SABABU ZA KULIHITAJI NENO LA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza sababu au umuhimu wa kila mtu kulihitaji Neno la MUNGU.
Sababu mojawapo ya kulihitaji Neno la MUNGU ni kwamba Tunalihitaji Neno la MUNGU ili likafanye mabadiliko ndani yetu, Hivyo ni muhimu sana kila mtu kulihitaji sana Neno la MUNGU.
 ''Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.-Mathayo 4:4''
Litokalo katika kinywa cha MUNGU ni Neno la MUNGU.
MUNGU ameshazungumza kupitia Biblia na amezungumza sana kupitia watumishi wake ndani ya Biblia ili kutusaidia sisi wanadamu.

MUNGU ametupa Neno lake Biblia ili;

1.  Tujue mpango wa MUNGU wa Wokovu kwetu.
Yohana 3:16-18  Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

2.   Ili tumwabudu katika kweli na kumtumikia.
 Yohana 4:24 ''MUNGU ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.''

3. Ili tujue jinsi ya kuwa watakatifu na tuwe watakatifu kwa kulitii.
 Yohana 15:3 ''Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.''

4.   Ili tusitende dhambi.
Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''


5.   Tujue ahadi za MUNGU na kulitumia Neno hilo la MUNGU kwa halali.
2 Timotheo 2:15 ''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.''


6.   Ili lituondolee ujinga na kutupa nuru ya MUNGU.
Zaburi 119:130 ''Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.''


7.   Ili tuliishi Neno hilo na kuukulia Wokovu.
1 Petro 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''


8.   Ili litujulishe yaliyopita, yaliyopo na yanayokuja mbele yetu wanadamu.
Mwandishi mmoja wa Biblia aliambiwa ''Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.-Ufunuo 1:19'

9.  Ili Litupe akili nzuri na  maarifa ya MUNGU.

Mithali 1:7 '' Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.''

10.  Ili litufanye kuwa viumbe wapya waliotengeneza na MUNGU kwa njia ya Neno lake.
2 Kor 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. "

Ni muhimu sana kulizingatia Neno la MUNGU.
Usiposikia na kuzingatia Maneno ya MUNGU utayasikia maneno ya watu, ukiendelea zaidi kuyasikia maneno ya watu unaweza kujikuta unasikia maneno ya shetani, kisha kwa hayo maneno ya shetani unaweza ukajikuta unapata cheti cha dhambi.
Ni ni muhimu kukumbuka kwamba wenye vyeti vya dhambi wasipopata neema ya KRISTO inayowataka kutubu, hakika wanaweza kujikuta jehanamu.
Ndugu, Penda kusikia Neno la MUNGU halisi na fanyia kazi Neno la MUNGU.

Neno la MUNGU ni muhimu sana, na Biblia inasema 
''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.-Waebrania 4:12''

 Kiini cha Neno la MUNGU ni ukombozi kwa mwanadamu ambao ukombozi huo huja kwa njia ya KRISTO, Kumpokea na kuishi maisha matakatifu kwa kulifuata Neno la MUNGU.
Warumi 10:17 ''Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''

Ni muhimu sana kujua pia kwa wewe ambaye tayari umeshalipokea Neno la MUNGU, Usikubali kuitwa tu mlokole Bali okoka kwelikweli.
Neno la MUNGU ukilitii litakusaidia kumpendeza MUNGU.
 Kama umemkosea MUNGU kwa mwaka uliopita basi jitahidi sana kumpendeza MUNGU mwaka huu, mtii MUNGU sasa na litii Neno lake. Kumbuka Neno la MUNGU halitapita kamwe, hivyo ni heri tu kulitii hilo.
''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35''

 Inawezekana kabisa umepewa kuishi mwaka huu kwa kusudi la wewe kutengeneza njia zao.
Ndugu jitahidi sana kumtii MUNGU na tii neno lake.

Ndugu usipokee neno ilimradi neno Bali pokea Neno la KRISTO maana hilo lina uzima wako.
 Kama huna uzima hata hizo pesa zako nyingi zitakusaidia nini?
YESU analo neno la uzima, mtii yeye utapata uzima wake. Mtu asiye na Neno la MUNGU Siku zote ni mtu wa kulalamika tu maana kukosekana kwa Neno la MUNGU ndani ya mtu kunaweza kukatoa nafasi ya neno la shetani kumtumia mtu huyo.

Ndugu, Ahadi za MUNGU kwako ni kweli na amina. 
Tatizo la watu wengi ni kutokukaa katika kusudi la MUNGU na kuanza kujichafua kwa dhambi. 
Ndugu kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa na mafanikio. songa mbele na BWANA YESU wala usikubali kurudi nyuma.
Litii Neno la MUNGU na liishi hilo.
 
Lakini pia kama wateule wa KRISTO inatupasa kuwa 
VIUMBE VIPYA WENYE AFYA.
Yohana 4:10 "YESU akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya MUNGU, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai."

YESU ana chakula cha uzima ambacho ni Neno lake.
YESU ana maji ya uzima yaliyo hai, kumpokea yeye na kuishi maisha matakatifu katika yeye huko ni kunywa maji yaliyo hai ambayo hutupa uzima wa milele.
YESU ana maji ya uzima.
YESU ana uzima na uzima huo wa milele ametuandalia wateule wake.
Matokeo ya sisi kula chakula cha uzima na kunywa maji yaliyo hai ni kutufanya tuwe viumbe vipya.
Ukidumu katika neno la KRISTO na kuishi maisha matakatifu katika yeye hakika unakuwa kiumbe kipya.

2 Kor 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya. "
Wateule wa MUNGU ni viumbe Vipya.
Neno la MUNGU hutufanya tuwe wapya kama tukilitii.
Ndugu yangu hakikisha unakuwa kiumbe kipya.
Kiumbe kipya hakiendi kwa waganga.
Kiumbe kipya sio mzinzi wala mwasherati.
Kiumbe kipya sio muongo wala mwizi.
Kiumbe kipya huchukia dhambi na hukaa mbali na dhambi.
Viumbe vipya ni watakatifu waliokubali kubadilishwa na neno la MUNGU na kuwa wapya.
 Ndugu hakikisha unakuwa Kiumbe kipya kilichookolewa na Bwana YESU.


Jambo jingine ni muhimu  kulizingatia kwa watoto wa MUNGU wote ni kwamba 
WATOTO WA MUNGU NI LAZIMA TUKUE.

Wote tuliompokea YESU tumefanyika watoto wa MUNGU.
Watu wote ni watu wa MUNGU lakini sisi ni zaidi ya watu wa MUNGU, sisi tuliookoka ni watoto wa MUNGU.
Sio watoto wa kimwili Bali ni watoto wa kiroho.
Roho zetu zimezaliwa upya na MUNGU.
Ndani yetu kunatakiwa kuwepo utakatifu ambao ndio tabia ya uungu, tunatakiwa tuwe na tabia ya uungu.
Kwa njia ya kumwamini na kumpokea YESU KRISTO tumekuwa watoto wa MUNGU.
Wote tuliomwamini YESU tumefanyika watoto wa MUNGU.

Yohana 1:12-13 ".Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

Wokovu wa KRISTO ndio hutufanya kuwa karibu na MUNGU wetu.
Wokovu wa KRISTO ndio uliotufanya tuwe wana wa MUNGU.
Ni kitu kikubwa sana hiki na kwa jinsi hiyo tunatakiwa tuishi kama watoto wa MUNGU, na si watoto wa dunia.
Sasa kama watoto wateule na wapendwao tunatakiwa sana tukue kiroho.
Kila mtoto wa MUNGU anatakiwa kukua kiroho.
Na ili tukue kiroho ni lazima tuyatamani na kuyanywa maziwa ya akili yasiyoghoshiwa ambayo ni Neno la MUNGU.
Mtoto mchanga kiroho bila kunywa maziwa haya ya haki hawezi kujua kiroho na hawezi kuishi kiroho muda mrefu.
Biblia inatushauri sana kuhakikisha tunakuwa kiroho.
Ili tukue kiroho ni lazima sana tunywe maziwa ya ufahamu ambayo ni neno la MUNGU.

"1 Petro 2:2-3 "Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili."

Ili tukue kiroho tunahitaji kula chakula kizuri ambacho ni neno la MUNGU.
Tunahitaji chakula ambacho hakijaharibiwa .
Tunahitaji neno la MUNGU ambalo li hai siku zote.
Kwanini ni muhimu sana kuokoka na kuukulia wokovu?
Kwanini sana ni muhimu sana kuishi maisha matakatifu ya wokovu?
Ndugu zangu kuna hukumu kwa waovu wote.
Kuna adhabu ya milele kwa wanaomkataa YESU na wokovu wake.
Biblia inajulisha kwamba kuna siku ya mwisho na ni hatari sana kwa wanaomkataa YESU na wanashindwa kuishi maisha matakatifu.
Mathayo 16:27 "Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa BABA yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. "


Ili tuishi vyema tunatakiwa tuwe safi na sio wachafu.
Safari ya mbinguni inahitaji watakatifu tu.
Neno la MUNGU ni chakula cha uzima na hilo tunatakiwa tulitii sana.
Kwa Neema ya MUNGU ya kutuokoa tunatakiwa sana tuishi maisha ya kumpendeza MUNGU wetu aliyetuokoa.

" MUNGU na atufadhili na kutubariki, Na kutuangazia uso wake. Njia yake ijulike duniani, Wokovu wake katikati ya mataifa yote. Watu na wakushukuru, Ee MUNGU, Watu wote na wakushukuru. -Zaburi 67:1-3

YESU alikufa kisha akafufuka, kisha akaenda mbinguni na kisha atarudi tena.
Ndugu yangu naomba ujue kwamba YESU atarudi tena na Siku hiyo atawahukumu wanadamu wote wakiwemo unaowajua wewe hivyo unatakiwa sana wewe uishi maisha matakatifu na saidia wengine kuishi maisha matakatifu ya wokovu wa YESU KRISTO.


Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments