CHIMBUKO LA UTATA WA MIGONGANO YA TAFSIRI YA BIBLIA-3

Na Askofu mkuu Siliyvester Gamanywa.


Wakati ninajiandaa kuhitimisha mada hii katika toleo hili kwenye ukurasa huu; ninapenda kuitambulisha kwako “nadhari mpya ya theolojia” ambayo sikuitaja hapo awali. Nadharia hii imepata umaarufu hivi karibuni kwa mkazo wake wa kuzisahihisha nadharia kongwe mbili zilizotangulia kuwepo. Kabla ya majumuisho yangu naomba tuipitie kwa muktadha wa nadharia mbili ambazo tayari tumezigusia kwenye makala zilizopita.
NADHARIA MPYA INAYOSHINDANA NA NADHARIA ZA DP NA CT
‘Nadharia Mpya ya Agano’ (New Covenant Theology-NCT) ni theolojia mpya ya Kikristo inayoitafsiri Biblia kwa kuzingatia Nafsi na kazi ya Yesu Kristo kuwa ndio msingi mkuu katika Biblia. Sheria za Agano la Kale zimebadilika au kufutwa na kifo cha Yesu msalabani na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na sheria ya Kristo ya Agano Jipya. Hii ‘Nadharia Mpya ya Agano’(NCT) inafanana kwa baadhi ya maeneo lakini ni tofauti na nadharia kongwe za ‘Nadharia ya Mpango’ (DT) na ‘Nadharia ya Agano’(CT)
Mtindo na mbinu za kuitafsiri Biblia za watheolojia wa NCT ni kulifanya Agano Jipya litoe tafsiri ya Agano Kale. Tunajifunza yaliyomo katika Agano la Kale kwa tafsiri iliyomo katika Agano Jipya. Agano la Kale haliwezi kulitafsiri Agano Jipya kwa sababu lenyewe ni kivuli tu cha Agano Jipya.
MISINGI 6 YA NADHARIA MPYA YA AGANO(NCT)
1. Mpango mmoja wa Mungu unaomlenga Yesu Kristo
NCT inaamini ya kwamba katika Biblia nzima kuna mpango mmoja wa Mungu ambao mlengwa wake mkuu ni Yesu Kristo. Na mpango huu ulitarajiwa kutimilizwa ndani ya Yesu Kristo katika Agano Jipya. (Efe.1:8-10). Wakati ambapo ‘Nadharia ya Agano’ (CT) hutafsiri kuwa ni ‘agano la neema’; hii nadharia ya NCT yenyewe hupinga ikisema hakuna ushahidi wa kibiblia wa unaotaja kuwa ‘agano la neema’ linajumuisha maagano yote ya kibiblia. NCT inakazia kwamba kila agano lazima litazamwe katika muktadha wa upekee wake na ni kwa jinsi gani unachangia mengine kwa jumla.
2. Agano la Kale lazima litafsiriwe katika mwangaza wa Agano Jipya
NCT inasisitiza ya kwamba Agano la Kale lazima lisomwe na kutafsiriwa kwa mwanga wa utimilifu wa Agano Jipya katika Yesu Kristo. (Ebr.1:1-2) Kupitia NCT tunajifunza jinsi ya kutafsiri Agano la kale kutoka kwa Yesu na mitume wake.
3. Agano la Kale lilikuwa la mpito
Sehemu ya tatu inayoifanya NCT kuwa tofauti na nadharia nyingine ni mtazamo wake kuhusu Agano la Kale kwa kulitafsiri kuwa lilikuwa ni la mpito huku likisubiriwa Agano Jipya ambalo mpango wa Mungu ungetimizwa kikamilifu.
NCT inasimamia maandiko yenye kuonyesha kwamba walio ndani ya Kristo hawapo chini ya sheria tena. (1 Kor. 9:20, 2 Cor. 3, Rum. 6:14, 7:6, Gal. 3:23, 5:18, Ebr. 8). Na kitabu cha Wagalatia kiko wazi zaidi kuhusu hoja hii. “Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.” (Gal.3:23) “Lakini mkiongozwa na Roho hampo chini ya sheria.” (Gal.5:18)
4. Hakuna mgawanyiko wa makunda matatu ya sheria katika torati
Nadharia ya Agano (CT) huigawa torati katika makundi matatu yafuatayo: kimaadili (Moral), kijamii (Civil) na kiibada (ceremonial). ‘Nadharia Mpya ya Agano’(NCT) inakanusha ikisema katika Agano la Kale na sheria zake vimewasilishwa kama katiba moja bila migawanyiko na hakuna ushahidi wa kibiblia wenye kuanisha migawanyiko kati yake.
NCT inasisitiza kwamba Musa aliwasilisha torati nzima kama ilivyoandikwa: “Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyonena BWANA tutayatenda.” (Kut.24:3) na mahali pengine imeandikwa: “Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, hayo yote aliyonena BWANA tutayatenda, nasi tutatii.” (Kut.24:7)
Na kwa habari ya kushika Sabato NCT inasema Agano Jipya limetoa tafsiri kama ifuatavyo:“Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.” (GAL. 4:9, 10); “Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.” (RUM. 14:5); “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” (KOL. 2:16-17)
5. Hatuko chini ya Torati ya Musa; bali chini ya Sheria ya Kristo
Kama hatuko chini ya sheria maana yake hatuna sheria kabisa? Jibu lake ni hapana. Ila hatuko chini ya Sheria za Musa, na badala yake tuko chini ya Kristo. Hata hivyo msamiati wa Sheria ya Kristo unapatikana sehemu moja katika Wagalatia 6:2: “Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.”
Isipokuwa nukuu muhimu ya nadharia ya NCT ni ile iliyoanndikwa katika 1 Wakorintho 9:20-21) “Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. (1 KOR. 9:20-21) Vifungu hivi vinajitosheleza katika kufafanua uwepo wa sheria ya Kristo katika Agano Jipya ambayo si sheria ya torati ya Musa wa Agano la kale.
6. Jamii nzima katika Agano Jipya imempokea Roho Mtakatifu
Msingi wa sita wa NCT ni imani yake kuhusu asili ya jamii ya Agano Jipya. Tofauti na wakati wa Agano la Kale, kila mwamini amezaliwa upya kiroho na kupewa Roho Mtakatifu. Manabii wa Agano la Kale walisubiria kwa hamu kushuhudia wakati ambapo Mungu atamshusha Roho Mtakatifu kutoka mbinguni (Eze. 36-37, Yo 2, Isa. 32:15, 44:3). Na hii ndiyo tofauti mojawapo kubwa kati ya Israeli asilia na kanisa.
NCT haikubaliani na CT inayoamini Israeli ni sawa na Kanisa. Wala haikubaliani na DT inayoamini Israeli na kanisa havina uhusiano. NCT inamlenga Kristo ambaye ni kiunganishi mwenye kutambua vyote Israeli na kanisa. Waamini wa Agano Jipya wanamekuwa uzao wa Ibrahimu kwa njia ya Yesu Kristo
MAJUMUISHO KUHUSU NCT
Kwa mujibu wa ‘Nadharia Mpya ya Agano’ (NCT) hakuna ‘Agano la Matendo’ (Covenant of Works) ambalo lilifanywa kwa Adamu. Biblia haitaji kitu cha namna hii. Wala hakuna kitu kama ‘Agano la Neema’ (Covenant of Grace) linalojumuisha maagano yote mawili ya Agano la Kale na Agano Jipya kwa wakati mmoja, na Mungu kutuachia tumefungwa kwenye sheria za kimaadili za Agano (Moral Law). Hatuwezi kuondoa sheria zote za kiibada (ceremonial laws) kutoka kwenye sheria za Agano la Kale, na tukaamua kuendeleza sheria za kimaadili (moral laws) kama tupendavyo. Kwa mantiki hii, sheria zote za Agano la Kale zimetimilizwa katika Agano Jipya.
Kwa hiyo, NCT inatafsiri ya kwamba Agano Jipya limetilimiliza na kuchukua nafasi ya Agano la Kale lote, na kuzifanya sheria zote za Agano la Kale kutokuwabana waamini wa Agano Jipya, kwa mantiki ya kwamba zimekwisha kutimilizwa katika Agano Jipya. Tofauti kubwa kati ya maagano haya mawili ni kwamba, uhusiano wetu na Mungu katika Agano Jipya, Mungu mwenyewe ameziandika sheria zake mioyoni mwetu. Na kwa kuwa Mungu mwenyewe ndiye ameandika sheria yake mioyoni mwetu kwa muujiza wa kuzaliwa mara ya pili katika roho na mchakato wa kutufundisha tunaweza kutimiliza sheria kutokea rohoni mwetu.
Mpaka hivi sasa, ‘Nadharia Mpya ya Agano’ (NCT) inaonekana kupokelewa kama mafundisho ya kweli ya kibiblia na wafuasi wa Calvin (Calvinists) kuliko ‘Nadhari ya Aano’(CT) ambayo ilipata umaarufu wake tangu karne ya 17.
MSIMAMO WANGU BINAFSI KUHUSU NADHARIA ZOTE 3
Nimetumia muda kuelezea shule za nadharia tatu kwa makusudi mema ya kuonesha ya kwamba migongano ya kitheolojia inayooendelea hivi sasa katika jamii ya Kristo ulimwenguni inatokana na nini. Kwa upande wangu najua kila nadharia inayo mambo sahihi ambayo yanafaa kujenga imani yetu. Hata hivyo, kigezo changu cha kukubali au kukataa mawazo ya nadharia hizi ni “tafsiri sahihi ya kibiblia” ambayo ndio mwongozo wangu. Ninajua kuna maandiko yanayotafsirika kwa mtindo wa mifano, na maandiko yanayotafsirika kwa mtindo wa uhalisia.
Lakini kinachotakiwa kuzingatiwa ni “usahihi wa tafsiri husika kwa maandiko husika kwa mujibu wa lugha za kibiblia.” Ninakubaliana na “Nadharia ya Agano” (CT) kwa 15%, na ‘Nadharia ya Mpango’ (DT) kwa asilimia 30%, na ‘Nadharia Mpya ya Agano’ (NCT) kwa 45% na ninabaki na 10% ambazo ni yale ambayo hayajaguswa na nadharia zote 3. Katika makala zijazo nitazielezea hoja ambazo hazijazingatiwa katika nadharia zilizopo hizi leo.

Comments