UNAJIANDAAJE KUINGIA KWENYE NDOA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Yeremia 29:6 '' oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.''

Ndoa ni mpango wa MUNGU kwa watu wake.
Kijana anaweza kumchumbia binti na wakafunga ndoa na kuendelea na maisha yao.
Binti ana uhuru wa kumchagua mchumba amtakae ili kwa utakatifu wafunge ndoa na kumtukuza MUNGU.
Wazazi ni mashahidi tu wa tukio la vijana wao kufunga ndoa takatifu.
Kanisa ni mashahidi tu ya vijana wao kufunga ndoa.
Ndoa ni takatifu na inatakiwa wanandoa watembea katika utakatifu ili ndoa ibaki kuwa takatifu.
Ndoa ni agano la kudumu na sio kujaribu.
Kijana anatakiwa sana amhusishe MUNGU katika uchumba hadi ndoa ili kutengeneza misingi imara ya ndoa. 
Kijana katika maandalizi ya kuoa au kuolewa anaweza akajiandaa katika jambo moja lakini jambo la pili lililo la muhimu sana ameliacha, ndio maana tunajifunza leo kama sehemu ya kukumbushana katika maandalizi ya ndoa na kisha ndoa yenyewe.

Kipi muhimu Kwa wachumba katika maandalizi ya ndoa yao, ambacho wachumba wengi hukipa kipaombele cha kwanza?
✔ je ni shela na suti?
✔ je ni maombi?
✔ je ni kamati?
✔ je ni mipango ya baada ya kufunga ndoa yao?

✔ je ni wapi wataenda Honey moon?

 Kwa uzoefu wangu wachumba wengi hunawaza kamati, shera , suti . Harusi iweje Maombi yaweza kua ya mwisho. Lakini kama vijana hao hawajamhusisha MUNGU vya kutosha wakati mwingine ndoa ile inaweza kupeperuka siku chache kabla ya kufunga ndoa hiyo maana shetani hapendi kabisa Mwanadamu afunge ndoa takatifu mbele za MUNGU.

Yeremia 17:5 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.''

Ni makosa makubwa wachumba kutokumtegemea MUNGU.
Shetani hapendi ufunge ndoa takatifu kanisani.
Shetani anataka binti utoroshwe, shetani anataka kijana uvute tu mwanamke kisha baada ya miezi kadhaa useme binti huyo hakufai, unamwacha huku akiwa mimba na kuoa mwingine ukiona kama sio dhambi, ukijifariji kwamba uchumba sio ndoa.
Ni muhimu sana vijana wakamtegemea Bwana YESU katika uchumba wao ili waifikie ndoa njema.
Ni vyema sana wachumba wakamhusisha sana MUNGU katika uchumba wao ili waifikie ndoa njema.
Silaha kubwa ya kuwafanya vijana wachumba waingie katika ndoa takatifu njema na ya kumpendeza MUNGU ni vijana hao kukataa kufanya ngono wakati wa uchumba.
Vijana ni muhimu sana mkafanya maandalizi ya ndoa huku mkijua ya kwamba MUNGU ndio aliyeiumba ndoa hivyo ni lazima mumuombe sana na kumtegemea na kutii Neno lake.
Kama kijana ukimtegemea MUNGU kwa maombi na kumtii Neno lake linasema; ''Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.-Kumb 31:8'' 

Nabii namba moja Wa maisha yako ni Neno la MUNGU.
Nabii Wa Pili Wa maisha yako ni wewe mwenyewe.

Tii Neno la MUNGU katika hatua zao zote za ujana, uchumba hadi ndoa takatifu.
Hata kama hujapata mchumba nakuomba ndugu Muombe MUNGU ambaye ndiye aliyewaumba hao wachumba, atakupa mzuri sana wa kuendana na wewe na kukufaa sana.
Kumbuka  Hawawezi kukupenda wote kama ambavyo hawawezi kukuchukia wote.
Hawawezi kukusema vibaya wote hata kama baadhi yao hukusema vibaya.
Ninachojua thamani yako ni kubwa sana kama tu unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.

Mwenzi wako wa ndoa yupo na atakuja kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Ongeza tu juhudi katika kumtumikia MUNGU na kumtii.
Akisema Amesema MUNGU Wa Yakobo, Akisema Itakuwa Hakika Itakuwa.
MUNGU Muumbaji wako anasema ''
'' oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.-Yeremia 29:6 ''
  Hivyo songa mbele ukimcha MUNGU na kutenda kwa akili.
Jitunze na tunza ujana wako.
Tunza Wokovu wa KRISTO kwako ulio wa thamani sana.
Weka mipango vizuri na kwa sababu wewe ni muombaji hakika MUNGU atakupa baraka yako hivyo hata usione tatizo kupanga jinsi utakavyoishi ukiwa katika ndoa yako maana MUNGU aliyeahidi ni mwaminifu na wa haki hakika atakubariki tu.
Nimeshuhudiwa wengi waliodhani hawataolewa lakini waliolewa kwa ushindi na baraka kuu.
Nimeshuhudia wengi waliodhani kwamba hawawezi kupata mwanamke wa kuoa lakini MUNGU aliwapa na sasa katika ndoa zao ni shangwe.
Nimewahi kuona waliojiona ni wabaya wa sura lakini walipojikubali na kumtegemea MUNGU na Kumtumikia kwenye injili yake hakika walifanikiwa sana na sasa ndoa zao ni moja ya ndoa kielelezo cha matendo mema.
MUNGU wetu anaweza na ataweza kwako.
Usikubali kuwategemea wanadamu tu bali mtegemee JEHOVAH Mungu wa uzima na ushindi mkuu sana.
 Isaya 1:19 ''Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;''

Wakati mwingine kuna vijana ROHO MTAKATIFU  huwajulisha kwa ndoa ili wajue waombeje na kushinda. MUNGU anazungumza sana na watu wake lakini tu wakati mwingine mazingira yetu na ufahamu wetu unafanya tusielewe kipindi MUNGU nazungumza na sisi ili kutupeleka katika mema yake.
Mfano MUNGU anaweza kusema na wewe kwa ndoto au kwa maono lakini wala hujali maono hayo.
Mfano
Unaweza kuota  ulikokulia yaani mara kwa mara unaota uko kijijini ulikokulia au kusomea
Maana ya kwanza ni kwamba kuna kitu kimefungwa na adui zamani kuhusu wewe hivyo omba ukipatilisha kila laana ya zamani au maagano ya zamani.
Maana ya Pili kurudishwa nyuma kimaisha na adui hivyo pambana kiroho utashinda Kwa jina La YESU.
Maana ya tatu ni kwamba una muda mrefu hujaenda kwa wazazi hivyo nenda ukawasalimie, kuwasalimia huko kunaweza kutengeneza baraka yako.
Huo ni mfano mmoja katika mingi ya kujua ufanyeje pale ambapo MUNGU amesema na wewe.
Jambo moja muhimu la kujua ni kwamba hakuna msaada popote Wa kukusaidia ila ni Kwa Bwana YESU KRISTO pekee.
Yohana 14:13 ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana(YESU).''

 Wakati mwingine maandalizi ya kijana kuingia katika ndoa yanaweza kukwamishwa na wanaomzunguka au anaowategemea katika ushauri.
Ndugu, Watu ni wengi lakini binadamu ni wachache.
Sio kila ndugu ni rafiki mzuri.
Sio kila mtu ana lengo zuri na wewe na sio kila unayemweleza siri zako ana kutakia mema.
Ndugu ni Heri ukamtegemea YESU na kumweleza siri zako yeye YESU mwenye uzima wako wa milele.
Ukimtii YESU utafanya vyema sana.



Ni muhimu sana kufanya maandalizi ya kuoa au kuolewa huku utakatifu ukiwa maisha yako halisi.
Sio utakatifu wa kanisani tu lakini usiku uko vichochoroni ukifanya dhambi. hiyo itakuzuia tu kufanikiwa katika mpango wa MUNGU.
Kila kijana anatakiwa atambue kwamba anawajibika kwa MUNGU hivyo kushikilia dhambi ni kujiangamiza.
Ni kweli kabisaaaa kwamba kuendekeza dhambi ni kutanguliza kabisa kichwa kwenye ziwa la moto kinabaki kiwiliwili tu ambacho kitaenda huko Siku ile, ndio maana utakatifu katika Bwana YESU unahitajika sana ili tu kukatisha safari ya jehanamu na sasa iwe safari ya mbinguni
1 Petro 1:14-16 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments