WAPINDISHA MASHAURI


Na Askofu Mkuu Josephat Gwajima
Matendo ya Mitume 13:36-37 “Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu. Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu.”
Kuna kusudi la maisha yako kama unaishi. Mungu ni Mungu wa kusudi na kila unachokiona kina makusudi yake. Mtu wa Mungu hawezi kufa mpaka atimize lile kusudi alilopewa na Bwana. Unapokuwa ndani ya kusudi lako adui anapiga magoti mbele yako na kukusujudia hatakama adui anatisha sana kama upo ndani ya Mungu huwezi kumwogopa kwasababu unalitimiza kusudi lako. Mungu anakuja kufanya kazi pamoja na wewe pale unapofatimiza kusudi lako na kila atakayeshindana na wewe atakuwa anashindana na Mungu na kamwe hataweza kukushinda.
Wana wa Israeli walipokuwa wanakwenda kwenye nchi ya ahadi njiani walikutana na kabila la Amaleki wakawaomba wapite kwa amani kwenye njia inayopita nchi yao bila kugusa chochote, lakini amaleki walikataa kuwaruhusu wakatoka na majeshi yao ili wawapige Israeli, Israeli waliambiwa na Mungu waende kwenye nchi ya ahadi watakuta asali na maziwa lakini njiani walipigana vita na Mungu hakuwazuia Amaleki pale walipowazuia Israeli wasipite, Mungu hakuwapiga Amaleki kwasababu alitaka awaache Israeli wapigane vita ili waende kwenye kusudi walilopewa na Mungu.
Mungu anapenda watoto wake tupigane vita ili tuelekee kutimiza makusudi yetu, Mungu anaitwa Mungu wa Vita (Kutoka 15:3 Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake.) maana yake sisi hatutapigana vita wenyewe bali Mungu atatupigania.
Israeli walipopigana vita ile na Amaleki Mungu alimwambia Musa apande mlimani na ile fimbo aliyompa. Wakati Musa anainyanyua fimbo yake juu kule mlimani, Joshua na Israeli walikuwa anawapiga Amaleki na kuwashinda.
“Unapoona mahali vita inashinda ujue yupo Musa amenyanyua mikono juu na fimbo yake.”
Pamoja na Mungu kuwa Amewaambia Israeli waende wakamiliki nchi yao lakini njiani walikutana na Amaleki waliowazuia na ilibidi kupigana nao ili wapite kwenda mbele. Mungu anatufundisha unaweza ukawa unaenenda kwenye kusudi lako ukakutana na pingamizi la amaleki njiani usijiulize je ni kusudi la Mungu au sio cha kufanya simama upigane vita utalishinda kwa msaada wa Mungu.
“Bwana akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu.” Kutoka 17:14
“Basi itakuwa, hapo atakapokwisha kukupumzisha Bwana, Mungu wako, katika adui zako wote walio kando-kando, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi uimiliki, ndipo uufute ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu; usisahau. “Kumbukumbu la Torati 25:19
Mungu alitoa amri juu ya Amaleki kwamba kizazi chao chote kifutwe juu ya nchi ili ijulikane kwamba kumpinga aliyetumwa na kuelekezwa kwenye kusudi lake ni kujiangamiza mwenyewe. Wale waliokupinga Mungu atawafuta juu ya nchi kwa jina la Yesu.
Mungu aliinua mtu maalum kwaajili ya kuwaangamiza Amaleki wote na Mfalme wao Hagagi na mifugo yao na mali zao zote kupitia kwa Mfalme Sauli. Sauli alipopewa agizo hilo na Mungu lakini hakufanya kama alivyoambiwa badala yake alichukua mifugo iliyonona ya ngombe na mbuzi pamoja na Mfalme wao.
Baada ya hayo nabii Samweli alimwendea Sauli kumuuliza 'mbona umewaacha mifugo na mfalme Hagagi hai wakati Mungu amekuamuru awaangamize wote?’
“Mungu hataki Mali za aliyekutesa zije zikunufaishe bali anataka uanze mwenyewe ili akubariki na uzidi kustawi na ujue yeye ndiye aliyekuwezesha”
Baada ya hayo yote Nabii Samweli alimwamuru Mfalme Sauli amlete mbele yake mfalme wa amaleki (Hagagi) akamkata kichwa na kumtamkia Mfalme Sauli ‘kama ulivyokataa kuwaua Amaleki Mungu amekuacha kuanzia leo.’
“Ukishindwa kutimiza kusudi lako, maisha yako yatakuwa mafupi sababu Mungu atakuacha”
“Walewale waliokuchelewesha kwenye kusudi lako, waliokutesa,waliokupinga Mungu atawaangamiza wote mbele yako kwa jina la Yesu. Juhudi na mipango ya kujiokoa ya wale waliokuchelewesha igeuke na kuwa laana kwao kwa jina la Yesu. Amen”
Tangu siku ile Mfalme Sauli alipoacha kutumikia kusudi alilopewa na Mungu, Mungu alimwinua Mfalme mwingine aitwaye Daudi ambaye alilitumikia kusudi alilopewa na Mungu mpaka mwisho.
Mungu alipomalizana na Amaleki aliamua kumtafuta mtu mwingine ampe kusudi la maisha yake liwe kuwachinje wafilisti(wapalestina) wote.
Nabii Samweli alienda kwenye nyumba ya Yesse na kuwakuta kaka zake Daudi kina Elishama na watoto wengine wa mzee Yesse lakini wote Mungu hakuwachagua japo walikuwa ni wanajeshi wanazo sifa zote za kupigana vita, Nabii Samweli alimuuliza mzee Yesse hao ndio watoto wake wote lakini Mzee Yesse akamwambia yupo mwingine ambaye kwa muonekano hafai yupo porini anachunga.
“Kusudi lako likianza Mungu atakufuata kokote ulipo ili ulitimize”
Daudi aliitwa akaenda nyumbani. Nabii Samweli alipomwona alimmiminia mafuta na Roho wa Bwana akamshukia saa ileile tayari kutimiza kusudi lake.
“Unaweza ukawa unajiona umefikia mwisho wakutimiza kusudi lako lakini unatakiwa ujue Mungu anajua kusudi lako na litatimia haijalishi umefikisha umri gani, Mungu atakubeba wewe uliocheleweshwa vilevile ulivyo na watoto wako, na familia yako, na mume wako Mungu anakubeba uende kwenye kusudi lako leo kwa jina la Yesu.”
“Sara alipata kusudi lake la kuzaa kwa bila shida yeyote ile japo alikuwa mzee sana, kusudi la Sara lilikuwa kuwa ni kumzaa Isaka ili Yakobo azaliwe yapatikane makabila kumi na mawili ya Israeli. Hata wewe haijalishi umri ulionao utatimiza kusudi lako bila shida yeyote kwa jina la Yesu”
Daudi kusudi lake lilikuwa ni kuwaangamiza wafilisti wote, akaanza kulitimiza kwa kupiga kinanda ili kutoa pepo kwa Mfalme Sauli.
Daudi alipoingia kwenye utawala wa Sauli, kazi yake ya kwanza kweye kutimiza kusudi lake alienda kupigana na Goliath ambaye alikuwa akua akiwatukana Wayahudi kila siku asubuhi na jioni huku akiwadhihaki Wayahudi wamtoe wanajifanya watumishi wa Yehova kumbe ni watumishi wa Sauli basi wamtoe mtu mmoja apigane naye.
Daudi alitumwa kupeleka chakule ndipo akaona jambo hilo na kukereka sana huku tayari alikua ameshapakwa mafuta kwaajili ya kutimiza kusudi lake hilo.
Daudi aliposia maneno yale aliuliza ni nani mtu huyu hata ayatukanaye majeshi ya Bwana akaambiwa ni Goliathi wa Gati mtu wa vita, Daudi akauliza je atapewa nini mtu atakayempiga mtu huyu, akaambiwa atapewa mtoto wa Mfalme awe mke wake, Daudi akaamua kutaka kupigana naye lakini ndugu zake walimwona kama mtu mbinafsi aliyeacha kuchunga kondoo kwa tamaa zake lakini Daudi alitaka kupigana na Goliathi kwasababu tayari alikuwa ameshaanza kutumikia kusudi lake.
“ wale ndugu zako waliokudharau usiwasikilize songa mbele sababu wewe utakuja kuwa kuhani wao kwenye familia yako kwa jina la Yesu”
Daudi alienda kwa mfalme Sauli kujitambulisha ili apigane na Goliathi, kwenye eneo la vita Goliathi alikua na watu wanne wa kumsaidia kubeba Silaha, Daudi yeye alikuwa amebeba mawe matano kwaajili ya kila mmoja wao na hakuna jiwe lililo mkosa mtu hata mmoja.
Goliathi alipomwona Daudi amekuja alimcheka sana na kumdharau kwa kumjia kwa fimbo akidhani yeye mbwa! (inawezekana wakati ule mbwa walikuwa wakipigwa kwa mawe na fimbo) Goliathi alimlaai Daudi na mawe yake kwamba alikuwa ni mtoto mdogo kupigana naye, (Adui anatabia ya kutisha usiogope, waache waandae yale wanayoyaandaa juu yako na waseme yale wanayoyasema wewe simama kwenye kusudi lako usiogope kwasababu Mungu yupo upande wako”.
“Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.” 1 Samweli 17:45-46
Kumbuka Goliathi alikuwa amevaa kichwani kinga ya chuma lakini jiwe la Daudi lilimpiga na kumwangusha chini “Adui zako wanamambo ambayo yanawakinga dhidi yako wewe usiyaangalie hayo simama kwenye kusudi lako utafanikiwa kuwashinda kwa jina la Yesu”.
Baada ya Daudi kumshinda Goliath Mfalme sauli, aliamua kutaka kumwangamiza Daudi akamtuma Daudi kwenda kuwatahiri Wafilisti mia na hamsini na amletee govi zao zote(ili afie huko sababu ilikua si jambo la kawaida) lakini kwenye kuwauwa Wafilisti lilikuwa ndilo kusudi la Daudi, Basi alienda na jioni ile akarudi na kikapu chenye govi za wafilisti kama alivyotumwa na Mfalme Sauli. Daudi akawa anatafutwa ili auwawe lakini hakufa kwasababu kusudi lake lilikuwa bado halijatimia.
“Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli.” 2 Samweli 21:17
“Kila mtu anakusudi lake na kusudi lake huwezi kufa kabla kusudi lako halijakamilika kwa jina la Yesu.”
Unapotembea kwenye kusudi la Mungu huwezi kufa mpaka apatikane mtu wa kupindisha kusudi lako, kama ilivyotokea kwa Mfalme Sauli alishindwa kutimiza kusudi lake Mungu akamuacha.
Daudi alikuwa anamshauri wake aliyekuwa anaitwa Ahithofeli ambaye alikuwa akiongea ni kama Mungu ameongea, mtoto wa Daudi Absalom alimwasi Baba yake ili awe mfalme na Ahithofeli akaungana naye.
“Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili.Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho lake limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.Daudi akamwambia, Ukienda mbele pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu;
lakini ukirudi mjini, na kumwambia Absalomu, Nitakuwa mtumishi wako, Ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako tokea zamani, ndivyo nitakavyokuwa mtumishi wako sasa; ndipo utayavunja mashauri ya Ahithofeli kwa ajili yangu.” 2Samweli 15:31-34
Daudi aligundua kwamba Mwanaye Absalom akipita kwenye kila ushauri wa ahithofeli atafanikiwa kumwangusha, Ndipo Daudi aliamua kumtuma Hushai aende akajifanye naye amemsaliti ili apindishe mashauri yote yatakayotolewa na Ahithofeli.
Wakati ule Absalom akawaita wote waliungana naye ili toe mawazo la kumwangamiza Daudi, Ahithofeli alitoa wazo la kumkimbiza daudi usiku uleule kwa kutumia askari wachache Bila kuungana na Absalom nao wangemshida, lakini Hushai alipoona shauri alilotoa Ahithofeli aliamua kulipinga na kumwambia Absalom shauri la Ahithofeli ni zuri lakini halifai kwa muda ule bali asiende kumkimbiza Daudi kwasababu atakuwa anahasira nyingi naye atawaangamiza, hivyo walale kwanza kesho Absalomu pamoja na askari waungane kamwangamize Daudi wakiwa wameshajipanga tayari, Bahati nzuri Absalom akaona ni kweli shauri la Hushai ni zuri na jema, wapumzike usiku ule kwasababu tayari wameshaiteka Ikulu ya Daudi na asubuhi watakwenda kupigana na Daudi wakiwa wameshajipanga na nguvu nyingi.
Ahithofeli alipoona shauri lake la kumfuata Dadui usiku ule limekataliwa akaenda kujinyonga kwasababu alijua kabisa kwa mashauri ya hushai hawatafanikiwa kumpiga Daudi, alimjua Hushai ni mpindishaji wa mashauri ya Mungu kwasababu alikuwa naye kwa Daudi hivyo anafahamu mashauri yake yote ni ya kupindisha.
Hushai alipoona shauri lake limepita, alimtuma mtu aende kwa Daudi akamwambie alale kwa amani kwasababu ameshaliondoa shauri la Ahithofeli.
“Kila maisha yana hushai wake, ukitaka kufanikiwa ujanja ni kumtambua Hushai wa maisha yako”
Mungu akisimamisha huduma ikatembea kwenye kusudi lake, nchi itatetemeka na itastawi kwasabau kusudi limetimizwa. Hata wewe hautakufa wala hutalala mpaka shauri la Mungu kwenye kizazi chako litimie kwa damu ya Yesu.
Absalom alipoamka alienda kulitumikia shauri lisilo la Mungu na siku ile akashindwa na kufa.
Kwenye maisha yetu kuna makusudi mengi yamepindishwa kwa watu. Wapo wanaotaka kuwa wafanya biashara, waalimu, mawaziri, wakurugenzi n.k wamepindishwa kusudi lao, wapo ambao walitakiwa kuwa maaskofu lakini wamepindishwa na kufungwa kama Yule mtu wa mji wa Dekapoli.
Acha kusikiliza maneno ya watu wewe simama kwenye kusudi lako ukiaibika na upo kwenye kusudi lako wewe simama songa mbele, wakisema hufai wewe simama songa mbele utafika na kufanikiwa kwa jina la Yesu.
Kuna watu wametumwa na shetani kupindisha kesho yako ili uliasi kusudi lako na uangamie, wapo watu maalum ambao kazi yao ni kupindisha shauri la maisha yako wale unatakiwa wwaangushe kwa jina la Yesu.
Mpindisha shauri wa Absalom alikuwa hushai ambaye alijua kwamba shauri lile la Ahithofeli lingetimiza kusudi la Absalom kuua Bada yake Daudi, hata wewe wapo wakina hushai wanaokujaza ndani yako tabia ya hasira ili usifanikishe shauri lako, wapindisha mashauri wanajua njia unayoielekea ni njia ya kufanikiwa wanaamua kukupa tabia ambazo zitakuaharibia watu kesho yako, kuna tabia ya kususa, kukataa, kuzira, uzinzi, uacherati, wivu, umbea n.k hizo zote zinaweza kuwekwa ndani yako ili shauri la kesho yako lisitimie, unaweza ukawekewa mapepo ya tabia mbaya au hisia ambazo zinapindisha kesho yako isitimie kataa tabia hizo kwa Damu ya Yesu.
Hatakama una miaka hamsini au mia Mungu atakukutanisha na kusudi lako. Wa kina Hushai wapo wanaijua kesho yako wapo wanataka kukupindisha njia yako,wewe usiogope njia yako itanyooka kwa jina la Yesu.
Unaweza ukafa moyo kwasababu ya mchumba aliyekuchumbia amekuacha usife moyo Mungu amefanya kazi ya kukupindisha usiolewe naye au usimuowe ili usije ukaolewa/oa mtu mwenye kusudi lisilo la kiMungu akakuharibia, usiogope na kuumia simama usife moyo Mungu atakukutanisha na mtu wa kuungana na wewe utimize shauri la maisha yako, Mungu amekuhifadhia nchi yenye kutiririka asali na maziwa na wale wanaopindisha kesho yako wanajisumbua na wataanguka kwa jina la Yesu.
“Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.” Mithali 8:17
“Mungu kwetu sisi ni Mungu wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.” Zaburi 68:20
“Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Mathayo 2:2
Watu wanapoona nyota yako wanaifuata, shetani anawatuma waganga wa kienyeji na wachawi na wasoma nyota ili waipindishe, hakuna dini inayoweza kumsaidia mtu, hakuna dhehebu linaloweza kumsaidia mtu kinachotakiwa kukusaidia ni maarifa ya kuomba na kuwapiga wale wanakuja kwako kupindisha shauri lako ulilopewa na Mungu kwa jina la Yesu.
Kama umeshamwona hushai kwenye maisha yako hata kama hujafanikiwa bado tayari umeshafanikiwa unachotakiwa kufanya ni mshuhulikia na kesho yako itatimia kama Mungu alivyokupa kwa jina la Yesu Amen.

Comments