Jinsi Roho Mtakatifu anavyotumia “Pendo la Kristo” ndani yetu,

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe sana sana!
Leo nataka tutafakari na kujifunza pamoja, jinsi Roho Mtakatifu anavyotumia “Pendo la Kristo” ndani yetu, ili kutuongoza katika kujitoa kwetu kama sadaka, au kutoa vitu kama sadaka kwa Mungu.
Kujitoa mwenyewe kama sadaka au kutoa vitu kama sadaka – ni njia mojawapo muhimu ya kumtumikia Mungu! Na ikiwa unapenda kumtumikia Mungu kwa njia hizi mbili, unahitaji kulifuatilia somo hili leo kwa umakini mkubwa!
Kati ya onyo muhimu toka kwa Mungu kwenda kwa watu wake ni hili: “Ujihadhari usitoe sadaka zako …kila mahali upaonapo; bali katika mahali atakapopachagua Bwana …ndipo utakapotoa sadaka zako…,ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo” (Kumbukumbu 12:13,14).Hii ina maana – watu wake hatutakiwi kujichagulia mahali pa kutoa sadaka au mahali pa kujitoa sadaka – ki – muda au ki – nguvu kazi; bali tunatakiwa tuongozwe na tuelekezwe na Mungu juu ya hili.Tukienda kinyume na onyo hili – tutakuwa tunaasi onyo na agizo la Mungu! Na kufuatana na 1 Yohana 3:4 uasi ni dhambi!
Tunaposoma biblia tunaona ya kuwa, njia mojawapo ambayo Mungu anawaongoza watu wake, na kuwaelekeza kwenye utoaji wa sadaka; ni kwa Roho Mtakatifu kutumia “pendo la Mungu” ndani ya watu!
Mungu alipokuwa anampa Musa maagizo juu ya kupokea sadaka kwa ajili ya ujenzi wa “hema ya kukutania”, hakumpa ruhusa ya kuchukua na kupokea sadaka kutoka mahali popote.Mungu alimpa Musa maelekezo haya: “Waambie wana wa Israel kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda, mtatwa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii….Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo…” (Kutoka 25:2,3,8,9).
Musa hakuwa na ruhusa ya kuchukua sadaka toka kwa mtu yo yote, bali toka kwa yule tu “ambaye moyo wake wampa kupenda…”! Kwa tafsiri nyingine ni kwamba mtu huyo ataongozwa na upendo katika utoaji wake – toka moyoni mwake!Na hivi ndivyo Musa naye alivyotoa maelekezo kwa watu wake. Musa aliwaambia watu hivi: “Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema, katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo….” (Kutoka 35:4,5)
Agizo hili lilimlazimu Mungu kuweka huo upendo unaotakiwa ndani ya watu hao…ili aone utii wao utakuwaje katika kutekeleza agizo hilo alilowapa!
Biblia inasema: “Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, na kwa utumishi wake, na kwa hayo mavazi matakatifu” (Kutoka 35:21).
Kwa hiyo moyo ulio na “upendo wa Mungu” ndani yake
(i) – “utamhimiza” mtu aweze kutoa sadaka (Kutoka 35:21);
(ii) “utamfanya mtu kupenda kutoa sadaka” (Kutoka 35:21);
(iii) Utamfanya mtu kutoa aina ya sadaka inayotakiwa (Kutoka 35:22-28);
(iv) Utamfanya mtoa sadaka aone kutoa sadaka huko ni kumtii Mungu, ingawa amelisikia agizo la utoaji huo kupitia kwenye kinywa cha “Musa” (Kutoka 35:29);
(v) Utaendelea kumhimiza kutoa sadaka hadi vitapopatikana vitu vilivyokuwa “vyatosha kwa kufanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi” (Kutoka 36:4 – 7).
Kwa nini Mungu aliamua kutumia upendo ili kuhimiza na kuongoza utoaji ndani ya mioyo ya watu?
Ni kwa sababu hata yeye mwenyewe anatumia upendo wake katika utoaji wake kwa wanadamu!
Biblia inasema: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee…” (Yohana 3:16). Kwa hiyo pendo la Mungu kwetu, tunaliona katika utoaji wake kwa ajili yetu!
Ndiyo maana imeandikwa hivi: “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu alimtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye” (1 Yohana 4:9).
Lakini pia – biblia inatuonyesha ya kuwa kiwango cha upendo kinapimwa na utoaji wa mtu! Biblia inasema: “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohana 15:13). Soma pia Warumi 5:8 na Wagalatia 2:20.
Hata “wazee” wa kiyahudi walilithibitisha wazo hili, walipokuwa wanamwomba Yesu amponye mfanyakazi wa “akida mmoja” aliyekuwa anaumwa!
Wazee hao wa kiyahudi “walimsihi sana” Yesu wakimwambia, “amestahili huyu umtendee neno hili; maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi” (Luka 7:5). Nadhani unaona ya kuwa walipima na kuona upendo wa akida kwa taifa lao, kwa utoaji wake uliowajengea sinagogi!
Kwa muhstari nataka ufahamu yafuatayo:
1. Njia mojawapo inayoonyesha upendo wako kwa Mungu wako, ni njia ya utoaji wako wa sadaka.
2. Chanzo cha msukumo wa moyo wako kukuhimiza kutoa – ndiko kunakotofautisha kati ya utoaji ulio sadaka, na ule utoaji ulio msaada! “Sadaka” inasukumwa na kiwango cha upendo wa Mungu wako kilichomo moyoni mwako; na “msaada” unapoutoa haukulazimishi kuunganisha utoaji wa msaada na Mungu. Kumbuka hili: Mungu hahitaji msaada wako, bali anahitaji sadaka toka kwako.
3. Ili iwe rahisi Mungu kumtumia Roho Mtakatifu kutuongoza na kutuelekeza katika utoaji sadaka, “pendo la Mungu” lilimiminwa “katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” (Warumi 5:5) – siku ile tulipookoka!
4. Lengo mojawapo la “pendo la Mungu” kumiminwa na Roho Mtakatifu katika mioyo yetu, ni ili kama vile pendo hilo lilimhimiza Yesu kujitoa nafsi yake iwe sadaka kwa ajili yetu; na sisi tuwe tunahimizwa na pendo hilo hilo katika utoaji wetu. Ufahamu huu tunaupata tunaposoma 1 Yohana 3:16 – 18, na 1 Yohana 4:19, na Waebrania 6:10, na Waefeso 5:1,2.
5. Ingawa utoaji sadaka unatakiwa uwe ni kwa imani, ili kukujengea mipaka ya utoaji kwa kutumia neno la Mungu (Warumi 10:17), na ili kuweka ubora wa sadaka yako (Waebrania 11:4); lakini bila upendo, utoaji huo na imani uliyoitumia, havitakufaidia chochote (Wakorintho 13:2,3).
6. Kumbuka imani haifanyi kazi peke yake – bali inafanya kazi pamoja na matendo (Yakobo 2:17,20,26). Na matendo ya kiimani ni matokeo ya upendo wa moyo wa mtendaji huyo kwa Mungu husika. Ndiyo maana biblia inasema “imani hufanya kazi kwa upendo” (Wagalatia 5:6).
7. Unaposikia hali ya kumpenda Mungu ndani yako – ujue ni Roho Mtakatifu anakuandaa na utoaji sadaka ulioko mbele yako.
8. Unaposikia moyoni kumpenda Mungu anayemtumia mtumishi fulani …ni ishara ya Roho Mtakatifu kukuhimiza kutoa sadaka na kumpa mtumishi huyu – ili ushiriki naye kwenye utumishi huo.
9. Palipo na imani pana amani (Warumi 5:1), na palipo na “pendo la Mungu” pana “uhuru wa Kristo”. Unaposikia viashiria hivi “kwa pamoja” moyoni mwako, hasa unaposikia habari ya utoaji sadaka – ina maana usisite kuitoa hiyo sadaka kwa kiwango unachosukumwa kutoa!
10. Unaposikia moyoni mwako “kudaiwa kupenda”, ujue Roho Mtakatifu anatumia pendo la Mungu ndani yako kukusukuma kutoa sadaka – kwa ajili yake – hapo upendo wake unapokuelekeza kutoa. Hii ndiyo maana nyingine ya maneno haya ya Warumi 13:8 yanayosema “Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana…”
11. Imani au neno la Mungu linapokusukuma kutoa sadaka, lakini moyo wako unakuwa mzito kutoa …ina maana unahitaji kuuombea utoaji huo kabla ya kutoa. Baada ya kuomba halafu ukasikia moyoni mwako kupenda kutoa au ukasikia moyoni mwako uhuru wa kutoa – basi toa. Lakini hata baada ya kuomba ukaendelea kusikia “uzito” moyoni au “kusita” au “kufungika” au kukosa amani – ina maana usitoe. Ukitoa sadaka huku moyoni ni kama unalazimishwa kutoa, basi usitegemee faida yoyote kwako katika utoaji huo. Hii ni kutokana na 1 Wakorintho 13:2.
Ninakuombea ya kuwa: “Kristo akae moyoni mwako kwa imani, ukiwa na shina na msingi katika upendo; ili upate ufahamu jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina, na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, upate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu”. Nimekuombea hayo sawa na Waefeso 3:17 – 19. Amina.

Comments