KWANINI YESU ALIKATA ROHO SAA TISA?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU apewe sifa ndugu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Luka 23:44-46 "Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. YESU akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee BABA, mikononi mwako naiweka roho yangu."


Ilikuwa Giza kuanzia saa 6 mchana hadi saa 9 siku ambayo Bwana YESU alikuwa anatukamilisha Wokovu wetu.
Saa 9 alasiri ndio muda ambao YESU alikufa.
Ulishawahi kujiuliza kwanini iwe saa 9 na sio muda mwingine wowote?
Hata Mimi huwa najiuliza lakini kwa sehemu acha nikujulishe.

Jambo la kwanza naomba tujue kwamba YESU alikuwa mwanakondoo wa MUNGU ambaye alipata kutolewa sadaka ili kuwa upatanisho, tunapatanishwa na MUNGU kwa damu ya YESU KRISTO.

Yohana 1:29b " Mwana-kondoo wa MUNGU, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!"


YESU ni mwanakondoo wa MUNGU aichukuaye dhambi ya wanadamu wanaotubu.
YESU alikuwa sadaka ya hatia.


1 Petro 1:18-20 " Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya KRISTO. Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa mwisho wa zamani kwa ajili yenu;"

Hivyo YESU kama kondoo wa sadaka ya upatanisho ilipasa atolewe sadaka kwa njia ya kifo chake ili kuwa upatanisho wa dhambi zetu tunaotubu na kumtii.
Yeye ni kondoo aliyechinjwa, aliyetolewa sadaka ili kutununua sisi.


Ufunuo 5:8-10 "Hata(YESU) alipokitwaa kile kitabu, hao wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne wakaanguka mbele za Mwana-Kondoo(YESU), kila mmoja wao ana kinubi, na vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, ambayo ni maombi ya watakatifu. Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa MUNGU wetu; nao wanamiliki juu ya nchi."

Kama sadaka ilipasa atolewe sadaka muda wa kutoa sadaka ambao pia ni muda wa ibada maana sadaka hutolewa wakati wa ibada.
Kwa taratibu za Waisraeli saa 9 ulikuwa muda wa ibada na muda wa kutoa sadaka.


Matendo 3:1 "Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, SAA YA KUSALI, SAA TISA."
 
Saa Tisa alasiri/Adhuhuri ilikuwa muda wa ibada katika taratibu za waisraeli, na katika ibada na sadaka zilitolewa, hivyo hata YESU kama sadaka ya upatanisho alikuja kama sadaka huo.

Kulikuwa na muda wa kutoa sadaka za jioni na masaa ya adhuhuri yalihusima na ni masaa hayo hayo ambayo YESU kama mwanakondoo alitolewa sadaka na MUNGU ili kuwa upatanisho.
Tunajua kabisa kwamba jioni huanza saa kumi hivyo sadaka za jioni zilikuwa zinatolewa masaa hayo hayo.
Ona mfano huu.
1 Wafalme 18:29 "Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia."


Na huu
Danieli 9:21 "naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni."

Wakati wa Dhabihu za jioni ulikuwa ni muda uliokuwa umetengwa kila siku. Hivyo muda huo kulikuwa na ibada na katika ibada hiyo sadaka zilizotewa.
 Jambo kubwa ndugu zangu sio kujua saa tu ambayo Bwana YESU alikufa na kukufuka bali jambo muhimu sana ni kumpokea kama Mwokozi na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
 Tukumbuke kwamba Mwanadamu anayemkataa YESU KRISTO kama Mwokozi wake huyo ndugu hana MUNGU ila ana mapepo tu ambayo ndiyo anayaabudu.
Biblia iko wazi mno juu ya hilo.

1 Yohana 2:23 "Kila amkanaye Mwana(YESU), hanaye Baba(MUNGU); amkiriye Mwana(YESU) anaye Baba(MUNGU) pia."
Unaweza ukasema hivi;
Anayemkataa YESU kuwa Mwokozi wake moja kwa moja mtu huyo anakuwa amemkataa MUNGU kuwa MUNGU wake.

Ukimkataa MUNGU unakuwa umekataa uzima wake wa milele.
Ukimkataa YESU KRISTO unakuwa umemkataa ROHO MTAKATIFU na unakuwa umeikataa kweli ya MUNGU na unakuwa umeukataa uzima wa milele.


Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."

Hakika ni Neema ya MUNGU mimi na wewe tuokolewe na Bwana YESU ni vyema kuitumia Neema ya MUNGU vizuri.
 Haki ya MUNGU haipatikani kwa matendo Bali haki ya MUNGU hupatikana kwa neema baada ya kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Jambo kubwa kujua ni kwamba usiichezee neema ya MUNGU.
Jambo jingine ni kwamba usiitumie neema ya MUNGU vibaya.
Jambo jingine utakatifu katika KRISTO ndiko kunakoleta neema juu ya neema.
Neema ya MUNGU inatufundisha kukataa ubaya wote.
Kama unafanya dhambi ukitegemea neema ya MUNGU hakika wewe hujitambui.
Neema ya MUNGU haipatikani kwa sheria au matendo ya sheria Bali kwa wokovu wa KRISTO YESU.
Warumi 3:21-26" Lakini sasa, haki ya MUNGU imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya MUNGU iliyo kwa njia ya imani katika YESU KRISTO kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;
kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa MUNGU;
wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika KRISTO YESU; ambaye MUNGU amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake,ili aonyeshe haki yake ,kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa MUNGU dhambi zote zilzotangulia kufanywa.
apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye YESU."


 MUNGU akubariki na pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
mabula1986@gmail.com
Umeshashare sana jumbe zisizo na maana leo
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments