UZINZI NA UASHERATI NI DHAMBI YA KUIKIMBIA TU NA SIO VINGINEVYO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kufanya mapenzi kati ya mwanamume na mwanamke ni halali katika ndoa tu, Ndivyo Biblia inafundisha.
Kufanya mapenzi baina ya watu wasiooana ni dhambi ya uasherati.
Kufanya mapenzi baina ya mtu aliye kwenye ndoa na asiye kwenye ndoa ni dhambi ya zinaa.
Dhambi hii inawakosesha mbingu watu wengi sana.
Dhambi hii ya ngono inawakosesha wengi sana.
Ndugu zangu, Tukitaka uzima wa milele ni muhimu sana tuokoke na tujitenge na dhambi zote ikiwemo dhambi ya uzinzi na uasherati.
Uasherati na uzinzi sio dhambi ya kuombewa ili itoke Bali ni dhambi ya kuikimbia. 
 Waefeso 5:3-5 '' Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu; wala aibu wala maneno ya upuzi wala ubishi; hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru. Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa KRISTO na MUNGU. ''

=Waasherati Ni Wale Ambao Hawajafunga Ndoa Wakifanya Ngono Wao Kwa Wao Au Hata Wakifanya Ngono Na Wale Walio Kwenye Ndoa Ni Dhambi Kuu
=Wazinzi Ni Wanandoa Wakitoa Nje Ya Ndoa Zao Ni Machukizo Makuu.

Hebu ngoja tujifunze kwa Yusufu ambaye mke wa potifa alipotaka kufanya naye ngono, Yusufu alikimbia.

Mwanzo 39:7-13 ''Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose MUNGU? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, '

Kumbe dawa ya kuepuka dhambi ya uzinzi ni kuikimbia na kuyakimbia maeneo hatarishi na kuwakimbia marafiki wabaya wanaokushawishi kufanya dhambi hiyo.
Kwa Yusufu tunajifunza kwamba alimkimbia mtu mbaya aliyetaka kumwingiza dhambini.
Aliyakimbia mazingira hatarishi.
Alikimbia hila za shetani kutaka kumwingiza katika dhambi. Hivyo unaweza ukakemea sana uzinzi ukutoke lakini kama mazingira yako hatalishi unaendelea nayo basi hakika utaendelea na uzinzi. 
Mteule wa MUNGU hatakiwi kuwa mzinzi wala mwasherati.
Mtumishi wa MUNGU kuwa mzinzi ni dalili mojawapo ya kuacha kumtumikia MUNGU kwa kuanza kumtumikia shetani kupitia uzinzi wako, ni hatari sana hiyo.
1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.'' 

 Kama mtu ana mapepo yaani majini mahaba basi hayo tunaweza kuyakemea kwa jina la YESU KRISTO na yakatoka ila kuukemea uzinzi ili umtoke mtu hiyo haipo ila tumfundishe tu mtu huyo kuukimbia uzinzi au uasherati. 
=Tumfundishe mtu huyo kuweka neno la MUNGU ndani yake na sio picha za ngono na video za ngono. 
=Tumfundishe kujitenga na marafiki wabaya na tumfundishe kumcha MUNGU na kutumia muda wake mwingi kwa MUNGU. Ukweli ni kwamba kila mtu ana uwezo wa kuukimbia uzinzi na na uasherati, maana kama chakula chenye sumu mtu akiambiwa asile huacha kula chakula hicho wala hawezi tena kukisogelea basi hata uzinzi anaweza kuuacha kama ukiamua. 
Kumbuka Uzinzi una madhara makubwa kuliko sumu zote hivyo ni rahisi sana kuuacha uzinzi na uasherati.
 Uzinzi na uasherati unaweza kumpeleka mtu jehanamu hivyo dhambi hiyo ni mbaya sana. 
Ufunuo 21:8 ''Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.''

Watu wengi hawapendi kukaa katika kweli ya KRISTO na kupelekea hofu ya MUNGU kuondoka kwao ndio maana wanaendekeza uzinzi.
 Ndugu zangu dhambi hii ni mbaya sana na tuikimbie.
 Kumbuka kuwa Kuna watakaoishi uzimani milele na kuna watakaoishi motoni milele.
Bwana YESU atusaidie maana hakuna njia nyingine ya uzimani nje na Bwana YESU.
Ukimkataa YESU na Wokovu wake unakuwa umeukataa pia uzima wa milele.

Bwana YESU ndio anakataza uzinzi na uasherati hivyo ukitii uasherati na uzinzi hakika unajitenga na Bwana YESU mwenye uzima wako wa milele.


Tunasoma katika Biblia kwamba Mke alitoka katika ubavu wa Mume,sasa.
Sasa Leo kama MUNGU akisema. kila ubavu urudi kwenye nafasi yake!
Wewe mume utarudishiwa mbavu ngapi, Wewe unayeoa wake wengi?
Na wewe mke utarudia wapi,wewe uliyeungwa na mume mwenye mke mwingine?

Ni saa ya kutubu na kuokoka.
Mathayo 3:2 '' Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.''
YESU yuko hapo ulipo ili akuokoe, ni kazi yako tu kumpokea na kutubu na kuanza kuishi maisha matakatifu.

dhambi ya uzinzi na uasherati ina madhara mengi sana nje na ziwa la moto.
 Kama uchumba wenu una vita lakini hamjawahi Kuzini naomba endeleeni na maombi lakini kama ni wachumba na mumewahi kuzini basi tambueni kwamba kupitia uasherati wenu huo shetani alipanda magugu ambayo itakuwa vigumu kwenu kuyang'oa. Toba ya kweli inahitajika ila baada ya kuacha uzinifu huo basi basi msirudie tena dhambi hiyo maana mkiendelea shetani atapanda magugu ambayo yatasababisha muachane kwa machungu mengi na maumivu mengi kisha ndio itakuwa
"Nimekusamehe lakini sitakusahau" kumbe dhambi waliyoifuga ndio sababisho.

1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.'

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana

Comments