BAADA YA YESU KRISTO KUFA MSALABANI HAYA YALITOKEA.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mathayo 27:51-54 '' Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda YESU, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa MUNGU.''

1. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili kutoka juu hadi chini.
 
Kwanini ilikuwa hivyo?
YESU alifanya hayo ili Katika maombi yetu na kukubaliwa kwetu na MUNGU basi tuwe sawa wote tuliookolewa na yeye YESU KRISTO.
Kwa njia hiyo MUNGU aliondoa tofauti ya patakatifu na patakatifu pa patakatifu ili kila Mteule awe na kibali cha kupaingia patakatifu pa patakatifu kwa njia ya maombi.
Kumbuka Mwanzo waliokuwa wanaruhusiwa kuingia patakatifu pa patakatifu alikuwa ni mtu mmoja tu yaani kuhani mkuu, na yeye aliingia mara moja kwa mwaka.
Kwa Njia ya YESU KRISTO kila mwamini sana anaweza akaingia patakatifu pa patakatifu na kujibiwa hitaji lake na MUNGU.

Biblia inajibu juu ya hilo, Waebrania 9:8-12 ''ROHO MTAKATIFU akionyesha neno hili, ya kwamba njia ya kupaingia patakatifu ilikuwa haijadhihirishwa bado, hapo hema ya kwanza ilipokuwa ingali ikisimama; ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye, kwa kuwa ni sheria za jinsi ya mwili tu, vyakula na vinywaji na kutawadha kwingine kwingine, zilizoamriwa hata wakati wa matengenezo mapya. Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. ''

Maana yake kila mtu sasa katika KRISTO YESU anaweza kumwendea MUNGU Baba kwa njia ya maombi na kukubariwa, sio lazima awe kuhani au mchungaji au askofu bali kila aliyempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake anauwezo wa kuomba kwa MUNGU Baba na kujibiwa.

2. Nchi ikatetemeka.
 
YESU KRISTO ndiye aliyeiumba Nchi yaani ardhi yote hivyo ardhi ilipata shinda sana kuupokea Mwili wa aliyeiumba.
Yohana 1:2-3 ''Huyo mwanzo alikuwako kwa MUNGU. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. ''
 
Pasipo YESU hakuna ambacho kingeumbwa, hivyo yeye ni muumbaji na aliumba hadi ardhi.
Ardhi ilitamani kukataa kuupokea Mwili wa YESU maana ardhi inajua hadhi ya Bwana YESU.
ardhi haikudhani kama hata siku moja mwili wa muumbaji ungeingia katika ardhi hivyo alidhi ilitetemeka sana na kuogopa maana ilijua YESU KRISTO ni nani.
Ardhi ni kama iliwaza ''Ni wapi tutamweka YESU?''
Maana hakukuwa na uwezekano wa YESU muumbaji wa ardhi kuingia ardhini.

3. Miamba ikapasuka.
 
Jambo la kwanza kujua katika hili ni kwamba YESU KRISTO ni Mwamba wa miamba yote.
1 Kor 10:4 ' wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni KRISTO. ''

Kwanini miamba ilipasuka?
Miamba ilipasuka kwa sababu ilikuwa inajisalimisha kwa Mwamba wa Miamba ambaye ni YESU KRISTO.
Miamba iliwakiliha watu wakubwa na mamlaka kuu, zote zilijisalimisha kwa Bwana YESU ndio maana hakuna mamlaka yeyote inayoweza kwenda kinyume na YESU ikafanikiwa.
Wateule wa MUNGU pia ni miaka ambayo iko chini ya Mwamba wa miamba ambayo ni YESU KRISTO.
Marko 16:18 ''Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. ''

Kumbuka pia kwamba YESU kama Mwamba hakika ukijenga nyumba yako juu mwamba uo hakika hakuna upepo wa kishetani au mvua za kichawi zitaiangusha nyumba yako.
Yaani ukimtegemea YESU na utakatifu hakuna anayeweza kukushinda aliye upande wa shetani.
Luka 6:48 ''Mfano wake ni mtu ajengaye nyumba, na kuchimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na kulipokuja gharika, mto uliishukia nyumba ile kwa nguvu, usiweze kuitikisa; kwa kuwa imejengwa vizuri.''
 
Hakika hakuna Mwamba kama MUNGU wetu ndio maana Miamba ilipasuka yaani ilijisalimisha kwake.
Isaya 44:8 '' Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko MUNGU zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine. ''
 
Hakika Miamba ilijisalimisha kwa Mwamba wa miamba maana Biblia inasema kwamba hakuna Mwamba kama JEHOVAH.
Kumbuka maana ya JEHOVAH ni MUNGU anayeokoa.
Na Sasa MUNGU anaokoa kupitia YESU KRISTO aliye mwamba wa milele.
Isaya 26:4 '' Mtumainini BWANA siku zote Maana BWANA YEHOVA ni mwamba wa milele.''
 
Hakika miamba ilikuwa na sababu za kujisalimisha kwa Mwamba wa milele.
Wateule wa MUNGU hatuogopi maana tunaye Mwamba wa milele.
Isaya 62:1-2 '' Nafsi yangu yamngoja MUNGU peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana ''

4. Makaburi yakafunuka na watakatifu wakafufuka na kuuenea mji.
 
Kuna siri kubwa juu ya hilo lakini kwa ufupi ni kwamba;
YESU KRISTO ana mamlaka yote hata aliweza kuwafufua watakatifu wote wa zamani na kuwahamishia mji mtakatifu.
Watakatifu sasa wala hawako kuzimu, wala hawako makaburini na wala hawako hewani bali wako mji mtakatifu.
Kila matakatifu wa KRISTO anapokufa duniani huenda mji mtakatifu ambao ni mbinguni na Bwana YESU ameshaandaa makazi huko ya watakatifu.
Yohana 14:1-3 ''1 Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini MUNGU, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. ''

Nyumbani mwa MUNGU kuna makao mengi, nyumbani mwa MUNGU ni mbinguni.
Ndio maana Bwana YESU alisema kwamba mteule wake akifa duniani anakuwa anaishi maana anakuwa yuko tayari mji mtakatifu.
Yohana 11:25-26 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? ''

Mtume Paulo kwa kulijua hilo alisema kwamba anatamni akaishi huko aliko KRISTO yaani mji takatifu ambapo ni mbinguni, Hata wateule wa KRISTO tunaoishi maisha matakatifu hakika tukiondoka duniani tutaenda mji mtakatifu.
Ona hii kiu ya Mtume Paulo ya kutaka kwenda kuishi mji mtakatifu.
Wafilipi 1:23 '' Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na KRISTO maana ni vizuri zaidi sana; ''

Kuna mambo mengi sana yalitokea baada ya Bwana YESU kufa na baadae kufufuka, nimekupa hayo manne yaliyo katika andiko moja tu lakini ukweli ni mambo mengi tu yaliyokea baada ya Bwana YESU kufa.
Nimalizie kwa kusema kwamba YESU KRISTO alikufa na kuzikwa na kisha akafufuka na sasa yu hai milele.
Mtume Yohana baada ya kumwona YESU akiwa katika utukufu wake baada ya kufufuka alianguka Yohana kwa hofu, Lakini Bwana YESU alijifunua kwa Yohana na kwako na kwangu kwamba yu hai milele na ana mamlaka yote.
Tumkimbilie tu yeye ili tuokoke.
Ufunuo 1:17-18 '' Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.''
MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments