WAITWAO, WATEULE NA WAAMINIFU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Ndugu mmoja aliniuliza swali hili
''Naomba nisaidie tofauti ya Mtoto wa Mungu, na mtumishi wa Mungu na mwana wa Mungu.''

Ndugu huyo nilimjibu swali lake lakini  swali hilo  naomba litufanye tuongezeke zaidi kiroho kupitia somo la leo.
Ngoja nianzie kitabu cha ufunuo.
Ufunuo 17:14 '' Hawa watafanya vita na Mwana-Kondoo, na Mwana Kondoo atawashinda, kwa maana Yeye ni Bwana wa Mabwana, na Mfalme wa Wafalme, na hao walio pamoja naye ndio walioitwa, na wateule, na waaminifu.'' 
Katika nyakati za mwisho shetani na jeshi lake atafanya vita na Bwana YESU lakini shetani atashindwa na majeshi yake yote.
Katika andiko hilo tunaona kwamba Bwana YESU alikuwa pamoja na watakatifu wake ambao Biblia inawaita kwa majina ya aina tatu tofauti yaani;
1 Walioitwa.
2. Wateule.
3. Waaminifu.
Hizo ni hatua ambazo kila mteule wa MUNGU anatakiwa kuwa nazo katika maisha yake ya Wokovu.
Tuliitwa tuokoke, Tulipotii tulimpokea YESU kama Mwokozi wetu na kwa jinsi hiyo tukafanyika wateule.
Hatutakiwi kuishia kuwa wateule tu bali tunapaswa kuwa wateule waaminifu.
Kumbuka '' Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.-Mathayo 22:14''
Sio wote walioitwa ili waje kwenye wokovu waliamua kufanyika wateule wa KRISTO.
Kuitwa ni hatua ya kwanza tu lakini kutii wito wa Wokovu na kuanza kuenenda katika witohuo  huko ndiko kufanyika mteule, lakini pia ni Muhimu sana mteule kufanyika Mteule mwaminifu.
 
=Mtoto wa MUNGU ni yule aliyezaliwa Mara ya pili au niseme ni yule aliyeokolewa na Bwana YESU na anaishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO.
Yohana 1:12-13 "Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."


Watoto wa MUNGU ndio hao hao wana wa MUNGU na wanaishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO huku wakiongozwa na kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU. "

=Mtumishi wa MUNGU ni mtu anayeifanya kazi ya MUNGU. Mtumishi wa MUNGU ni mtu anayetoka katika kundi la watoto wa MUNGU.
Mtumishi Ni Neno Linalotokana Na Neno "TUMIKA"
Mtumishi Wa MUNGU Ni Mtu Aliyetokana Na MUNGU Na Ametumwa Na MUNGU.
Mtumishi haanzi tu kujiita kwamba yeye ni mtumishi ila watu wakiona utumishi ndani yake na akitumika watamwita tu ''Mtumishi''.
Hebu ona mfano wa Danieli kama mtumishi wa MUNGU. Mfalme alimtambua Danieli kama Mtumishi wa MUNGU na alimwita kwa jina hilo la utumishi. Danieli 6:20 "Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danielii kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danielii, Ee Danielii, mtumishi wa MUNGU aliye hai, je! MUNGU wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? ". 
MUNGU alimponya mtumishi wake.

Pia Danieli katika maombi alijitaja kama mtumishi wa MUNGU, Danieli 9:17 "Basi sasa, Ee MUNGU wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya BWANA."

=Mwana wa MUNGU ndio mtoto wa MUNGU. 
Hivyo sisi tu watoto wa MUNGU kama tu tumeokolewa na Bwana YESU.
Sisi tuliookoka ndio watoto wa MUNGU
Watu wote ni wa MUNGU lakini waliookolewa na KRISTO ni watoto wa MUNGU na wanangoja uzima wa milele.

2 Kor 6:17-18 "Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,"
Ni muhimu tukayajua haya;
Waitwao ni wengi lakini wateule ni wachache.

Sifa za wateule ni hizi;

1.  Wateule ni wavumilivu.
2.  Wateule ni waaminifu.
3.  Wateule ni wakweli.
4.  Wateule ni wacha MUNGU.
5.  wateule humtii KRISTO.
6.  Wateule huenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
7.  wateule huishi maisha matakatifu.
8.  Wateule huongozwa na Neno la MUNGU.
9.  Wateule hutenda haki.
10. Wateule husamehe na kusahau.


Ni Heri kuwa mteule wa KRISTO.
Je wewe ni mteule wa MUNGU?
Waitwao ni wengi lakini Wateule mi wachache.
Ndugu nakuomba amua kuwa mteule.
Amua kuokoka na ishi maisha matakatifu ili kukamilisha uteule wako kwa KRISTO.

Wakolosai 3:12-13 '' Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa MUNGU, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu.'' Kama wateule wa MUNGU inatupasa pia tukue kiroho na kuongezeka.

Ili ukue kiroho unatakiwa kufanya mambo matatu kwa juhudi kubwa. 

1. Kuishi maisha matakatifu katika KRISTO. 
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; '' 

2. Kujifunza Neno la MUNGU kila Mara na utii unachojifunza. 
 Wafilipi  4:8-9 '' Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na MUNGU wa amani atakuwa pamoja nanyi.''

 
3. Uwe muombaji sana.
 Luka18:1 ''Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa.''

 Hutakiwi kuridhika na kiwango ulichopo Bali unatakiwa kupanda viwango vya Neno la MUNGU

 Kama Utaokoka Harafu Ndugu Zako Wakaanza Visa Tambua Kwamba Hawakuchukii Wewe Bali Wanamchukia Huyo YESU Aliyeingia Ndani Yako, Wanataka Wamuondoe Ndani Yako Ili Wamrudishe shetani Ndani Yako. Hapo Ni Mgongano Wa Madhabahu Maana Nuru Na Giza Havikai Pamoja. Songa Mbele Bwana YESU Maana Ana Uzima Wako Wa Milele.
Wewe umeamua kumpokea YESU na kufanyika mteule wa MUNGU hivyo usikubali kurudi nyuma.
Jifunze Kusikia Kutoka Kwa Watu Wema, Jifunze Huheshimu Watu, Pokea Roho Ya Kunyenyekea.
 Kataa Kujiinua Pia Kataa Kujiachia Kwa Kila Mtu, Jifunze Kunyenyekea, Salimia Wanaume Na Wanawake Bila Kujali Hali Zao Za Maisha. 
Ishi Kama MUNGU Apendavyo kwako mteule wake. 

Warumi 8:33 ''Ni nani atakayewashitaki wateule wa MUNGU? MUNGU ndiye mwenye kuwahesabia haki''
 
Baada ya kumpokea YESU hakika MUNGU alituhesabia haki.
Damu ya YESU ilituandika huru na sasa tuko huru katika KRISTO YESU Mwokozi wetu.
SasaNi wakati wetu wa kutenda Mema ayatakayo MUNGU wetu.
Jambo lolote jema alifanyalo mtu ndani yake kuna kusudi la MUNGU.
Siku moja niliamua kuwatia moyo marafiki zangu wote kwenye simu yangu, nikawaandikia meseji, lakini baadhi yao katika hao waliniandikia meseji wakishukuru sana.
Mtu mmoja alisema kwamba ujumbe niliomtumia ulikuwa wake haswaaa, akasema kwamba alikuwa anaumwa wiki 2 mfululizo na kuamka tu kitandani ilikuwa shida na alikata tamaa sana.
Lakini baada ya meseji ile kuingia akasoma na kupata nguvu za kuamka kisha akaomba kidogo tu na kupona, alinipigia simu akishangaa sana jinsi ujumbe wa meseji ulivyombadilisha ghafla.
Ndugu, kila jambo jema ulifanyalo ndani yake kuna kusudi la MUNGU.

Siku moja nilikuwa kwenye wakati mgumu sana kwa sababu nilitakiwa kusafiri siku iliyofuata kwenda Mwanza kwenye tukio la muhimu sana, hadi jioni nilikuwa sioni hata dalili za kusafiri na nilikuwa mbali na ubungo stend ya mabasi ya mkoa, Mwanza nilikuwa nasubiriwa sana na ni muhimu sana, nikiwa nawaza sana nitawezaje kusafiri ghafla mtumishi mmoja rafiki yangu akanipigia simu akiniambia vitu vilivyonipa nguvu za ajabu, katika hali ya ajabu nilisafiri baada kukuta stend Ubungo kuna kampuni moja ya mabasi imeleta mabasi mapya hivyo kwa sababu ni Mara ya kwanza basi basi ilikuwa haijajaa abiria, nikafanikiwa kusafiri kwa basi hiyo na Mwanza nikawahi na kila kitu kikawa safi.
Ndugu, kila jambo jema ulifanyalo ndani yake kuna kusudi la MUNGU.

Ni wakati wako mteule wa MUNGU kufanya mema.
 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments