HII NDIO MISINGI SABA(7) YA NDOA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

HII NDIO MISINGI SABA(7) YA NDOA

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ndoa nyingi hazisomeki kwa sababu hazina YESU hivyo ndivyo naweza nikaanza kusema leo.
Hakuna raha kama kumfahamu MUNGU aliye hai na kumtegemea.
Ukimfahamu MUNGU aliye hai hutaogopa wala kuwahofia wanadamu.
Ukimfahamu MUNGU aliye hai na kumtegemea hutawaogopa wachawi wala majini.

 Uzima wetu uko mikononi wa MUNGU wetu, tusonge mbele na Wokovu wa KRISTO hakika kuna kunashinda
Kumbuka kwamba adui naye hutaka ubia katika ndoa yenu lakini mnaweza kumshinda tu kama mtamtii MUNGU.

 Katika ndoa kuna mambo mengi sana. 
Ingawa ni kweli kabisa kwamba baba ni kichwa cha familia lakini ni muhimu pia kujua kwamba mama ni moyo ya familia.
Ukiuona moyo haufai kwa sababu wewe ni kichwa basi tambua pia kwamba kichwa bila moyo hakiwezi kufanya lolote.
Ukikiona kichwa hakifai kwa sababu tu wewe ni moyo tambua kwamba bila kichwa wewe huwezi kwenda.

 Haki sawa kwa wote ni jambo ambalo wanandoa wengi hasa kinamama hulidai sana . mimi niseme hivi; Haki sawa kwa wote katika ndoa ni jambo jema na linaloondoa utumwa ila inatakiwa ijulikane kwamba haki sawa hiyo sio uongozi wala Mali Bali ni utakatifu sawa katika ndoa, yaani kila mmoja akae kwenye utakatifu kama Neno la MUNGU linavyoagiza. 
Haki sawa kwa wote sio Kibiblia ila ni kibinadamu.
Hayo ndio naweza nikasema juu ya haki sawa katika ndoa. Sio baba chapombe na mama ndio mlezi wa watoto, hapo hakuna haki sawa. Sio baba anashughurikia matibabu ya watoto huku mama yuko kwa jirani anapiga umbea, hapo hakuna haki sawa. Haki sawa kwa wote ni kutenda matenda mema kwa wote na mambo hayo yawe yanampendeza MUNGU wa mbinguni.
 
Baada ya kusema hayo sasa naomba tuingie katika Misingi saba ya ndoa kwa mjibu wa mimi Mwinjilisti Peter.


MISINGI YA NDOA NI;

1. Uaminifu kwa wanandoa.

 2 Kor 8:21 ''tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za BWANA tu, ila na mbele ya wanadamu.''

 Uaminifu kwa wanandoa ndio msingi mkuu sana wa ndoa kustawi.
Kama hakuna uaminifu katika ndoa basi hapo hakuna ndoa ila kuna ndoano tu.
Uwe  mwema si kwa MUNGU tu bali hata kwa wanadamu akiwemo mwenzi wako wa ndoa.
Tuwe waaminifu kwanza sisi ndipo tumuombe MUNGU wetu awafanye na wengine wawe waaminifu. 
Uwe mwaminifu kwanza wewe mama ndio upate kumuombea mumeo ili awe mwaminifu. 
Uwe mwaminifu kwanza wewe baba ndipo upate kumuombea mkeo ili awe mwaminifu. 
Uwe mwaminifu ndugu yangu ndipo umwombee mchumba wako ili naye awe mwaminifu. 
Uwe mwaminifu kwanza wewe binafsi ndipo uweze kuwaombea na wengine wanaokuhusu ili wawe waaminifu. 
Uaminifu ni vazi jema ambalo anatakiwa kulivaa mteule wa MUNGU siku zote. 
Uwe mwaminifu na ishi maisha ya uaminifu siku zote. 
Uwe mwaminifu katika mema tu yanayompendeza MUNGU Muumbaji wako. 
Umekuwa mwaminifu sana kwa shetani kwa miaka mingi lakini Leo nakushauri anza kuwa mwaminifu kwa KRISTO YESU mfalme wa uzima na utapata uzima wake.
 Wakolosai 3:9 '' Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;''

2. Kumcha MUNGU na kuwajibika kwa MUNGU.

Zaburi 34:9 ''Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.'' 
 
 MUNGU ni wa wote hivyo wanandoa wote mnatakiwa kumcha MUNGU na kumwabudu katika roho na kweli.
Sio Mama tu ndio mcha MUNGU huku baba kazi yake ni kumtumikia shetani.
 Sio baba tu ndio mcha MUNGU huku mama ni machawi.
Kumcha MUNGU na kuwajibika kwa MUNGU ni msingi mkuu wa ndoa yenu, shikeni hilo na ndoa yenu itaitwa paradiso ndogo.
Kama wanandoa mnapaswa sana kumcha MUNGU maana hiyo ndio italeta afya ya ndoa yenu.
Kuna Faida kubwa sana kudumu katika MUNGU mkiwa na watoto wenu na wapendwa wenu maana kudumu katika Wokovu wa KRISTO ni kupalilia taji ya uzima na kuwafanya watoto wako kumcha MUNGU aliye hai na jambo hilo kuwa baraka kwao na kwa MUNGU na kwa familia pia. 

3.Maombi.

 Maisha ni maisha ya Mkristo.
Maombi ni msingi mkuu wa ndoa.
Maombi ndio mkono mrefu kuliko yote wa kupokea ushindi kutoka kwa MUNGU.
Wanaondoa wengi hushindwa kutambua jambo hili kwamba muujiza ambao ulipatikana kwa maombi unatakiwa pia muujiza huo utunzwe kwa maombi. Matatizo mengi ya ndoa wakati mwingine hutokea kwa sababu muujiza Wa kupata mke au mume haukuutunza
Hii ni kanuni ya kibiblia kwamba ukipewa muujiza na MUNGU kupitia maombi yako unatakiwa kuutunza muujiza huo kwa maombi vilevile. 
 Waefeso 6:18 ''Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika ROHO, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;''

Kumbe maombi ni muhimu sana.
Kumbe kuombea wengine ni muhimu sana na kumbe  kuombea watakatifu wengine akiwemo mwenzi wako wa ndoa ni nmuhimu sana.
Huwezi kupewa ndoa kisha usiiombee ndoa hiyo harafu matatizo yasitokee.
Unaweza ukaanza kuwaza labda hukupewa baraka hiyo na MUNGU, kumbe ulipewa na MUNGU ila umesahau kwamba muujiza uliopatikan kwa maombi huwa pia unatunzwa kwa maombi. 
Ukiomba upewe mtoto haina maana kwamba ukipata mtoto basi unaacha kumuombea mtoto, ukifanya hivyo unaweza ukamkosa huyo mtoto na kudhani kwamba hukupewa na MUNGU kumbe umesahau jinsi ya kuutunza muujiza wako kwa maombi maana muujiza huo uliupata kupitia maombi
 Marko 11:24 ''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''

4. Kuvumiliana.

Waefeso 4:2-3 ''kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. ''

Wakati mwingine  kukwazana katika ndoa hutokea, iwe kwa bahati mbaya au kwa sababu zingine, lakini uvumulivu ni msingi muhimu wa ndoa kudumu katika uhai wake.
Kuna ndoa zingine kitendo cha baba kufukuzwa kazi au kusimamishwa kazi ndio na ndoa inaingia katika migogoro mibaya.
Ndugu zangu haitakiwi kuwa hivyo, ni heri kuvumiliana maana sio lazima kesho iwe kama ilivyokuwa leo.
Hata kama kwa bahati mbaya mmefilisika mnatakiwa kuendelea kupendana na kuvumiliana maana mkimuomba MUNGU kesho njema itakuja tu.
Sio kwamba mama kwa sababu hana uzao basi hiyo ndio iwe nafasi ya baba kumpiga mama na kumsaliti, haitakiwi kuwa hivyo. Wanandoa ni muhimu sana mkavumiliana huku mkimuomba MUNGU maana yeye ni mwaminifu na wa  haki atawabariki tu tena.
Kuvumiliana ni msingi thabiti sana wa ndoa kudumu katika furaha na amani.

5.Kusaidiana kiroho na kimwili.


Wagalatia 6:1-3 ''Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya KRISTO. Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.''

Mwanandoa kumsaidia kiroho mwenzi wako hakika utakuwa unapanda jambo jema sana ambalo litafuta kusalitiwa baadae maana mtu akiwa na hofu ya MUNGU hakika hawezi kukutenda mabaya.
Kila mtu ana madhaifu yake hivyo ni muhimu pia kubebeana mzigo kwa upendo.
Kama mzigo ni dhambi basi usimbebee mwenzi wako bali mshauri kurudi kwa KRISTO kwa toba lakini madhaifu mengine ya kawaida ni muhimu sana mkabebeana mizigo hiyo.
Baba mmoja mwanandoa alikuwa mpole na asiyependa kuongea ongea. Kipindi ambacho alitakiwa kuongea sana hasa mbele za watu mke wake alikuwa akimsaidia kwa haraka sana na huwezi kujua kama anamsaidia, huko ni kuchukuliana mizigo.
Mama anaweza kuwa hayuko katika kutaka kufanya tendo la ndoa, ni kazi yako baba kumtia moyo na kumvumilia maana kuna kesho pia, sio lazima leo hivyo ndivyo kuchukuliana mizigo.
Kuna baadhi ya ndoa mama akiumwa hiyo ndio inakuwa nafasi ya baba kumsaliti, huo ni  ushetani mkubwa. Kumbuka kuna leo na kesho hivyo ni muhimu sana kubebeana mizigo kwa upendo.
Saidianeni kiroho na kimwili maana huo ndio msingi wa ndoa njema.
Mama mhimize mumeo kwenda kanisani na Baba mhimize mkeo kwenda kanisani maana Neno la MUNGU mtakalojifunza ibadani kanisani litawasaidia kiroho na kuisaidia ndoa yetu.

6. Kupendana.


1 Petro 4:8 '' Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.''

Mama, kwa sababu umekubali huyo baba akuoe basi naamini ulimpenda ndio maana ukamkubalia. Upendo huo huo wa mwanza unatakiwa kuwepo siku zote katika ndoa yenu.
Baba, kwa sababu huyo mama ndio uliomuona ni mrembo kuliko wote duniani na ukamchagua awe mke wako basi upendo huo wa mwanzo unatakiwa uwepo siku zote za kuishi kwenu duniani.
Upendo husitiri madhaifu.
Upendo ni msingi mkuu wa ndoa yenu, ishini kwa kupendana na mtastawi sana.
Kukikosekana upendo katika ndoa hata maendeleo yanaweza yakakosekana.
Upendo ni muhimu sana katika ndoa yenu.
Upendo hautakiwi kupoa bali unatakiwa kuongezeka.
Kama unampenda mwenzi wako naamini huwezi kumsaliti na huwezi kumtendea mabaya.
Upendo ni muhimu sana katika ndoa.


7. Kusameheana 

Wakolosai 3:13-14 ''Mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.''

Ni muhimu sana wanandoa kusameheana.
Kinyume cha kusamehe ni kuchukia na chuki hutokana na hasira na Biblia iko wazi sana ikisema kwamba 
''Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu-Mhubiri 7:9'' 

Hasira ya namna hii hukaa katika vifua vya wapumbavu.
Usikubali kuwa mpumbavu kwa kushindwa kumsamehe mwenzi wako.
Kusamehe ni sheria na sio hiari.
Biblia inasema wasiosamehe na wao MUNGU hatawasamehe na wasiposamehewa na MUNGU hawawezi kuingi uzima wa milele.
Kusamehe ni muhimu sana tena ni lazima.
Kusameheana ni msingi mzuri sana katika ndoa.
 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.-Mathayo 6:14-15'' 

Ubarikiwe sana, na somo hili litakuwa kwenye kitabu kwa ufafanuzi mkubwa zaidi, ukipenda kunichangia kwa ajili ya kuchapisha vitabu ubarikiwe sana.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments