TUSIHUKUMIANE KUHUSU KUADHIMISHA KRISMASI

Na Askofu Mkuu Silyvester Gamanywa.
Yamekuwepo malumbano ya miaka mingi kuhusu uhalali kwa Mkristo kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo tarehe 25 Desemba kila mwaka. Kila upande una utetezi wa kulinda misimamo yake. Hata kwenye mitandao ya kijamii kama hii, malumbano haya yanaendelea na hakutakuwepo muafaka unaowaridhisha wote.
Kwa sababu nami nimeulizwa kutoa maoni yangu kuhusu mtazamo au imani yangu katika mjadala huu, nimemwomba Roho Mtakatifu anipe neno la hekima kwa ajili ya kila mwenye kutafuta kujifunza kitu bora cha kumsaidia kiroho. Majibu yangu kuhusu Krismasi ni kama ifuatavyo:
Ninajua kabisa kihistoria ya kwamba Yesu hakuzaliwa tarehe 25 Mwezi Desemba. Pia ninajua ya kwamba Biblia haijatuagiza kuadhimisha siku za kuzaliwa Yesu au binadamu yeyote. Lakini pia ninajua ya kwamba Yesu Kristo alizaliwa duniani kama binadamu kamili (MT.1:18-21). Na pia ninajua kwamba kama vile Biblia haijaagiza kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu, pia Biblia hiyo hiyo haijakataza kuadhimisha kuzaliwa kwake duniani! Biblia imekaa kimya pande zote. Haijaruhusu na pia haijakataza.

Pili, katika mazingira kama haya ya maadhimisho kuhusu siku kwa ajili ya Mungu; Mtume wetu Paulo ametupa mwongozo kwa kila mtu binafsi kufuata dhamiri yake inavyomshuhudia kwa habari ya kuadhimisha au kutokuadhimisha:
"Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu." (RUM.14:5-6)
Kwa mujibu wa mwongozo wa Paulo, pamoja na kutoa uhuru kwa kila mtu kuongozwa na dhamiri yake; pia ametahadharisha kuhusu kutokuhukumiana kati ya asiyeadhimisha dhidi yake aadhimishaye: “Basi mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;..” (Kol.2:16)

TAHADHARI YA KUTOKUACHA KUKUSANYIKA
KAMA ILIVYO DESTURI YA WENGINE

“Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” (Ebr.10:25)

Kwa wale wasiokubaliana na kuadhimisha sikukuu ya Krismasi kwa sababu zao nzuri za kiimani; tunashauriwa kutumia fursa ya sikukuu kama hii ya Krismasi kukusanyika pamoja, kwa ajili ya matumizi yaliyo na tija ya kiroho.

Wakati wengine wanaadhimisha na kusherehekea kidunia bila kuzingatia miiko ya maadili ya kiimani; sisi tunapia muda na fursa hiyo kujengana kiroho na zaidi kujenga mahusiano ya kuwafikishia ujumbe waa kweli ya Injili ya Yesu ambaye wanadhimisha siku yake pasipo kuwa na mahusiano naye kiimani.

Tuandae semina, makongamano, au hata mijumuiko ya kijamii kwa mwavuli wa sikukuu na kuwaalika wale tunaodhani hawana imani sawa na sisi ili tupate kuwashuhudia na kuwaelimisha kuhusu kweli ya Injili. Kususa kukusanyika ati kwa sababu Biblia haijaagiza jambo lakini wakati huo huo pia haijakataza huko ni kupitiliza mipaka (extremism).
Ubarikiwe sana.

Comments