SABATO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalomu watu wa MUNGU.
Karibu tujifunze ujumbe huu.
Sabato maana yake ni pumziko au kupumzika.
Sabato ni siku ya saba ya wiki ya kiyahudi.
Sabato maana yake ni kupumzika baada ya kazi.
Waisraeli waliamriwa kuishika sabato siku zote.


Kutoka 31:16-17 "Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika."


Na sisi wateule wa MUNGU ambao ni kabisa lake, baada ya kumaliza kazi yetu duniani itafuata pumziko ya milele yaani sabato ya milele.
Waisraeli walikuwa na siku moja ya kupumzika na kuabudu, lakini kanisa sasa linaagizwa kuukomboa wakati ili baada ya kumaliza kazi duniani ifuate pumziko ya milele ambayo ni sabato ya milele.
Biblia inaliagiza kanisa la MUNGU kwamba;
'' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.-Wakolosai 4:5 ''

 
Tena Biblia inasisitiza kwamba ni lazima kanisa liukomboe wakati.
Waefeso 5:15-17 " Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya BWANA."


Kanisa la MUNGU ni lazima sana liukomboe wakati kwa kuamua kufanya yaliyo ya MUNGU wakati wote.
Kanisa halina muda wa kupoteza katika yaliyo ya kidunia.
Kanisa linatakiwa kuukomboa wakati.
Kanisa sio jengo Bali wateule wa KRISTO wote.
Kanisa sio Israeli ndio maana sio maagizo yote ya Israeli ni maagizo ya kanisa pia.

Ni muhimu sana kila mtu kumwabudu MUNGU kila wakati na sio jumapili tu au jumamosi tu.
Hatujamaliza kazi yetu duniani hata tupumzike.
Wenye ROHO MTAKATIFU wanasema " Neno Moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na kutafakari hekaluni mwake.-Zaburi 27:4"


Ni heri tukawa wa nyumbani wa MUNGU siku zote.
Wanaoenda nyumbani mwa MUNGU Mara moja tu kwa wiki ni ngumu sana kukua kiroho hivyo inatupasa sana kuwa watu wa Nyumbani mwa MUNGU siku zote.
Kumbuka Biblia inasema, 1 Yohana 2:17 "Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."


Ni muhimu tufanye yampendezayo MUNGU siku zote.
Ni muhimu sana kuwa katika ushirika wa ROHO MTAKATIFU na ni muhimu sana kuishi maisha matakatifu siku zote.
Bwana YESU anasema " imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa.-Luka 18:1"

 
Kumbuka Bwana YESU ndiye Bwana wa sabato na ataileta sabato ya milele yaani pumziko ya milele kwa sisi wateule wake.
Sabato ya wayahudi ilikuwa ni Sabato ya mwilini yaani kupumzika mwilini,sasa YESU baada ya kuja aliileta Sabato ya rohoni.
Watu wanapokuwa katika dhambi wanakuwa katika utumwa,muda wote wanakuwa wamebeba mizigo kadha wa kadha hata kama wamepumzika mwilini lakini rohoni wanakuwa wamebeba mizigo,wanakuwa bado wapo kwenye utumwa bado wanakuwa wamelemewa na mizigo,kama mizigo ya Rushwa,pombe,mizigo ya uzinzi,mizigo ya wizi, uongo, uchawi na dhambi zote.
Sasa mtu anapompokea YESU kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake yaani anapotubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziaacha dhambi hizo,mtu huyo sasa anakuwa anaondolewa mizigo ile ya rohoni iliyokuwa inamwelemea na sasa mtu huyo anakuwa huru kabisa,anakuwa sasa amepumzika rohoni hata kama anakuwa anatembea anakuwa yupo katika pumziko, rohoni anakuwa yuko katika pumziko ambalo ndio Sabato na anayetuondolea mizigo hiyo ni YESU kwa kumpokea yeye kwa kutubu dhambi kwa kumaanisha kuziacha dhambi zote.
Kumbuka Luka 6:5 inasema "Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato."

 
Bwana YESU ataileta pumziko ya milele kwa kanisa lake.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments