KUNA FAIDA KUBWA ZAIDI KATIKA KUTOA KULIKO KATIKA KUPOKEA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Shalom mteule wa KRISTO upendwaye sana na MUNGU BABA.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Matendo 20:35 ''Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana YESU, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.''

Ukitoa utasababisha aliyepokea amshukuru MUNGU na jambo hilo kukuongezea kitu wewe mtoaji maana wewe ndio chanzo cha shukrani hiyo. 
Utoaji wako utakupa sifa na heshima.
Lakini pia ukitaka kuwa mtoaji anayetoa katika mpango wa MUNGU basi Fanyika kwanza wewe kuwa sadaka ndipo utoe sadaka.
Ukifanya hivyo utabarikiwa sana rohoni na mwilini.

''Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU , itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU , ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. ''

Jambo muhimu pia la kukumbuka ni kwamba MUNGU hataki matoleo ya ubatili.
Matoleo ya ubatili ni sadaka isiyo sahihi mfano huwezi kuiba pesa harafu ukasema ''ngoja niipeleke kanisani ili MUNGU anibariki zaidi''. Hapo utakuwa unajidanganya wewe mwenyewe na huo ni ubatili mkubwa. Matoleo ya ubatili ni pamoja na kupeleka sadaka isiyo sahihi mfano una laki 1 mfukoni lakini unamtoleaMUNGU Tsh. 100. hii sio haki na kumbuka kwamba hata hiyo laki moja uliyonayo ni MUNGU kakupa na MUNGU hapa anaangalia tu utii wetu sio kwamba ana shida na pesa.

Lakini utoaji wa sadaka safi ni zaka kamili ni muhimu sana na ni agizo la MUNGU kwetu lenye matokeo mazuri sana kwetu watoaji.
Biblia inasema kwamba ni heri kutoa kuliko kupokea.
Maana yake nini?

Kuna faida kubwa zaidi katika kutoa kuliko katika kupokea.

FAIDA NNE(4) ZA KUTOA MATOLEO SAHIHI KWA MUNGU.

1. Ukitoa utakuwa unaweka hazina mbinguni ambapo hakuna atakayeiondoa.

Mathayo 6:19-21 '' Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.''
-Kutoa matoleo sahihi ni kuweka hazina mbinguni.
Hazina ni nini?
Hazina ni ni mali au vitu vya thamani  vinavyohifadhiwa eneo zuri kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Kwa serikali, hazina ni mahali ambapo shughuli za serikali zinazohusu fedha zinaendeshwa.
Kiroho tunaweza kusema kwamba hazina ya wateule wa MUNGU ni mahali mbinguni ambapo matokeo ya utoaji wa mteule huonekana na kufanyiwa kazi yenye manufaa sasa kwa mteule huyo na baadae kwenye uzima wa milele.
Wako Malaika wa MUNGU walio katika kitengo cha uhazini mbinguni kiasi kwamba hakuna hazina ya mteule inayoweza kupotea wala kuibiwa wala kuondolewa.
Mhazini ni mtunza fedha au mali katika eneo zuri na salama, mbinguni wako Malaika katika eneo hilo hivyo Mteule unapotoa kwa moyo na kwa upendo kwa MUNGU hakika hazina yako mbinguni inaongezeka, ndio maana Biblia imesema kwamba ni heri kutoa kuliko kupokea.
Kuna faida kubwa katika kutoa kuliko katika kupokea.
Roho yako itakapokuwapo katika ufalme Wa MUNGU ndipo na hazina yako ya utoaji wako itakapokuwa.

2. Kitendo cha wewe kutoa maana yake unamjaribu MUNGU ili akukuze zaidi.

Malaki 3:10-12 ''Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi.''

Kuna watu shetani huwapangia magonjwa mara kwa mara lakini hawaumwi kwa sababu MUNGU anamkemea mharibifu wa afya zao kwa sababu tu ya utoaji wao sahihi na kwa uaminifu na upendo wa fungu la kumi na sadaka.
 MUNGU anataka tumjaribu kwa matoleo.
MUNGU ameahidi madirisha ya mbinguni kufunguka. Madirisha ya mbinguni yakifunguka kwako kwa sababu ya utoaji wako sahihi na wa kudumu hakika huko mbinguni zitatoka baraka nyingi na upendeleo katika kazi, uchumba, ndoa na chochote kinachokuhusu.
MUNGU anaposema atakubariki kwa sababu ya uaminifu wako sio kwamba atakubariki pesa tu bali ni mambo mengi ya kukubariki.
Mwanzoni mwa maisha yangu ya wokovu nilikuwa na ugumu wa kutoa fungu la kumi lakini katika miezi ambayo sikuzingatia kutoa fungu la kumi nilikutana na matatizo ambayo nilitumia pesa mara tatu hadi saba zaidi ya fungu la kumi ambalo nilitakiwa kutoa.
MUNGU anaposema kwamba atamkemea yeye alaye uchumi wako hakika atamkemea.
Hata kama ni magonjwa ya mlipuko kitaifa lakini wewe mtoaji mwaminifu utashangaa tu uko salama, hapo MUNGU amemkemea anayetaka kukuharibia.
Mama mmoja alienda kwa mganga wa kienyeji na kupewa dawa ili kumpata baba mmoja aliyeokoka ambaye alikuwa mwaminifu kwa MUNGU, Yule dada alipewa nyoka ili nyoka yule amtume kwa yule kaka ili yule kaka amchukuie mkewe na kwa njia hiyo ampende yule dada wa nje. Yule dada akiwa na nyoka wake aliikaribia nyumba ya yule kaka na akamtuma yule nyoka ili akafanye mambo kwenye nyumba ile. Yule nyoka alienda na kurudi haraka akiwa amejeruhiwa na alipofika alimwuma yule aliyemtuma kisha akatokomea kusiko julikana. Wale watu wa MUNGU wala hawakumuona yule nyoka katika familia yao lakini yule dada aliteseka sana na hadi akaenda kwa mganga na mganga akaanza kumwambia hana dawa ya kumtibu huku akimtukana. Hakika MUNGU humkemea mharibifu katika mazingira ambayo sisi hatujui, ila uaminifu wetu kwa MUNGU katika utoaji wa zaka na saka hakika MUNGU hutuzingira.
Ukweli ni kwamba hakuna aliye mwaminifu hata mmoja ambaye akimtolea MUNGU habarikiwi, bali wote hubarikiwa katika maeneo mbalimbali katika maisha yao.
Hakika kuna faida nyingi sana katika utoaji.

 
3. Utoaji wako utakuwa sababisho la wewe kupata kitu fulani kutoka kwa MUNGU.
Mwanzo 8:16-22 '' Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina. Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma. '
Baada tu ya Nuhu kutoka ndani ya safina alimjengea MUNGU Madhabahu kisha akatoa sadaka nzuri kwa MUNGU.
MUNGU baada tu ya kuikubali sadaka ya Nuhu alitoa baraka.
MUNGU alisema  Hatailaani nchi  wala kuipiga kwa gharika dunia yote, Hiyo ni baraka ya MUNGU inayodumu hata leo kwa sababu ya sadaka za Nuhu. Hata iweje leo haiwezekani dunia nzima kuzama kwenye maji kama ilivyotokea wakati wa Nuhu, hiyo ni baraka kwa Nuhu na uzao wake wote ambao ni mimi na wewe.
  MUNGU akiikubali sadaka yako hakika tarajia Muujiza wa MUNGU maishani mwako.
Kuna njia nyingi za MUNGU kukubariki kama utazingatia utoaji wa sadaka safi na zaka sahihi.
Sadaka inaweza ikafufua yale yaliyo kufa maishani mwako.
Dorkasi alikufa lakini sadaka zake zikawa muujiza wa kumfufua.
Hata leo yako mambo yaliyokufa maishani mwako lakini sadaka yako inaweza kuyafufua.
Utoaji wako unaweza kuzifufua baraka zako zilizokuwa zimekufa.
Hebu jifunze katika maandiko haya.
Matendo 9:36-41 '' Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani.  Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi.  Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. ''


4. Sadaka yako itakuwa ukumbusho mbele MUNGU.
Matendo  10:1-8 '' Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,  mtu mtauwa, mchaji wa MUNGU, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba MUNGU daima. Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa MUNGU, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU. Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro. Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.  Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima; na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.'
Sadaka ya Kornelio ikawa ukumbusho kwa MUNGU.
Kuwa ukumbusho sio jambo dogo, Malaika alishuka kwa Kornelio kwa sababu ya utoaji wake sahihi wa matoleo kwa MUNGU.
Ni neema ya MUNGU malaika aje kwako ametumwa na MUNGU.
sadaka sahihi inaweza kumfanya MUNGU amtume Malaika.
Malaika wa MUNGU akishuka kwako ni kwa kusudi la MUNGU.
Sadaka kuwa ukumbusho kwa MUNGU ni jambo la muhimu sana.
Naamini kuanzia sasa utakuwa mwaminifu kwa MUNGU katika kutoa zaka kamili na sadaka halisi ili MUNGU akutendea Mema aliyoyakusudia maishani mwako.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments