KIFUNGO CHA UOVU

Na Mtumishi Dk Frank P. Seth
“Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu” (Matendo ya Mitume 8:23).
Umewahi kufikia hatua ya kutaka kufanya jambo JEMA lakini unasita au kuona uzito kwa sababu ya sauti fulani inayokunong'oneza moyoni (nafsini) mwako na kukusuta kwamba, “nawewe unaweza kufanya hivi baada ya kosa/dhambi ile uliyofanya!”? 

Uovu ni zaidi ya dhambi au kosa. Uovu ni hali ya ndani inayomfanya mtu ATENDE kosa au ASITENDE jambo jema. Mara nyingi watu wamejitahidi kupambana na dhambi bila kujua kwamba UOVU ndani yao ndio chanzo ya kufanya dhambi, kwahiyo hawakushughulika na uovu; bado dhambi inawasumbua na hawajui dawa. Dhambi ni matokeo, uovu ni chanzo. Jifunze kushughulika na chanzo.

Uovu unapokuwa ndani ya mtu humfanya mtu MFUGWA au MTUMWA, ndipo maana halisi ya “mtumwa wa dhambi” inakuja. Mtumwa hana maamuzi ila bwana wake. Ukitaka kuelewa, jiulize ni kwanini unachukia dhambi fulani lakini huwezi kuacha kuifanya; kwa sababu wewe ni mtumwa wa hiyo (Warumi 7:14-24).
Mara nyingi, uovu hustawi vizuri zaidi mahali penye UCHUNGU. Ukiacha mambo yakuumize tu, na ukakosa kusamehe, unajijengea mazingira mazuri sana ya KUPANDA uchungu na UOVU utasitawi hapo pia. Ndio maana ukitaka kuwa MAWINDO rahisi ya Ibilisi, we achia tu UCHUNGU ujae ndani yako. Hutaamini utakavyokuwa baada ya muda, utajishangaa kama ni wewe unafanya hayo au ni mwingine.

Mtu mwenye uchungu ni rahisi sana kuingiwa na UOVU na hatimaye kuanza kufanya DHAMBI hata zile ambazo hazikuwahi kuingia akilini. Ule uchungu utajenga mazingira mazuri ya uovu kusitawi. Kadri mtu anatenda dhambi, majeraha yanazidi. Mtu anajikuta hana Amani na furaha; taratibu na hasira za ajabu-ajabu zinazaliwa humo. 

Kadri amani na furaha vinakosekana, mtu anajikuta anazidi kufanya dhambi huku akijifariji kwa sababu UCHUNGU unamwongoza kufanya hayo. Ghafla! mtu anajikuta kwenye KIFUNGO kigumu sana; kila akitaka kufanya jambo JEMA anakuwa mzito na kama mwenye aibu na kuogopa watu. Anakuwa kama amefungwa miguu na mikono. Hawezi kuacha dhambi na wala hawezi kutenda mambo ya maana tena. Majuto ya mwisho yanakuwa mazito kuliko ya mwanzo.

Aheri ujiambie sasa basi! Fanya jambo JEMA hata kama Ibilisi anakuzomea kwamba HUSTAHILI. Kumbuka, “kila tawi lizaalo husafishwa ili lizae zaidi” (Yohana 15:2). Unapoanza kufanya mambo MAZURI, ile mbegu inazaa mambo mazuri zaidi, unazidi kusafishwa na kuongezwa hadi unakuwa mtu mwingine kabisa. Kazi ya kukusafisha ni ya BABA, sio yako (Yohana 15:1).

Fikiri Mtume Paulo, pale alipoitwa Sauli, angesikiliza kelele za Adui na kuona HASTAHILI kufanya kazi ya HUDUMA, eti kwa sababu alilitesa kanisa. Wakati Paulo anajaribu kufanya jambo JEMA, mitume wanamkimbia, wanamwona MUAAJI na hatari kuliko JAMBAZI, Paulo naye anajitahidi tu hadi kikaeleweka...Hata kama kwa sasa unaitwa jambazi, kahaba, muuaji na majina mengi, endelea kufanya mambo mazuri...kitaeleweka tu! Utasafishwa wewe na kuwa mpya! Weka nia leo.
Neema na izidi kwenu,
HAPPY NEW YEAR, 2017!
Frank P. Seth

Comments