ULINDE UTAKATIFU WAKO KATIKA KRISTO YESU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Baada ya kumpokea YESU umekuwa mtakatifu na utakatifu huo unatakiwa kuulinda sana na kuutunza sana. 
Utakatifu ni hali ya kuwa mtakatifu.
Mtakatifu ni mtu yule aliyeokoka na anaisha maisha kwa kulitii Neno la MUNGU.
Kwa njia ya YESU KRISTO, MUNGU hututakasa na kutuhesabia haki mbele zake.
1 Petro 1:2 ''kama vile MUNGU Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na ROHO, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya YESU KRISTO. Neema na amani na ziongezwe kwenu.''

MUNGU anataka wewe ndugu uliyempokea YESU uendelee kuishi maisha matakatifu.
Umehesabia haki bure mbele za MUNGU na sasa unatakiwa kuishi maisha matakatifu yasiyo ya kujichafua tena dhambini.
Tii Neno la MUNGU na lijaze hilo moyoni mwako.
Jitenge mbali na marafiki wabaya walikushawishi zamani kuingia maovuni.
Zaburi 1:1-2 ''Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.'' 

Dumu sana katika wokovu huku ukizaa matunda ya kazi njema siku zote mbele ya MUNGU.
Ni muhimu sana ukakua kiroho huku ukiongeza utii na unyenyekevu kwa MUNGU.
MUNGU anataka tuishi maisha ya haki siku zote.


 Ndugu, Unaweza ukajua ulikotoka na unaweza ukajua ulipo lakini hujui uendako.
Ndugu yangu, unamhitaji sana Bwana YESU kwa ajili ya huko uendako ili uende uzima wa milele.
Ndugu, usipomhitaji YESU sasa huko uendako haitakuwa uzima wa milele bali ziwa la moto.

Kwa sababu umempa YESU maisha yako hakika umeokoka, na kwa sababu umeokoka basi hakikisha unatunza utakatifu wako siku zote.
Kataa ushawishi wowote unaoweza kukupeleka dhambini.
Biblia inakushauri vyema sana ikisema,
'' Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi, Wewe usikubali. Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi, Na tuvizie ili kumwaga damu; Tumwotee asiye na hatia, bila sababu; Tuwameze hai kama kuzimu, Na wazima, kama wao washukao shimoni. Tutapata mali yote ya thamani, Tutazijaza nyumba zetu mateka. Wewe utashirikiana nasi; Tutakuwa na vitu vyote shirika. Mwanangu, usiende njiani pamoja nao; Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.   -Mithali 1:10-15''


Wanadamu wengi wanaichezea neema ya MUNGU.
Ndugu, Kuna tofauti kubwa kati ya thamani ya mtu kwa MUNGU na thamani ya MUNGU kwa mtu.
Thamani yako mwanadamu kwa MUNGU ni kubwa sana japokuwa thamani ya MUNGU kwako imepungua kwa sababu kwa sasa hata humtii MUNGU Bali unaendekeza tu uzinzi wako na uongo, unaendekeza tu wizi wako na uchawi na machukizo yote uyatendayo.
Ndugu, japokuwa thamani yako kwa MUNGU ni kubwa sana ndio maana akakuletea Mwokozi YESU ili akuokoe, lakini mwanadamu wengi wamemkataa Mwokozi na Wokovu wake ulio wa thamani sana. 
Ndugu zangu, kuendelea na dhambi ipo Siku thamani ya mwanadamu kwa MUNGU itaondoka kabisa, ndipo kutakuwa na kilio na kusaga meno katika jehanamu ya moto.
Ukipata ufahamu wa kukielewa Neno hili basi tubu, okoka na acha dhambi zote, Bwana YESU atakupokea haijalishi una dhambi kuliko wote katika kabila lako, au mji wako; ukimpokea YESU hakika atakuokoa.

Na baada ya kuokoka anza kuishi maisha matakatifu.
Waefeso 1:4-6 '' kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake.  Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa.'' 

Ashukuriwe MUNGU aliyetuchagua ili tuwe watakatifu.
Watakatifu wametengwa kwa ajili ya MUNGU na kuwa wa MUNGU kwa njia ya imani katika KRISTO YESU.
Hatuna muda wa kubaki tena kwa shetani bali ni wasaa wetu kumpendeza MUNGU wetu aliyetuchagua ili tuurithi uzima wa milele ulio tayari kwa ajili yetu katika KRISTO YESU.
Shetani naye hujaribu kuwaondoa watakatifu katika kusudi la MUNGU la uzima lakini kwa kulitii Neno la MUNGU tumeshinda.
Kwa kuwa na ROHO MTAKATIFU na kumtii yeye tunashinda na zaidi ya kushinda.

Ndugu uliyeokoka nakuomba anza sasa kuwasaidia na wengine ili waje kwa YESU kwenye wokovu na uzima.
Ni kweli kabisa  shetani huwa hakai kwenye miti Bali anakaa kwenye miili ya watu wanaomtii.
Wanaomtii shetani hakika hao wanakaa nae na kama wataendelea kukaa nae na kumtii hakika majina yao  itakuwa ngumu kuwemo kwenye kitabu cha uzima cha Bwana YESU.

Hivyo kazi yetu ni kuwasaidia ili wajitenge na shetani.
Wajitenge na dhambi na wajitenge na machukizo ya dunia.
Ndugu mtii MUNGU na fundisha watu kumtii MUNGU siku zote.
Wafundishe watu kumtii MUNGU maana ndilo kusudi la MUNGU.
Wafundishe watu kunyenyekea kwa MUNGU huku na wewe mwenyewe ukinyenyekea kwa MUNGU.
Neno la MUNGU linasema,
  ''
Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.-Yakobo 4:7-10 ''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana

Comments