BINTI UNATAKA KUOLEWA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
 Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu,
Karibu tujifunze Neno la MUNGU katika zamu ya leo.
Hili ni somo langu la  632 Tangu nimeanza huduma hii ya kufundisha kwa njia ya mtandao.
Leo nazungumzia mabinti au wanawake ambao hawajaolewa ila wanajiandaa kuolewa.
Ni mpango wa MUNGU mwanamke aolewe na awe na familia yake.
Mwanzo 2: 18 ''BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.''

Kumbe kila Kijana anaweza akamuomba MUNGU ampe mke wa kufanana naye ili awe mkewe wa ndoa takatifu.
Kumbe Kila Binti anaweza akamuomba MUNGU ili ampe mume  aliye wake ambaye yeye binti atakuwa msaidizi wake.
Najua kabisa kila mtu anatamani apate wa kufanana nae japokuwa kuna siri kubwa sana katika ''Kufanana nae'' ila leo sio zamu ya kuzungumzia hilo.
 Ni heshima kubwa binti kufunga ndoa takatifu kanisani kwa utakatifu na utii kwa MUNGU.
Najua kabisa wapo mabinti au wamama ambayo wanatarajia katika maisha yao kuingia katika ndoa takatifu.
Ni mpango wa MUNGU hakika.
Mwanzo 2:24 ''Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.''
Ni jambo jema sana kuingia katika ndoa lakini nataka ujifunze yafuatayo kabla ya kuingia katika ndoa takatifu.
 
Binti; Je unataka kuolewa?
 Kabla ya kukubali kuolewa naomba ujilidhishe katika haya yafuatayo;

1. Hakikisha unaolewa na Mwanaume unayempenda.

Hesabu 36:6 '' BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao.''
 Andiko hilo linaonyesha kusudi la MUNGU ni Binti kuolewa na Mwanaume anayempenda.
Hao walikuwa ni mabinti na MUNGU aliagiza waolewe na wanaume wanaowapenda wao na sio vinginevyo.
Binti ukitaka kuolewa kwanza hakikisha kwamba unampenda huyo mwanaume.
Mpende yeye na sio pesa zake wala elimu yake.
Mpende yeye na sio mwili wake au umbo lake.
Mpende yeye na sio familia yake bora anayotoka.
Olewa na mwanaume unayempenda wewe na sio wanaempenda tu watu wako wa karibu.
Ukizingatia hilo itakuwasidia kuwa na ndoa ambayo ina afya njema.

2. Hakikisha unaolewa Mwanaume kutoka kundi la watakatifu wa KRISTO.

Nehemia 13:25 ''Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.''
 Andiko hili linaonyesha kwamba ni makosa makubwa sana kwa Binti kukubali kuolewa na mtu asiyeokoka.
Nehemia alikuwa anawaonya waytu wa MUNGU.
Andiko linawaonya watu wa MUNGU kwamba hawatakiwi kuruhusu binti zao kuolewa na wasio mcha MUNGU katika KRISTO YESU.
Andiko hili linawakataza waisraeli kuwaoza binti zao kwa watu wa mataifa yaani watu ambao hawajaokoka na pia andiko linawakaza waisraeli kama wateule wa MUNGU kuoa au kuolewa kwa watu wasiookoka.
Binti kumbuka ili umpate Mwanaume mtakatifu inakupasa na wewe uwe mtakatifu.
Kama Mwanaume anayetaka kukuoa hajaokoka na haishi maisha matakatifu huyo hakufai kabisa.
 Nakusihi sana usiolewe bora tu kuolewa bali  olewa na mteule wa MUNGU ambaye ana hofu ya MUNGU.
Tangu zamani Biblia inakataza watu wa MUNGU kuolewa na watu wasiomcha MUNGU.
Ukilishika hilo hakika hutaangukia pabaya.

Madhara ya kuolewa na mwanaume asioyeokoka;
A. Kwake sio dhambi wala kosa kukuingilia kinyume na maumbile.
B.  Kukupiga kwake ni jambo la kawaida tu.
C.  Anaweza kumtumkia shetani ana akakulazimisha au kukuambukiza na wewe ukawa unamtumkia shetani na mwisho ukakosa uzima wa milele.

 3. Upendo wako kwa YESU uwe zaidi ya upendo wako kwa mwanadamu yeyote akiwemo mchumba wako huyo ambaye mnatarajia kufunga ndoa.

Luka 10:27 '' Akajibu akasema, Mpende BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.''

Hakuna anayetakiwa kuchukua nafasi ya MUNGU katika maisha yako.
 Ni heri ukawa tayari kumtii KRISTO kuliko mwanadamu yeyote.
Mwenzi wako ni wa Muhimu sana kwako lakini hawezi kuwa wa muhimu kuliko YESU KRISTO aliyekuokoa.
Hiyo ni kanuni ya kiroho unayotakiwa kuishika maisha yako yote.
Kuna watu wenzi wao wamewageuza miungu na kuwa machukizo kwa Kanisa la MUNGU na kwa MUNGU, Ni hatari sana.
Ndugu ishike kanuni hiyo ya ''YESU kwanza'' ili hata ukiolewa basi Mume wako asiwe na uwezo wa kumwondoa YESU moyoni mwako na kujiweka yeye au kuweka vitu vingine.
Kumbuka huyu Mume wako hamtaishi naye milele duniani lakini Kwa kumtii KRISTO na Neno lake hakika utakuwa na KRISTO milele.
Mwanadamu ana mwisho, uhusiano wenu una mwisho lakini kama unamtii MUNGU hakika uhusiano naye ni wa milele.
Nakuomba izingatie sana hiyo kanuni ndugu na ndipo utakuwa kielelezo chema.

 4. Ukiingia kwenye ndoa usimsahau MUNGU wala Kanisa la MUNGU.

Luka 17:26-27 '' Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.''
Hata wakati wa gharika ya Nuhu watu walikuwa wanaolewa na kuoa lakini waovu wote waliangamiza isipokuwa wanawake wanne tu na wanaume wanne tu.
Biblia inasema hata katika zama hizi za YESU KRISTO watu huolewa na kuoa lakini ni hatari kwake anayemsahau MUNGU na utakatifu.
Kuna watu baada ya kuolewa basi huo ndio ukawa mwisho wa huduma zao, ukawa mwisho wa kumtumikia MUNGU, Ukawa mwisho wa kwenda ibadani kwa kuwahi.
Kuna wamama wengi sana walikuwa wanahudhuria sana ibada kanisani na hawakuwa wanakosa ibada za mikesha kanisani lakini kitendo cha kuingia tu kwenye ndoa ndio wakaacha ibada na mikesha.
1 Kor 7:34 '' Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. Yeye asiyeolewa hujishughulisha na mambo ya BWANA, apate kuwa mtakatifu mwili na roho. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe.'
Ndugu Biblia inakuonya kwamba usikubali kuwa mtumwa wa ndoa au mtumwa wa mume wako.
Ndugu yangu ni bora ukajua kwamba unawajibika kwa MUNGU maisha yako yote haijalishi uko katika ndoa au bado hauko katika ndoa.
Zingatia hilo ni muhimu sana kwako.
Hata baada ya kuolewa nakuomba baki wewe ukiwa ni yule yule Mcha MUNGU asiye na mawaa.
Waefeso 4:17 '' Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika BWANA, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao''

 5. Ukimwacha mumeo na kwenda kwa mwingine unakuwa mzinzi.

Marko 10:12 '' na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.''
Ni muhimu sana kujua kwamba ukiingia katika ndoa hakuna kuachana hadi kifo kiwatenganishe.
Tabia mbaya ya kumsaliti mumeo iache na usikubali kuwa na tabia hiyo chafu.
Nakuomba itunze ndoa yako na kuilinda ndoa yako.
Hakuna haja ya kutamani wanaume wengine wakati unaye aliye wako.
Kama utakubali kufunga naye ndoa basi hakikisha unaiheshimu ndoa yako.
Zingatia hilo maana ni muhimu sana.

 6. Usiache maombi hata ukiingia katika ndoa.

1 Yohana 5:14-15 ''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.''


Maombi ni maisha ya mkristo Yeyote.
Usikubali kuacha maombi hata baada ya MUNGU kujibu hitaji lako na kupata mume na sasa unaenda kuingia katika ndoa.
Kumbuka kwamba muujiza uliopatikana kwa maombi basi muujiza huo unalindwa pia kwa maombi.
Itunze hiyo kanuni katika maisha yako na itakusaidia sana sana.
Kuna wamama leo baada ya kuingia katika ndoa waliacha maombi na baada ya muda ndoa ikawa na matatizo yasiyoisha.
Kuna wengine hata hudhani kwamba hawakupewa na MUNGU hao waume zao.
Ndugu zangu wakati mwingine ni MUNGU kabisa alikupa huyo mume mwema wako lakini ukisahau maombi basi shetani anaweza akapanda magumu katika ndoa yako na magugu hayo yakakusumbua kuyang'oa.  Maombi ni muhimu sana kwa kila mteule wa MUNGU hata akiwa ndani ya ndoa yake.
Inawezekana kabisa wewe uliomba sana kipindi hujaolewa lakini baada ya kuolewa umesahau maombi na ndio maana adui anakuletea migogoro katika ndoa yako.
Nakuomba wewe ambaye unatarajia kuingia katika ndoa basi hakikisha unakuwa muombaji na endelea na maombi maisha yako yote.
Kumbuka maandiko yanasema  

 ''ombeni bila kukoma;-1 Thesalonike 5:17''


7.  Tambua kwamba ikitokea umeachana na mumeo basi hauruhusiwi kuolewa na mwingine yeyote.

1 Kor 7:11 ''lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.''

Kama ndoa yako itakushinda nakuomba utambue kwamba kanuni ya Kibiblia ni kwamba huna ruhusa ya kuolewa  na mwanaume mwingine.
Kama umeachana na mumeo na unatamani ndoa basi rudi kwa mumeo.
Kama unatamani ndoa na tendo la ndoa basi rudi kwa mumeo msuruhishe na kuendelea na ndoa yenu.
Unaweza tu kuolewa na Mwanaume mwingine ikiwa tu kwa habati mbaya mumeo amefariki.
Lakini isiwe wewe ndio umemuoa mumeo ili uolewe, hiyo ni laana na ni dhambi mbaya sana.
Ndugu lengo langu ni kukujulisha kwamba kama itatokeo umeingi katika ndoa na bahati mbaya ikakulazimu kuacha na mumeo labda kwa tabia zake au kwa tabia zako basi huna ruhusa ya kuolewa na mwingine.
Omba tu maombi ya kumtengeneza mumeo ili atimie kwenye vigezo vyako, kuolewa kwingine ni dhambi na utakuwa mzinzi maisha yako yote, hivyo kabla ya kuingia katika ndoa basi jilidhishe vyema ndipo uamue.
Ukizingatia mambo hayo sana basi nakutakia ndoa njema.
Mr & Mrs  Mabula.
Namshukuru MUNGU pia wakati naandika somo hili nimeona kwa maono kuna wamama wanawafundisha mabinti somo hili langu.
Namshukuru MUNGU hata kama sijui ni wapi huko na anayefundisha ni nani na anayefundishwa ni nani.

MUNGU akubariki na pia Ukipenda kunisapoti kwa sadaka katika huduma yangu karibu sana na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.

0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments