![]() |
Na Mtume na Nabii: Josephat Elias Mwingira |
Wewe uliyeokoka uwe sababu ya kuwafanya
wale waliomjua Mungu kwa kupitia wewe wasirudi nyuma. Usikubali kuwa
sababu ya kuwaumiza wengine kwa tabia yako au maneno yako na kusababisha
wale Mungu aliokupa kuwalea wakashindwa kusonga mbele.
Imani sio kwenda Kanisani tu bali Imani pia ni kuwapenda wengine na kusababisha wavutwe na kumfuata Mungu.
Mtu aliyeokoka na kukua kiroho anapokutana na changamoto anatakiwa kutiwa moyo ili asonge mbele sio kubembelezwa.
Huu ni mwaka wa kujibiwa maombi yetu,
lakini ili maombi yetu yapate kujibiwa ni lazima tufanye mapenzi ya
Mungu kwa kukubali kuzaa matunda na matunda yetu yapate kukaa, sio
unazaa matunda baada ya miaka miwili yanakufa. Kama ambavyo binadamu
akibeba mimba ikaharibika anaumia ndivyo hivyo Baba yetu wa Mbinguni
anahuzunika mtu anapookaka na kurudi nyuma. Ili uweze kuwa bora katika
maisha yako ni vizuri kuhakikisaha hauwi sababu ya kuwakwaza wengine kwa
maneno au matendo yako.
Katika utaratibu wa Mungu Mume anatakiwa
kumfurahisha Mungu kwa gharama yoyote, lakini mke anatakiwa
kumfurahisha Mume wake na watoto wanatakiwa kumfurahisha mama yao.
Mwanaume asiye na akili anasubiri mke wake akatafute pesa kwaajili ya
kutunza familia, lakini mwanaume mwenye akili nzuri anatafuta pesa kwa
bidii analeta chakula nyumbani na mke anampikia na kumpetipeti.
Unapokubali kufanya hivyo unasababisha
Amani, furaha na ustawi mkubwa katika familia yako na ugomvi
hautakuwepo. Watoto lazima wamuheshimu mama yao na wakati mama
anapomuadhibu mtoto wewe baba usimtetee mtoto hii itasaidia watoto wako
kuwa na adabu. Mama kujua kuomba sana kusikufanye umpuuze mumeo kwani
yeye ni kichwa cha familia.
Unapokubali kuoa ina maana umekubali
kubeba majukumu ya familia, ukubali kuambiwa sukari imeisha, chumvi,
kitenge na unapoambiwa usikasirike kwani ni jukumu la baba kutunza
familia sio mama. Kwa asili wanaume hawapendi kelele ndio maana Mungu
amesema ishi na mke wako kwa akili na sio maombi, wewe baba usianze
kufanya maombi ili sukari ije bali nenda kafanye kazi kwa bidii na
umtumikie Mungu kwa bidii ndipo utaona baraka katika familia yako,
katika kitabu cha mwanzo kimeeleza nafasi ya mwanamke kuwa ni msadizi na
msaidizi hatoi amri kwa kichwa(mume). Ukikubali kuolewa ukubali
kukandamizwa kwa sababu kichwa kiko juu yako(mume) na wewe ni kama
kiwiliwili. Ukikubali kuyafanya haya utamwona Mungu kwa sababu Mungu
anaonekana sana katika familia.
Ni hatari sana familia ambayo haiwezi
kumsikiliza mama yao na kwa kufanya hivyo hiyo familia itaharibikiwa.
Kazi ya baba ni kuonyesha njia na akisha onyesha njia mama ana kazi ya
kuielekeza familia yake namna ya kupita katika ile njia. Mama unatakiwa
kukaa mkao wa mama na baba unatakiwa kukaa mkao wa baba na wewe binti
kaa mkao wa mwanamke sio unakaa kama dume, unatakiwa uonyeshe kuwa
unafaa kuwa mama wakati wowote.
Mwanaume mwenye akili hata mke wake
anajisikia fahari kuolewa nae. Unatakiwa kuangalia je tabia yako
inamuonekano wa Mungu au unaonyesha una shetani? Unapokubali kufanya
mapenzi ya Mungu, utaona mapenzi ya Mungu katika maisha yako kwani Mungu
sio dhalimu.
Siku hizi wanawake wanataka faraja kwa
waume zao lakini biblia haisemi hivyo bali inasema mume anatakiwa kuwa
faraja kwa Mungu na mke anatakiwa kuwa faraja kwa mume na watoto
wanatakiwa kuwa faraja kwa mama yao, ndio maana neno linasema mwana
mpumbavu ni mzigo wa mama yake. Binti na Kijana wa kazi wanatakiwa
kumsaidia mke na sio wewe mwanaume, kazi yako wewe mwanaume ni kutafuta
pesa ni ujinga kupangiana na mume wako zamu ya kupika. Mwanaume lazima
ukubali kuchoka, mwanaume ni mpiganaji. Onyesha wewe umekubalika na
Mungu kwakuweka familia yako katika hali ambayo Mungu akikaa kule juu
anatamani kuitembele hiyo familia,
Tabia yako inaambatana na mawazo yako na
mawazo yako yanaambatana na maombi yako na tabia yako inaonyesha maombi
yako yatakuwa ya namna gani, jitahidi kwa nguvu zako zote kutafuta
mapenzi ya Mungu. Mungu hawezi kuku bariki wakati wewe hautunzi familia
yako. Haulindi heshima ya Mungu watu wanamtukana Mungu kwa sababu ya
tabia yako pale nyumbani. Unaonaje ukapiga magoti ukamwambia Mungu ni
dhambi gani inayonifanya nisiwe furaha yako? Mungu ni mwaminifu
atakuonyesha ili ubadilike na usonge mbele.
Comments