BARAKA NA ULINZI JUU YA BARAKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU la ushindi kwetu.
Hesabu 6:24-26 '' BWANA akubarikie, na kukulinda; BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.''

Katika maandiko haya tunaliona agizo la MUNGU kwa Musa na Musa aliamuriwa awafundishe makuhani ili Makuhani hao wawafundishe watu wa MUNGU wote ili wajue kutembea katika baraka za MUNGU na baraka hizo zidumu.
Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kwamba maneno hayo ni muongozo wa baraka za MUNGU na juu ya kuzilinda baraka hizo ili zidumu.
MUNGU kukubariki sio kazi kubwa na wala sio tatizo kabisa, lakini unaweza ukaishiwa baraka hiyo uliyoiomba kwa MUNGU kwa sababu tu umesahau kumuomba MUNGU ailinde baraka yako aliyokupa.
Damu ya YESU siku zote ipo tayari kulinda baraka yako ila mpaka uombe.
Jina la YESU lipo tayari kuwa ulinzi katika baraka yako ila ni mpaka uombe kwanza.
Ufunuo huu ni muhimu kuufahamu na kuuzingatia kwamba; ukiomba baraka kwa MUNGU basi omba pia ulinzi wa MUNGU kwenye hiyo baraka yako.

Zaburi 121:7 ''BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.''
Ni kweli kabisa MUNGU atakulinda na mabaya yote lakini mpaka umuombe ili akulinde.
Ni hadi umuombe ili ailinde baraka yako ndipo atailinda.
Kama ulivyomuomba MUNGU baraka basi muombe pia na ulinzi kwa kiwango hicho hicho cha kuomba baraka.
Kumbuka kwamba muujiza wowote uliopatikana kwa maombi, muujiza huo  utalindwa pia kwa maombi, zingatia hilo itakusaidia sana.

Hesabu 6:25 ''BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;''
Katika baraka akupayo MUNGU hakikisha pia unamuomba MUNGU aambatane na wewe na kukufadhili, usipofanya hivyo kuna baadhi ya baraka zinaweza kuja kwako na kuyeyuka kwa sababu wewe hujataka MUNGU aambatane na wewe katika baraka hiyo uliyoomba na amekupa.
Mfano unaweza ukamuomba MUNGU akupe Mchumba  na ukafunuliwa kabisa kuhusu huyo Mchumba na ukamjua, lakini kama MUNGU hatakuwa na wewe mchumba huyo anaweza akakukataa siku ukimwambia.
Unaweza ukaomba MUNGU akupe huduma kubwa lakini kama MUNGU hatakufadhili utashindwa kuiendesha huduma hiyo, kama MUNGU hatailinda hiyo huduma yako hakika haitadumu.
Ndio maana Biblia ikatoa  Kanuni  kwenye maandiko tuliyoanza nayo ya kwamba kama ukiomba MUNGU akubariki basi omba pia MUNGU akulinde na ailinde baraka yako ndio maana ya Hesabu 6:24 ''BWANA akubarikie, na kukulinda  ''

 Ukiomba tu kubarikiwa ukasahau kuomba  kulindiwa baraka yako hakika wakati mwingine baraka hiyo inaweza kuyeyuka hata ukadhani hukupewa na MUNGU kumbe wewe ulisahau Kanuni ya baraka na ulinzi juu ya baraka.
Kwanini  ''BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;-Hesabu 6:25''
 Ni kwasababu MUNGU akikufadhili watu watamuona MUNGU kabla ya kukuona wewe.
Akikufadhili MUNGU  maadui zako watakutana na moto wa MUNGU kabla ya kukufikia wewe.
Akikufadhili MUNGU watu wakipanga kukuabisha wataabika wao na sio wewe.
Usiishie kumwambia MUNGU akubariki tu bali mwambie akulinde pia na kuilinda baraka yako.
Mwambie MUNGU akubariki na kukufadhili.
Ni muhimu sana nuru za uso wa MUNGU ziambatane na wewe.
Musa kwa kujua umuhimu wa nuru za uso wa MUNGU kuambatana nae basi alimwambia MUNGU maneno haya;
'' Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.-Kutoka 33:15''

Omba MUNGU akubariki lakini pia omba MUNGU aambatane na wewe kwenye baraka yako hiyo.

Pia omba MUNGU ailinde baraka yako maana kukupa baraka ni jambo tofauti na kuilinda baraka yako.
Kuna wanandoa waliomba MUNGU awape mtoto. Ni kweli MUNGU akalifungua tumbo tasa na wakafanikiwa kupata mtoto kama walivyoomba. Wao wakasahau kuombea baraka yao waliyopewa hivyo baada ya muda kadhaa mtoto yule akafariki. Iliwasumbua sana lakini ni kwa sababu waliomba baraka wakapewa lakini wakasahau kuomba ulinzi juu ya baraka yao. Ndio maana hiyo kanuni ya baraka za MUNGU katika Hesabu 6:24-26 ni ya muhimu sana kwa kila mtu.
Ndugu yangu hakikisha MUNGU anakubariki kwa kupitia maombi yako na utakatifu katika KRISTO lakini pia usisahau kumuomba MUNGU ailinde baraka yako hiyo na usisahau kumwambia MUNGU aambatane na wewe katika baraka yako hiyo.

Kuna mtu aliwahi kuomba apewe Mchumba na MUNGU akampa lakini siku chache baada ya kufunga ndoa mwenzi wake akafariki. Yule ndugu alilia sana na kudhani kwamba hakupewa na MUNGU na wakati mwingine ilimchanganya sana. Ndugu zangu ni muhimu sana kumuomba MUNGU akubariki lakini pia omba MUNGU ailinde baraka yako.
Unaweza ukafunga na kuomba ili Bwana YESU akubariki gari unapewa gari na siku chache baadae gari ile inapata ajali na kuharibika utapata faida gani?
Ndugu omba kwa MUNGU ili akubariki lakini omba pia MUNGU akulinde na ailinde baraka yako, omba MUNGU aambatane na baraka yako hiyo na akufadhili ndio utastawi sana.

Kuna watu hufunga na kuomba ili MUNGU awabariki jambo fulani lakini baada ya kubarikiwa huacha na wokovu na ndio maana wengi sana katika hao huja kujuta na kulia baada ya ulinzi wa MUNGU kutokuwepo katika baraka zao.
Ndugu usiombe upewe ndoa kisha ndoa hiyo iwe mwiba kwako kwa sababu tu hukumwambia MUNGU ailinde na amlinde mwenzi wako.
Ndugu usiombe MUNGU akupe kazi na kisha kazi hiyo ikawa tanzi kwako hata ukajikuta badala ya kumtumikia MUNGU, wewe kupitia kazi yako unamtumikia shetani, kwa sababu tu ulishindwa kufuata kanuni ya baraka za MUNGU kwamba ukiomba kubarikiwa basi omba pia ulinzi wa kiMUNGU juu ya baraka hiyo na omba MUNGU aambatane na wewe katika baraka yako hiyo, omba Bwana YESU akufadhili katika mambo  yote ndipo baraka yako itakuwa njema na katika uzuri.
Yusufu yeye alifanikiwa sana kwa sababu MUNGU alikuwa naye, MUNGU alimfadhili na MUNGU alimpa kibali.
Mwanzo 39:21 ''Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.''

Ndugu yangu hakikisha MUNGU anakuwa pamoja na wewe katika baraka yako atakayokupa.
Jinsi ya MUNGU kuwa pamoja na wewe ni kuishi maisha matakatifu na kuitii sauti yake daima.
Hakikisha MUNGU anakufadhili maana yeye fadhili zake ni za milele kwa wanaomtii na kunyenyekea kwake.
Zaburi 107:1-2 ''Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.''

Hakikisha ndugu unakuwa na kibali cha MUNGU.
Kama huna kibali cha MUNGU hata kazi uitakayo hutapata hata kama vyeti vyako ni vizuri.
Kama huna kibali cha MUNGU hata mchumba wako kutoka kwa MUNGU anaweza akakukataa hadi ukashangaa.
Omba MUNGU akubariki na omba MUNGU ailinde baraka yako na tena omba MUNGU aambatane na wewe katika baraka hiyo.
Katika maandiko yetu ya kanuni za baraka za MUNGU mstari wa 26 wa hiyo Hesabu 6 unasema ''BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.''

 Katika maombi yako usiishie tu kumwambia MUNGU akubariki bali ni muhimu sana ukaambatanisha na amani ya MUNGU.
Amani ya MUNGU ni muhimu sana.
Hata kama utabarikiwa lakini bila amani ya MUNGU juu ya baraka hiyo hakika hutafanikiwa.
Omba MUNGU akupe amani katika baraka yako hiyo.

 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.


Comments