NI HERI KUTUBU DHAMBI ZOTE NA KUZIACHA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU KRISTO atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Dhambi sio kitu cha kujificha.
Hata ukificha dhambi zako sasa lakini ipo siku dhambi hizo zitakuwa wazi tu, ukificha zaidi dhambi hizo basi jehanamu itakuumbua tu.
Ni muda wa kutubu na kuacha dhambi.
Ni muda wa kukimbilia kwa YESU kwa toba ili mzigo wa dhambi uondolewe kwako, na sasa uwe huru ndani ya KRISTO YESU Mwokozi wako.


 Imeandikwa "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha
atapata rehema.-Mithali 28:13"

 
Hakuna mafanikio katika kuficha dhambi.
Hakuna ushindi wa kiroho katika kuficha dhambi.
Hakuna baraka za MUNGU katika kuficha dhambi.
Hakuna ulinzi stahiki kwenye dhambi.
Hakuna nguvu za kumfukuza shetani kwenye dhambi.
Hakuna uponyaji kwenye dhambi.
Hakuna kukubaliwa na MUNGU.
Ndugu, Biblia inasema anayetubu na kuziacha dhambi utapata msamaha na kuachiliwa.
Kwanini usiwe wewe kutubu Leo na kuacha dhambi?


Imeandikwa "Tubuni kwa maana ufalme wa MUNGU umekaribia-Mathayo 3:2"

Imeandikwa "Tubuni na mrejee ili zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwapo kwake Bwana YESU-Matendo 3:19"
Ndugu usipoteze muda wako kwa shetani.
Ni saa ya kutubu na kuacha dhambi zako zote.
Je unataka kutubu na kuacha dhambi hata jina lako likaandikwa kwenye kitabu cha uzima na ukawa mmoja wa wateule wa Bwana YESU walio tayari kwa uzima wa milele?
Kama jibu la moyo wako ni ndio basi imeandikwa 


" Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake.
Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli;
bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.-1Yohana 1:5-9.


Ndugu yangu, ni wewe uliyekusudiwa Leo.
Damu ya YESU KRISTO tayari kukusafisha na kukufutia dhambi zako zote, ukimpokea YESU Leo na kutubu.
MUNGU yupo tayari kukupa rehema ukiokoka Leo na kuacha dhambi zako zote.
Rehema ni neno kubwa sana.
Rehema ni zaidi ya msamaha.


Rehema za MUNGU huanganisha mambo matatu;
1. Kusamehewa kwa kufutiwa dhambi zako zote.

2. Kuachiliwa kila uovu ulioutubia.
3. Kufutiwa hati zote za mashtaka kukuhusu.
 
Hata dhambi zako zilikuwa ni mbaya sana au ni nyingi sana, Bure kabisa MUNGU Baba anakusamehe kwa wewe kumpokea Mwanaye YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.
Ni muhimu sana sana kutubu na kuacha dhambi.

Imeandikwa Marko 1:15 kwamba "Wakati umetimia, na ufalme wa MUNGU umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili."


Ni muda wa kuiamini injili ya KRISTO na kuiishi.
Uzima wa milele upo na uzima huo unawahusu tu watakatifu katika KRISTO YESU.
Injili ya KRISTO ndilo fundisho kuu la Biblia wakati huu wa kanisa.


Injili ya KRISTO inahitaji mambo haya Kumi(10);

 
1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mkombozi, na kwa njia hiyo unafanyika mtoto wa MUNGU aliyeandaliwa makao mbinguni, Yaani KUOKOKA
Yohana 1:12 ''
Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake;''
Kumpokea YESU kama Mwokozi ndio kuokoka.
 Yohana 14:1-3  ''Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini MUNGU, niaminini na mimi(YESU). Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.''
 Kuokoka ndiko kutengenezewa mako mbinguni.
Ni muhimu sana kumpokea YESU kama Mwokozi ili makao au kwa jina lingine makazi yako yaandaliwe mbinguni.
Bila YESU hakuna uzima wa milele.
 Matendo 4:12 '' Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''


2. Kutubu na kuacha dhambi zote
Matendo 3:19 ''
Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; ''
Injili iko wazi ikitutaka kutubu na kuacha maovu yote.
MUNGU yuko tayari kuwapokea wanaotubu na kuacha maovu yao.
Isaya 55:6-7'' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.''
 na ni muhimu sana kumkimbilia Bwana YESU kwa ajili ya msamaha maana damu yake tu ndio inaweza kuondoa dhambi katika mwanadamu.
 warumi 6:23'' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''

3. Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa YESU KRISTO.
1 Petro 1:15-16 ''
bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. '' 

 Injili inatutaka kuishi maisha maisha matakatifu.
Tena Bila utakatifu mwanadamu hawezi kumwona MUNGU, ni muhimu sana kuwa watakatifu.
 Waebrania 12:14 '' Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;''

 
4. Kumtumikia MUNGU kwa kuipeleka injili ya KRISTO mbele.
Marko 16:15-16 ''
Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.''
Ni agizo la Bwana YESU ambaye ndiye mwenye injili kwamba tuhubiri injili yake.
Ni kazi ya kila mteule wa KRISTO kuihubiri injili, ni kanuni ya MUNGU kwamba tumtumikie.
Mathayo 28:19-20 '' Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la BABA, na MWANA, na ROHO MTAKATIFU; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.''

5. Kuishi katika ROHO MTAKATIFU na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU huku tukimtii.
Wagalatia 5:25 ''
Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''
Wateule wote wa MUNGU inawapasa kuishi kwa ROHO MTAKATIFU na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Baada ya kumpokea YESU hakuna wa muhimu kama ROHO MTAKATIFU kwa Mwamini.
ROHO MTAKATIFU ni muhimu sana.
Wenye ROHO MTAKATIFU na wanamtii hao ndio waliookoka, hao ndio watoto wa MUNGU.
Warumi 8:9,14 ''Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

6. Kulitii Neno la MUNGU na Maombi.

Yohana 6:27 ''Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, MUNGU.''
Neno la MUNGU ndilo chakula cha uzima kidumucho milele.
YESU KRISTO hutoa chakula cha uzima ambacho ni Neno lake.
Elimu za kidunia na mambo ya kidunia ni vyakula vya kuharibika tu baada ya muda, Ndio maana Biblia inakushauri kwamba usikitendee kazi chakula chenye kuharibika bali kitendee kazi chakula cha uzima ambacho kiko kwa BWANA YESU tu, chakula hicho ni Neno la MUNGU.
Injili pia inatuhimiza katika maombi.
 Yohana 15:7 ''Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.''


7. Kuzaliwa upya katika damu ya YESU KRISTO na kuachana na mambo ya dunia maovu.
2 Kor 5:17 ''Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya ''


Mtu akiwa ndani ya KRISTO ni mtu wa thamani sana.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO inabidi ya kale yapite na yasirudie tena.
Mtu akiwa ndani ya KRISTO ya kale anatakiwa ayaache na sasa afuate mapya yanayofundishwa na Biblia.


8. Kuzitumia kwa utukufu wake MUNGU karama na vipawa alizotupa.
1 Kor 4:1 '' Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU.''

Kumbe wateule wa KRISTO wote ni watumishi wa KRISTO na mawakili wa siri za MUNGU.
Kazi yetu ya uwakili iko katika kuipeleka injili ya KRISTO kwa watu wote.
Karama ya kila mtu inatakiwa itumike vizuri.
Karama yako mteule lazima uifanye kwa utukufu wa MUNGU na ukimpendeza MUNGU.
Kama una karama ya uimbaji basi mtumikie MUNGU, Kama una karama ya kufundisha basi fundisha neno la MUNGU.
Kipawa chako chochote kitumie katika kazi ya MUNGU na sio vinginevyo.
1 Kor 12:4-11 '' Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na BWANA ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana.  Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ''
 
9. Kuvumilia mpaka mwisho.
Mathayo 24:13 ''Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.'' 

MUNGU ametupa neema kubwa sana sisi Kanisa lake, Injili inatutaka kuvumilia katika maisha haya.
Ni lazima tutunze heshima ambayo MUNGU ametupatia.
Tunahitaji kuvumilia hadi mwisho.


10. Kuishi kama wasafiri na wapitaji duniani.
  1 Petro 2:9-11 '' Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.Wapenzi,nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. ''
Dunia sio kwetu hivyo inatupasa sana kuishi kama wasafiri na wapitaji.
Mtu kama anasafiri hakika atakuwa macho na atakuwa amejiandaa muda wowote kwenda safari yake, Kanisa ni wasafiri duniani hivyo ni muhimu sana kuishi kama wasafiri na sio wenyeji.

MUNGU akubariki sana kama utatubu na kuiamini injili ya KRISTO na kutii.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
 Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments