Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Labels

Thursday, January 12, 2017

INJILI YA AMANI YA UZIMA WA MILELE

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU kwa njia ya YESU KRISTO Mwokozi.
Lengo la kwanza na MUNGU kupitia injili yake ni kutuokoa wanadamu na lengo la pili ni kutuweka huru mbali na uonevu wa giza.
Marko 1:1,15 ''Mwanzo wa Injili ya YESU KRISTO, Mwana wa MUNGU. akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.'' 

Bwana YESU alipoanza tu huduma yake jambo la kwanza ni kuitangaza injili yake inayookoa kwa kila aaminiye.
Injili ni Neno la MUNGU la wokovu unaotengeneza maisha matakatifu yenye kibali cha uzima wa milele.
Ni lazima injili ihubiriwe maana kuna hukumu kwa wasioitii injili ya MUNGU.
Injili ya kweli huwaleta watu kwenye toba ya kweli kisha wanaanza kumtii MUNGU na injili yake. 
Injili ya KRISTO huambatana na nguvu za ROHO MTAKATIFU.
1 Thesalonike 1:4-5 '' Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.'' 
 
 Kiini cha Biblia ni injili ya YESU KRISTO iokoayo na kuwasogeza wanadamu karibu na MUNGU Muumba wao.
Injili halisi ni ile ya YESU KRISTO akiokoa wanadamu.
Kazi ya Kanisa hai la MUNGU duniani ni kuhubiri injili ya ufalme wa MUNGU ambao uko katika KRISTO pekee.
Bwana YESU baada ya kulianzisha kanisa lake duniani aliliagiza kanisa kuhubiri  injili yake akisema;
''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.-Marko 16:15-18 '' 

Injili halisi ni ile ambayo inampeleka msikiaji katika kumtii MUNGU na kutubu na kuishi maisha ya wokovu.
Injili ya KRISTO huambatana na miujiza ya MUNGU.
Hatuhitaji kuhubiri vitu vingine bali injili ya KRISTO tu inatosha maana hiyo huja na uponyaji kwa wanadamu.
 Injili ni neno hai la MUNGU ambalo lina uponyaji ndani yake.
Kama kuna jambo muhimu kabisa katika Biblia ni fundisho la injili ya YESU KRISTO iokoayo. 
Marko 13:10 ''Na sharti Injili ihubiriwe kwanza katika mataifa yote.''

Kibiblia huu ni wakati wa injili ya KRISTO tu.
Ni wakati huu MUNGU anatutaka tuhubiri injili yake ya wokovu wa KRISTO YESU.
Injili ya KRISTO haitakiwi kufichwa bali inatakiwa iwekwe wazi siku zote.
2 Timotheo 4:5 ''Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.''

Ndugu Usiifiche injili ya Wokovu wa KRISTO bali iseme siku zote na kwa ujasiri wa KRISTO.
Nakuombea kwa MUNGU kwamba Nuru ya KRISTO ikamate kinywa chako na ufahamu wako ili utembee kwenye mpango wa MUNGU wa injili ya uzima.

Mitume walihubiri injili ndio maana hata injili hiyo ikatufikia mimi na wewe.
Mitume hawakuona aibu kuhubiri injili hivyo na wewe usikubali kuona aibu kuhubiri injili ya KRITO iokoayo.
Mtume Paulo kama mfano wa watumishi wa MUNGU waliohubiri injili ya KRISTO bila woga wala kuona aibu anasema ''Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa MUNGU uuletao wokovu, kwa kila aaminiye,-Warumi 1:16A''
 Tena Mtume Paulo anasema ''tena ole wangu nisipoihubiri Injili!-1 Kor 9:16C  ''

 Kwa kanisa la MUNGU duniani ni jambo la lazima kuipeleka injili ya KRISTO kwa wanadamu wote.
 Injili haihubiriwi kwa akili bali kwa uwezo wa MUNGU na mamlaka ya MUNGU.
Ukiihubiri injili kwa akili itakushinda na badala ya kumhubiri KRISTO anayeokoa sasa utaanza kujihubiri wewe au utaanza kuhubiri dhehebu lako badala ya kumhubiri Mwokozi YESU.

MUNGU siku zote anawaita wanadamu kwa injili yake hivyo kanisa ni lazima sana liipeleke injili ya KRISTO mbele.
Hakuna habari njema kama injili ya KRISTO hivyo ni lazima sana tuipeleke injili ya KRISTO mbele.
Kupitia injili ya KRISTO tunajifunza kuhusu MUNGU na mpango wake kwetu wa wokovu.
Hakika huu ni upendo wa MUNGU wa ajabu kwetu wanadamu.
2 Timotheo 2:13-14 '' Lakini imetupasa sisi kumshukuru MUNGU sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa MUNGU amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na ROHO, na kuiamini kweli; aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu YESU KRISTO.''

Kuna watu baada ya kudumu katika wokovu  kwa muda, tamaa zao huwadanganya na hurudi nyuma wakiiacha kweli ya injili, hao hujipoteza na ni makosa makubwa hayo.
Ndugu yangu wewe nakusihi usiwaige hao bali songa mbele na wokovu wa Bwana YESU wenye injili ya uzima wa milele.
Kumbuka MUNGU haangalii wanaorudi nyuma bali anangalia wanaoendelea mbele na wokovu wake, huku yeye MUNGU wakati huo akiwaandalia uzima wa milele.
Ni vyema sana kudumu katika  Neno la MUNGU ambalo ni injili ya MUNGU kwetu.
Mtume Paulo analishauri kanisa la MUNGU kudumu katika kweli ya MUNGU ambayo ni injili ya KRISTO.
Wakolosai 1:23 ''mkidumu tu katika ile imani, hali mmewekwa juu ya msingi, mkawa imara; msipogeuzwa na kuliacha tumaini la Injili mliyosikia habari zake, iliyohubiriwa katika viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu; ambayo mimi Paulo nalikuwa mhudumu wake.''

Ndugu usikubali kuwa miongoni mwao wanaorudi nyuma na kumwacha Bwana  YESU na wokovu wake.

 Unapolisikia Neno la MUNGU linasema na wewe kama hivi hiyo ndio nafasi yako ya kubadilika kutoka kupunguza mwendo kwa YESU na sasa ongeza sana mwengo kwa YESU na mtii siku zote maana ni yeye ana uzima wako wa milele.
Neno la MUNGU la injili huleta usalama na ushindi.
Kumbuka  injili ya KRISTO ni kwa ajili ya watu wote na sio sehemu fulani tu ya watu au jamii.
Kila mwanadamu kama anataka kuokolewa na MUNGU basi ni kupitia injili ya YESU KRISTO.
Mwanadamu anayeutaka uzima wa milele basi ni muhimu kwake kuitii injili ya MUNGU kwa kumpokea YESU KRISTO mwokozi na  kuanza kuishi maisha mataktifu ya wokovu katika yeye.
Wakolosai 1:5-6 '' kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya MUNGU katika kweli;'

Ndugu nakuomba kaa ndani ya Neno la MUNGU la injili ya KRISTO na kubali Neno la MUNGU likutengeneze.
Neno la MUNGU likiingia ndani yako linakuletea uhakika wa uzima wa milele.
Neno la MUNGU likikaa ndani yako unashinda.
Ni muhimu sana pia kuishi sawasawa na injili ya MUNGU itakavyo.
Tumeipokea injili ya KRISTO ni lazima sasa tuishi kama injili itakavyo.
Hatutakiwi kuwa na injili ya midomoni tu bali hata matendo yetu yanapaswa kuwa masafi kama injili ya KRISTO itakavyo.
Wakolosai 3:12-17 ''Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.'

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

0 comments: