MLANGO WA KISHETANI WA MATESO.

Na Pastor Dr. Godson Issa Zacharia (SNP), Ufufuoa uzima Morogoro


Duniani hapa yapo mateso mengi sana ya aina tofauti tofauti. Kila mmoja wetu kuna wakati aliwahi kupata mojawapo ya mateso haya kwa namna moja au nyingine. Yesu Kristo mwenyewe aliwahi kupata mateso hata akasulubiwa msalabani. Tukisoma katika KUTOKA 3:7 neno la Mungu linasema hivi...”Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;”. Kwa maandiko haya, Mungu anasema “ameona na kusikia” mateso ya wana wa Israeli waliokuwa wakiteswa huko Misri.
Hata kwa wewe uliyeokoka, ujue kuwa mateso bado yapo, tena siyo machache. Ndiyo maana katika ZABURI 34:19 imeandikwa hivi…(Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.). Kumbe ukiwa mwenye haki mateso yapo pale pale, tena siyo moja wala mawili wala matatu; ni mateso mengi. Cha kufurahia ni kwamba, Mungu ameahidi kutuponya na mateso haya yote. Kwa nini atuponye? Ni kwa sababu mateso haya pamoja na wingi wake, hayajatoka kwa Mungu. Kwa hiyo Mungu anakuja kutuponya na mateso haya yatokayo kwa yule muovu shetani, na kutuweka huru.
Katika MAOMBOLEZO 3:33 imeandikwa hivi “Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.” Ni dhahiri kuwa, Mungu wetu hapendi kutuona tukiwa katika mateso na huzuni. Siyo kweli ktuiana moo na kusema ni mapenzi ya Mungu kwa mtu afukuzwaye kazi, ambayo alimuomba Mungu ampatie!! Siyo sahihi pale unapopata ujauzito na baadae mimba kuharibika kusema eti hayo ni mapenzi ya Mungu. Fahamu kuwa, mateso yote ya aina hii hayatoki kwa Mungu, kwa kuwa Mungu wetu hapendi kutuhuzunisha.
Wapo watu wanaojiliwaza kwa kusema “mwenzenu nimeingia katika majaribu” au “mwenzenu nimeingia katika madeni” au mwingine “mwenzenu nimeingia katika mateso” na mwingine pia kusema “mwenzenu nimeingia katika magonjwa”.. Usikiapo kauli za watu wa aina hii ujue kuwa, kuna mlango wa mateso na shida wa kishetani uliofunguliwa, na mtu huyo akaingia katika huo mlango bila kujua. Ni rahisi sana kuingia katika mlango wa mateso wa kishetani.
Kwa kawaida, mlango wa kuingia katika raha, au utajiri na mafanikio ni mwembamba sana, na wachache sana wanaweza kuuona na kuingia ndani mwake. Lakini ule mlango wa mateso wa kishetani, ni mpana sana kiasi kwamba watu wengi wanaingia na kujikuta tayari wamenaswa na mambo ya dunia yaliyomo mle ndani. Wapo walinzi wanaozuia watu kuingia katika mlango wa baraka. Lengo lao ni kuachilia watu wasiuone na waingie ule mlango mpana wa kishetani na kukaa katika mateso siku zote. Sio rahisi upatapo mateso kuwapata watu wa kukushauri uende kanisani, sanasana wengi watakushauri ubaki na dini yako au uende kwa waganga wa kienyeji n.k.
Kwa kawaida mlango ni mahali pa kuingilia. Mlango wa kishetani humfanya mtu kuingia katika ngome ya mateso, na siyo rahisi kutoka humo labda apatikane mpakwa mafuta wa Bwana aliyeandaliwa maalumu ili akutoe humo. Yesu mwenyewe aliwahi kutangaza kazi yake ya kuja hapa duniani, tunaposoma katika LUKA 4:18…”Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa”. Kwa hiyo wafungwa waliopo ndani ya magereza wataachiwa tu na aliyetumwa kuifanya kazi hiyo, yaani Yesu Kristo pekee. Yesu mwenyewe ndiye mlango wa baraka zetu. Imeandikwa katika YOHANA 10:1 “Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi”.
UKIRI
Nakataa kuingia katika mlango wa mateso kwa Jina la Yesu. Ewe mlango mpana wa kishetani ulioandaliwa ili mimi niingie humo nakataa mimi na nyumba yangu kuingia mlango huo kuanzia sasa kwa Jina la Yesu. Nakataa kupanda farasi aliyeandaliwa kunipeleka kwenye mateso, kwa Jina la Yesu. Amen

Katika kipindi cha zamani, miji ilijengwa kwa kuta kuizunguka na kuweka malango / au mlango wa kuingilia. Ndivyo ilivyofanyika katika miji kama Yeriko na hata Yerusalemu (malango 12). Lengo la kufanya yote hayo ni kuimarisha ulinzi, kujilinda. Hata hivyo, katika nyakati zetu hizi, ulinzi wetu siyo wa kimwili bali kupambana na maadui wetu katika ulimwengu wa roho. Imeandikwa katika EFESO 6:12…”Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” na pia katika 2KORINTHO 10:3-4 imeandikwa hivi “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; 4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)”. Malango ni mashetani, na walinzi wake ni mashetani na ngome yenyewe ni ya kishetani, ila wanaoingizwa mle ndani ni wanadamu kama wewe na mimi.
Kila penye mlango pana mlinzi wa kuruhusu watu kuingia au kutoruhusu waliomo ndani kutoka. Ndivyo ilivyoandikwa katika YOSHUA 2:1-3 (Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko. 2 Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi. 3 Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi.). Jambo la kujiuliza hapa ni, Mfalme alijuaje kwamba kuna wapelelezi walioingia humo mjini?. Ni kwa sababu walinzi wa kutazama kutokea juu ya ukuta walikuwepo na ndio waliowaona wale wapelelezi waliotumwa na Yoshua.
Mlango wa Mateso wa Kishetani unao walinzi ambao nao ni mashetani, wanaokaa mlangoni mwa ngome za mashetani. Unapoyaona mateso katika mwili wako, ujue kuwa mateso hayo yalishatengenezwa katika ulimwengu wa roho kabla ya kudhihirishwa katika mwili. Unaweza kuwa tayari umeshakamatwa, na ndiyo maana unakiri kuwa umeingia katika mateso!!. Anayetaka kukuingiza katika mateso anakaa katika mlango, na ujue kuwa milango hii ni ya kiroho.
Mashetani yanayolinda malango yapo katika idara kuu tatu:
1. IDARA YA KUKAMATA (Arresting Department).
Hawa hufanya kazi ya kuwinda watu, kisha kuwakamata na kuwaingiza mle kwenye lango la mateso. Kwa hiyo ukiona yupo mwenye mateso (mfano: mwenye magonjwa, dhiki, uzinzi, ulevi n.k), ujue aliwahi kuwindwa, akakmatwa na kuingizwa mle kwenye ngome hiyo ya mateso.

Imeandikwa katika 1PETRO 1:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, akitafuta mtu ammeze.” Watu wanapokamatwa na kuingizwa humo ngomeni, huteswa sana. Mateso ya magonjwa, hasara, kukataliwa, kuachwa, ndoa kuharibika n.k. Endapo teso moja likiisha hutokea teso lingine. Mungu mwenyewe anayajua haya, na ndiyo maana akasema “Mateso ya mwenye haki ni mengi sana” Misukule wengi wanakamatwa katika idara hii. Na wengi wa watu waliowahi kukaa msukuleni utakuta wakihadithia mateso ya aina hii (kulishwa pumba, damu za watu n.k). Mashetani wanaotesa watu waliomo humu langoni ni wenye wivu sana. Ukionekana unakula vizuri, watakuwinda na kukuingiza katika hayo mateso ili usiweze kula vizuri tena.
Ni wajibu wetu tuliookoka kuingia magotini na kuomba kwa bidii ili kuwatoa watu walionaswa katika hizi ngome mateso za mashetani. Kuna watu leo hii ni wezi sugu na hata wakiaambiwa waache wizi wanashindwa kabisa. Watu wengine wana tabia ya ukahaba, na imekuwa ngumu kwao kuiacha tabia hii. Wengine ni watumiaji wa dawa za kulevya, tena hata wanajidunda sindano za dawa hizi, pamoja na maumivu ya kujjidunda sindano yalivo lakini bado wapo tayari kuvumilia tu!!. Mateso yote haya husababishwa na mashetani wanaotesa watu wakiwa katika hizi ngome za mateso. Leo tuanze kwa kumpiga huyu anayekamata watu (Arrester) yaani shetani na kumlazimisha kutachia kwa Jina la Yesu.
UKIRI
Leo wale wote wanaowinda maisha yangu ninawaponda, ninakushinda ewe mzimu, ewe joka, imeandikwa kila silaha ya uwindaji iliyopangwa inipate haitafanikiwa, imeandikwa nao wakamshinda kwa Damu ya Mwanakondoo, nami nawashinda wawindaji wote wa maisha yangu kwa Damu Ya Mwanakondoo. Mashetani wa mateso leo ninawaponda kwa Jina la Yesu. Amen
Hata hivyo katika idara hii, mtu anaweza kuteswa kwa kitambo kidogo tu, pengine siku au wiki moja au hata mwezi au mwaka. Wanaweza kumuacjhim mtu na baadae wakaja tena kumwinda upya.

2. Idara ya Kulinda Mtu abaki katika mateso aliyo nayo milele
Hawa hawataki kabisa aliyekamatwa aachiliwe au kuwekwa huru. Katika idara hii, mashetani wake hawaachi mtu kuwa huru. Imeandikwa katika ISAYA 14:17… “Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao? ”. Mtu akeshaingizwa kwenye idara hii, asitarajie kuwa huru, ni sawa na kifungo cha maisha. Mashetani haya hukasirika yanapoona kuna watu wanaofanya juhudi ili mtu wawekwe huru. Ndiyo maana, utaona baadhi ya ndugu wakizuia mgonjwa asipelekwe kanisani ili kuombewa. Uonapo watu wazuiaji wa aina hii, ujue ni wale ambao wanafanya kazi na mashetani katika idara hii ya kuzuia, na hufanya kazi ya kumfanya mtu abaki katika mateso yake.

Katika ZABURI 24:7-10 Imeandikwa hivi “Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Inukeni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia.8 Ni nani Mfalme wa utukufu? Bwana mwenye nguvu, hodari, Bwana hodari wa vita.9 Inueni vichwa vyenu, enyi malango, Naam, viinueni, enyi malango ya milele, Mfalme wa utukufu apate kuingia. 10 Ni nani huyu Mfalme wa utukufu? Bwana wa majeshi, Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.”. katika hili, utaona kuwa zipo familia au koo zenye mateso ya jkufana fanana. Mfano ni pale Sara mke wa Ibrahimu alikuwa tasa, na hakuzaa kwa muda tarajiwa, na hata alipompata Isaka uzeeni, shida hii ilijirudia kwa kumpata Rebeka mke wa Isaka kwa kutopata mtoto kwa wakati, na baadae shida hii ikampata pia Leah mke wa Yakobo.
Hayo ni mashetani yazuiayo, na hata katika familia na koo mbalimbali yanakuwepo ili kusababisha mateso ya kufanana.
3. Idara ya Kufunga Mlango wa Baraka
Haya ni mashetani yatakayomzuia mtu kuingia katika baraka zake. Mashetani haya yanajua kuwa mtu huyu ni mwaminifu na kwamba yameshindwa kuingia ndani yake au hata kumkamata kwenye mateso. Mashetani haya yatakaa mlango wa baraka za mtu na kufanya kazi ya kumzuia mtu huyu, kwa sababu yanajua kuwa akipenya hapo basi maisha ya mtu huyu syatakuwa mazuri mno kupindukia. Mathalani mtu akitaka kuoa, au kufanya bishara fulani nzuri au fursa nzuri ya kujiendeleza kimasomo, mashetani haya yatahakikisha kuwa mtu wa aina hiyo hawezi kupenya hapo. Mashetani haya ni ya kuzuia mtu asifikie ufanisi wa anachokifanya.

Yesu na wanafunzi wake waliwahi kuzuiliwa kuuingia Mji wa Wagerasi. Tukisoma katika MATHAYO 8: 28-34 imeandikwa “Naye alipofika ng'ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. 29 Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? 30 Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. 31 Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. 32 Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. 33 Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia. 34 Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao). Huu mji wa Wagerasi uliitwa pia Decapolis (maana yake ni miji 10 iliyoungana pamoja). Ndani ya watu hawa wazuiaji yalikuwepo mapepo yaliyoweza kuingia ndani ya kundi la nguruwe 2,000 nao wakakimbilia baharini na kuangamia wote. Mji wa Wagerasi ulikuwa umezuiliwa watu kutouingia, na wazuiaji wake walikuwa ni wakali mno. Ndivyo ilivyo hata kwako leo hii, kwamba unapotaka kuingia katika eneo la baraka zako, watajitokeza wazuiajjji ili usifanikiwe.
Hata hivyo wazuiaji hawa hawana shida ya kuwazuia watu wale wasiomwamini Yesu, kwa sababu watu wa aina hiyo wepesi kumsujudia shetani katika muda wowote ule. Ndiyo maana shetani alimjaribu Yesu ili eti amsujudie kama sharti la kumpatia fahari za dunia hii. Imeandikwa LUKA 4:5-7 “Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. 6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo. 7 Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako). Ndiyo kusema, wapo watu waliotajirika leo hii lakini kupitia njia za kumsujudia shetani na mawakala wake (waganga wa kienyeji, wachawi, wasoma nyota n.k).
Kwa wewe uliyeokoka unachopaswa kufanya kinyume na mashetani yanayozuia mlango wa baraka zako ni kuamka kama shujaa wa Bwana na kuyang’oa hayo malango na kisha kuwapiga walinzi wake kwa Jina la Yesu. Amua leo kuingia katika baraka zako kwa kuomba kwa Bidii kwa Jina la Yesu. Kumbuka alichokifanya mnadhiri wa Mungu Samsoni pale alipozuiliwa na lango la mji ule wa Gaza, alichokifanya ni kuling’oa lile lango na kuondoka nalo. Yesu Kristo anayetuponya na mateso yupo hapa leo kwa ajili yako. Leo tutayang’oa malango yanayozuia baraka zetu na kisha kumiliki yale Bwana aliyokusudia kwetu kwa Jina la Yesu.
========== AMEN ========

Comments