UNAKIRI NINI BAADA YA KUMALIZA KUOMBA?

Na Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Najua kila mmoja anajua maombi ni nini na anajua umuhimu wa maombi, ila ongeza ufahamu wako kupitia somo hili.
Ukipokea Kidogo Kutoka Kwa MUNGU Zaidi Ya Kile Ulichoomba Basi Tambua Kwamba Imani Yako Ni Ndogo Na Inaendana Ulichopokea.
Kiwango Chako Cha Imani Ndio Kiwango Chako Cha Kupokea Kutoka Kwa  MUNGU.


Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''

Biblia inatufundisha kwamba maombi yenye majibu ni yale ambayo yanaambatana na imani ndio maana ya hilo neno
 '' Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu''

Watu wengi wana imani ya kuongea tu lakini sio vitendo.
Watu wengi ukitaka kujua kwamba wanaomba bila imani ni ule ukiri wanaoukiri(Tamka) wakiwa katika maisha ya kawaida nje na muda wa maombi.
Ndugu mmoja alinielezea kwamba yeye ni muombaji sana na hufunga sana lakini ni miaka mitatu sasa hajapokea lolote katika yale aliyoomba. Katika maelezo yake akasema anahisi ana mikosi na anahisi MUNGU hampendi. Pia akasema itakuwa MUNGU hamsikii na anadhani maombi yake huwa hayamfikii MUNGU.  Kwa maelezo yake tu nikagundua kwamba ni yeye mwenyewe ndio chanzo cha kutokujibiwa maombi yake, ni yeye ndio hujiwekea mipaka. Hebu jiulize umeomba na umefunga mara kadhaa na katika maombi unakiri kwamba ''Naamini katika jina la YESU nitapokea hitaji langu'' lakini kesho yake unaanza kusema MUNGU hakusikii mara una mikosi, sasa kwa maneno hayo ya baada ya maombi ni uthihilisho kabisa kwamba mtu kama huyo hana imani ila anajaribu tu kuwa na imani.
Bwana YESU akasema ''Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''

 Ulimwengu Wa Roho Unaenda Kwa Matamshi, MUNGU Anaangalia Neno La Mtumishi Alilolitamka Ili Alidhibitishe. 
Mtumishi huyo ni wewe muombaji na ni wewe ambaye MUNGU analiangalia Neno ulilotamka la maombi ili akutendee lakini kabla MUNGU hajakutendea ndipo wewe huanza kumwekea MUNGU mipaka, mara hakusikii, mara una laana wakati kwenye maombi uliifuta hiyo laana, mara una mkosi wakati kwenye maombi uliufuta mkosi huo kwa jina la YESU. Hayo ndio yanaweza kukufanya usipokee hitaji lako wakati mwingine.
Kiwango Chako Cha Imani Ndio Kiwango Chako Cha Kupokea.
kufanikiwa kwako kimwili ni matokeo ya kufanikiwa kwako kiroho.
Kiroho unaomba na kuyafuta maombi yako kwa kauli zako ndio maana katika ulimwengu wa mwili hufanikiwi.


Yakobo 1:6- 7 ''Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani ya kuwa atapokea kitu kwa BWANA.''

Wengine huomba bila kuamini ndio maana hawapokei.
Wengine huomba kwa mashaka ndio maana hupokea mashaka na sio mahitaji yao.
Mashaka katika kuomba ni kama mtu mgonjwa anayejilazimisha kufanya kazi ngumu,
· Mashaka ni kirusi cha kuharibu imani ya mtu
· Mashaka yanahamisha imani ilipo na kuipeleka sehemu nyingine kwamfano kama ukiomba mchumba na MUNGU alishakuthibitishia labda kwa ndoto au maono au kwa Mtumishi kuja kwako kukamilisha uhakika huo, usipoamini kile ulichoonyeshwa na MUNGU umeruhusu roho nyingine ya kuja kuharibu imani yako na hapo watu wengi huwa wanajikwaa sana ,
  Kama huwezi kuamini kupokea muujiza wako kutoka kwa MUNGU basi maishani mwako usitarajie jambo jema, maana hata ukiomba ni kama unapoteza muda wako bure.


Yako mambo  mengi ambayo yanaweza kuwa kizuizi pia cha maombi yako.
Labda niseme hivi ondoa jiwe ili ujibiwe maombi yako.
Kuwasema watu vibaya ni mawe yanayoweza kusababisha usipokee hitaji lako.
Kusema uongo ni jiwe na hilo linaweza kusababisha usipokee hitaji lako.
Dhambi ni jiwe na hilo linaweza kusababisha usipokee hitaji lako.
MUNGU ana mpango mzuri juu yako, alipokuokoa alitaka pia kukuondolea moyo wa jiwe na kukupa moyo wa nyama unaolitii Neno lake.
Sijui kama unamtii MUNGU hata moyo wa jiwee usiwe ndani yako.
Sina Mengi ila ondoa moyo wa jiwe ili ujibiwe maombi yako.


Ezekieli 36:26-27 '' Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.''

 Linalopangwa na mwanadamu linaweza likafanikiwa au lisifanikiwe. La MUNGU tu ndio ambalo hufanikiwa 100%.
Ndugu, muombe MUNGU kwenye mipango yako ili yeye ndio aifanikishe.

 Kama watu wa MUNGU tuliompa BWANA YESU maisha yetu wakati mwingine tunaweza kupita kwenye vikwazo vingi na wakati mwingine kuonewa au kushambuliwa kiroho kisa tu tunamtangaza YESU kwa mataifa yote.
Lakini licha ya hayo yote kama kweli unaujua uzuri wa BWANA YESU huwezi kurudi nyuma na kuwa mpagani eti tu kwa sababu ya kukwazwa au kutokujibiwa maombi yako.

Tafuta sababu ya kutokujibiwa maombi yako na sio kulaumu tu huku ukifuta maombi yako kwa kinywa chako kile kile ambacho kilikiri katika maombi na sasa kinafuta yale maombi kupitia ukiri ule ule.
Mithali 18:20-21''Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.''
Tumbo lako litajazwa matunda ya midomo yako.
Hitaji lako utalipata kupitia maombi yako na ukiri wako sahihi.
Kwenye kinywa chako kunaweza kutoka maeno ya uzima au ya mauto yaani kunaweza kutoka maneno ya ushindi wako au maneno ya kushindwa kwako.
Inawezekana kwenye maombi unakiri ushindi kwa kinywa chako lakini baada ya maombi unafuta maombi yako kwa kinywa chako, hiyo haifai ndugu,
Omba kwa imani na kiri ushindi kwa jina la YESU KRISTO siku zote. Dumu katika utakatifu na jifunze sana neno la MUNGU maana kwa hilo utapata uhakika wa mambo ya rohoni.

Zaburi 116:1-2 ''Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.''

Hebu leo omba maombi yafuatayo kisha kiri ushindi kwa jina lla YESU huku ukiishi maisha matakatifu siku zote.
=Haribu roho zote za shetani za kukufanya uwe mtumwa wa shetani.
=Haribu roho zote za kukuondoa katika mpango wa MUNGU na kusudi la MUNGU la baraka kwako.
=Haribu roho za kipepo za kutaka kukutawala ili usipokee mambo ya MUNGU.

 =Kataa roho ya mazoelea kwenye Neno la MUNGU.
=Haribu roho za kuwatawanya watu wa MUNGU ili tu wasimwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
=Omba kibali cha kiutumishi katika kazi ya MUNGU.
=Ombea utoaji kwenye kazi ya MUNGU.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments