SALA YA TOBA NI YA MUHIMU SANA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza kwa habari ya sala ya toba.
Mtu mmoja akaniuliza "Nimeshabadili majina Mara nyingi sana, je jina langu nikiokoka litaandikwa vipi kwenye kitabu cha uzima?
Hata humu mtandaoni nimeshabadili jina zaidi ya Mara 10, je kwenye kitabu cha uzima Siku nikimpokea YESU jina langu litaandikwa lipi?"
 

Ndugu huyo alitamani kumpokea YESU lakini majina yake kuwa mengi ilimchanganya sana.
Kama uko mtu wa aina hiyo naomba nianze kwa kesema kwamba.
Roho yako ndio jina lako hivyo hata kama huna jina kabisa duniani na hakuna mwanadamu amewahi kukuita jina lakini kama ni mdhambi jehanamu utaenda na kama ni mteule mtakatifu wa MUNGU uzima wa milele utaenda tu.
Kubadilibadili majina inaweza ikakuathiri wewe katika maisha ya duniani lakini sio baada ya hapo.
Kuna haki zako duniani unaweza usizipate kabisa kwa sababu ya kubadilibadili majina, lakini katika maisha ya baada ya kuondoka kwako duniani yataamuliwa na matendo yako na utii wako kwa MUNGU na Neno lake Biblia.

 Bwana YESU anasema ''Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. - Yohana 10:28'' 
Kwa njia gani Bwana YESU anatupa uzima wa milele?
Ni kwa kumpokea yeye kama Mwokozi na kuanza kumwabudu MUNGU katika kweli yake ya Biblia kisha kuishi maisha mataktifu daima.
Katika kumpokea YESU ni lazima tumpokee kwa kukiri kwa imani sana.
Warumi 10:9-10 ''wa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.'' 
Kumkiri huko YESU hata unapata uzima wake ndiko kunaitwa Sala ya Toba.
Sala ni nini? 
Sala ni maombi kwa MUNGU.
Sala ya toba ni nini?
Sala ya toba ni maombi maalumu ya kutubu kwa MUNGU kisha kuahidi kuanza kuishi kwa kumpendeza MUNGU.
Kwa kila anayempokea YESU ni lazima ajue kwamba sala ya toba ya kinywa ni lazima ihamie katika matendo, Hilo ndilo kusudi la MUNGU.
Kama umekiri kwamba sasa utaanza na YESU kwa kumtii na kulitii Neno la MUNGU hakika unatakiwa ufanye hivyo katika matendo, hilo ndilo kusudi la MUNGU.
Katika sala ya toba najua ulisema kwamba ''Naufunga ukurasa wa dhambi na ninafungulia ukurasa wa matendo mema'' maana yake unatakiwa uache dhambi na uanze kutenda mema, unaanza kwa kukiri kisha unaanza kuishi sawasawa na ulivyokiri mbele za MUNGU.

Ndugu yangu, Jambo muhimu sana nakuomba Fanyia Kazi Sala Ya Toba Uliyoongozwa Siku Ulipompokea BWANA YESU. 
Sala Hiyo Ya Toba Ni Maungamo Ambayo Unatakiwa Uyaishi
Waebrania  4:14 ''Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, YESU, Mwana wa MUNGU, na tuyashike sana maungamo yetu.''
 Biblia inatuagiza sana kuyashika sana maungamo yetu.
Ungamo ni nini?
=Ungamo ni jambo unalolikiri kuwa ni kosa, hivyo baada ya kukiri unaomba msamaha na kubadilika kwa kutokutenda kosa lile tena.
1 Yohana 1:9 ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye(MUNGU) ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.''

 =Ungamo ni hali ya kuungama.
=Kuungama ni kukubali ukweli wa mambo uliyofanya lakini baada ya hapo unaapa kutokurudia makosa yale tena.
Yakobo 5:16 '' Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.''

=Kuungamisha ni kumfanya mtu aombe msamaha.
Kwa MUNGU tunaungama dhambi zetu zote kisha tunakubali Bwana YESU awe mwokozi wetu na damu yake inatutakasa na tunakuwa safi.
Tangu zamani za Biblia watu walioamua  kuokoka, waliungama na kuacha uovu wao wa kwanza.
Matendo 18:19-20 ''Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la BWANA lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. ''
Kama hujamkiri YESU ni muhimu sana ukamkiri na kuanza kumtii.
Kama hujaongozwa sala ya toba hakikisha unawafuata wachungaji ili wakuongoze sala hiyo kisha wakusaidie kiroho ili uendelee kuishi maisha matakatifu.

 Biblia inatushauri kwamba tunashike maungamo yetu yaani tusibadilike kutoka katika hali yetu ya kumkiri Bwana YESU kama Mwokozi wetu.
Tusirudi dhambini tena maana tuliungama na kuziacha dhambi zetu.
Waebrania 10:23-25 '' Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.''

 Najua Ulimpokea YESU Kwa Imani(Warumi 10:9-10) Hivyo Mshike Sana YESU Na Kila Kile Akitakacho Yeye. Najua Uliapa Kuacha Dhambi Zako Zote, Endelea Kuacha Dhambi Zote. 
Najua Ulitubu(Matendo 3:19).
 Endelea Kubaki Katika Utakatifu. 
Najua Uliufunga Ukurasa Wa Dhambi Na Ukaufungulia Ukurasa Wa Mema Tu. 
Shika Maungamo Yako hayo Ndugu.
Tangu zamani wateule wa MUNGU waliungama dhambi zao.
1 Timotheo 6:12 '' Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi.''
 Ulitubu mbele za watu wengi, hakikisha hurudi tena katika dhambi.
Ulimkiri YESU mbele za mashahidi wengi, hivyo hutakiwi kumkana tena. Kumbuka kutenga dhambi ni kumkana YESU, ni hatari sana.

Kumbuka Bwana YESU Alitoa Maisha Yake Bure ili tu kutuokoa mimi na wewe.
Yeye Anasema Katika Yohana 10:18 Kwamba "Hakuna Mtu Anayeninyang'anya Maisha Yangu; Mimi Nayatoa Kwa Hiari Yangu Mwenyewe. Ninao Uwezo Wa Kuyatoa Na Uwezo Wa Kuyachukua Tena. Hivi Ndivyo BABA Alivyoniamuru Kufanya. "

Ndugu Zangu, YESU Ana Uwezo Wote Alitoa Maisha Yake Kwa Ajili Ya Watu Wa Mataifa Yote Ili Kwamba Wote Wamwamini Na Kuokolewa.
Ni Heri Ndugu Uhakikishe Kwamba Wewe Ni Mmoja Wa Wale Waliookolewa Na BWANA YESU. 





 Wokovu Wa KRISTO Ndicho Kitu Pekee Kinachoweza Kukutofautisha Wewe Na Watu Wa Dunia Kama Tu Utautii Na Kuuishi Wokovu Huo. 
Utakatifu Ulionao Unatakiwa Uutunze Wewe Mwenyewe Binafsi Na Sio Watu Wengine Wakutunzie. 
Wachungaji Hawatakiwi Wakutunzie Utakatifu Wako Bali Utunze Mwenyewe. 
 Habari Za Kuwa Mtakatifu Ukiwa Jirani Na Mchungaji Au Kanisa Tu hazifai. Kama Unavyokuwa Mtakatifu Kanisani Hakikisha Na Nyumbani Unakuwa Mtakatifu Pia.
Shika ungamo lako la kuacha dhambi zote na kuanza kumtii Mwokozi YESU na neno lake.
 Mithali 28:13 ''Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.''
Ni muhimu sana kuziungama dhambi zako zote na kuziacha.

 Wokovu Ulionao Katika KRISTO Utunze Na Uuishi, Dumu Katika Wokovu Wa Bwana YESU. 
Huwezi Kusema Umeokoka Wakati Huishi Maisha Matakatifu.

Neema Ya MUNGU Ni Ya Bure Lakini Ni Ya Thamani Sana Kwako Na Unatakiwa Kuitunza Sana Neema Ya MUNGU. 
Usiichezee Wala Kuijaribu Neema Ya MUNGU. 
Ndani Ya Neema Ya MUNGU Kwa Wanadamu Kuna Wokovu Wa KRISTO, Kuna Huduma Za ROHO MTAKATIFU, Kuna Utakaso Kwa Wanaoamua Kutubu na Kuna Vipawa Na Karama 

Bwana YESU alifanya kazi kuu mno kwa ajili yako na kwa ajili yangu.
Ni muhimu sana tukashika maungamo yetu na tuendelee kuishi maisha ya wokovu mataktifu katika yeye Bwana YESU.
 Ufunuo 5:9 Inasema "Basi Wakaimba Wimbo Huu Mpya, Wewe Unastahili Kukitwaa Hicho Kitabu Na Kuivunja Mihuri Yake. Kwa Sababu Wewe Umechinjwa, Na Kwa Damu Yako Umemnunulia MUNGU Watu Kutoka Kila Kabila, Lugha, Jamaa Na Taifa.".
Ndugu Zangu, YESU KRISTO Anatupenda Sana, Anataka Wewe Unayesoma Ujumbe Huu Uende Uzima Wa Milele, Mpokee Tu Bwana YESU Leo Ili Jina Lako Liandikwe Kwenye Kitabu Cha Uzima Mbinguni kisha anza kuishi maisha matakatifu ndani ya wokovu huo wa ajabu sana wa injili ya KRISTO.
Wewe Unapendwa Sana Na Bwana YESU. 

Simama Kwa BWANA, Songa Mbele Kwa BWANA, Mche BWANA Na Mtii BWANA. 

Baada ya kumpokea YESU Tunatakiwa Kumtumikia MUNGU Katika Uaminifu Na Uaminifu Huo Unatunzwa Na Utakatifu.

Kuwepo Kanisani Ili Ujifunze Neno La MUNGU Ni Neema Ya MUNGU Maana Sio Wote Wana Uwezo Wa Kuona Kama Unavyoona Wewe Hata Wawe Kanisani Kujifunza Neno La MUNGU. 
Sio Wote Wana Uwezo Wa Kutembea Kama Wewe Hata Waje Kanisani Kujifunza Neno La MUNGU.
 Sio Wote Wanaweza Kusikia Kama Wewe Unavyosikia Hata Walisikie Neno La MUNGU Kama Wewe. 
Itumie Vizuri Neema Ya MUNGU Ndugu.

 Jambo jingine ni kwamba unapoamua Kufanya Jambo Jema La KiMUNGU Hiyo Ni Hatua Yako Iliyo Hai Ya Kukua Kiroho. Mtume Petro alimkana YESU Mara 3 lakini ilibidi pia petro athibitishe Mara 3 kumkiri kwake upya YESU.
Petro aliulizwa "Je wanipenda" 
 Yohana 21:15-17 ''Basi walipokwisha kula, YESU akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia , Naam ,Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. YESU akamwambia, Lisha kondoo zangu.   ''
kumbuka mwanzo petro alisema alipokuwa anamkana YESU kwamba "Simjui YESU" lakini wakati huu Petro ulisema "Ndio Bwana wewe wajua kwamba nakupenda" Petro alikuwa anatakaswa wakati huu.
Ni vibaya sana kumkana YESU na wakati mwingine kuna gharama kubwa hadi urudi kwenye utakatifu wa kwanza.
Ndugu nakuomba tubu wakati huu na simama imara kwa YESU bila kurudi dhambini tena.
kwa wasoma Biblia naamini wamejifunza kitu kutokana na tukio la Mtume Petro kumkana YESU Mara 3 kisha baadae akatakiwa kumkiri YESU Mara tatu kama anampenda.
Kuna sehemu  Biblia Kwenye moja ya nyaraka za Yohana  inasema kwamba
''Wanaofanya dhambi ni kwa sababu hawakumjua MUNGU.''

Ndugu nakuomba usiwe kwenye kundi la ambao hawakumjua MUNGU.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Ubarikiwe sana Na nakuomba nisaidie kushare kwa marafiki zako ili na wao wajifunze Neno la MUNGU.

Comments