UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU UKOJE?

 Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU .
Leo ninazungumzia ubatizo wa ROHO MTAKATIFU.
Hili swali la ''ubatizo wa ROHO MTAKATIFU  ukoje'' nimewahi kuulizwa na watu wengi sana. Kupitia somo hili naamini nitakuwa nimejibu swali hilo.
Jambo la kwanza kujua ni kwamba ROHO MTAKATIFU ana sifa ambazo ni MUNGU pekee aliyenazo.
ROHO MTAKATIFU ni kama jicho linaloona kote, ni Nafsi inayotambua yote.
ROHO MTAKATIFU anaweza yote na anaweza kutenda lolote alitakalo wakati wowote.
Kanisa lililofunguliwa hata likajua ROHO MTAKATIFU ana kazi gani kwa mwamini mmoja mmoja hakika kanisa hilo litakua vizuri sana kiroho.

Mkristo yeyote kama anataka afanikiwe rohoni ni lazima ahakikishe hawi mbali na ROHO MTAKATIFU.
Bwana YESU alitutangazia kuja kwa ROHO MTAKATIFU, hii iko Yohana 14:26 ''Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

ROHO MATAKTIFU ni muhimu sana kwa kila mwamini maana hutufundisha, hutukumbusha na kutujulisha.
ROHO MTAKATIFU Yupo Kwetu Kwa Sababu Maalumu. Yeye Hutusaidia Katika Yote Ambayo Hatuyawezi. 
ROHO MTAKATIFU Ni Mwalimu Wetu, Ukihudhuria Vizuri Darasa La Mwalimu Huyu Utashinda Yote Ya Dunia. 
ROHO MTAKATIFU Ndio Mwalimu Pekee Wa Kweli.  
ROHO MTAKATIFU ndiye ambaye hutushuhudia kuhusu Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO.
Bwana YESU anasema 
''Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa BABA, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa BABA, yeye atanishuhudia.-Yohana 15:26''

Tukizungumzia ubatizo basi ni muhimu tukajua kwamba kuna batizo mbili ambazo ni ubatizo wa maji na ubatizo wa ROHO MTAKATIFU.
Kwanza Ubatizo Wa Kikristo Ni Mzuri Sana.
Ubatizo Wa Kikristo Uko Hivi; Mtumishi Humbatiza Mwamini Kwa Maji Kisha YESU KRISTO Humbatiza Mwamini Huyo Kwa ROHO MTAKATIFU. 
Ubatizo Wa Maji Ni Ishara ya nje ya Utakaso Wa Ndani Ya Mtu Lakini Pia Ni Muhimu Kujua Kwamba Ubatizo Wa Kikristo Ni Wa Maji Mengi.

Sasa naingia kwenye ubatizo wa ROHO MTAKATIFU baada ya kudonoa kidogo kuhusu ubatizo wa maji.
Yohana Mbatizaji ndiye wa kwanza kutangaza juu ya ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ambao utafanywa na Bwana YESU kwetu wateule wake.
Mathayo 3:16 ''Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa ROHO MTAKATIFU na kwa moto.''  

Ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ni nini?
=Ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ni  mabadiliko anayoyafanya ROHO MTAKATIFU ndani ya Mwamini kwa kumfanya mwamini huyo awe na ushirika mzuri na MUNGU pamoja  YESU KRISTO.

Ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ndio pia ubatizo wa Moto.
Moto wa ROHO MTAKATIFU ukipita ndani ya mwamini hakika huyo mteule wa KRISTO  hatabaki kama alivyo maana moto utaunguza visivyofaa vyote ndani ya mwamini huyo na kumfanya ayaishi matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU kwa urahisi bila kuona kama ni mzigo.


MAMBO MUHIMU KATIKA KIPENGELE CHA UBATIZO WA ROHO MTAKATIFU.

1. Jambo la kwanza kujua ni kwamba Ubatizo wa ROHO MTAKATIFU hutufanya tuwe na ushirika na  ROHO MTAKATIFU na ushirika na kanisa hai la MUNGU ambalo ni wateule wote wa KRISTO.
1 Kor 12:13 '' Kwa maana katika ROHO mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa ROHO mmoja.'' 

2. Jambo la pili linalotokea katika ubatizo wa ROHO MTAKATIFU ni kipawa cha kunena kwa lugha.
Marko 16:17-18 '' Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa LUGHA MPYA; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.''

Kwa sababu kunena kwa lugha ni kipawa basi wakati mwingine sio kila mteule anacho, hata kama kipawa hicho kwa mjibu wa Bwana YESU ni ahadi ya kila mteule.

Kuna viwango vya aina  tatu vya ujazo wa ROHO MTAKATIFU kwa mwamini.
(A). Kuokoka au wakati mwingine, kunena kwa Lugha mara ya kwanza baada ya kuokoka hutengeneza  ubatizo wa ROHO MTAKATIFU(Matendo 10:44-45)
(B). Kufurika ROHO MTAKATIFU(Waefeso 5:18B)
(C). Kutiwa mafuta na ROHO MTAKATIFU(Luka 4:18-19)

Karama za ROHO MTAKATIFU ni matokeo ya kiwango cha nguvu za ROHO MTAKATIFU ndani ya mwamini. 
Sio waamini wote wamebatizwa ROHO MTAKATIFU, sio waamini wote  hufurika ROHO MTAKATIFU na sio waamini wote wametiwa mafuta na ROHO MTAKATIFU.
Juhudi ya mwamini, mafundisho sahihi ya KRISTO, Utakatifu na maombi ndivyo vinaweza kumfanya mwamini kufikiwa hatua ya kutiwa mafuta na ROHO MTAKATIFU hata akatumika kwa viwango vizuri.

3. Ubatizo wa ROHO MTAKATIFU hutufanya tujae nguvu za MUNGU za kushinda.

Matendo 1:5-8 Bwana YESU anasema  '' ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika ROHO MTAKATIFU baada ya siku hizi chache. ..............   Lakini MTAPOKEA NGUVU, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.'' 

Ukibatizwa ROHO MTAKATIFU hakika unajaa nguvu za MUNGU sana.
Kwa mara ya kwanza mimi Mabula nanena kwa lugha nilijisikia nguvu za ajabu. Nikawa siwezi kuogopa chochote na nikawa na hasira za kuhubiri injili kwa wazanzibari wote maana nilikuwa naishi Zanzibar.
Tatizo la watu wengi ni kutokutunza huo muujiza walioupokea wa nguvu za ROHO MTAKATIFU.


4. Kubatizwa ROHO MTAKATIFU huonekana kupitia matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU kwa Mwamini.

Wagalatia 5:22-25 ''Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa KRISTO YESU wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.'' 

Mtu asiye na matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU huyo hana ROHO MTAKATIFU.

Ubatizo Wa ROHO MTAKATIFU Ni Muhimu Sana Kwa Kila Mkristo. 
=Ni Haki Ya Mkristo(Matendo 2:38-39 
=Ni Wajibu Wako Mwamini Kutafuta Kwa Imani Hadi Upokee Haki Yako Hii(Luka 24:49)

 Ubatizo Wa ROHO MTAKATIFU Dalili Mojawapo Yake Ni Kunena Kwa Lugha Mpya Kama Vile ROHO MTAKATIFU Anavyojalia Kunena. Hivyo Mwamini Anapojazwa Ujazo Wa ROHO MTAKATIFU Kwa Mara Ya Kwanza Atanena Kwa Lugha Nyingine Kwa Uwezo Wa ROHO MTAKATIFU.
Ona mfano huu.
Matendo 2:4 '' Wote wakajazwa ROHO MTAKATIFU, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama ROHO alivyowajalia kutamka.'' 

 Ubatizo Wa ROHO MTAKATIFU Humpa Mwamini Uwezo Wa Kuwa Shahidi Mwaminifu
Matendo 4:31 ''Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.''.
Ujazo Wa ROHO Ni Muhimu Sana. 
Kujazwa Ni Muhimu Na Kufulika ROHO Ni Jambo Endelevu. Ndugu, Tamani Kujazwa ROHO Na Ambaye Umejazwa Tunza Muujiza Wako Huo Daima. Kama Hujajazwa Tamani Kujazwa Na Hudhuria Mafundisho Ya Neno La MUNGU Kanisani. Dumu Katika KRISTO Na Hakikisha Unakuwa Mtu Wa Maombi Sana.

  NGUVU YA MAOMBI YA KUOMBA KATIKA ROHO MTAKATIFU. 

Waefeso 6:18 Biblia Inafunua Kwamba Ni Muhimu Kuomba Maombi Katika ROHO MTAKATIFU, Biblia Inasema "Kwa Sala Zote Na Maombi Mkisali Kila Wakati Katika ROHO, Na Mkikesha Kwa Jambo Hilo Na Kudumu Katika Kuwaombea Watakatifu Wote".
  ROHO MTAKATIFU Ni ROHO Wa MUNGU Ambaye Anatenda Kazi Sana Katika Siku Hizi Za Mwisho Ili Kuwakamilisha Wateule Wa KRISTO. 
ROHO MTAKATIFU Huweka Wazi Yaliyokuwa Yamefichwa  Tusijue ila katika ROHO MTAKATIFU tunayajua.
Warumi 8:26-27 ''Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.  Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU.'' 

Lakini pia Kuna Watu Wana Nguvu Za Kuomba Lakini Sio Maombi Katika ROHO MTAKATIFU. 
Kama Hakuna Nguvu Za ROHO MTAKATIFU Maombi Yako Yatakuwa Ya Kukatikakatika, Yatakuwa Maombi Makavu, Yatakuwa Maombi Yasiyopiga Sehemu Sahihi. Mchinjaji Wa Kuku Au Ng'ombe Anaweza Kusumbuka Sana Kumchinja Mnyama Huyo Kama Kisu Chake Ni Butu. Huu Ni Mfano Wa Mwombaji Anayeomba Bila Nguvu Za ROHO MTAKATIFU. 
 Maombi Katika ROHO Ni Muhimu Sana. 
Maombi Unayoelekezwa Na ROHO MTAKATIFU Ndio Maombi Muhimu Kwako Kuliko Yote.

ROHO MTAKATIFU Ndiye Mwenye Kuweka Muhuri Ndani Yetu Hata Tunapata Uthibitisho Wa Mambo Ya Rohoni. 
Waefeso 2:18-22 '' Kwa maana kwa yeye(YESU) sisi sote tumepata njia ya kumkaribia BABA katika ROHO mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake MUNGU. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya MUNGU katika ROHO.''
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako maana swali hili huulizwa swali, basi kwa njia hii watakuwa wamepata majibu.

Comments