHO wa milele alijitoa nafsi yake kwa MUNGU kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu MUNGU aliye hai? Na kwa sababu hii ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele.''

Ni kweli kabisa kwamba YESU hakuzaliwa tarehe 25 December lakini tunaiathimisha siku hiyo kwab MUNGU kwa sababu hakuna andiko katika Biblia linalotukataza kuiadhimisha siku kwa BWANA.
Siku hii ni siku kama zilivyo siku zingine na tunaitumia siku hii kwa MUNGU kama tunavyozitumia siku zingine pia kwa MUNGU.
Tunasherekea christmas kwa kumwabudu MUNGU na kuonyesha upendo kwa wengine na kuhakisha kwamba YESU anatenda jambo jipya mioyoni mwetu ili tuzidi kuishi katika neema yake maana kwa ajili yake na kwa neema yake alituhamisha kutoka kwa shetani na sasa tuko huru mbali na kuonewa na wachawi na hata nguvu zozote za giza.
Leo inawezekana ni Birthday ya kina Emmanuel wengi maana akina Emma wengi huzaliwa December 25. Lakini Leo pia sisi tunakumbuka ujio wa ukombozi duniani ndio maana Leo ni Kusanyiko la KRISTO yaani Christmas na sio Birthday, leo sio siku ya birthday bali ni kukumbuka kuja kwa ukombozi kwa wanadamu.

Baada ya maelezo hayo Mambo muhimu ya kujua ni haya.


1. Mkristo bila kuwa na KRISTO YESU moyoni ni bure. 
Hivyo ni lazima kila mtu asiishie kuitwa tu Mkristo Bali aishi na KRISTO moyoni mwake.
Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;  waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

2. Hakuna uzima wa milele kokote ila kwa kupitia YESU KRISTO tu.
Matendo 4;12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''

Hivyo yeyote na wa dini yeyote kama anautaka uzima wa Milele basi ampe YESU maisha yake na aanze kuishi maisha matakatifu katika YESU.

3. YESU anataka tumpokee na tuliishi Neno lake tu ambalo linaagiza utakatifu.
1 Petro 1:14-16 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;  kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.  ''

4. Watu wote duniani wanaungoja ujio wa YESU ili yeye YESU awahukumu. 
Ufunuo 22:12-13 ''Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. 
Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.''

Hivyo kumkataa YESU ni kuukataa uzima wa milele.
Kama unamngoja YESU aje akuhukumu maana ni lazima akuhukumu, na kisha wewe bado haumuhitaji hakika atakuhukumu kwenda jehanamu.
Dini ziko nyingi na madhehebu ni mengi na imani ni nyingi sana. lakini jambo la ajabu na muhimu ni kwamba atakayewahukumu wote ni YESU KRISTO tu na Neno atakalolitumia ni Biblia pekee hivyo ni muhimu sana kumpokea YESU na kuishi maisha matakatifu katika yeye.

5. Kuja kwa YESU ndio kukawa mwanzo wa majira yote na nyakati.
Mwanzo 49:10 ''  Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.''

Hata Leo tuko miaka 2016 baada ya KRISTO kuja duniani. Hiyo ina maana kwamba KRISTO YESU akiingia maishani mwako kila kitu chako kinatakiwa kibadilike.
 Ulikuwa unaitwa mtenda dhambi sasa baada ya kuokoka utaitwa mtakatifu kwa MUNGU.
 Wachawi walizoea kukutesa sasa watakuogopa maana majira yamebadilika maana ya YESU mbadilisha nyakati kaja maishani mwako.
Ukimpokea YESU dhambi zako zinafutwa na majira yake hayatakumbukwa tena kwa MUNGU, sasa unaanza majira mapya ya kuukulia wokovu wa KRISTO.
MUNGU akubariki sana na nakutakia sikukuu njema.
Tuitumie tu Siku hii kwa furaha, upendo na utakatifu.
Merry Christmas and Happy New Year.
Mwokozi YESU azaliwe moyoni mwako na mtii yeye miaka yako yote utapata uzima wa milele.

Yohana 3;17-18 ''
Maana MUNGU hakumtuma MWANA ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.  Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la MWANA pekee wa MUNGU.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana

Comments