MAJUKUMU YA MKE KATIKA NDOA.

Na Peter & Scholar Mabula.
Watenda kazi katika shamba la BWANA YESU.


BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia majukumu ya Mke katika ndoa.
Nimewahi kuzungumzia majukumu ya mume katika ndoa lakini leo nazungumzia majukumu ya mke katika ndoa.
Mke ni mtu muhimu sana katika ndoa.
Mke ni moyo wa ndoa.
Mke ni mtunzaji wa ndoa.
Kwa sababu Mke ni wa muhimu sana katika ndoa basi Biblia inawashauri  kwamba '' Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.-Waefeso 5:33''
Ewe mume usisubiri wenzako wamsifie mkeo ndipo na wewe ujue kwamba mkeo ni mzuri.
Mpe thamani yake mkeo maana huyo ndio wako.
Inawezekana wewe mume ni mbeba maono lakini maono yako hayawezi kutimia kama hushirikiani na mkeo.
Mke ndio zawadi bora kuliko zote ambazo wewe baba umepewa na MUNGU, Mtunze mkeo na mpe haki yake yote kwa usahihi wote.

Waefeso 5:28 ''Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.''

Ni kweli kabisa kuna majukumu ya mume katika ndoa lakini pia na majukumu ya mke katika ndoa yapo.
Kuna majukumu pia sio maalumu kwa mume tu au kwa mke tu bali ni majukumu ya kusaidiana wanandoa wote.
Mama ni vyema sana ukawajibika na ndoa yako na hakikisha husifii tu ndoa za wengine huku ndoa yako umeshindwa kuitunza.


Majukumu ya mke kwenye ndoa ni; 

1.  Kutunza familia.
1 Timotheo 5:8 ''Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.''



Kutunza familia sio jukumu la baba tu bali na mama pia anatakiwa ahakikishe anaitunza familia yake.
Kama mna watoto hakika unatakiwa mama kuwatunza watoto wako na kuwasaidia kiroho ili wampendeze MUNGU katika Wokovu wa KRISTO YESU.
Maana ya Neno kutunza familia ni kuiweka familia chini ya uangalizi wako ili isiharibike au isidhulike.
 

Unaweza ukaitunza familia yako kwa.
A.  kuhakikisha usafi kwa familia yako yote uko vizuri.
B.  Kuombea familia yako kila siku ili mabaya yaliyokusudiwa yasifike.
C.  Kunahikisha wana furaha na amani wakiwa nyumbani.
D.  Kuhakikisha ratiba njema mlizojiwekea kama familia zinafuatwa na  kila kitu kiko sawa.
E.  Kuifundisha familia yako Neno la MUNGU na jinsi ya kumtii MUNGU.
F.  Kunahikisha familia wanatoa fungu la kumi na sadaka kanisani pia majukumu ya kijamii yanayoihusu familia hakikisha mnatimiza.
G. Tunza familia yako kwa Kupanga mipango ya mizuri ya familia. 


  2.  Kumhudumia mumewe.

Mithali 27:18 '' Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa.''
 Ukimhudumia mumeo vyema hakika hata akiwa mbali atakukumbuka wewe, kwa kumhudumia vyema hakika atakuheshimu.
 Mhudumie pia kwa Kumwombea mmewe.
Mhudumie kwa kumsaidia pale anapohitaji msaada.
Hata kama ana madhaifu wewe mhudumie kwa upendo na mtunzie siri. Kumbuka huyo ni wako na hata kama atadhalilika basi na wewe umedhalilika pia.
Wakati mwingine kama mmeo ataonekana labda yuko vibaya kimavazi basi wa kulaumiwa ni wewe mkewe.
Kumhudumia maana yake ni kumsaidia.
Ngoja nikupe mfano mmoja.
Siku moja nilikuwa nahubiri kanisani, ghafla nikaanza kupiga chafya na Leso siku hiyo sikubeba, dakika ile ile mke wangu akaniletea Leso yake na kwa njia hiyo alinistili sana maana nilikuwa mbele za watu madhabahuni wakinifuatilia kwa makini sana.
Huo ni mfano wa kumhudumia/Kumsaidia mmeo.
Mwanamke hakika mmeo haaibiki kwa lolote mbele za watu au popote.
Wakati mwingine naweza kuwa nafundisha lakini mke wangu yuko busy ananiombea, huko ndio kusaidiana.
Wakati mwingine mmeo anaweza kupitia jangamoto kazini lakini ukimhudumia vyema wewe hakika utamfanya awe sawa kabisa na asahau mambo ya kazini yaliyomkosesha raha.

3.  Kumshauri mumewe.

Mithali 12:20 ''Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu; Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.''
Kama mwanaume anafanya maamuzi mabaya kazini au Kanisani wakati mwingine ni kwa sababu ya ushauri mbaya wa mkewe.
Ni vyema sana mke kuwa anamshauri mumewe vizuri ili kusiwe na tatizo popote.
Mithali 11:14 ''Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.''
Kama Mwanaume huwa hafuati ushauri wako nakuomba usichoke kumshauri na kumuombea maana maombi yanaweza kumtengeneza hata akakubariki sana kwa kufuata ushauri wako mzuri.
Kama jambo huna uelewa nalo nakuomba usikurupuke bali ombeni kwanza ndipo mshauriane.
Wakati mwingine mwanaume anaweza kutaka kufanya mabaya hivyo mke ni muhimu sana kumshauri vizuri.
Ni kweli mwanaume ana nguvu lakini wewe mke hakikisha nguvu za mumeo hazitumiki vibaya na pabaya.
Umekuwa mkewe ili pia umsaidie kiroho hata asikose uzima wa milele hivyo hakikisha unamshauri hasa kwa mambo matakatifu ambayo yatawasaidia roho zenu na familia yenu.
Ukiwa unamshauri vizuri hata anafanikiwa hakika itafika kipindi hatafanya jambo bila kukushirikisha maana atatambua kwamba kwako kuna neno la maarifa na hekima la kumsaidia ili asikwame.

4. Kuzaa watoto.

Mwanzo 1:28 '' MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.''
Agizo la MUNGU ni zaeni na kuongezeka.
Utaratibu wa kuzaa idadi muitakayo ya watoto ni muhimu sana.
Sio lazima mzae watoto 10, hata wawili tu wanatosha kama mmejiwekea malengo hayo lakini ukibeba ujauzito usiutoe kisa malengo yenu ni watoto wawili.
Niliumia sana simu moja baada ya ndugu mmoja kuniambia kwamba ameshatoa mimba akiwa ndani ya ndoa yake, kisha hataki kuzaa tena. Kama hataki kuzaa tena kwanini anafanya tendo la ndoa katika siku za hatari?
Kuna watu hudhani kwamba kutoa mimba sio dhambi ndio maana ni rahisi tu kumkuta mtu yuko katika ndoa na ameshatoa mimba hata 4, ndugu zangu huo ni uuaji na Biblia inasema hakuna uzima wa milele kwa wauaji, ni heri kutubu leo na kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi na kuacha mchezo huo mchafu wa kutoa mimba.
Baada ya Siku ya Mwisho Biblia inasema hivi
 ''Huko nje(jehanamu) wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na WAUAJI, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya-Ufunuo 22:15''
Tatizo kubwa jingine katika dunia ya leo kuna wamama wanandoa hawataki kuzaa. Unakuta Mama aliolewa akiwa ameshazaa huko nyuma kwa sababu ya uasherati wake. Sasa anaingia katika ndoa hataki kuzaa, hiyo haifai. 
Kesi za watu wa jinsi hiyo zipo sana.
Kuna wadada wengine hawataki kuzaa kwa sababu tu wataharibu maumbo yao.
Kuna dada mmoja alisema hataki kuzaa kwa sababu atazeeka mapema na ataonekana mbaya. Binafsi mimi huo utamaduni wa Mwanandoa kutunza mwili kwa kutokuzaa wakati hawana hata mtoto nauona kuwa ni utaratibu mbaya.
Leo wanaotoa mimba sio mabinti tu, hata wanandoa wengine hutoa mimba na kujibebea laana na dhambi nyingi tu.
Kuzaa na kulea ni jukumu la mama na baba pia.
Usikatae kuzaa ukiwa katika ndoa yako kwa sababu zako Binafsi zisizo na maana.
Wengine akishaolewa na kukuta maisha magumu hugoma kuzaa akijidanganya kwamba ataachana na mwanaume huyo na kuolewa kwingine ambako huko atazaa, huo ni utoto wa kiroho na ni machukizo.
Umekubali kuolewa basi kubali na kuzaa pia katika malengo lakini ni marufuku kutoa mimba.

5.  Kumtii mumewe katika Bwana YESU.

Waefeso 5:22 '' Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu.''
Kumtii Mume katika Bwana YESU ni agizo la Biblia.
Kumtii Mume katika Bwana maana yake kumtii katika mema na sio dhambi.
Mithali 14:25 ''Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu; Bali atoaye uongo hudanganya.'' 
Ewe mwanamke uwe shaidi wa kweli ili kuponya nafsi  ya mumeo.
Kweli ni Neno la MUNGU hivyo hakikisha unakuwa shaidi wa Neno la MUNGU ili kumsaidia mumeo.
Wanawake wengi sio watii kwa waume zao.
Baadhi ya Wanawake akijiona tu ana mshahara kuzidi mumewe basi huanza kiburi na dharau kwa mumewe, hiyo ni dhambi na wengi pia wameikosa mbingu kwa sababu ya kukosa utii kwa waume zao katika haki.
Mume ndie kiongozi wa familia hivyo mtii mumeo katika upendo.
MUNGU hakuagiza baba amtii mkewe bali MUNGU aliagiza mama amtii mumewe katika KRISTO YESU, Ukishindwa kumtii mumeo katika haki ya MUNGU hakika unakosea na ni dhambi.
Hutakiwi kumtii mumeo katika maovu  na katika dhambi au mambo yanayoweza kukuingiza dhambini lakini katika mema hakika mke anatakiwa kumtii mume maana ni agizo la MUNGU.
Mume ni mtawala wa familia hivyo katika mema anatakiwa apewe haki yake.
Kumheshimu mumeo ni sehemu ya kumtii.
Kumfariji mumeo kwa upendo ni sehemu ya kumtii.


Majukumu mengi ya mke kwenye ndoa ni sawa na majukumu ya mume lakini mume kwenye ndoa ana majukumu mengi kuliko mke.

 Watu wengi tumeingiza sana mambo ya duniani katika ndoa.
Mfano, Msemo Wa haki sawa huo sio Wa kibiblia lakini kila mwanandoa ana haki zake.

Mke kumtii mmewe ni haki yake na mume kumpenda mkewe kama nafsi yake ni haki yake.
Wanandoa wakitembea kwenye hayo hakika ndoa itachanua.
Lakini pia mwanamke anapoambiwa amtii mumewe ni katika BWANA tu na sio vinginevyo.
Na kumtii mumeo katika BWANA ni kumtii katika mambo ambayo sio dhambi na ni kumtii katika Yale ambayo hayachochei dhambi au kunajisika.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments