FAIDA TANO(5) ZA MAOMBI YA TOBA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU



Shalom Mteule wa KRISTO upendwaye sana na MUNGU Baba.
 Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima wetu.

Kila leo tunasikia watumishi wa MUNGU wakuhubiri na kusisitiza sana kutubu.

Kila anayeamua kumpendeza MUNGU huanza kwa  kumpokea YESU kama Mwokozi kisha anatubu na kuanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU.

Mara nyingine kila kabla ya ibada kunakuwa na maombi ya kutubu.

Hakika maombi ya toba ni muhimu sana sana.
Naweza nikasema kwamba kama kuna maombi muhimu kwa mtu yeyote basi hakuna maombi muhimu kama maombi ya toba.

Na pia naomba ujue kwamba ni wema wa MUNGU ndio hutufanya tutubu.
Warumi 2:4-8 ''Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa MUNGU wakuvuta upate kutubu?  Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya MUNGU, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; ''

Ni muhimu sana kutubu toba ya kweli.

Kutubu ni nini?

=Kutubu ni kuomba msamaha kwa MUNGU kwa sababu ya makosa uliyofanya kisha kuacha kuyafanya hayo makosa.

 =Kutubu ni kujutia uovu wako kisha unaomba msamaha na kujitenga na uovu huo.

Toba ni nini?

=Toba ni kujutia  matendo uliyotenda kinyume na MUNGU na kisha unaomba msamaha na unayaacha mabaya hayo kwa kuanza kutenda mema ayatakayo MUNGU.

Kama kuna maombi muhimu basi maombi ya toba/Kutubu ndio maombi muhimu namba moja kwa kila mwanadamu.

Unapotubia dhambi kwa Bwana YESU  KRISTO ndiko hutengeneza Mwanzo wa kumwabudu MUNGU katika kweli yake.

Kuokoka ni matokeo ya kumpokea YESU na kutubu.
Kuokoka ni kubadilisha njia, ulikuwa unakwenda jehanamu lakini kwa njia ya toba katika KRISTO na kumpokea KRISTO kama Mwokozi wako basi njia yako inakuwa kuelekea uzima wa milele na sio jehanamu tena.
Kuokoka ni kusalimika, toba pekee kwa YESU na kumpokea kama Mkombozi kisha unaanza kuishi maisha matakatifu ndiko hutengeneza kuokoka kwako.

MUNGU tunamwita ni MUNGU mwenye rehema yaani anasamehe na kuachilia yote, rehema ni zaidi ya msamaha, rehema ni kusamehewa kulikounganika na kuachiliwa yote.
Hata kama ulitenda dhambi kubwa kiasi gani ukitubu katika Bwana YESU hakika MUNGU anakusamehe na kukuachilia, na jina lako linabadilika tangu muda ule, badala ya kuitwa mdhambi unaitwa mtakatifu kama ukidumu sasa katika kutii Neno la MUNGU.
Maombi ya toba ni ya muhimu sana.


FAIDA TANO ZA MAOMBI YA KUTUBU.

1. Unapotubu unasamehewa dhambi zako na kuachiliwa, pia hati za mashitaka zote hufutika.

Luka 24:46-47 '' Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba KRISTO atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.''

Unapotubu kwa kuamua hakika kutoka moyoni unasamehewa na kuachiliwa. Dhambi yako haibaki kuwa dhambi hata kama ilikuwa kubwa kiasi gani baada ya wewe kutubu katika  Bwana YESU hakika dhambi hiyo inafutika na wewe unakuwa huru.
Pia ni muhimu sana kujua kwamba MUNGU husamehe na kuachilia kwa wanaotubu, hivyo na sisi tunapaswa kuwasamehe wale wote waliotukosea kisha wanaotubu kwetu uovu wao huo.
Luka 17:3-4 '' Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe''

Usipomsamehe aliyekukosea kisha yeye akatubu hakika dhambi ya kutokusamehe itakuwa kwako na yeye kwa kutubu kwake akiwa huru na mwenye haki kwa MUNGU. Hivyo inatubasa pia kuwasamehe wote wanaotuomba msamaha, hata wasioomba msamaha ni muhimu pia kuwasamehe maana wasiosamehe hawataurithi uzima wa milele.
Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''


2. kutubu ni kuipisha ghadhabu ya MUNGU iliyokuwa tayari kuja.

Yona 3:6-10 ''Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?  MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.''

MUNGU alitaka kuwaangamiza watu wote wa Mji mkubwa wa Ninawi kwa sababu ya uovu wao, lakini walipotubu na kuacha uovu MUNGU alighairi.

Kutubu ni kuibisha adhabu ya MUNGU iliyokuwa ije kwa sababu ya uovu.

Kuna watu Bwana YESU aliwaambia watubu maana wasipotubu wataangamia.
Luka 13:3 ''Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.''

Kwa uovu wako ilikuwa ufe au uharibiwe lakini toba yako ya kweli inaweza kuifuta adhabu ambayo ilikuwa ikupate.
Laana uliyojisababishia inaweza kufutika tu kwa wewe kutubu kwa Bwana YESU kisha unaanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu.


3. Kutubu hutengeneza kukubaliwa na MUNGU.

Isaya 57:15 '' Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.''

Ulikuwa adui wa MUNGU kwa sababu ya dhambi zako na maovu yako lakini toba ya kweli itakufanya ukubaliwe na MUNGU.

Mfano ulifanya uasherati kabla ya ndoa  lakini neema ya MUNGU ikakugusa ukatubu na kuacha uasherati huo hakika unakubaliwa na MUNGU tena,  hivyo jitunze kwa kuishi maisha matakatifu hadi ndoa  na hadi siku ya kuondoka duniani.

Ulikuwa mwizi kazini, ukatubu na kuacha dhambi hiyo hakika unakubaliwa na MUNGU.

Watu wote tulikuwa adui wa MUNGU kwa sababu ya maovu yetu lakini kwa kumpokea YESU na kutubu  na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu hakika tumekubaliwa na MUNGU Muumba wetu.


4. Toba huleta nyakati za kuburudishwa.

Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

Ulikuwa dhambini uliteswa na mapepo lakini toba ya kweli katika KRISTO iliondoa nguvu za giza hizo ndani yako.

Ndugu mmoja alikuwa hasinzii usiku kwa sababu ya kukabwa na majinamizi na wachawi, alipookoka wale wachawi na majinamizi  hakuwaona tena, hizo ndizo nyakati za kuburudishwa.

Kuwa na amani na furaha kwa sababu jina lako limeandikwa katika kitabu cha uzima cha YESU KRISTO, Hizo ni nyakati za kuburudishwa.

Leo kuna watu kwa sababu ya dhambi zao huishi kwa hofu na wanaogopa kifo maana wanajua kabisa wakifa ni motoni.
Dhambi ni utumwa hivyo hivyo ukitubu na kuanza kuishi maisha matakatifu hakika utumwa unaondoka na nyakati za kuburudishwa zinaanza.

Kuburudishwa kukuu zaidi ni uzima wa milele ambao chanzo chake ni kutubu toba ya kweli katika KRISTO kisha kuishi maisha ya wokovu matakatifu yanayoagizwa na Neno la MUNGU.


 5.  Toba huleta uponyaji.

2 Nyakati 7:14 ''ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.''

MUNGU anasema ataiponya nchi yaani atawaponya wakazi pamoja na nchi yao, lakini kwanini MUNGU aseme hivi?
Ni kwa sababu kama tu watanyenyekea kwake na kutubu na kuacha dhambi zao.

Uponyaji mwingi sana umetokana na maombi ya toba tu.

Kama ni msomaji mzuri wa Vitabu vinne vya injili vya mwanzo katika agano jipya utakubaliana na mimi kwamba toba ndio ilikuwa muhuri wa uponyaji wa Bwana YESU.

Wengi sana aliowaponya Bwana YESU alikuwa anawaambiwa ''Umesamehewa dhambi zako'' na kwa Neno hilo uponyaji unatokea.
Hebu tuone mfano huu.
Luka 5:18-26 ''Na tazama, wakaja watu wanamchukua kitandani mtu mwenye kupooza; wakataka kumpeleka ndani na kumweka mbele yake. Hata walipokosa nafasi ya kumpeleka ndani kwa ajili ya lile kundi la watu, walipanda juu ya dari wakampisha katika matofali ya juu, wakamshusha yeye na kitanda chake katikati mbele ya YESU. NAYE ALIPOIONA IMANI YAO, ALIMWAMBIA, Ee RAFIKI, UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO. Basi, wale waandishi na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wakisema, Ni nani huyu asemaye maneno ya kukufuru? N'nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa MUNGU peke yake? Na YESU alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu? Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende? Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako. Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza MUNGU. Ushangao ukawashika wote, wakamtukuza MUNGU; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu. ''

Katika maandiko hayo hatuoni Bwana YESU akimuombea huyo aliyepooza bali alipoiona imani ya waliomleta akamwambia ''
''Ee rafiki, umesamehewa dhambi zako ''  Kisha akamwambia ainuke na uponyaji tayari umeshatokea.
Zamani pia magonjwa yalikuwa yanakuja kwa sababu ya dhambi hivyo toba ni muhimu sana katika kurudisha uponyaji.

Ndugu zangu hakika maombi ya toba ni muhimu sana.
Nafasi ni ndogo ningeshuhudia shuhuda zangu binafsi ambazo miujiza ilitokea baada ya toba ya kweli.

Nimetaja faida tano tu za maombi ya toba lakini ukweli zipo faida nyingi sana za maombi ya toba.
Kwa kufupisha naweza nikasema hivyo katika nyongeza ya faida zingine za kutubu ni;
=Kutubu ni kumruhusu MUNGU akusaidie.

=Kutubu ni kurudisha mahusiano yako na MUNGU.

=Faida nyingine ya kutubu ni kwamba kuna furaha mbinguni baada ya Mwenye dhambi mmoja atubuye, sasa mbingu zikifurahi kinafuata nini kwako?
Luka 15:7 '' Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.''

Kuokoka ni matokeo ya kutubu.
Ndugu nakuomba sana ishi maisha ya toba na usikubali kurudi dhambini tena.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments