ZUIA SAUTI YAKO USILIE, MAANA KAZI YAKO ITAPATA THAWABU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana wetu YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Yeremia 31:16 '' BWANA asema hivi, Zuia sauti yako, usilie, na macho yako yasitoke machozi; Maana kazi yako itapata thawabu, nao watakuja tena toka nchi ya adui; Ndivyo asemavyo BWANA.''

Naomba Neno hili likakutie moyo na kukuimalisha wewe unayemtumikia YESU KRISTO katika kweli yake japokuwa unapitia magumu kwa muda.
Zuia sauti yako usilie na macho yako yasitoke machozi maana kazi yako njema kwa MUNGU itapata thawabu.
Kila Mteule wa MUNGU ni Mtumishi wa MUNGU.
Kila aliyeokolewa na Bwana YESU ni mtumishi wa KRISTO.
Katika utumishi wako sio mara zote utapitia furaha tu, wakati mwingine unaweza kukutana na upinzani unaotoka kwa watumishi wenzako au jamii.
Inawezekana wewe una huduma na huduma hiyo inapigwa vita sana.
Inawezekana wewe ni muimbaji, inawezekana wewe ni mhubiri.
Inawezekana wewe ni mwana maombi au mwinjilisti.
Inawezekana wewe hufanya usafi kanisani au mtoaji.
Inawezekana wewe hukesha kanisani ukiombea kanisa.
Inawezekana wewe unamtumikia MUNGU vyema kabisa lakini hao hao unaotumika nao ndio wako kinyume chako.

Ngoja nikupe mfano; Wamama fulani walikuwa ni kikundi cha maombi kanisani na walikuwa na mikesha ya mara kwa mara wakiombea kanisa, lakini wanakanisa hao hao wanaoombewa kila siku ndio wanatoa kejeli za kila namna kwa wamama wale waombaji.

Mfano mwingine ni huu;
Kuna ndugu mmoja alikuwa ni mgonjwa sana na hata kutembea wakati mwingine alikuwa hawezi, nikawa namkaribisha kanisani maana alikuwa karibu na kanisani kwetu na mimi hupita njia ile kila mara. Baadae yule kijana akaja kanisani na tukawa tunamuombea ili apone na apate kazi. Nakumbuka siku moja mimi Peter nilimsaidia kutembea ili aende mbele ya kanisa kuombewa. Baada ya muda Bwana YESU akamponya ndugu yule na kumpa kazi njema ya kulipwa vizuri sana. Yule ndugu aliendelea vizuri katika Wokovu lakini baada ya mwaka akawa haji kanisani mara kwa mara. Kumbe ameacha wokovu baada ya kupona na kupata kazi nzuri. Muda ukaenda na siku moja mimi nikaandika ujumbe Facebook nikiwaonya watu waache kufanya uasherati maana ni dhambi. Yule ndugu akanitukana sana facebook mbele ya watu na kunisema vibaya mambo ambayo hata siyajui, Nilihuzunika sana na kubaki nashangaa. Yeye alidhani nimemwandika yeye kumbe hata sijui kama inamhusu na sikujua kama na yeye yuko katika mambo hayo, maana mimi ni utaratibu wangu kuhubiri mtandaoni. Kuna watu walinitafuta kwa sms wakiniomba niwasaidie na kuwashauri jinsi ya kujitenga na uasherati, niliwasaidia lakini huku nikibaki nimeduwaa sana kwa ajili ya yule ndugu ambaye aliamua kupolomosha matusi mengi sana kwa kunionea kabisaaa.
Ndugu yangu inawezekana katika huduma yako wewe unapitia magumu mfano wa hayo niliyokuambia.
Inawezekana watu wanakudharau kwa sababu tu umeokoka peke yako katika familia yenu au ukoo wetu.
Inawezekana wewe ukiimba ili kumtukuza MUNGU maana huduma yako ni uimbaji basi watu hukudharau sana kwa sababu ya huduma yako hiyo.
Inawezekana wewe kwenye huduma yako unapingwa sana bila hata sababu za msingi.
Inawezekana wewe huduma yako inapuuzwa sana tena na wapendwa kabisa.
Inawezekana wewe huduma yako japokuwa ni njema sana lakini ndio inayoongoza kwa kudharauliwa kanisani kwenu.
Ndugu naomba nikutie moyo kwamba, zuia sauti yako usilie maana kazi yako itapata dhawabu kwa MUNGU.
Kuna kwaya fulani hapa Dar walikuwa ni vijana tu wasio na elimu na wa kawaida sana ila walikuwa na juhudi sana katika kumtumikia MUNGU. Siku moja mama mmoja mgeni kutoka mbeya akaabudu kanisani kwao huku anauguza mumewe Mhimbili Hospital. Bahati mbaya yule mgonjwa akafariki na huyu mama akawa hana msaada lakini wanakwaya wale walijitolea kumfariji huyu mama katika msiba wa mumewe na wakasafiri naye hadi mbeya kuzika. Baada ya kuzika wale wanakwaya wakamuaga yule mama ili warudi Dar. Yule mama akawaita na kuwauliza kama wana kazi. Wote wakasema hawana kazi. Kisha akawaambia kila mmoja aseme anataka MUNGU ambariki kazi gani, wakataja kisha akamshukuru MUNGU yule mama na akawaambia mwaka huo huo wote watapata kazi nzuri za kuajiriwa zenye mishahara mizuri. Waimbaji wale wakarudi Dar es salaam na Baada ya miezi Saba kupita wale vijana kwaya nzima walikuwa wamepata kazi nzuri ya kuajiriwa japokuwa wengi walikuwa ni darasa la saba na form four iliyofeli. Kila mmoja alipata kazi yenye mshahara zaidi ya laki 4. Hiyo ni dhawabu kutoka kwa MUNGU kwa kwasababu ya utumishi.
Nimewahi kushuhudia waimbaji wakialikwa wakafanye huduma ya siku moja na kupewa zawadi ya gari la thamani zaidi ya milioni 25. Hiyo ni thawabu kutoka kwa MUNGU.
Nilipotaka kufunga ndoa mwaka 2014 niliwajulisha marafiki zangu mtandaoni kwamba namshukuru MUNGU maana naenda Mwanza kufunga ndoa, lakini baadhi ya marafiki zangu hao walinitumia jumla laki saba na nusu nikabaki namshukuru MUNGU kwa ajili yao kila siku. Hiyo ni thawabu kutoka kwa MUNGU.
Zuia sauti yako usilie na macho yako yasitoke machozi maana kazi yako itapata thawabu.
Wakati mwingine MUNGU anaweza hata kuiamuru baraka yako ikatoka kwa maadui zako au waliokupinga sana
Watumishi wa MUNGU wengi tu walipingwa lakini hawakupunguza spidi ya kumtumikia MUNGU.

Ona Mfano huu juu ya waliokuwa wanampinga Nabii Yeremia
Yeremia 18:18-23 '' Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. Niangalie, Ee BWANA, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.Kwa sababu hiyo, uwatoe watoto wao waone njaa, uwatoe nguvu za upanga ziwapate; wake zao wafiwe na watoto wao, na kufiwa na waume zao; wanaume wao wauawe, na vijana wao wapigwe kwa upanga vitani. Kilio na kisikiwe kitokacho katika nyumba zao, hapo utakapoleta kikosi juu yao kwa ghafula; kwa maana wamenichimbia shimo waninase, nao wameifichia miguu yangu mitego. Lakini wewe, BWANA, unajua mashauri yao yote juu yangu, ya kuniua; usiwasamehe uovu wao, wala usifute dhambi yao mbele za macho yako; bali wakwazwe mbele zako; uwatende mambo wakati wa hasira yako.''

Yeremia kama mfano wa waliookoka alikuwa anapingwa kama wewe mteule wa MUNGU unavyopingwa.
Watu wabaya walipanga kumpiga Yeremia kwa ndimi zao kama watu wanavyokunenea mabaya wewe .
Watu wanaweza kukupinga sana kwa sababu tu unafanya vyema kwa MUNGU na unatenda vyema katika utumishi aliokupa katika kanisa lake.
Ndugu, shinda vikwazo vyote na ongeza juhudi zaidi katika kumtumikia Bwana YESU.


Zuia sauti yako usilie maana kazi yako itapata dhawabu kwa MUNGU.
Sikukatazi kulia bali ondoa ule uchungu moyoni unaosababishwa na watu kukuharibia spidi yako ya kumtumikia MUNGU.
Kazi yako katika KRISTO itapata tu thawabu, endelea kumtumikia yeye na kumtukuza yeye tu maana kazi yako katika yeye Bwana YESU ina malipo duniani hapa hapa na malipo makubwa zaidi ni uzima wa milele.
Sio wewe mteule ndio wa kwanza kupingwa bali mitume na manabii walipingwa sana lakini walisonga mbele sana maana walikuwa wanamwangalia aliyewapa kazi ambaye ni MUNGU tu.
Kazi ya MUNGU ina thawabu kwa washindi.
Thawabu maana yake ni Malipo mema ambayo mteule wa KRISTO atayapata kutoka kwa MUNGU baada ya kutii maagizo yake.
Kazi yako katika Bwana YESU inaweza kupingwa lakini mwangalie aliyekuita na kukuokoa na kukupa kazi katika kanisa lake. Angalia thawabu utakayopewa na MUNGU na sio kuangalia wanaokupinga.

1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

Ndugu, Imarika zaidi kila leo katika Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.
Usikubali kutikiswa na watesi wako kila mara bali endelea mbele kwa maombi na utakatifu.
Zidi sana kufanya kazi ya MUNGU na timiza kusudi la MUNGU na kuitwa kwako katika Wokovu na Kanisa.
Ongeza juhudi katika utumishi wako kwa Bwana YESU maana kazi yako si bure.
Biblia inaposema kwamba kazi yako si bure katika Bwana YESU maana yake kazi yako ina malipo mema kutoka kwa MUNGU.
Ndugu yangu Mche MUNGU na endelea kufanya kazi yake ya injili.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili

Comments