Mambo yanayoweza kukusaidia, kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe milele.
Leo nataka tujifunze mambo yanayoweza kukusaidia, kuongeza usikivu wako kwa Roho Mtakatifu; na kwa njia anazotumia kukuongoza, ili utembee na uishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.
Jambo la 1: “Ongeza utayari wako wa kutaka kuwa na ushirika wa karibu na Roho Mtakatifu”.


Kumbuka – ni vigumu kupata msaada, au kutaka msaada, kutoka kwa yule ambaye hauko tayari kushirikiana naye.
Yesu anamtambulisha Roho Mtakatifu kama “msaidizi mwingine” (Yohana 14:16), aliyetumwa na Mungu, kwa ajili ya mtu ye yote anayehitaji msaada wake.Je, uko tayari kupokea msaada wa Mungu kupitia kwa Roho Mtakatifu kwa kiwango gani?


Kumbuka – jambo la usikivu ni zaidi ya kusikia tu! Pamoja na kusikia – usikivu unahusika pia na utendaji wa kile unachokisikia! Kibiblia – usipokuwa mtendaji wa kile ulichosikia, ni sawa mtu ambaye “hajasikia”. Na kutokusikia huku kunasababisha utayari wa Roho Mtakatifu kukupa uongozi wake kupungua!
Si vizuri kwa mtu kudai anampenda Mungu katika Yesu Kristo, lakini wakati huo huo anampinga Roho wake Mtakatifu. Soma Matendo ya Mitume 7:51 na Isaya 63:10.
Jifunze kujiombea – ikibidi jiombee kila siku – ya kuwa, “ushirika wa Roho Mtakatifu” (2 Korintho 13:14), ukae na wewe siku zote. Hii ni kwa sababu katika ushirika huo, utapata na msaada wa uongozi wake, kwa maana usikivu wako kwake utaongezeka!
Jambo la 2: “Soma na tafakari neno la Mungu la biblia”.
Hii ni kwa sababu “kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17).


Ikiwa “kusikia huja kwa neno la Kristo”, ina maana, ukitaka kuongeza usikivu wako, ongeza kwa kulisoma na kulitafakari neno la Kristo!
Ukisoma Zaburi ya 103:20, utaelewa ni kwa nini kusikia huja kwa neno la Kristo. Hii ni kwa kuwa, mstari huu unatuambia ya kwamba, kinachofanya malaika wawe hodari katika kulitekeleza na kulitenda neno la Mungu, ni kwa sababu wanaisikiliza “sauti” iliyo ndani ya neno lake!


Ndiyo maana mtume Paulo anatuhimiza akisema; “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote…” (Wakolosai 3:16). Na kwa kadri neno la Kristo linavyoongezeka moyoni mwako, na usikivu wako kwa Roho Mtakatifu unaongezeka vivyo hivyo!Tena – neno la Kristo likiwa jingi ndani ya moyo wako, na imani yako inaongezeka, na urahisi wa Roho Mtakatifu kukuongoza unaongezeka pia!


Kumbuka – unakuwa na neno la Mungu kidogo moyoni mwako, usikivu wako kwa Roho Mtakatifu unakuwa ni mdogo pia.Kumbuka – “neno la Mungu …lijepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo,…wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake…” (Waebrania 4:12,13).
Kwa hiyo, ukiwa na neno la kutosha moyoni mwako, linakuwezesha kuchambua moyoni mwako “sauti” ambazo zinakuja moyoni mwako ambazo si za Mungu!
Jambo la 3: “Unapofanikiwa usisahau kutoa sadaka zako kwa uaminifu ili moyo wako usilemewe na mafanikio ukashindwa kusikia Mungu akikusemesha”.


Mungu anasema hivi: “Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, sitaki kusikia” (Yeremia 22:21). Kwa maneno mengine ina maana ya kuwa, “mafanikio” yanaweza kumfanya mtu akatae na ashindwe kumsikia Mungu anapomsemesha!


Njia mojawapo ya kuufanya moyo wako, uendelee kuwa msikivu kwa Mungu, wakati wa kufanikiwa kwako; ni kwa njia ya kutoa sadaka – kwa kadri Mungu anavyokuwezesha moyoni mwako!
Hii ni kwa sababu – sadaka ikitolewa kwa imani, ni njia mojawapo muhimu ya kuweka moyo wako madhabahuni pa Bwana!
Kufuatana na Mathayo 6:2 – 4 “sadaka” yako na “hazina” yako, vina uwezo wa kuubeba moyo wako, na kuufanya moyo uwe mahali zilipo!


Lakini “sadaka” yako inapotolewa toka kwenye “hazina” (fedha) yako uliyofanikiwa kuipata, sadaka hiyo inatumika pia kuuficha moyo wako katika madhabahu ya Mungu!
Lengo la “sadaka” yako “kuulinda” moyo wako, ni ili mafanikio yako yasije yakaufanya moyo wako umsahau Mungu, na usimsikilize anapokusemesha!


Neno la Mungu linatupa angalizo hili tunaposoma hivi: “Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulichonacho kitakapoongezeka; basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako…” (Kumbukumbu ya Torati 8:12 – 14).


Neno la Mungu linaendelea kusema hivi: “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako kama hivi leo” (Kumbukumbu 8:18).
Njia mojawapo ya kumsahau Mungu – ni kule kutokusikia sauti ya maelekezo yake wakati unaishi katika mafanikio! Na njia mojawapo ya kumkumbuka Mungu – ni kule kusikia sauti ya maelekezo yake, na kuyatekeleza; wakati unaishi katika mafanikio!


Na njia mojawapo ya kuufanya moyo wako uwe mwepesi kumsikia Mungu na kumtii; wakati unaishi katika mafanikio, ni kwa wewe kukumbuka kutoa sadaka zako inavyokupasa!
Utoaji wako wa sadaka kwa imani – unaondoa moyoni mwako uzito wa kumpenda Mungu; na badala yake unalainisha moyo wako – uendelee kumpenda Mungu – na uwe na utayari wa kumsikiliza anachokuelekeza!
Tutaendelea wiki ijayo na vipengele vilivyobaki.
Mungu awabariki

Comments