MAELEZO YA KIUCHAMBUZI KUHUSU SIKUKUU YA KUZALIWA YESU-CHRISTMAS

Na Mwalimu Daniel Mwankemwa

“Kondoo wote huzaliwa nyakati zilizo sawa na tukio la kuzaliwa Yesu Kristo Noeli (Christmas).”
Kama ndivyo, Je kuna uthibitisho wowote kwamba Yesu alizaliwa wakati huo?
Kwa miaka mingi sasa, wachungaji na Walimu wengi wa Neno la Mungu wanasema, “hatujui kwa uhakika ni lini Yesu Kristo alizaliwa- hata hivyo kwetu si muhimu kujua wakati halisi au tarehe halisi ya kuzaliwa kwa Yesu.”
Wasiosherehekea kuzaliwa kwa Yesu wamekuwa wakifundisha kwamba, sikukuu ya Noel “ilibuniwa” katika karne ya nne au tano. Lengo la kuibuni sikukuu hiyo ilikuwa ni kumpa “Mkristo” sura ya unafiki au ushawishi kwa mpagani au sikukuu za kishetani zilizokuwa zikisherehekewa wakati wa baridi au wakati jua likiwa Kusini kabisa mwa Ikweta (solstice) ambazo ni siku fupi zaidi za mwaka.
Kama ndivyo, ukweli halisi ni upi? Je, kuna ushahidi wowote kwamba Yesu Kristo alizaliwa wakati wa mwezi wa Desemba?
Unapozichunguza kwa makini namba mbali mbali zinazotajwa na Biblia kuhusiana na suala hili, zinatoa mwanga na ushahidi kwamba ni kweli Yesu alizaliwa mwezi wa Desemba. Tarakimu hizo zinajikita zaidi kuelezea kusudi la Yesu kuja duniani katika mwili. Lakini pia zinatupa kushukuru kwa moyo wote, kufunuliwa yale yote yaliyoonekana yamefichwa ndani ya Neno la Mungu, ambayo, yanaweza kufunuliwa kwa wale tu wanaoyachunguza maandiko kupitia maombi ya kweli.

Kila Neno ndani ya Biblia lipo pale lilipo kwa sababu maalumu, na kwa sababu Mungu ameliweka hapo. Ana kusudi na kila Neno. Kwa hiyo, kuorodhesha kimpangilio nyakati za matukio, huku ukirejea mpangilio wa nasaba, na kadhalika kwa maombi halisi, vina umuhimu mkubwa, ambao, utakusaidia kuvumbua mambo hayo yote.
Katika kitabu cha Luka sura yote ya kwanza, Biblia inaelezea jambo ambalo kwa wengi linaonekana kama halina umuhimu wowote hasa kile alichokuwa akikifanya kuhani Zakaria alipotokewa na malaika wa Bwana na kumpasha habari kwamba yeye pamoja na mke wake Elizabeti wangelipata mtoto. Mtoto huyo angeitwa Yohana Mbatizaji, ambaye pia ndiye angetayarisha njia kwa ajili ya Masihi ajaye, Yesu Kristo.
Biblia inaeleza pia kwamba, mimba ya Yesu Kristo ilitungwa kwa Mariamu miezi sita baadaye tangu Zakaria kupewa habari za mke wake Elizabeti kubeba mimba ya Yohana. Kwa hiyo, iwapo kutungwa mimba kwa Yohana kungechunguzwa vyema, kwa vyovyote tarehe ya kuzaliwa Yesu ingefanyiwa hesabu na kujulikana tu.
Maandiko yanaanza kwa kusema: “Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kuhani mmoja jina lake Zakaria wa zamu ya Abia na mke wake alikuwa wa ukoo wa Haruni, jina lake akiitwa Elizabeti (Luka 1:5).
Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu… ” Luka 1:8
Hapa kuhani Zakaria nathibitisha uaminifu wake wa ajabu mbele za Mungu. Ijapokuwa alikuwa amepewa habari njema na za ajabu na malaika, kwamba yeye na mkewe Elizabethi wangelipata mtoto lakini hakurudi nyumbani kwake wakati ule ule, bali alibaki kutumika hekaluni hadi … “siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia, akaenda nyumbani kwake (Luka 1:23).
Na baada ya siku hizo mke wake Elizabeti akapata mimba na kutawa kwa muda wa miezi mitano…” Luka 1:23-24.
Fungu hilo la maneno linaeleza pia jinsi Malaika Gabrieli alivyokuja kwa Mariamu ili kumpa habari za kuzaliwa Masihi, Bwana Yesu. Maandiko yanasema: “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu…” (Luka 1:26-27)
“ Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,
akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.” (Luka 1:39-40).

Kilichomo ndani ya maandiko haya kinaonesha ni lini hasa Yesu alizaliwa. (Kumbuka Mungu huweka kila Neno na kila tendo au tukio mahali pake, kama vile Anavyotaka, kwa kusudi lake maalumu.) Mistari tuliosoma ndiyo ufunguo wa kujua nyakati.
Katika Luka 1:5 na Luka 1:8, tunaambiwa kwamba Zakaria alikuwa ni kuhani wa zamu ya Abia, na kwamba alitimiza zamu yake ya ukuhani. Ili tuweze kuelewa umuhimu wa zamu ya Abia na kuhusika kwake na kutungwa mimba ya Yohana Mbatizaji, ni muhimu turudi tuangalie jinsi Mfalme Daudi alivyozianzisha zamu hizo maelfu ya miaka nyuma kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo katika 1Nyakati 24:1-10, akielezea namna zamu za ukuhani zitakavyokuwa mara baada ya kujengwa hekalu. Katika mistari hiyo tunasoma: “Na zamu za wana wa Haruni ni hizi. Wana wa Haruni; Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. Lakini hao Nadabu na Abihu walikufa kabla ya baba yao, wala hawakuwa na watoto; kwa hiyo Eleazari na Ithamari wakafanya ukuhani.
Akawagawanya Daudi, na Sadoki wa wana wa Eleazari, na Ahimeleki wa wana wa Ithamari, katika utumishi kwa kadiri ya usimamizi wao. Wakaonekana wakuu wengi wa wana wa Eleazari kuliko wa wana wa Ithamari; wakagawanyika hivi; wa wana wa Eleazari kulikuwa na kumi na sita, waliokuwa wakuu wa mbari za baba zao; na wa wana wa Ithamari, sawasawa na mbari za baba zao, wanane.
Ndivyo walivyogawanyika kwa kura, wao kwa wao; kwani kulikuwa na wakuu wa patakatifu, na wakuu wa Mungu, wa wana wa Eleazari, na wa wana wa Ithamari pia.
Naye Shemaya, mwana wa Nethaneli, mwandishi, aliyekuwa wa Walawi, akawaandika mbele ya mfalme, na mbele ya wakuu, na Sadoki kuhani, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari, na wakuu wa mbari za baba za makuhani, na za Walawi; ikatwaliwa ya Eleazari mbari moja ya baba, na moja ikatwaliwa ya Ithamari. Kura ya kwanza ikamtokea Yehoiaribu, na ya pili Yedaya; ya tatu Harimu, ya nne Seorimu; ya tano Malkia, ya sita Miyamini; ya saba Hakosi, ya nane Abia"

Mtu wa zamu alitakiwa kuhudumu kwa mwezi mmoja kuanzia mwezi wa kwanza (Nisan) wa Kalenda ya Kiyahudi. (Kumbuka pia kwamba kalenda ya Kiyahudi ilikuwa inapanda na kushuka, ambapo mwezi huo wa kwanza wa Nisan unaweza kuanzia mwanzoni mwa mwezi Machi na mwanzoni mwa Aprili kwa kalenda yetu.) Wana wa Abia walipangwa kwenye zamu ya nane. Makuhani wa Abia akiwemo na Zakaria walipaswa kuhudumu zamu ya nane kwa siku kadhaa ndani ya zamu yao ya mwezi wa nane, ambao wakati mwingine kutokana na kupanda na kushuka kwa siku za kalenda ya Kiyahudi, kulianza mapema mwezi Oktoba kwa kalenda yetu.
Kwa hiyo Zakaria alipaswa kurudi nyumbani kwake mara baada ya utumishi wake hekaluni kuisha, na mimba ya Yohana kutungwa kati ya tarehe 15 Oktoba, au tarehe za mwisho wa mwezi huo.
Mara baada ya Elizabeti kupata mimba ya Yohana, maandiko yanasema, Elizabeti alitawa kwa muda wa miezi mitano. Kisha mwezi wa sita wa mimba hiyo ya Yohana ndani ya tumbo la Elizabeti (ambayo mahesabu yake yamekokotolewa hapo juu, mahesabu hayo yanaanzia tarehe 15 Oktoba, yaani, tangu Elizabeti amepata mimba na kutawa hiyo miezi mitano ambayo inaishia kati ya Mach 15 na kuendelea hadi Aprili 15 kwa kalenda yetu), ndipo malaika wa Bwana alipokwenda kwa Bikra Mariamu na kumtangazia kwamba angechukua mimba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kumzaa mtoto Yesu. Ikiwa tukio la kupata mimba Mariamu lilitokea kati ya tarehe 1 Aprili na kuendelea “kipindi cha kawaida cha kubeba ujauzito cha siku 270” kinaangukia kabisa tarehe 25 mwezi wa Kumi na Mbili.

Hili linakuwaje!
Yako maandiko mengine na mazingira ambayo yanathibitisha hili kwamba Yesu Kristo alizaliwa kipindi hicho. Katika kitabu cha Luka tunaposoma habari za kuzaliwa kwake imeandikwa, “ Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku” (Luka 2:8)
Wataalamu wa kilimo wanaweza kulithibitisha hili kwamba ni kweli Yesu alizaliwa kipindi hicho. Hii ni kwa sababu, wanajua kwamba, kipindi pekee ambacho wachungaji hukesha nje ya nyumba zao wakiwa na kondoo maporini ni kipindi ambacho kondoo wao huzaa. Kwa kawaida kondoo jike huanza kupandwa na madume kipindi cha baada ya tarehe 21 Juni, ambayo ndiyo ndiyo huwa siku ndefu zaidi katika mwaka. Kipindi cha kondoo jike kubeba mimba hadi kuzaa ni miezi mitano, yaani hadi katikati ya mwezi Desemba.
Kama ndivyo, maandiko yanamuelezea Yesu kwamba yeye ni Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu (Yoh 1:29). Je, angewezaje kuzaliwa tofauti na muda wazaliwapo kondoo wengine hasa ukizingatia kwamba yeye ndiye aliyekuja kufunga mlango wa kondoo kutolewa sadaka kwa ajili ya dhambi? Unabii ungevurugika!
Hivyo hivyo unamuona Yesu wakati wa kuteswa kwake msalabani, yaani, kutolewa kwake sadaka ya dhambi aliteswa nyakati zile zile ambapo kondoo wanyama walitolewa kafara hiyo.
Katika Agano la Kale kondoo wa Pasaka alichinjwa jioni. Tunasoma katika Kutoka 12:18-21 ‘Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni.
Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi.
Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.

Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka.”
Yesu alipozaliwa kama Mwanakondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu, nay eye alisulubiwa jioni ili kuitimiza nafasi ya Uanakondoo.
Katika Mathayo 27:45-50 tunasoma, “Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa. Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya. Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.
Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa. Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.”

Hapa Yesu anasulubiwa jioni kuanzia saa tisa.
Katika Marko 15: 33-37 tunasoma, “Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.”

Hapa pia Yesu amekata roho kuanzia jioni ya saa tisa.
Pia katika Luka 23: 45-47 tunasoma, “jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.”

Katika Yoha 19: 30-31 tunasoma, “Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe.”
Maandalio ya siku ya sabato kwa Wayahudi yalianza siku ya Ijumaa jua linapokuchwa na kuisha siku ya Jumamosi jua linapokuchwa tena.
Maandiko yote haya yametolewa ili kuthibitisha kwamba, kama vile katika Agano la Kale kondoo wa sadaka walivyochinjwa jioni, ndivyo ilivyokuwa pia kwa Yesu alipozaliwa akiwa Mwanakondoo wa Mungu.
Hoja kutokana na maandiko haya ni kwamba, Je, Yesu angetakiwa kutimiza jukumu la kuondoa dhambi kwa kusulubiwa jioni kama walivyofanyiwa kondoo wanyama wakati wa Agano la Kale, lakini asifuate muda wa kuzaliwa kondoo hao ambao ni mwezi wa kumi na mbili? Ilikuwaje basi alikubali kuzaliwa kwenye zizi la wanyama (a manger) ambako ndiko makao ya wanyama kama hakutakiwa kufuata utaratibu na mfumo wote wa wanyama hao? Haiwezekani lazima aliufuata tangu kuzaliwa hadi kutolewa sadaka.
Lakini pia kuna hoja nyingine kubwa, kwamba, Mungu alimtuma Mwanawe ulimwenguni ili awe Nuru ya ulimwengu. Siku za mwisho wa mwezi wa kumi na mbili wa mwaka, kwa kawaida huwa fupi na kwa hivyo giza huwahi kuingia. Yesu anasema, “Mimi ni Nuru ya ulimwengu.” (Yoh 8:12).
Kwa hiyo, katika kipindi cha mwaka ambacho kwa kawaida giza huwa ni kubwa kuliko kipindi cha nuru, Mungu, alimtuma Mwanawe ili aje kuwa Nuru.
Kumekuwa na mijadala mingi na malumbano yasiyo na faida kuhusiana na sikukuu ya Noeli au Christmas, bila kuzingatia hasa kusudi la kiunabii kuhusu wokovu kwa mwanadamu.
Hapa ndipo yanapogawika makundi mawili, moja likimpokea na kufanyika wana wa Mungu, na jingine ingawa alikuja kwao, lilimkataa.

Katika Yohana 1:12-13 tunasoma, “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
 Mungu akubariki sana.
By Mwalimu Daniel Mwankemwa

Comments