![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Ukitaka kuwakwaza watu waambie kwamba nyimbo za kidunia ni machukizo.
Kwanini wanakwazika?
Ni kwa sababu nyimbo hizo ndizo wamejaza mioyoni mwao.
Unakuta mteule wa MUNGU kwenye simu yake ana nyimbo 100 kati ya hizo 95 ni nyimbo za kidunia na nyimbo 5 ndizo za MUNGU. Huko ni kupungukiwa maarifa ya kiroho.
Nilipookoka mwaka 2008 nilikaa miezi mitatu na kujitathimini nikagundua Nina nyimbo za kidunia zaidi ya 400 lakini nyimbo za MUNGU Nina albamu tu moja ya Rose Muhando, moja ya Angela Chibalonza, moja ya Fanuel Sedekia, moja ya Bahati Bukuku, Moja ya  Shusho na Moja ya Upendo Nkone. Nyimbo hizo zilikuwa katika CD.
Baada ya kufanya tathimini hiyo roho yangu iliuma na nikajulishwa rohoni kwamba nyimbo za kidunia ni mapando ya shetani ili kuwafanya watu wasiwe upande wa MUNGU. 
Baada ya kujua hivyo nikatupa CD zote na DVD za nyimbo za kidunia, nikafuta nyimbo zote kwenye computer yangu na kwenye simu yangu. 
Namshukuru MUNGU alinihurumia na kujitenga na nyimbo za kidunia ndio maana nikaweza kupata nguvu za rohoni.
Ndugu Wewe una Nyimbo ngapi katika simu Yako au computer Yako?
Solomon alikuwa na Nyimbo 1050 na katika hizo hakukuwa na Nyimbo za kuzimu au za shetani.
1 Wafalme 4:32 ''Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.''
✓✓Ukitaka kuwajua watu walio mwilini asilimia kubwa utapawata katika kundi la wasikilizaji sana nyimbo za kidunia. 
✓✓Wenye tamaa mbaya wengi ni hao hao wasikilizaji wa Nyimbo za kidunia na binafsi Mimi sijawahi kumuona mtu anayefunga na kuomba kila Mara akiwa mshabiki sana wa nyimbo za kidunia, ataanzaje kwanza kufunga wakati moyoni mwake amewajaza tu wasanii wa nyimbo za kidunia.
Ngoja Leo kwa Neema ya MUNGU nijulishe ujumbe huu ambao ROHO MTAKATIFU alinipa mwaka 2015 nikauandika  lakini kwa Neema ya KRISTO leo mwaka 2025 ndio nauona kule nilikouandika.
Ni kwamba Kuna Nyimbo aina 3 ambazo watu husikiliza.
1. Nyimbo za MUNGU.
1 Nyakati 16:42 "na pamoja nao Hemani na Yeduthuni wenye baragumu na matoazi, kwa hao watakaovumisha sauti, na vinanda kwa ajili ya hizo NYIMBO ZA MUNGU; na hao wana wa Yeduthuni wawepo mlangoni."
Nyimbo za MUNGU kwa Jina lingine zinaitwa Nyimbo za Injili, hizi zinaweza kuhusisha Nyimbo za kawaida za Injili, Nyimbo za kumsifu MUNGU katika KRISTO YESU, tenzi za rohoni, Nyimbo za Wokovu, Nyimbo za kuabudu, pambio n.k
Nyimbo hizi zinaweza kuimbwa na kwaya au Mkristo mmoja mmoja.
2. Nyimbo za shetani.
Amosi 6:5 "ninyi mnaoimba NYIMBO ZA UPUZI pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi;"
Nyimbo zote za kishetani ni Nyimbo za kipuuzi mbele za MUNGU.
Amosi 5:23 ''Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.''
✓✓Ukiona Nyimbo MUNGU anaikataa ujue sio Nyimbo yake, na kama sio Nyimbo yake MUNGU ujue ni Nyimbo ya shetani.
Hizi ni Nyimbo ambazo chanzo chake ni shetani, Jina lingine zinaitwa Nyimbo za kidunia.
Ni Nyimbo ambazo ni za kuzimu ambazo sehemu kubwa ya wanaoziimba Wana mikataba na shetani au Wana ushirika na shetani.
Mahali pengine zinaitwa Nyimbo za walevi.
Zaburi 69:12 "Waketio langoni hunisema, Na nyimbo za walevi hunidhihaki."
3. Nyimbo za Mamlaka za kibinadamu za Duniani.
Nyimbo hizi ni Nyimbo nzuri kama hazina matusi ndani yake.
Nyimbo hizi mfano wake ni Nyimbo za Harusi.
Zaburi 78:63 "Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa NYIMBO ZA ARUSI,"
Nyimbo hizi ni kama Nyimbo za Taifa, Nyimbo za hamasa mfano kuhamasisha watu kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa n.k
Nyimbo za kushangilia ushindi wa kivita n.k
Mfano hai ni huu
1 Samweli 18:6-7 " Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake."
Hapa Wanawake hawa hawakuimba wimbo wa MUNGU Wala hawakuimba wimbo wa Shetani ila wimbo wa kujulisha kilichotokea katika Taifa lako wakishangilia ushindi dhidi ya Maadui zao.
Waliomba hawa walikuwa Watu wa MUNGU Biblia haisemi kwamba ilikuwa dhambi maana ni Nyimbo zinazoruhusiwa hata kiroho.
Leo Kuna Nyimbo mfano za kuhamasisha Askari kulinda nchi zao, Watoto kuzingatia Elimu n.k
Hizo nyimbo sio za MUNGU ila sio Dhambi kuziimba kwa Wewe mteule wa KRISTO.
Mfano hai ni Nyimbo za mashuleni ambazo zimejaa mafundisho na hamasa njema, ndio maana hakuna Mtu amawahi kuzilalamikia Nyimbo za shuleni.
◼️Nyimbo za MUNGU zinafahamika, zinampa MUNGU Utukufu, zinamwinua YESU KRISTO na zinadhihilisha Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
◼️Nyimbo za mamlaka za kibinadamu za Duniani zinafundisha, zinaelemisha, zinahamasisha mambo mema kwa jamii na zinaungamisha watu wa jamii husika.
◼️Nyimbo za shetani huhamasisha  watu kutenda dhambi, zinamwinua shetani, zinafundisha mambo mabaya, zinachochea mabaya, zinawatenga watu mbali na Bwana YESU KRISTO Mwokozi wa ulimwengu na Nyimbo hizo zinauvuvio wa Nguvu za giza.
Ndio maana ujumbe wangu unamtaka kila Mkristo mwenye akili timamu na anayetarajia uzima wa milele asizipe nafasi kwenye Maisha yake.
Ndugu zangu Biblia inasema kwamba msiipende dunia na mambo yaliyomo duniani yaliyo kinyume na MUNGU mojawapo ni miziki ya kidunia. 
1 Yohana 2:15 "Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake."
◼️Ukipenda nyimbo za kidunia lazima tu kumpenda MUNGU na kumtii kutaondoka ndani yako, kanisani utaona ni mzigo kwenda na kwenda mkesha hutapenda badala yake utaenda disko.
 Kama umezinduka akili leo  achana na Nyimbo za kidunia.
Usiharibu uhusiano wako na MUNGU kwa sababu ya marafiki.
Kama marafiki zako wanakushawishi kutenda dhambi ni bora sana ukavunja urafiki na wao.
 Nyimbo za kidunia ni mojawapo Wa mifano ya mfalme uzia.
 Isaya 6:1, hajatoka maishani mwako ni vigumu kuuona uso wa Bwana. 
Na ni vigumu kuiacha miziki ya kidunia kama mtu mwenyewe hajaamua kuifuta moyoni mwake na kumgeukia Bwana.
 Asante Yesu tangu unitoe Misri miaka mingi iliyopita ulifanikiwa kuniondolea hata hamu ya kusikiliza miziki ya kidunia. 
Wateule Wa Bwana YESU KRISTO tujitahidi kupanda Neno mioyoni mwetu na sio kujaza Nyimbo za shetani.
Je unapenda sana kusikiliza mziki?
Upo mziki wa MUNGU utafute huo kutoka katika Nyimbo hizo ambazo Biblia inazitaja.
1. Nyimbo za kumsifu MUNGU wa Mbinguni.
 Matendo  16:25 "Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba MUNGU na kumwimbia NYIMBO ZA KUMSIFU, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza."
2. Nyimbo za kumshukuru MUNGU wa Mbinguni.
Nehemia 12:46 ''Kwa kuwa siku za Daudi zamani, Asafu alikuwa mkuu wa waimbaji, na juu ya NYIMBO ZA SIFA NA  SHUKRANI kwa Mungu.''
3. Nyimbo za rohoni 
Waefeso 5:19 "mkisemezana kwa zaburi na tenzi na NYIMBO ZA ROHONI, huku mkiimba na kumshangilia BWANA mioyoni mwenu;"
4. Nyimbo za Wokovu wa KRISTO YESU.
Zaburi 32:7 "Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, Utanizungusha NYIMBO ZA WOKOVU.''
5. Tenzi za rohoni.
Wakolosai 3:16 "Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na TENZI ZA ROHONI; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu."
Asante kama unanielewa ndugu yangu.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU KRISTO? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO.
+255714252292.
Ubarikiwe sana kwa kusoma somo hili.

Comments