YESU ANAANDAA MAKAZI YA WATEULE MBINGUNI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU KRISTO asifiwe. 
Karibu ndugu yangu tujifunze neno la MUNGU.
Yohana 14:1-3 "Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini MUNGU, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo." 


Neno hili Bwana YESU alilisema kwa wanafunzi wake, Alilisema pia kwa wale ambao watamwamini na kumpokea, alilisema kwa ajili yako pia na kwa ajili yangu.

Kama tunaendelea katika tumaini la wokovu wa KRISTO.
Kama tunaendelea katika tumaini la uzima wa milele.
Kama tunaendelea kumtumikia MUNGU kwa mioyo yetu yote. Kama tunaendelea kusonga mbele na Wokovu wa KRISTO. Yeye anasema anatuandalia makao mbinguni.
Hakuna ahadi kama hii iliyowahi kutolewa na yeyote popote, YESU alijua anachokisema kwa sababu ni yeye pekee aliyetoka mbinguni kuja duniani. Anayo mamlaka kubwa sana, yeye anaandaa makao kwa ajili ya wateule wake, wale waliosafishwa kwa damu yake.
Wale walioona umuhimu wa kazi iliyofanyika kalvari, Wale waliojua ya kwamba mambo ya dunia yatapita, uongo wa shetani hauwezi kuwafikisha popote, sasa ni nafsi yao kuja kwa MUNGU aliye hai.
Na kuja kwa MUNGU ni lazima wapitie kwa KRISTO YESU maana ndio MUNGU alimteua KRISTO akamtuma aje duniani kwa ajili ya kuwaokoa watu wake. 

Yohana 3:16-18 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

Ni muhimu sana kila mtu kumpa YESU KRISTO maisha yako.

YESU anakuhakikishia mpendwa ya kwamba ukidumu kwenye utakatifu, ukidumu kwenye Neno lake, ukitenda Yale ayatakayo ameuandaa uzima juu mbinguni.
Wafilipi 3:20 ''Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana YESU KRISTO;'' 

Aliko YESU ni mbinguni na huko ndiko wenyeji wetu uliko.
Huko mbinguni ndiko makao yetu wateule wa YESU watakatifu.
Kuna watu hawaamini kama kuna kwenda mbinguni lakini kwa wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu hakika mbinguni ni lazima. Aliyeahidi ni mwaminifu sana, ahadi yake ni kwamba atakuja kutuchukua ili alipo ambako ni mbinguni na sisi tuwepo.
Tena Biblia inathibitisha kwamba wenyeji wetu ni mbinguni.
Kila mmoja autarajie uzima wa milele kwa maana tumempokea YESU.
Hatujampokea YESU ili tuaibike, tumempokea YESU ili tupate uzima wa milele. 

 ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu. - Warumi 6:23.''

Ndugu yangu songa mbele, tusonge mbele, tudumu kwenye wokovu, tufanye mema, tumtumikie KRISTO, tutende yaliyo ya MUNGU.
Tuachane na mambo ya dunia bali tumtukuze MUNGU aliyetuita.
Nakutia moyo nikiomba usonge mbele katika jina la YESU.

Hila za giza zisikurudishe nyuma, makwazo na mambo ya kidunia yasikurudishe nyuma.
Hata kama kanisani wako watu wanaokatisha tamaa.
Hata Kama wako viongozi wa dini unaowategemea unaona wanakuangusha.
Hata kama wako viongozi wa Dini unaona wanarudi nyuma, Wao hawana mbingu, mwenye mbingu ni YESU na yeye anakuandalia makao, mfuate huyo ambaye anakuandalia makao, litii Neno lake na dumu sana kwenye wokovu.


2 Yohana 1:7 "Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo."

Tuko katika zama ambazo wadanganyifu ni wengi sana.
Kila aliye kinyume na KRISTO huyo ni mdanganyifu na kazi yake ni kuwadanganya watu kwa kuwatoa kwenye wokovu wa YESU KRISTO.
Katika dunia ya Leo mafundisho ya uongo ni mengi sana.
Shetani anajaribu kuwatumia baadhi ya watu ili wasihubiri injili ya KRISTO iokoayo Bali wahubiri mambo mengine.
Wapinga Kristo wanajaribu kuwatoa watu kwa KRISTO.
Ndugu, kujitenga na wokovu wa YESU KRISTO ni kujitenga pia na uzima wa milele.
Ni muda wa kujifunza Neno la MUNGU la kweli maana ukizubaa unaweza kukutanana na neno la shetani.
Biblia inasema wadanganyifu wengi wametokea, kuwajua wadanganyifu hao ni rahisi sana maana hawahibiri injili ya KRISTO iokoayo.
Ni muhimu sana kila ndugu kuamua kuambatana na YESU kwa kumtii na kulitii Neno lake.


''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. - 1 Yohana 1:9.''

  Nakuomba ndugu dumu sana kwenye fundisho la wokovu wa YESU KRISTO.
Nje ya YESU kuna sanamu.
Nje ya YESU kuna shetani.
Nje ya YESU kuna matambiko na mizimu.
Nje ya YESU Kuna kusujudia mawe na wanyama.
Nje ya YESU kuna tiba mbadala.
Nje ya YESU kuna baba wa uongo.
Nje ya YESU yuko mpingaKristo.

Tenda mema na tenga muda kwa ajili ya MUNGU.
Tenda kazi ya MUNGU aliye hai. 

Ishi maisha mataktifu ya kumpendeza MUNGU Baba.
''Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU. Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo-Wafilipi 4:7-8 '' 
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments