USIWE KWAZO LA NAMNA YEYOTE

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU atukuzwe mpendwa wangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wakati mwingine si mara zote watu hukulaumu kwa kukusingizia, wakati mwingine jichunguze ili usiwe laumu au kwazo pasipo sababu.
2 Kor 6:3-10 '' Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe;  bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa MUNGU; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika ROHO MTAKATIFU, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa;
 kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.'
'


Mtumishi wa MUNGU hapaswi kuwa kwazo. 
Kama watu wanakwazika na wewe basi wakwazike kwa sababu ya injili, na kama wanakwazika kwa sababu ya injili basi wewe sio kwazo maana hujawakwaza lolote ila Neno la MUNGU ulisemalo ndilo limewakwaza, na Neno la MUNGU limekamilika na limejitosheleza ili kumsaidia mwanadamu haijalishi anakwazika au anafurahi.
Mtumishi wa MUNGU hutakiwi kuwa mtu wa kusambaza maneno ya uongo maana kwa hayo utakwaza watu.
Mtumishi wa MUNGU hupaswi kuwa mnafiki maana kwa unafiki huo utakwaza watu.
Kama wanadamu wanakusingizia wewe songa mbele maana wao wamekwishapata thawabu yao duniani na wewe endelea kuichuchumilia thawabu ya mbinguni yenye uzima wa milele katika Wokovu wa KRISTO..
YESU KRISTO akusaidie kama unaendelea kumtumainia yeye Mfalme wa Uzima wa milele ila usikubali kuwa kwazo.

Luka 17:1-4 '' Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!  Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe.''

Kuna baadhi ya watu wa kanisa wamegeuka kwazo hata kwa imani maana wanaipotosha kweli.
Unakuta mtumishi anaombea kwa pesa, huko ni kuwa kwazo na ni uovu.
Mathayo 10:8 '' Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.''
Badala ya kuulinda ufalme wa MUNGU wewe unauuza ufalme wa MUNGU?
Umekuwa Mkristo mbaya, umejitenga na KRISTO kwa kufuata tamaa zidanganyazo.
Umekuwa mtumishi mbaya, umejitenga mbali na KRISTO kwa kufuata tamaa zidanganyazo.




Wengine pia wamekuwa makwazo yanayosababisha hata watu waende jehanamu kwa sababu yao.
Wengine hata kweli inatukanwa kwa ajili yao kwa sababu ya uovu wao.
Kila Mteule wa KRISTO ni mtumishi wa MUNGU hivyo haiwapasi watumishi wa MUNGU kuwa makwazo ya kweli ya kuwafanya watu wasije kwa YESU hata wapate uzima.
Ni Mara ngapi umeikataa dhambi kama Yusufu alivyoikataa dhambi?
Ni Mara ngapi umeikimbia dhambi iliyokuwa inakunyemelea?
Ndugu yangu ni muhimu sana kuikataa dhambi na kuikimbia dhambi.
Kumbuka dhambi ni uasi kwa MUNGU, hivyo hatutakiwi kuwa waasi kwa MUNGU.

" Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza KRISTO; ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika YESU, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;
mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli. Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi. Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule ROHO MTAKATIFU wa MUNGU; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.-Waefeso 4:20-32"



Mtu mwingine anaweza kugeuka kwazo kwa sababu hajifunzi Neno la MUNGU hata akue kiroho.
Unakuta mtu ameokoka na huu ni mwaka wa 15 lakini hata akiambiwa kufunga masaa 12 tu hawezi.
Ndugu zangu ni muhimu kujua kwamba Mtu anayekua kiroho ni mtu yule anayejituma mwenyewe katika yaliyo ya KRISTO na MUNGU.
Warumi 12:11 "kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA;"
Je wewe unakua kiroho au umedumaa?
Je unakua kiroho au unashuka viwango vya kiroho?

Ukitaka kukua kiroho chukua kanuni ambayo ya Warumi 12:11  na zingatia maelekezo ya andiko hilo itakusaidia.

Kuna watu pia wamegeuka makwazo kwa sababu tu ya kutetea uovu.
Unakuta Mchungaji anatetea pombe.
Unakuta mtumishi anasifia nyimbo za kidunia.
Unakuta Mtumishi kwa sababu tu ya mapenzi yake kwa chama fulani au taasisi fulani ya kidunia au dhehebu fulani basi hutetea hata ujinga unaofanywa na kikundi hicho au kanisa hilo kwa sababu tu ni watu anaopendezwa nao.
Ndugu pendezwa na Neno la MUNGU na sio machukizo.
Je unaitetea kweli ya MUNGU au unatetea machukizo?
Ndugu, katika utumishi wako hakikisha unaitetea kweli ya injili ya KRISTO.

Hakikisha unakuwa muombaji na  kesha macho ya rohoni.
Omba MUNGU akupe macho ya rohoni ya kukesha.
Hata wakati umelala kimwili lakini macho ya rohoni ya kukesha huona kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho wakati huo.

 1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma;''

Je unataka kufanikiwa katika maisha yako?
Je unataka kufanikiwa kiroho na kimwili?
Jambo muhimu mpokee YESU kama hujampokea.
Ishi maisha matakatifu katika yeye na zingatia hii huku ukihakikisha kwamba wewe sio kwazo la kutafuta pesa kitapeli; 

Mithali 16:1-3 "Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA. Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huzipima roho za watu. Mkabidhi BWANA kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika."

Najua una matarajio mengi sana lakini kama huna YESU moyoni mwako ni hasara kwako. Biblia inasema
 "Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; Mtu mgeni wala si midomo yako wewe.-Mithali 27:1-2
Ukiwaza ushindi waza pia na utakatifu na hakikisha ushindi wako unambatana na utakatifu.
Ukiwaza ushindi katika MUNGU hakikisha unadumu katika utakatifu ndani ya Wokovu wa YESU KRISTO utafanikiwa.
Lakini katika yote usikubali kuwa kwazo kwa kanisa au jamii.


Vyanzo vya mtu kuwa kwazo ni.

1. Roho ya kiburi.
  1 Petro 5:5 inasema ''...MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.''
Kiburi ndio maana wa dhambi zote.
Kwa kiburi kunaweza kutokea makwazo mengi sana.


2. Dhambi.
1 Yohana 3:4 '' Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.'' 
Dhambi hutengeneza mambo mengi na hata kuna makwazo huja baada ya dhambi.
Fikria mwanakwaya anafanya uzinzi na kwaya nzima inaonekana ni wazinzi, na hata nyimbo zao wakiimba kanisani watu huona kama wanapoteza tu muda maana wanajulikana ni wazinzi wakati mzinzi ni mmoja tu na huyo amegeuka kwazo kwa kikundi kizima.
 
3. Kujihesabia haki.
Mathayo 7:1 ''Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi.'' 
Anayejihesabia haki siku zote huwaona wengine ni wabaya hata kama yeye ndiye mbaya.
Anaweza akawahukumu wengine hata kama yeye ndiye anapaswa kuhukumiwa.

4. Kujiona bora kuliko wengine.
Wafilipi 2:3 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.'' 
Ukijiona wewe ni bora kuliko wengine unakuwa unapishana Neno la MUNGU linalokutaka uwahesabu wengine ni bora kuliko wewe.
Ukijiona bora kuliko wengine hakika hutakuwa na unyenyekevu na kwa njia hiyo utageuka tu kwazo katika sehemu sehemu.
Kuna watu hata hawawezi kuwatii wachungaji wao kwenye kweli ya MUNGU na kwa njia hiyo hugeuka makwazo.
Kuna watu hata huwafuata baadhi ya washirika ili kuwarubuni ili wasifanye jambo fulani jema la kikanisa lililopagwa, kwa sababu tu wao hawakupewa kusimamia, huko ni kujiinua na kujiona bora na kwa njia hiyo mtu kama huyo lazima awe makwazo tu.

5. Tamaa.
Yakobo 1:14-16 ''Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti. Ndugu zangu wapenzi, msidanganyike.'
Ndugu tamaa zako mbaya zinaweza kuleta makwazo kwa jamii au kanisa au familia au majirani.
Usikubali kuwa kwazo lolote kwa sababu tu ya tamaa zako za kipepo.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments