USIENENDE KAMA MATAIFA WANAVYOENENDA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima wetu.


Waefeso 4:17-27 " Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika BWANA, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa MUNGU, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani. Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza KRISTO; ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika YESU,
mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi."


Wewe kama mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU unatakiwa uwe tofauti na watu ambao hawajaokoka, maana wewe umeijua kweli ya MUNGU na unaiishi sasa.
Usienende kama wamataifa waenendavyo.
Wamataifa ni watu wasiookoka na hawajampokea YESU kama Mwokozi wao na hawaishi maisha matakatifu ya wokovu katika yeye.
Watu wa mataifa wako gizani maana wameikataa nuru ambayo ni YESU KRISTO.


Yohana 3:17-19 " Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu."

Hao ndio watu wa mataifa, hawataki kuokoka na kuja kwa YESU kwenye nuru.
Biblia inakushauri kwamba usikubali kuwa kama watu wa mataifa.
Lazima iwepo tofauti kati yako wewe uliyeokolewa na YESU na hao watu wa mataifa.
Watu wa mataifa huenda katika ubatili wa Nia zao, wewe sasa enenda kwa ROHO MTAKATIFU huku Nia yako ikiwa ni kuishi maisha matakatifu katika KRISTO.
Watu wa mataifa wametiwa Giza na shetani na kwa njia hiyo wamefarakana na uzima wa milele wa MUNGU.
Ni kazi yako kuwafanya watu wa mataifa waje kwa YESU.
Lakini kama maisha yako hayana tofauti na yao hakika hutaweza kuwashuhudia maana wewe na wao mnafanya dhambi.
Hakikisha huenendi kama wamataifa wanavyoenenda.
Watu wa mataifa wana ugumu wa mioyo, wewe hakikisha unamtii KRISTO na neno la MUNGU.


Waefeso 4:28-32 " Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule ROHO MTAKATIFU wa MUNGU; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi."

Ni lazima kuwe na utofauti kati yako wewe mteule wa MUNGU uliyeokolewa na Bwana YESU, na watu wa mataifa.
Ni ajabu watu wa mataifa wanakwenda kwa waganga lakini na baadhi ya watu wa MUNGU huenda kwa waganga, ni hatari mbaya sana hiyo.
Tukio hilo linamaana ya kwamba wewe huna Mungu aliye hai.
Watu wa mataifa wanavaa kikahaba, wateule wa MUNGU wanatakiwa kuvaa kwa heshima na adabu njema.
Mtu wa kanisani hatakiwi kuvaa kwa heshima akiwa tu msibani, ukweni na kanisani, Bali anatakiwa kuvaa kiheshima popote.
Mteule wa MUNGU hakikisha unazaa matunda mema.
Matunda mema ni Matendo mema.
Matunda mema ni kazi njema ya kumtukuza MUNGU.
Bwana YESU anasema " Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.-Yohana 15:1-8"


Ndugu yangu, kaa katika kundi la watu wenye bidii.
Kaa katika kumtumikia MUNGU na kuishi maisha matakatifu.
Usikubali kuwa dhaifu Bali hakikisha una bidii katika kazi ya MUNGU.
Anayefanikiwa ni yule ambaye sio mlegevu, Bali mwenye bidii.
Usiutangulize ufahamu wako mbele, Bali mtangulize MUNGU mbele kwa maombi yako.
MUNGU anamtaka mtu wa bidii mwenye kuukomboa wakati.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments