MAMBO SITA(6)YA KUFANYA ILI UFIKE KAANANI(MBINGUNI)

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Safari ya kwenda Kaanani kwa Waisraeli ilianza kipindi walipoondoka Utumwani Misri.
Safari ya Kaanani kwa kila Mteule wa MUNGU  huanza kipindi mtu huyo anaokoka .
Baada ya kuokolewa na Bwana YESU ndipo safari ya kaanani(Mbinguni) inaanza.
Kuna mambo sita nimeandaa  ya kufanya ili ufike kaanani(Mbinguni).


1. Ukianza safari ya kaanani mwangalie na mtii anayekupeleka Kaanani ambaye ni YESU KRISTO.
Waebrania 12:2-3 '' tukimtazama YESU, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha MUNGU. Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.'
YESU aliacha enzi yake mbinguni ili aje akuokoe wewe kisha akuongoze kwenda Kaanani. Unatakiwa sana kumtazama yeye tu na kulitii Neno lake.
MUNGU yuko ndani ya YESU KRISTO ili akupeleke Kaanani.
YESU KRISTO yuko ndani ya Neno lake ili kukusaidia kujua na kukujulisha mambo ya kuzingatia katika safari yako ya Kaanani.


2. Usitangetange baada ya kuanza safari. 
Kumbu 15:39-40 '' nacho kitakuwa kwenu ni kishada, ili mpate kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya BWANA, na kuyafanya; tena kwamba msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na macho yenu wenyewe, ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza; ili mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa MUNGU wenu.''


Waisraeli walipokuwa wakienda Kaanani waliambiwa watengeneze vishada ili viwasaidie kutokutangatanga, wawe wanamkumbuka MUNGU na kumtii. Leo kanisa limepewa Wokovu na Neno la MUNGU hivyo tukidumu katika Wokovu na huku tukiishi maisha matakatifu hakika kutangatanga hakutakuwepo.
Sio leo unatamani Misri kidogo, mara unaanza manung'uniko. Simama kwenye Msingi ambao ni Neno la MUNGU kwa kulitii siku zote.

Kumbuka kwamba mara nyingine kuhama dhehebu sio kutangatanga, lakini kuacha wokovu kisha unarudi baadae kwenye wokovu huko ndio  kutangatanga.
 
3. Ukianza safari ya kaanani hakikisha unaishi maisha matakatifu daima.
1 Petro 1:14-21 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita BABA, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu; ambao kwa yeye mmekuwa wenye kumwamini MUNGU, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa MUNGU.'
Safari ya kwenda Kaanani inahitaji utakatifu sana.
Waisraeli waliokosa utii kwa MUNGU hawakuingia Kaanani.
Kuna wengine walikufa njiani kwa sababu tu ya kukosa utii hivyo kukosa utakatifu.
Ni Muhimu sana ndugu yangu ukaishi maisha matakatifu siku zote.

4. Ukianza safari ya kaanani Mtumikie MUNGU kwa kusudi la kuitwa kwako.
Waefeso 4:1-7 ''Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na ROHO mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. MUNGU mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kri. ''

 Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''
Ulimtumikia sana shetani ulipokuwa Misri, sasa ni zamu ya kumtumikia Bwana YESU mwenye hiyo Kaanani yako yaani Uzima wa milele.

Kumwabudu MUNGU katika kweli ni sehemu muhimu sana ya kumtumikia.
Uhusiano wako na anayekupeleka kaanani yaani MUNGU kupitia YESU KRISTO ndio muhimu zaidi.
Hakikisha unaubolesha uhusiano wako na MUNGU kila siku na tii kilicho cha MUNGU.


5. Ukianza safari ya kaanani usikumbuke mambo ya Misri tena.
Isaya 43:18 '' Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.''
Hakuna haja ya kutafakari mambo ya zamani ukiwa dhambini.
Hakuna haja ya kutafakari dhambi za zamani.
Unaenda Kaanani misri ya nini kuikumbuka?
Sio mara unakumbuka uzinzi wa Misri, mara unakumbuka starehe za misri au unakumbuka mambo ya Kimisri na miungu ya kimisri.

Ukianza Safari ya Kaanani usikumbuke mambo ya Misri Tena.


6. Tambua kwamba ukifika Kaanani(Uzima wa milele) kuna taji watapewa washindi hivyo palilia taji yako.
 1 Petro 5:4 ''Na Mchungaji mkuu(YESU) atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka''
Kuna taji wateule wa MUNGU watapewa, sio taji moja tu bali ni zaidi ya taji moja, japokuwa taji ya uzima watapewa wote. 
Palilia taji yako kwa kwa utakatifu.
Palilia taji yako kwa  matoleo.
Palilia taji yako kwa utu wema na fadhili.
Palilia taji yako kwa maisha ya haki na kila kiamriwacho na ROHO MTAKATIFU maana huyo yuko ndani yako na bila huyo safari yako itakuwa ngumu sana, hivyo unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU na kubali kuenenda katika yeye.
Bwana YESU anasema '' Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.-Ufunuo 3:11'

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments