KUFURAHIA THAWABU YA KASHFA ZA UONGO

Na Askofu Mkuu Silyvester Gamanywa.

Amini usiamini! Kumbe kuna thawabu kwa ajili ya kutungiwa kashfa za uongo! Haya si maneno yangu binafsi. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyesema haya kama ilivyoandikwa hapa chini:
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” (MT.5:11-12)
Maneno mazito ni haya ya “watakapowashutumu…….na kuwaudhi……..na kuwanenea……. Kila NENO BAYA kwa UONGO….” Kuna kushutumiwa na kulaumiwa na kunenewa vibaya lakini kwa mambo ya kweli, kwa makosa ya kweli. Hii ni kawaida kila mkosaji kulaumiwa kwa makosa yake.
Lakini si rahisi, na si kawaida, mtu asiye na hatia kabisa, kushutumiwa, kulaumiwa na kunenwa vibaya kwa tuhuma za kashfa za uongo. Tena tuhuma ambazo wahusika wanaweka mikakati ya makusudi huku wamepania kwa makusudi kumdhalilisha, kumvunjia heshima yake, huyo asiye na hatia “maskini wa Mungu” ili tu aabike, aadhirike, aharibikiwe, na ikiwezeka afilie mbali!!!
Kisa ni nini? Ati kwa kuwa tu yeye ni “mchaji Mungu”! Ati anawakera mno kwa kuwa ni “mshika maadili ya kibiblia”! Ati kwa kuwa kajitoa mhanga kutangaza habari za imani yake aliyo nayo kwa Mungu wake!!!
Tena wengine wamemkasirikia kwa madai ati “anajifanya mtakatifu sana, hataki kushiriki maovu; hatoi wala kupokea rushwa; kajitenga na ufisadi kwa sababu ya imani yake kwa Yesu!” Basi, kwa ajili hiyo tu, zinasukwa njama na kutengenezwa tuhuma za kashfa za uongo dhidi yake; ili tu kumkomoa na kumkomesha asiendelee na msimamo wake wa kimaadili. Haya ndiyo Yesu alimaanisha aliposema, “….na kuwanenea kila neno baya kwa uongo KWA AJILI YANGU..”
Sasa uzito wa ujumbe huu sio kusingiziwa na kuzushiwa kwa ajili ya imani. Uzito wa ujumbe huu ni jinsi “mtendewa, msingiziwa, mzushiwa,” anavyoagizwa jinsi ya kuchukuliana na hali ya namna hii. Anaagizwa na Yesu kwamba AFURAHI NA KUSHANGILIA AKITUNGIWA KASHFA ZA UONGO KWA AJILI YA KRISTO! Hapooooo!!! Kufurahi na kushangilia!!!!
“Ee Bwana Yesu nisaidie miye mtu dhaifu sanaa naomba unirehemu tu katika hili! Ninatamani kupata thawabu zako, ila kwa thawabu hii ninahitaji neema yako. Maana udhaifu wangu huu unaweza kunikosesha hata thawabu nyingine nisipokuwa makini sana katika eneo hili..AMINA” Duh! Samahani kwa kusali hadharani lakini najua ujumbe huu una walengwa wake.
Napenda kuhitimisha kwa kusema ya kwamba, tuache unafiki, ukweli inauma sanaaaa kunenwa vibaya kwa uongo. Lakini ni kwa sababu ya maumivu ya jinsi hii ndiyo maana Yesu naye kaweka njia ya kupona maumivu hayo. Anatutaka tuwe na mtazamo tofauti pale tunapopatwa na majaribu ya jinsi hii.
Kwanza kila unaposingiziwa kwa uongo, na wewe unajua kuwa huo ni uzushi, kumbuka shahidi wako wa kwanza ni Mungu. Wakati watu wengine wasiojua ukweli wanatapokuwa wanakulaumu na kukutukana kwa kashfa ambazo chanzo chake sio wewe; kumbuka, laana zao zitageuka kuwa baraka kwako mbele za Mungu.
Lakini ili baraka hizo zidumu lazima kwanza uishinde hisia ya uchungu na maumivu ya nafsi, kwa kuwasamehe bure wale wanaokuudhi. Unaishindaje hisia hiyo hasi ya uchungu? Kwa kuruhusu hisia chanya ya furaha, na hata kushangilia kwa ajili ya THAWABU KUBWA INAYOKUSUBIRI MBINGUNI.
Msomaji wangu, usikubali kumaliza mwaka huu ukiwa na uchungu moyoni kwa sababu ya kashfa za uongo. Sisi sote tutakutana siku moja mbele za Kiti cha hukumu cha Kristo na ukweli utajulikana wakati huo. Hivi sasa furahi na kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa hayo ndiye mapenzi yake pale tunapoteswa isivyo haki….. “Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivya haki.” (1 Pet.2:19)
Nakutakia baraka za Krismasi na mwaka mpya. Kama ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like na pia warushie marafiki zako wengine wapate kupona kiroho. Ubarikiwe sana!

Comments