UMEMFUATA MWOKOZI YESU AU UMEFUATA DINI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Huko mbinguni kipo kitabu kimoja cha usajiri ambapo majina ya wanadamu wote waishio na watakaoishi  huko yameandikwa katika kitabu hicho.
Ikiwa mtu hakusajiriwa katika kitabu hicho hawezi kutambulika kuwa ni raia wa Mbinguni, naye mtu huyo kamwe hawezi kuishi mbinguni kwa sababu jina lake halikuandikwa katika kitabu hicho cha usajiri. Kitabu hicho kinaitwa kitabu cha uzima.

Siku ya mwisho kitatumika kitabu hicho ili wale ambao majina yao yamo katika kitabu hicho wataenda uzima wa milele, na ambao majina yao hayatakuwa katika kitabu hicho wataenda jehanamu ya moto wa milele.
Ufunuo 20:12-13 '' Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. '''

Kwenye kitabu cha uzima hayumo kila mtu bali watakatifu tu waliokombolewa kwa damu ya thamani sana ya YESU KRISTO. Hapo ndipo tunaona tofauti ya Mwokozi na Dini. Katika kutaka kuingia uzima wa milele Mwokozi ni muhimu kuliko dini iwayo yoyote.
Washika dini wapo tangu zamani lakini dini haikuwafikisha mbinguni bali waliomtii Mwokozi YESU na Neno lake na wakamkiri kila mahali, MUNGU aliwapa uzima hao.
Ndugu zangu Madhehebu yako katika sheria za serikali na taratibu za kiserikali lakini sio sheria ya mbinguni. Dhehebu ni la muhimu sana kama tu dhehebu hilo linahubiri Wokovu wa KRISTO na utakatifu autakao MUNGU.
Ni muhimu sana tena ni lazima sana tuwe na madhehebu lakini tukiwa na madhehebu sio tutii dhehebu au kuliabudu dhehebu bali ni muhimu kumtii Mwokozi YESU na kumwabudu MUNGU katika kweli yote.
Sio madhehebu yote yanafundisha kweli ya KRISTO, Wengine ni mawakala wa shetani ili kuwatoa watu kwenye wokovu wa YESU KRISTO.
2 Timotheo 3:13 '' lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.'' 

Kumbuka dini ni mipango ya wanadamu hivyo inaweza ndani yake ikawa na ubinadamu ambao wala sio mpango wa MUNGU.
Je wewe umemfuata Mwokozi YESU au umefuata dini?

Dini yeyote iliyo kinyume na Wokovu wa YESU KRISTO hiyo dini ni ya shetani na inasimamiwa na mawakala wa shetani.

Wakati mwingine dhehebu  lako linaweza kuambatana na maagano mabaya ndio maana unatakiwa kumshika YESU na sio dini wala dhehebu. Dini ukiishika sana itakufanya uione Dini ni muhimu kuliko Mwokozi wakati ukweli ni kwamba hakuna Dini itakayomfikisha mtu mbinguni Bali utakatifu katika KRISTO ndio pekee utakufikisha uzima wa milele.

1 Petro 1:15-19 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita BABA, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO.'' 
 
Ndugu, Dini utaiacha hapa lakini YESU kama umempokea na kuliishi Neno lake hakika utakuwa naye hata baada ya kuondoka kwako duniani.
Kuna watu ukiwauliza kipi muhimu kati ya Dini na Mwokozi YESU watakuambia Dini ni muhimu wakati ukweli ni kwamba mbinguni hakuna Dini wala dhehebu Bali mbinguni kuna watakatifu tu waliosafishwa kwa damu ya YESU KRISTO. 

Warumi 3:24-26 ''wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika KRISTO YESU; ambaye MUNGU amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye YESU.''
 
Kama wewe humtii KRISTO na Neno lake basi hakika wewe huitaki mbingu.
Ndugu mtii YESU KRISTO na Neno lake Biblia hapo ndipo utaubariki moyo wa MUNGU.

Kuwa MTEULE sio kazi ndogo, ni kumkataa shetani na watoto wake wote na kukimbilia kwa YESU KRISTO kisha ukajazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na baada ya hapo unamtii ROHO MTAKATIFU milele.


Kuifuata dini tu wakati mwingine kunaweza kukufanya uone kawaida tu kufanya dhambi.
Ndugu mmoja akaniuliza kwanini watoto wa wachungaji wengi hawajasimama katika wokovu kama baba zao?
 Nikamwambia ni kwa sababu wamefuata dini ya baba zao na sio kumfuata Mwokozi YESU. Wamezaliwa ndani ya dini na wameendelea kuwa kwenye dini, hivyo kama hawatajua kwamba wanatakiwa kumfuata Mwokozi YESU na kumtii hakika watabaki kuwa wanadini na sio wateule wa MUNGU.
Kufuata dini tu wakati mwingine kunaweza kukufanya uone dhambi ni jambo la kawaida tu.
Kuna mtu anajisifu kwamba yeye hufanya dhambi ndogo ndogo tu.
Biblia inamwambia hivi dhambi zote ni kubwa Tena hazifai.
"
Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. Yakobo 2:11''

Miguu ya watu wengi ni myepesi sana kukimbilia disko kuliko kukimbilia kwenye mikutano wa injili, miguu ya watu wengi ni myepesi sana kukimbilia tamasha la bongo fleva kuliko kukimbilia maombi kanisani.
Ni heri kutafuta uzima wa milele kuliko kukimbilia machukizo.

Watu karibia wote unaowaona wana dini na madhehebu yao na kanisani huenda kila mwisho wa wiki lakini kimazoea maana wameshika dini tu inatosha, hivyo hofu ya MUNGU haiko ndani yao kwa sababu hajamfuata Mwokozi YESU KRISTO.
Kuna mpaka wazee wa kanisa huenda kwa waganga na kanisani kila jumapili yupo na amekaa kiti cha mbele. Huyo yuko tayari muda wote kutetea dhehebu lake lakini hayuko tayari kumtii Mwokozi YESU ambaye ni yeye pekee anayeweza kumpeleka uzima wa milele.
Watu wamebaki na dini tu ila hawana Mwokozi YESU wala wokovu wake hawautaki.
Watu wako na dhehebu tu ila hawana Mwokozi YESU wala hawauhitaji wokovu wake.
Watu kama hao ukilisema vibaya kidogo dhehebu lao watakushambulia mpaka utashangaa lakini Wokovu hawana habari nao.
Wako tayari kutetea dhehebu lao na dini yao kuliko kuishi maisha  matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
Ukiwaambia KUOKOKA kwao ni machukizo na watakuona kama unakufuru maana wameshika matakwa ya dhehebu na sio matakwa ya MUNGU kupitia KRISTO YESU.
Kuna madhehebu mafundisho yao makuu sio Wokovu wa KRISTO wenye injili ya Uzima, bali wao wako busy na vitu vingine kabisa.
Huu ni wakati wa Wokovu hivyo kipaombele cha kila kanisa kuhubiri ingekuwa Wokovu na utakatifu Maana haya mengine hayawezi kutufikisha mbinguni bali Wokovu wa KRISTO na utakatifu katika KRISTO.
Wokovu ndio kuokoka kwenyewe.
 Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''


Hata kupumzika nayo ni kazi lakini kwa sababu ya injili ya KRISTO hatutapumzika ili watu waliopendwa na mbingu waokoke wote.
Ndugu, ukishaokoka sasa hakikisha unajificha ndani ya KRISTO YESU ukiwa mtatakatifu asiye na mawaaa ya aina yeyote.
Lakini pia kumbuka kwamba Kama huna ROHO wa MUNGU utabaki ukimjua YESU KRISTO kama mtu tu na sio Mwokozi.


Wenye dini leo wako busy na dini tu huku hawafundishi utakatifu .
Washika dini  leo  ndio hao hao wanaoimba nyimbo za kidunia na kujisifu kwamba wanafanya vyema.
Waimbaji wote nyimbo za kidunia karibia wote wana dini na huhudhuria ibada mwisho wa wiki na viongozi wao hawawakemei bali huwasifia na kusifu vipaji vyao ambayo vinatumika kipepo kabisa.
Ninyi mnaoimba nyimbo za kidunia MUNGU anasema juu yenu leo  kwamba '' Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.-Amosi 5:23''

Kumtumikia shetani kupitia nyimbo za kidunia ni kujiweka hukumuni kabisa.
Nakuonya kwa jina la YESU acha kuimba nyimbo za kidunia na sasa okoka kisha karama hiyo hiyo anza kuimba nyimbo za injili.
Hata kama ungepata vyote uvitakavyo kwenye nyimbo zako za kidunia lakini kukosa uzima wa milele ni jambo baya kuliko yote.


Ndugu kama umeamua kumfuata Mwokozi YESU hakika ubarikiwe sana na ninakuomba usitangetange baada ya kuokoka maana kutangatanga kunaweza kukurudisha Misri.
Kutangatanga kunaweza kukuondolea huduma yako njema.
Kutangatanga kunaweza kukufanya uwatumikie watu na sio kumtumikia MUNGU.

Ulipokuwa Misri(Kabla hujaokoka) uliwanyenyekea sana wanadamu lakini hukufanikiwa kwa lolote, hebu leo anza kumnyenyekea MUNGU mwenye Uzima wako wa milele.
Uliwanyenyekea sana mabosi zako kazini lakini hata cheo hawakukupandisha. Leo anza kumheshimu Bwana YESU mwenye uzima wako wa milele.

Jambo jingine muhimu kujua ni kwamba kazi yako ya kuajiriwa au kujiajiri haina sehemu katika uzima wa milele, Biashara yako ya duniani haiwezi kukuongezea lolote katika uzima wa milele.
Maisha matakatifu katika KRISTO ndio tiketi yako ya uzima wa milele, shika utakatifu kwanza na sio mengine.
Sio kwamba usifanye kazi kabisa ili kujipatia kipato bali uwe na kiasi ili upate muda wa kumwabudu MUNGU kanisani na kujifunza Neno lake kanisani kila mara na sio jumapili tu.
MUNGU wala hatakuacha wala kukupungukia.
Umeanza na YESU sasa, hivyo hakikiksha unamaliza na YESU.


 Wakolosai 2:6-10 '' Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa MUNGU, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. ''.

Ndugu nakuomba  ongeza ufahamu wako kwenye Neno la KRISTO itakusaidia.

 Ili uwe na taarifa sahihi za Ki-MUNGU moyoni mwako lazima kwanza uwe umebadilishwa na MUNGU.
Kuokoka ni mlango wa kubadilishwa na MUNGU.
Ezekieli 36:26-27 ''Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.''


MUNGU ametuahidi kutupa moyo wa nyama yaani moyo wa upole, moyo wa kusikiliza ushauri mzuri,na ni moyo wa kumsikiliza ROHO MTAKATIFU.
Heri Kung'ang'ania Kwa YESU Kuliko Kumkimbilia shetani Ambaye Atakuchekea Wiki Ya Kwanza Harafu Wiki Inayofuata Anakuchinja Kama Kuku Ili Mkaishi Nae Jehanamu Milele.
Kuna Watu Leo Mioyo Yao Inatamani Sana Kumpokea BWANA YESU Ila Miili Yao Inakataa Na Wao Wanaitii Miili Yao Ambayo Huwatendesha Dhambi Kila Siku. Ndugu Mwili Wako Usipokuwa Makini Unaweza Kukupeleka Motoni, Usikubali Mwili Wako Ukufanye Umkosee MUNGU. BWANA YESU Anakupenda Sana Na Hataki Kabisa Uende Motoni.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments