Namna Roho Mtakatifu anavyowaongoza watu, katika kutembea na kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.

Na Mwl Christopher Mwakasege
Bwana Yesu asifiwe sana!
Tunaendelea na mfululizo wa somo hili, tunalojifunza juu ya namna Roho Mtakatifu anavyowaongoza watu, katika kutembea na kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.
Ukiweza kulijua hilo na ukalifuata – itakuwa ni vyepesi kuujua pia mpango ambao Mungu anao kwa ajili ya maisha yako, na ukautekeleza!
Leo tujifunze namna Roho Mtakatifu anavyotumia “neno la Mungu” lililomo katika biblia, kwa ajili ya kukuongoza katika mapenzi ya Mungu, na katika mpango wa Mungu – kwa ajili ya maisha yako.
Ukitaka kufanikiwa katika jambo hili, ni muhimu ujizoeze kujiombea uweze “kusikia sauti ya neno la Mungu” na pia uweze “kulielewa neno la Mungu”!
Hii ni kwa sababu zifuatazo:
(i) Kufuatana na Mathayo 13:13 unaweza kusikia neno lakini usisikie “sauti” ya neno hilo! Neno la Mungu lina “sauti” ndani yake (Zaburi 103:20), na usiposikia itakuwa ina maana ya kuwa “umesikia” lakini “hujasikia” – kwa msemo wa Yesu wa Mathayo 13:13,14.
(ii) Kufuatana na Mathayo 13:19 unahitaji kuelewa neno unalosikia – la sivyo halitakaa muda mrefu moyoni, na kwa ajili hiyo halitaweza kukusaidia katika maisha yako! Yesu Kristo alisema: “Kila mtu alisikiapo neno la ufalme na asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake”.
(iii) Ni rahisi kulitekeleza lile neno la Mungu ambalo wewe umelisikia na kulielewa ya kuwa linakuhusu wewe binafsi! Hii ni kwa sababu, njia mojawapo ambayo Mungu anaitumia kukusaidia, na kukuongoza, ni kwa kutumia neno lake – wewe binafsi! (Zaburi 107:19,20 na Isaya 55:11 na 2 Timotheo 3:16,17).
Kwa mantiki ya sababu hizo hapo juu – hatua muhimu kwako baada ya kujiombea maombi hayo – ni kujiuliza maswali yafuatayo na kisha kupata majibu yake.
Maswali hayo ni haya: Swali la 1: Unaisikiaje sauti ya neno lake “unaposoma” neno la Mungu – na ukajua ni Roho Mtakatifu anaongea na wewe binafsi?
Swali la 2: Unasikiaje sauti ya neno lake, “unaposikiliza” mahubiri au mafundisho ya neno la Mungu – na kiasi kwamba ukajua ni Roho Mtakatifu anaongea na wewe binafsi?
Swali la 3: Unasikiaje sauti ya neno lake, “unapoletewa” kwenye mawazo kumbukumbu ya mstari fulani, au neno fulani la biblia – na ukaweza kujua ya kuwa hayo si mawazo binafsi – bali ni Roho Mtakatifu anaongea na wewe binafsi kwa nja hiyo?
Njia zifuatazo zitakusaidia kutambua ikiwa Roho Mtakatifu anakusemesha wewe binafsi, kwa kupitia neno la Mungu unalosoma, au unalosikia, au linalokujia mawazoni mwako:
Njia ya 1: Kwa wewe kupata ufahamu moyoni mwako ya kuwa neno unalolisoma linakuhimiza kuchukua hatua ya kufanya.
Unaposoma kitabu cha Danieli 9:1 – 3 utaona ya kuwa Danieli anasema “kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii….” Ufahamu alioupata Danieli moyoni mwake – ulimsukuma kuombea kile kilichokuwa kwenye neno alilolisoma ili kitimie!
Pamoja na kwamba “neno” halikuwa limeandikwa ya kuwa Danieli ataliombea – lakini Roho Mtakatifu alimpa “kusikia na kuelewa” alichotaka “kwake” juu ya neno lile alilolisoma! Umenipata ninachotaka ukione hapo?
Ndilo tunaloliona pia tunaposoma yaliyotokea wakati wa kipindi cha kuhani Mkuu aliyeitwa Ezra. Biblia inasema: “Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa” (Nehemia 8:8)
Ukizifuatilia zaidi habari hizi, utaona ya kuwa kila walichopata ufahamu walipokuwa wakisoma neno la Bwana, walikuwa wanapata msukumo wa kukitekeleza!
Watu wa kanisa lililokuwa Korintho walipata “huzuni ya Mungu” mioyoni mwao waliposoma waraka ulioandikwa na mtume Paulo.
Unaposoma kitabu cha 2 Wakorintho 7:8,9 utaona ya kuwa “huzuni ya Mungu” waliyoipata waliposoma waraka ule, ilikuwa ni ujumbe kwao toka kwa Roho Mtakatifu ya kuwa walitakiwa “watubu” kabla hawajapata msaada (wokovu) toka kwa Mungu!
Kwa hiyo – na wewe fuatilia kwa karibu, “ufahamu” unaoupata unaposoma neno la Mungu; maana inawezekana kabisa, ndani yake, kuna “ujumbe” wa Roho Mtakatifu kwa ajili yako binafsi!
Njia ya 2: Kwa wewe kuangalia moyoni mwako umepokea kitu gani toka kwenye neno unalolisikia likifundishwa au likihubiriwa!
Kwa mfano, neno linalomfanya msikiaji atetemeke anapolisikia, ina maana neno hilo limebeba ujumbe wake binafsi toka kwa Roho Mtakatifu – ili aufanyie kazi. Soma Isaya 66:2,5.
Mwingine badala ya kutetemeka anaposikia neno, yeye huwa “analia”; au “anasikia msukumo moyoni mwake kuchukua hatua”; au “anapata uhakika moyoni mwake juu ya kile anachokisikia…yaani anapata “amani”; nakadhalika!
Njia ya 3: Kwa wewe kuona “neno” lililoingia moyoni mwako linatengeneza “mkakati” wa kiutekelezaji ili ufanikiwe katika ulifanyalo
Tena – wakati mwingine linatangulia kuingiza “wazo” moyoni mwako ambalo linafanana na mstari wa neno la Mungu. Na unapoendelea kulitafakari linatengeneza mtiririko wa mawazo unaokupa “mbinu” ya kiutekelezaji.
Unaposoma Isaya 55:8 – 11 na Waebrania 4:12,13 utaona ya kuwa kuna uhusiano kati ya “wazo” na “neno la Mungu” na “njia” (mbinu/mkakati).
Mungu alipotaka wafalme wahusike na ujenzi wa hekalu – utaona ya kuwa Mungu aliweka neno lake mioyoni mwao kama “wazo” – lililokuwa na “mbinu” za kiutekelezaji ndani yake.
Juu ya jambo hili tuangalie jinsi Mungu alivyoweka “mawazo” moyoni mwa mfalme Koreshi wa Uajemi; na mfalme Sulemani wa Israeli.
Mungu alipoweka wazo hilo moyoni mwa mfalme Koreshi – biblia inasema “Bwana akamwamsha roho yake Koreshi”. “…ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa…” (Ezra 1:1).
Mungu alipoweka wazo kama hilo moyoni mwa mfalme Sulemani – biblia inasema juu ya: “mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya…”; yaliyohusu “…kuijenga nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme…” (1 Wafalme 9:1).
Nakuombea na wewe ili uwe unaweza kujua Roho Mtakatifu anapotumia neno la Mungu katika kukuongoza binafsi!

Comments