MWISHO WA MASWALI

Na Askofu Mkuu  Zakaria Kakobe.
L
eo, katika Siku ya Kuichambua Biblia, tunajifunza na kutafakari mistari iliyobaka katika Sura ya 16 ya Kitabu cha YOHANA.  Kwa jinsi hii, leo tunajifunza YOHANA 16:23-33.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo, ni “MWISHO WA MASWALI“, hata hivyo, kuna mambo mengine ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele tisa:
(1)            MWISHO WA MASWALI (MST. 23, 25);
(2)            KUMWOMBA BABA KWA JINA LA YESU (MST. 23-24);
(3)            OMBENI NANYI MTAPATA (MST. 24);
(4)            JINSI YA KUWA NA FURAHA TIMILIFU (MST. 24);
(5)            SIWAAMBII KWAMBA NITAWAOMBEA (MST. 26-27);
(6)            KUJA KWA YESU KRISTO DUNIANI MARA YA KWANZA (MST. 24);
(7)            WANAFUNZI KUELEWA BAADA YA MWALIMU KURUDIARUDIA SOMO
            (MST. 29-31);
(8)            KUTAWANYIKA KILA MMOJA KWAO KWAO WAKATI WA DHIKI (MST.
32);
(9)            ULIMWENGU MNAYO DHIKI (MST. 35).

(1)      MWISHO WA MASWALI (MST. 23,25)
“Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote“, ni maneno ya Yesu kwetu.  Wanafunzi wa Yesu hapa, walikuwa na maswali mengi.  Maswali mengine yalikuwa miongoni mwao tu, na hata kabla ya wao kuyauliza, Yesu alijua kwamba wana maswali hayo katikas mioyo yao (MST. 19).  Siosi nasi ni vivyo hivyo.  Tunajifunza neno la Mungu, na kulitafakari, kunakuwa na maswali mengi ambayo yanajitokeza, yasiyokuwa na majibu.  Kwa mfano Sura ya Mungu ikoje?  Mungu alitoka wapi, na ilikuwaje akawako?  Sisi wanadamu tuliumbwa, Je Mungu yeye ilikuwaje mpaka akawepo? n.k.  Hatuna haja ya kuumiza vichwa vyetu na kujitaabisha kwa maswali ya namna hii.  Tukiweka miyoyo yetu kuwaza juu ya majibu ya maswali ya jinsi hii, hali hiyo itatutoa katika imani badala ya kutujenga kiimani.  Kwa sasa, tunapaswa kuridhika na mambo yale tu tuliyofunuliwa.  Yale yaliyosalia ambayo yanakuwa ni siri iliyofichika, hayo ni ya Bwana, na siku moja tutapata ufahamu wote juu ya mambo yote.  Siku ya kuonana na Yesu ana kwa ana, iko karibu sana.  Mara tutakapomwona, tutakuwa na ufahamu usio wa kawaida na tutayafahamu yote.  Siku hiyo itakuwa mwisho wa maswali yote.  Subira yavuta heri (KUMBUKUMBU LA  TORATI 29:29; 1 WAKORINTHO 13:12).  Neno la Mungu linasema nasi sehemu nyingine kwa jinsi ya fumbo au mithali, siku hizi, lakini tutayafahamu yote waziwazi siku ile.

(2)      KUMWOMBA BABA KWA JINA LA YESU (MST. 23-24)
Tukitaka kupata majibu ya maombi, hatuna budi kumwomba Mungu Baba kwa Jina la Yesu.  Katika maombi, hatupaswi kutumia vitu vinavyoonekana kwa macho kama rozari, sanamu ya Mtakatifu fulani, uvumba, maji ya baraka, msalaba n.k.  Mungu ni roho, bila kutumia lolote la kuonekana kwa macho, isipokuwa Jina la Yesu asiyeonekana kwa macho (YOHANA 4:23-24).  Hatupaswi kumweka mtakatifu fulani, Bikira Mariamu, au Malaika yoyote katikati yetu na Mungu.  Mpatanishi kati yetu na Mungu, ni  mmoja tu Yesu Kristo, ndiyo maana tunaomba kwa Jina lake pekee (1 TIMOTHEO 2:5).  Siyo hilo tu, tunapoingia katika maombi, hatuna budi kufahamu kwamba tunamwomba Mungu aliye Baba yetu wa mbinguni.  Ikiwa baba zetu wa duniani pamoja na uwezo wao mdogo, hufanya kila njia kuhakikisha kile ambacho wameombwa na watoto wao, wanawapa hichohicho, iwe ni mkate, pipi, viatu n.k., ni zaidi sana kwa baba yetu wa mbinguni mwenye uwezo wote (ZABURI 103:13; LUKA 11:11-13).  Ni muhimu vilevile kufahamu pia kwamba Jina la Yesu, ni kama sahihi ya mtu inayotambulika Benki.  Sahihi ya mwenye akaunti Benk, ndiyo yenye uwezo wa kumfanya mtu anayepeleka cheki au hundi, kulipwa fedha kutoka katika Akaunti hiyo.  Mtu hawezi kulipwa fedha zozote ikiwa sahihi yake haitambuliki Benki.  Tunapolitumia Jina la Yesu, katika maombi, ni muhimu kutokuwa na mashaka yoyote, maana vyote vizuri vilivyo mbinguni na duniani ni mali yake Yesu (MATHAYO 28:18), na hivyo kupewa Jina la Yesu kulitumia katika maombi, ni kupewa cheki au hundi yenye sahihi ya mwenye fedha katika akaunti.  Uhakika wa kupokea mahitaji yetu ni mia kwa mia, tunapolitumia Jina la Yesu, mradi tu, tuamini jambo hili.

(3)      OMBENI NANYI MTAPATA (MST. 24)
Hakuweza  kuwa na uhakikisho mkubwa namna hii juu ya kupokea kwetu tunapoomba.  Mungu si mtu hata aseme uongo, akiahidi, atatimiza (HESABU 23:19; TITO 1:2).  Ahadi zake ni Amini, yaani HAKIKA (2 WAKORINTHO 1:20).  “Ombeni nanyi mtapata“, ni ahadi ya Mungu kwetu iliyo ya hakika, tunapoomba kwa Jina la Yesu.  Hatupaswi kuongozwa na hisia za namna zozozte zile tunapoomba.  Hata tukiona tuliloliomba linachelewa kuja kwetu, moyo wetu uwe kwenye ahadi hii ya Mungu, na siyo kuuweka moyo wetu kwenye kuchelewa huko!

(4)      JINSI YA KUWA NA FURAHA TIMILIFU (MST. 24)
Njia moja kubwa ya kuwa na furaha timilifu, ni kufanya maombi.  Kuomba nyakati zote, kunaambatana na furaha timilifu (1 WATHESALONIKE 5:16-17).  Tukijaa huzuni, mawazo, mashaka au woga n.k., ufumbuzi wake ni kufanya maombi, ili tupate furaha timilifu, na siyo kuendelea kujaza mawazo kichwani.  Tukiwa waombaji, tutajiweka katika hali ya kuwa na furaha hata katika mazingira magumu.

(5)      SIWAAMBII KWAMBA NITAWAOMBEA (MST. 26-27)
Yesu Kristo muda awote alipokuwa duniani, alikuwa anatuombea.  Pale msalabani, bado Yesu alikuwa anazidi kutuombea (LUKA 23:24).  Mwisho kabisa, Yesu alichukua muda kuwaombea wanafunzi wake na kutuombea sisi pia (YOHANA 17:9,15,20).  Hata hivyo baada ya yeye kutuombea hivi, anatupa uwezo wa kipekee wa sisi nasi, kuomba kwa Jina lake na kupokea, akituhakikishia kupokea kama Yeye alivyopokea kwa Baba.  Hatupaswi leo kuwaomba watakatifu fualani waliokufa watuombee.  Kuwaomba wafu, ni machukizo makubwa kwa BWANA (KUMBUKUMBU 18:10-14).  Pamoja na jinsi ilivyo mpango wa Mungu kuombewa na Watumishi wa Mungu (YAKOBO 5:14), hata hivyo, ni muhimu kila mmoja wetu kukumbuka pia kwamba KILA AOMBAYE HUPOKEA (LUKA 11:10).  Tukipatwa na lolote wakati wowote tuombe kwa Jina la Yesu.  Baba anatupenda kwa kuwa tumempenda Yesu na kumsadiki, hivyo tumwombe naye ataudhihirisha kwetu upendo wake.
(6)      KUJA KWA YESU KRISTO DUNIANI MARA YA KWANZA (MST. 28)
Yesu Kristio alipozaliwa ulimwenguni, hakuanzia tumboni mwa Bikira Mariamu.  Alikuja tu duniani na kufanyika mwili, hata hivyo alikuwepo kabla ya msingi ya ulimwengu kuwako.  Alitoka kwa baba na kuja ulimwenguni mara ya kwanza, kwa kufanyika mwili (MIKA 5:2; YOHANA 1:14; 1 TIMOTHEO 3:16; WAKOLOSAI 1:17-18).  Baada ya kukaa ulimwenguni, Yesu alipaa kwenda kwa Baba tena.  Atatokea mara ya pili duniani, wakati atakapokuja na watakatifu kuutawala ulimwengu miaka 1,000, baada ya miaka saba duniani ya Dhiki Kuu itakayotanguliwa na Kunyakuliwa kwa Kanisa (WAEBRANIA 9:28; YUDA 1:14).

(7)      WANAFUNZI KUELEWA BAADA YA MWALIMU KURUDIARUDIA SOMO (MST.
      29-31)
Baada ya Yesu kurudia tena na tena mafundisho yake, ndipo wanafunzi wake wakasema, “SASA TUMEJUA“.  Hapo mwanzoni, mafundisho hayo yaliwapita tuputu.  Hili ni fundisho kubwa kwetu Waalimu wa Biblia.  Hatuna budi kuwa tayari kurudia tena na tena mafundisho yaleyale kwa wanafunzi wetu ili waelewe na kuyatendea kazi.  Yesu Kristo kwa kuelewa haya, aliwafundisha wanafunzi wake mafundisho yaleyale MLIMANI na kuyarudia akiwa MAHALI TAMBARARE (MATHAYO 5:1-3; LUKA 6:17-20).  Kwa mfano, hatupaswi kusita kuutaja mstari wa YOHANA 3:16, kwa kuwaza  kwamba wote wanaufahamu.  Sikuzote inatupasa kufundisha na kurudiarudia yale tuliyokwisha kuwafundisha wanafunzi wetu bila kujali tu kwamba walijifunza safari iliyopita.

(8)      KUTAWANYIKA KILA MMOJA KWAO KWAO WAKATI WA DHIKI (MST. 32)
Wanafunzi wa Yesu walimwandama Yesu wakati wa furaha, baraka na miujiza, lakini mazito yalipotokea, walimwacha wote wakakimbia (MATHAYO 26:55-56).  Wakatawanyika kila mmoja kwao kwao.  Wako watu wengi leo wenye hali hii pia.  Wako tayari kumwandama Yesu katika wokovu na sheria zote za Yesu wakti wa furaha, baraka na miujiza lakini dhiki ikitokea, majibu ya maombi yakichelewa, wakifukuzwa kazi au kuendelea kuwa tasa, wakiachwa na waume zao, n.k., wanatawanyika kila mmoja kwao kwao na kumwacha Yesu peke yake.    Haitupasi kufanya hivi.  Huku ni kupandwa penye miamba (MATHAYO 13:20-21).  Mtu aliyepandwa kwenye udongo mzuri hatamwacha Yesu kwa sababu ya dhiki (LUKA 1:5-7; WARUMI 8:35-39).

(9)      ULIMWENGUNI MNAYO DHIKI (MST. 33)
Kuokolewa lazima kuambatane na dhiki pamoja na udhia (2 TIMOTHEO 3:12; WAFILIPI 1:29-30).  Hata hivyo tukikabiliana na dhiki hizi, tujipe moyo na kuwa na amani, maana tunashinda katika Yesu aliyeushinda ulimwengu wenye dhiki, kwa niaba yetu.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Comments