MANENO 9 AMBAYO MKRISTO HAYATAKIWI KUMHUSU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu tujifunze.
Leo mimi Peter kazi yangu ni kufafanua tu maneno haya 9 ili ikusaidie wewe kuelewa na kuachana nayo na kujitenga nayo na ili uweze kumtii MUNGU.
Sio kwamba ni maneno haya tu 9 ndio mwisho bali yapo mengi tu ambayo hayatakiwi kumhusu Mkristo ila mimi leo nimependa kukuletea haya 9.

1. UNAFIKI.
Maana ya Mnafiki ni mtu anayetoa ahadi njema kisha asitimize.
Mnafiki ni mtu anayesema kinyume na anavyotenda, anasema mema lakini hayatendi hayo Mema.
Mteule wa KRISTO hutakiwi kuwa MNAFIKI.
Mathayo 23:13-14 '' Ole wenu waandishi na Mafarisayo, WANAFIKI! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. [Ole wenu waandishi na Mafarisayo, WANAFIKI! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]''

2. KIBURI.
Kiburi ni hisia za mtu kujiona yeye ni bora au mkubwa kuliko wengine.
Mtu mwenye kiburi ni mtu anayedharau wengi kwa kujiona yeye ni bora kuliko wao.
Kiburi huzaa Majivuno na Maringo yaani mwenendo au tabia ya kujiona.
Mteule wa MUNGU hatakiwi kuwa ni mtu mwenye kiburi kwa MUNGU na hata kwa watu wa MUNGU wote.
Mithali 16:18-20 '' KIBURI hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko. Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye KIBURI. Atakayelitafakari neno atapata mema; Na kila amwaminiye BWANA ana heri.''

3. UONGO.
Uongo ni tabia ya kudanganya.
Uongo ni kusema maneno yasiyo ya kweli.
Uongo ni kusema au kufanya kitu kisicho sahihi.
Wateule wa MUNGU haiwapasa hata dakika moja kuwa waongo.

Waefeso 4:25 ''Basi uvueni UONGO, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.'' 
 
Tena Biblia inatutaka tusivumishe habari za uongo.
 
''Usivumishe habari za UONGO; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.-Kutoka 23:1''
 
Tena hatutakiwi kuwazushia watu uongo.
 
''Wala usimshuhudie jirani yako UONGO.-Kumbukumbu 5:20''

Na Biblia inasema mwisho wa waongo ni jehanamu.
Hivyo Kanisa la MUNGU hatutakiwi kuwa waongo bali tuseme kweli na tuitende kweli ya MUNGU bila upendeleo.

4. USALITI.
Kusaliti ni kutoa siri kwa mtu asiyetakiwa kwa lengo la kuwaharibia wenzako.
Kusaliti ni kutoa siri za wenzako ili wakamatwe au wakwame.
Kusaliti ni kwenda kinyume na makubaliano mema mliyoyafanya na wenzako au mwenzako.
Msaliti ni mtu mtu anayeshirikiana na maadui za mtu ili kumharibia mtu huyo.
Msaliti ni mtu anayechonganisha watu ili wagombane au waachane au wapigane.
Msaliti ni adui katikati ya kanisa.
Kusaliti kanisa la MUNGU ni kuwa kinyume na kazi ya MUNGU.
Kanisa la MUNGU lina adui mmoja tu ambaye ni shetani na majeshi yake.
Kama katika kanisa yuko mtu ambaye hajaokoka vyema yaani anashirikiana na shetani kuliharibu kanisa au kuleta matatizo kwa Kanisa la MUNGU huyo mti ni Msaliti.
Kuwafitini wanakwaya wenzako huo ni usaliti.
Kuwasema vibaya wachungaji kwa kuwaonea huko ni kuisaliti kazi ya MUNGU.
Kuwazuia watu wasitoe sadaka na zaka kwa sababu tu wewe una wivu na Akofu au Mchungaji huko ni kuisaliti kazi ya MUNGU na huko ni kuzuia baraka za hao unaowadanganya.
Usikubali kulisaliti Neno la MUNGU maana utaishia pabaya.
Usikubali kuisaliti ndoa yako.
Mteule wa MUNGU hatakiwi kuwa msaliti.
Kusalitiana ni dalili moja wapo ya siku za mwisho.
Biblia inasema ''Na ndugu ATAMSALITI nduguye ili auawe, na baba ATAMSALITI mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha.Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.-Mathayo 10:21-22''

5. UFISADI.
Ufisadi ni tendo la kuleta maovu au uharibifu katika jamii.
Fisadi ni mtu anayemshawishi mwingine ili wawe na uhusiano wa kimapenzi.
Kumbuka kanisani hatuhitaji uhusiano wa kimapenzi bali uhusiano wa kirafiki, uhusiano wa kimapenzi ni ndani ya ndoa tu kwa wanandoa watakatifu wawili wa jinsia mbili tofauti waliofunga ndoa kanisani.
Fisadi ni mtu mwenye kuharibu vitu au watu.
fisadi ni mtu anayekwenda kinyume na maadili ya kanisa.
Ufisadi ni upokeaji au utoaji wa rushwa.
Ufisadi ni wizi wa mali.
Ufisadi ni ufujaji wa mali.
Wateule wa KRISTO haiwapasi kuwa mafisadi.
Biblia inakata ufisadi wa aina yeyote usiwe katika maisha ya mteule wa MUNGU.
1 Petro 4:2-5 '' Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya MUNGU, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika UFISADI, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika UFISADI ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.''
 
Mafisadi watakuja lakini yakupasa mteule wa MUNGU wewe usijihusishe na ufisadi.
2 Petro 2:2-3 '' Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.'' 


6. UBATILI.
Ubatili ni hali ya kutenda jambo batili.
Batili ni kuvunja makubaliano.
Ubatili ni kufanya mambo yasiyokubalika.
Ubatili ni uongo.
Ubatili ni kutangua makubaliano mazuri mliyokubaliana mwanzo.
ubatili ni kufanya mambo yasiyokubalika na yasiyo sahihi.
waefeso 4 17-19 '' Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika UBATILI wa nia zao; ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa MUNGU, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.'' 
 
Kuna wengine leo hufundisha ubatili.
 
1 Tomotheo 1:6-7 ''Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya UBATILI; wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti'' 
Mteule wa MUNGU haimpasi kuwa mtu wa ubatili.
 
.
7. USINGIZIAJI.
Kusingizia ni kusema mtu fulani ametenda jambo fulani na kumbe si kweli.
Kusingizia ni kutoa sababu za uongo ili kujikinga dhidi ya adhabu au lawama.
Kusingizia ni kudanganya.
Kusingia ni kusema neno  lisilo la kweli kwa ajili ya kuwafanya walifikirie jambo hilo kuwa la kweli.
Kanisani hatakiwi kuwapo mtu msingiziaji katika jambo lolote.
Mteule wa KRISTO hutakiwi kumsingizia mtu katika jambo lolote na hautakiwi kusingizia kwa kutoa sababu za uongo ili tu usilaumiwe kwa uovu wako au usiadhibiwe kwa sababu ya uovu wako.
Yakobo 4:11-12 '' Ndugu, MSISINGIZIANE; amsingiziaye ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, huisingizia sheria na kuihukumu sheria. Lakini ukiihukumu sheria, huwi mtenda sheria, bali umekuwa hakimu. Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine? ''

Na tena Biblia inasema kwamba anayesingizia watu ni mpumbavu.
Mithali 10:18 '' Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye ASINGIZIAYE ni mpumbavu.''
 
8. UTAPELI/WIZI/KUIBA
Utapeli ni wizi.
Utapeli na wizi hujumuisha kuiba.
Biblia inakataza kuiba.
 Haimpasi mteule wa MUNGU kuiba kwa njia yeyote ile, iwe njia ya wizi au njia ya utapeli.
Utapeli ni ni tendo la kulaghai ili kuwadhulumu haki zao.
Utapeli ni kuwa mtu wa dhuluma.
Dhuluma ni tendo analolifanya tapeli.
Dhuluma ni kutenda jambo lisilo la haki.
Dhuluma ni kutenda jambo la uonevu.
Ni kumnyima mtu haki yake, ni kuonea, kutaabisha na kutesa.
Na huyo anayefanya dhuluma hizo ni tapeli.
Mteule wa MUNGU hatakiwi kuwa tapeli katika hali yoyote.
Tapeli ni mtu anayewalaghai watu ili wadhulumu mali zao au haki zao.
Mtumishi wa MUNGU hatakiwi kuwa tapeli maana utapeli ni dhambi na hakuna mbingu ya matapeli.
Waefeso 4:27-29 ''wala msimpe Ibilisi nafasi. MWIBAJI ASIIBE tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.'
Haijalishi unaiba kwa njia gani lakini Biblia inasema anayeiba asiibe tena.
Kama unaiba kwa utapeli acha mara moja.
Kama unaiba kwa kwa yeyote acha sasa maana ni dhambi.
Walawi 19:11-12 ''MSIIBE, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la MUNGU wako; Mimi ndimi BWANA.''
 
9. KULAUMU/KUSHUTUMU.
Kushutumu ni kulaumiana.
Kumshutumu mtu ni kumlaumu kwa sababu ya ubaya au makosa aliotenda. 
Sio kazi yetu kumshutumu mtu yeyote bali kumweleza ukweli na kumsaidia ili asirudie kosa hilo.
Kuna tofauti kati ya kumwambia mtu ili ajirekebishe na kumshutumu mtu.
Shutuma hutengeneza hasira na kukosana kusiko na sababu.
Kushutumiana Ni kumwambia mtu kuwa ndiye sababu ya mambo fulani kutokufanikiwa. 
Hata kama kwa mfano Mchungaji ndio chanzo cha kanisa kutokuongezeka. Kumshutumu mchungaji huyo haitasaidia kanisa kuongeneza bali ndio kwanza mashutumu hayo yatawaondoa watu kwa YESU, ni makosa kulaumiana
 Lawama ni maneno yanayotolewa kuonyesha kutokulidhishwa  na maneno au matendo ya mtu ya tabia ya Mtu.
Kuna vitu vingine kama wewe unaweza kuvifanya katika Kanisa la MUNGU ni heri ukavifanya na sio kubaki kila siku ukiwalaumu wateule  ambao wameshindwa kuvifanya.
Luka 6:37 ''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; MSILAUMU, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.''
 Tena Biblia inasema
''Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,
  mpate kuwa wana wa Mungu wasio na LAWAMA, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,-Wafilipi 2:14-15''
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments