mambo mengine zaidi yanayoweza kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu.

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe sana !
Wiki iliyopita nilikupa mambo matatu, ambayo yanaweza kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu, ili iwe rahisi kwake kukuongoza utembee katika mapenzi ya Mungu.
Ninapozungumzia juu ya “Usikivu” – ujue inahusisha pia juu utendaji wa hicho unachosikia. Usikivu kwa Roho Mtakatifu, bila kutekeleza hicho unachosikizishwa, ni sawa na kutokuwa msikivu!
Leo naendelea na somo hili, kwa kukupa mambo mengine zaidi yanayoweza kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu.
Jambo la 4: “Jizoeze kuomba kwa muda mrefu kwa mfululizo ili kuuthibiti mwili wako”.
Je, unafahamu Yesu alikuwa ana maana gani aliposema “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41).
Kwa kusema hivyo, Yesu alitaka tujue ya kuwa “mwili” usiothibitiwa kwa maombi, unaweza ukawa kikwazo kwa mtu, ili asiwe msikivu, katika kuyatenda mapenzi ya Mungu!
Yesu mwenyewe, alikuwa anapitia katika upinzani wa namna hiyo alipoomba akisema: “Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe” (Mathayo 26:39).Changamoto hiyo Yesu aliishinda kwa njia ya maombi. Na ukisoma habari hiyo vizuri, utaona ya kuwa, kuomba kulikomsaidia awe “msikivu” ili aweze kutekeleza mapenzi ya Baba yake, kulikuwa na mambo mawili makuu:
(i) “Kuomba kwa kukesha” – ambako ni kuomba kunakolenga kurudisha “utayari” moyoni mwa mwombaji. Neno “kesheni” lina maana ya “muwe na utayari”.
“Kesheni, mwombe” ina maana ya kuomba hadi utayari urudi moyoni mwa mwombaji, unaompa ushindi dhidi ya upinzani wa mwili.
(ii) Muda aliotaka tujue, kuwa unaweza kurudisha utayari wa usikivu kwa Roho Mtakatifu, ni kule kuomba kusikopungua muda wa saa moja ukiwa katika maombi!
Yesu aliwaambia hivi wanafunzi wake; “Je, hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:40,41).
Kwa hiyo – tumia njia hii ya kuomba, tena kwa muda mrefu na kwa mfululizo ili kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu, wakati mwili unakuletea upinzani!
Jambo la 5: “Jizoeze kuomba kwa kunena kwa lugha ili kuijenga nafsi yako”Mtume Paulo alisema: “Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake…” (1 Wakorintho 14:4). Neno “kujenga” kunaashiria ya kuwa kinachojengwa – au kilibomoka, au kilianza kujengwa lakini hakikukamilika, au kilijengwa vibaya!
“Nafsi” ya mtu inapokuwa katika hali mbaya, inamfanya mhusika asiwe msikivu kwa kile ambacho Roho Mtakatifu anamsikizisha! Kuomba kwa kunena kwa lugha, kunaongeza usikivu ndani ya mtu anayeomba hivyo!
Tena – ukiweza kujizoeza kuomba mara kwa mara kwa kunena kwa lugha – na kwa muda mrefu – utaona usikivu wako kwa Roho Mtakatifu ukiongezeka hatua kwa hatua!
Kwa mfano – unaposoma biblia na unapata shida kuelewa unachosoma – omba kwa kunena kwa lugha kwa muda, halafu rudia kusoma eneo ulilokuwa unalisoma katika biblia bila kuelewa, utaona unaanza kulielewa.
Tena – ikiwa unasikiliza mahubiri, au mafundisho ya neno la Mungu, na unashindwa “kusikia” ujumbe wa kukusaidia; anza kuomba kwa kunena kwa lugha taratibu, bila kusumbua waliokaa jirani na wewe – utashangaa kuona unaanza kuelewa unachosikia!
Jambo la 6: “Tii na utekeleze unachoambiwa kwanza, kwani itakuwa rahisi kusikia kinachofuata baada ya hicho cha kwanza”.
Kumbuka: “Obeying the first step, qualifies you to be given instructions for your second step”. Hii ina maana ya kuwa kutii kwako kwa hatua ya kwanza, kunatoa uhalali wa wewe kupewa maelekezo yanayohusu hatua yako inayofuata!
Fahamu hili ya kuwa “utii” wako kwa Roho Mtakatifu, unaongeza “usikivu” wako kwake!
Tunasoma habari ya Filipo ya kuwa, alipokuwa kwenye mji wa Samaria akifanya kazi ya Mungu, alipewa maelekezo haya: “Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkiayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa” (Matendo ya Mitume 8:26).
Biblia inasema Filipo “akaondoka, akaenda…” (Matendo ya Mitume 8:27). Alipofika huko alikoelekezwa alimwona mtu wa Kushi, akiwa garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya, alipokuwa anarejea toka Yerusalemu alikokuwa amekwenda kuabudu.
Baada ya Filipo kutii maelekezo ya hatua hiyo ya kwanza, akawa amejitengenezea mazingira ya kupewa maelekezo yaliyohusu hatua yake iliyokuwa inafuata baada ya hiyo ya kwanza!
Biblia inasema: “ Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo” (Matendo ya Mitume 8:29). Je, umeona jambo ninalotaka uone katika habari hii ya Filipo na mtu wa Kushi?
Ninalotaka uone katika habari hii ni kwamba: usikivu wa Filipo, na utekelezaji wa alichosikizishwa mwanzoni, kulifungua mlango wa usikivu wake wa maelekezo yaliyofuata!
Hebu jiulize mwenyewe – je, ni kwa nini Roho Mtakatifu aongeze usikivu wako, kwa hatua zilizo mbele yako, ikiwa maelekezo yake ya hatua unayotakiwa kuchukua kwanza hutaki kuisikia wala kuitekeleza?
“Jifunze kushirikiana na Roho Mtakatifu anapotumia moto kukuongoza ili utembee kwenye mapenzi ya Mungu”! Hili ndilo somo letu leo.
Biblia inafundisha ya kuwa wana wa Mungu huwa wanaishi, na wanatakiwa waishi kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu (Warumi 8:14,16,17).Njia mojawapo anayotumia Roho Mtakatifu kumwongoza mwana wa Mungu, ni kwa kutumia “moto” wa Mungu anaokuja nao ndani ya mtu, anapoingia kukaa kwake!
Biblia inasema juu ya Yesu ya kuwa; “Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto” (Luka 3:16). Na siku ya Pentekoste, wakati wanafunzi wa kwanza wa Yesu, walipokuwa wamekutanika pamoja: “kukawatokea ndimi zilizogawanyika, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu…” (Matendo 2:3,4).
Unaposoma na kutafakari jambo lililotokea siku hiyo ya Pentekoste, utajua kuwa kuna uhusiano kati ya “ndimi za moto” juu ya “kila mmoja wao”; na kule kujazwa Roho Mtakatifu kwa kila mmoja wao.
Ni dhahiri ya kuwa Roho Mtakatifu anaingia ndani ya “kila” mwana wa Mungu akiwa pia na “moto” wa Mungu pamoja nao!
Kazi mojawapo ya “moto” huo, ni ili Roho Mtakatifu autumie kumwongoza mtu “kwa kuuvuta moyo wake uweze kuwa msikivu kwa kile ambacho Mungu anamtaarifu, kinachohusiana na mapenzi ya Mungu kwake”.
Mfano wa 1: “Nguzo ya moto iliyowaongoza wana wa Israeli wakiwa jangwani wakati wa usiku”
Kitabu cha Kutoka 13:21,22 kinapozungumza juu ya safari ya wana wa Israeli, ya kuelekea Kaanani wakitokea Misri, utasoma hivi:
“Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu”.
Tunaona ya kwamba, nguzo ya moto ilikuwa ni ishara ya kuwa, Mungu alikuwa pamoja nao, “ili awaongoze njia...na kuwapa nuru wapate kusafiri … usiku”!
Unaposoma Yeremia 9:12, utaona ya kuwa Mungu aliwaongoza wana wa Israel “kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea”. Wazo hili unalipata pia, unaposoma Kumbukumbu la Torati 1:33.
Je, umewahi kujiuliza kwa nini, Mungu aliwaongoza kwa utaratibu tofauti “mchana” na kwa utaratibu mwingine “usiku”? Naamini ni ili tujue ya kuwa, Mungu anaongoza watu wake kwa namna tofauti –tofauti kwa kufuatana na “msimu” wa maisha wanaopitia.
Kwa hiyo “mchana” ni msimu tofauti, na “usiku” ni msimu tofauti. Roho Mtakatifu anakuongoza wakati wa msimu wako wa “mchana” kwa utaratibu tofauti; ukilinganisha na jinsi anavyokuongoza wakati wa msimu wako wa “usiku”.
Kipindi cha mtu cha “usiku” – kiroho – ni wakati ambapo anapitia kipindi kigumu kimaisha – kiasi kwamba anaona amezungukwa na “giza” kimaisha!
Mtu akiendelea kwa muda mrefu, kwenye kipindi kigumu kimaisha kama cha usiku au giza; bila Mungu kumpa uhakikisho (assurance) ya kuwa yupo pamoja naye, anaweza akafikiri ya kuwa Mungu amemwacha!
Ndio maana mtu anapopitia kipindi kigumu kimaisha, mara kwa mara, atasikia moyoni mwake uwako wa “moto”, ambao utawaka kwa muda kadhaa - kwa masaa au kwa siku kadhaa mfululizo!
Hali ya uwako wa moto moyoni mwako wa namna hiyo, ikikupata wakati wa msimu wako wa maisha yako unaofanana na “usiku” au “giza”, ujue Mungu anakupa uhakikisho ya kuwa, yupo pamoja nawe katika Roho Mtakatifu – kukupa mwanga ili kukuonyesha njia uipasayo kuipitia – ili uvuke hicho kipindi chako kilicho kigumu kimaisha!
Mungu azidi kukubariki na somo hili. Tuonane tena wiki ijayo kwa muendelezo wake.

Comments